Monday, November 26, 2012

El Nino Tanzania

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UCHUKUZI
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

Simu ya mdomo: 255 22 2460 735/2460 706-8
FAKSI: 255 22 2460 735/700 S.L.P. 3056
Simu pepe: met@meteo.go.tz DAR ES SALAAM
Tovuti: www.meteo.go.tz

24 Novemba, 2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA

MREJEO WA HALI YA EL NIÑO NA LA NIÑA

Taarifa hii inatoa mrejeo wa hali ya joto la bahari (El Niño na La Niña) kwa kipindi cha Julai hadi Novemba, 2012.

Hali ya sasa na mwelekeo wa Hali ya joto la Bahari:

Katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2012, hali ya joto la bahari ukanda wa tropikali wa Bahari ya Pasifiki iliongezeka na kuwa juu ya wastani hali iliyoashiria kuwepo kwa El Niño hafifu, hata hivyo hali ya mifumo ya upepo, mgandamizo wa hewa katika usawa wa bahari na mawingu vilishindwa kuwiana na ongezeko hilo hafifu la joto la bahari.

Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni hadi sasa hali ya joto la bahari katika ukanda wa tropikali wa Bahari ya Pasifiki imekuwa ya wastani, hali hii haiashirii kuwepo kwa aidha El Niño au La Niña. Aidha katika ukanda wa Bahari ya Hindi unaopakana na nchi yetu pamoja na joto la bahari kuwa la juu ya wastani, mifumo ya upepo na mgandamizo wa hewa vimeendelea nyevunyevu katika anga. Hali hii ya mabadiliko ya joto la bahari na mifumo ya hali ya hewa si ya kawaida na haijawahi kutokea katika miaka iliyopita.

Kutokana na hali hii isiyokuwa ya kawaida taasisi zinazohusika na masuala ya hali ya hewa katika Kanda ya Pembe ya Afrika (ICPAC) na Kanda ya Kusini mwa Afrika (SADC-CSC) kwa mara ya kwanza zimeandaa warsha ya wataalamu wa hali ya hewa ikiwemo Tanzania, kufanya  uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mrejeo wa mwelekeo wa mvua za msimu katika ukanda huu. Mikutano hii itafanyika tarehe 29 hadi 30 Novemba, 2012 Nairobi, Kenya na tarehe 5 hadi 13 Disemba, 2012 Lusaka, Zambia. Baada ya taarifa hiyo ya kikanda, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itapitia taarifa hiyo na kutoa mrejeo wa utabiri wa msimu wa mvua nchini.

Tathmini ya mvua kuanzia mwezi Oktoba hadi Novemba 2012:

Katika maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka, hususani maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga) mvua zinaendelea  kunyesha, wakati maeneo ya nyanda za juu Kaskazini mashariki (mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara) na pwani ya Kaskazini (mikoa ya Pwani, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba) kumekuwa na mvua ambazo ni za chini ya wastani.

Aidha, katika maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka, hususani maeneo ya Kigoma, Mbeya, Njombe, Iringa, Tabora, Katavi na Singida mvua zimeanza na zinaendelea . Mtawanyiko wa mvua hizo si wa kuridhisha katika baadhi ya maeneo.

Ushauri:

Katika maeneo ambayo mvua iliyonyesha mpaka sasa ni chini ya wastani, wananchi wanashauriwa kutumia maji kwa uangalifu na kuhifadhi malisho kwa ajili ya mifugo.  Pamoja na mabadiliko hayo ambayo si ya kawaida yaliyojitokeza kuna uwezekano wa kuwepo kwa vipingi vifupi vya mvua kubwa hivyo wananchi wanashauriwa kuendelea kuchukua  tahadhari.

Mamlaka ya hali ya hewa inaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na itaendelea

kutoa taarifa “update” za mara kwa mara.

Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

No comments: