Saturday, October 29, 2016

Taarifa Kutoka CCM

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Ndugu Christopher Ole Sendeka, Msemaji wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa akizungumza kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika leo tarehe 28/10/2016 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba jijini Dar es salaam.

Ndugu wanahabari,

Kwa muda sasa kumekuwepo na usambazaji wa taarifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa wakishirikiana na baadhi ya vyombo vya habari zinazolenga kukejeli, kudhihaki, kukatisha tamaa, kubeza na kudhoofisha jitihada zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi na Serikali zake katika kuleta maendeleo kwa Watanzania.

Kumekuwepo na makala zinazoandikwa na magazeti mawili ya nje ambazo hutolewa kila baada ya miezi miwili na ambazo zinapotosha na kuandika habari zisizo za kweli kuhusu Tanzania.

Pia, yapo magazeti mawili ya ndani ambayo yamekuwa yakitoa makala mfululizo kwa kila wiki zinazolenga kumchafua Mheshimiwa Rais na kuichafua taswira ya nchi yetu.

Tumesikitishwa na waandishi wa makala hizo walioamua kujivua uzalendo na kushiriki mpango wa kuiharibu heshima na taswira ya nchi yetu kwa maslahi ya maadui zetu wa nje na baadhi ya wanasiasa. Tunafuatilia kujua nini kinawasukuma kufanya hivyo na kwa maslahi ya nani ilhali sote ni Watanzania. Je ni tamaa ya madaraka tu au mengine? Hakuna anayepinga ukosoaji bali unapaswa uwe ukosoaji wenye nia njema kwa nchi.

Ndugu wanahabari,
Mtakumbuka hivi karibuni aliyewahi kuwa Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa tuhuma za ufisadi ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa, alisambaza taarifa kwa vyombo vya habari aliyoiita ya tathmini ya mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015.

Katika taarifa yake hiyo, alidai kuwa alileta msisimko mpya katika siasa za Tanzania, kwamba ameshirikiana na wenzake kuionyesha nchi yetu maana ya demokrasia na kukosoa juhudi za serikali na wateule wa Rais.

Demokrasia kimsingi ni dhana inayohusisha ushiriki na kuheshimu mawazo ya wengi katika kufikia uamuzi. Ikiwa maana halisi ni hii, tunajiuliza ni ipi demokrasia aliyoionyesha Lowassa ambayo leo anajisifu kuwa nayo?
-          Tulishuhudia akiwa mgombea urais wa chama ambacho hakijui, hakushiriki kukijenga wala kutoa mchango wowote unaompa hadhi ya kupeperusha bendera huku katiba na kanuni ya chama hicho  ikivunjwa.  Kidemokrasia, anayepewa fursa ya kupeperusha bendera ya chama chochote makini duniani ni kiongozi au mwanachama aliyethibitika kwa imani na matendo, kuzielewa, kuzitekeleza, kuzitetea falsafa, itikadi na malengo ya msingi ya chama hicho. Mgombea ni taswira halisi na alama muhimu inayoakisi dhamira ya chama husika machoni kwa wananchi.

-          Demokrasia ya kweli lazima ianzie ndani ya chama, ni demokrasia ipi iliyotoa mamlaka kwa vyama vinavyounda UKAWA kuwanyima wanachama wao haki ya kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera za vyama walivyoviasisi, kuvitetea, kuvigharamia na walivyovitumikia kwa kuamua kumteua mgombea “MTUNGUO” (ambaye hajapimwa wala hajawahi kuvipigania). Kitendo hicho cha kutowashirikisha wanachama na kuwanyima haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kilidhihirisha usaliti wa hali ya juu wa misingi ya demokrasia.

-          CHADEMA watuambie njia iliyotumika kuwapata wabunge wa viti maalumu. Ni demokrasia gani inayotoa fursa kwa baadhi tu ya viongozi  kuteua wabunge ambao wanakiwakilisha chama chote. Ambapo kila kiongozi aliteua maswahiba zake na wengine kwa ugeni wao ndani ya CHADEMA walikosa watu wanaowafahamu na kuamua kuwateua wanawake maswahiba wao ndani ya CCM. Msingi wa kawaida wa kupata wabunge wa viti maalum ukiacha kura za maoni, kigezo kingine muhimu ni mchango wa mgombea/mwanachama huyo katika kukijenga na kukitumikia chama chake. Yaliyotokea kwa CHADEMA kwenye wabunge wake wa viti maalum ni mapya kwenye ulimwengu wa demokrasia. Inahitaji wataalamu wa sayansi ya siasa kufanya utafiti wa aina hii mpya ya demokrasia.
Tulidhani baada ya mwaka mmoja kupita, wenzetu hawa wangelikuwa wamejifanyia tathmini, kujikosoa, kujisahihisha na hata kufanya uungwana wa kuwaomba radhi wanachama wao kwa uvunjifu mkubwa wa misingi ya demokrasia, katiba na kanuni za vyama vyao.

Tunatoa wito kwa vyama vya siasa nchini kutochukulia kwa wepesi masuala ya demokrasia na mabadiliko, yasiwe ni nyimbo za kuburudisha au kutoa matumaini hewa kwa wanachama na wananchi. Kanuni mojawapo ya demokrasia ndani ya vyama ni lazima ionekane katika muundo wake na katika utekelezaji wa muundo huo.

Umefika wakati vyama vya siasa vinapaswa kujifunza kuuza sera ili kujijenga na sio kusubiri matukio kwa ajili ya kupata huruma ya wananchi. Tunasubiri kushuhudia na kusikia demokrasia itakavyoendeshwa katika uchaguzi wa ndani wa vyama hivyo ambapo kuna taarifa mmoja wa vigogo amefanikiwa kupata kiasi cha dola milioni 15 zitakazomsaidia kupanga safu yake ya uongozi.

Katika kutimiza mpango huo, tayari yapo mawasiliano ya mara kwa mara ya baadhi ya viongozi wakitoka Zanzibar na sehemu zingine za nchi kuja Dar es Salaam, na imeonekana dhahiri mazungumzo yao kutowashirikisha viongozi wenzao waandamizi kwani yanalenga kufanikisha mpango huo.

Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli, ameendela kufanya juhudi kubwa katika kuijenga nchi kwa kuimarisha utendaji na nidhamu ya utumishi serikalini, kukusanya mapato na kusimamia matumizi sahihi ya fedha, kupambana na kuzuia mianya ya rushwa pamoja na kusimamia haki, usawa na wajibu kwa raia. Mwenzetu anayaona haya kuwa ni kuufanya utumishi wa umma kaa la moto.

Juhudi hizi na nyinginezo ikiwemo ununuzi wa ndege mpya, ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, afya kwa kununua vitanda vya wazazi, kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari  na nyinginezo hazipaswi kukatishwa tamaa kwa maslahi ya wachache, ni vyema kuziunga mkono kwa maslahi ya taifa letu.

Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Rais Dk. Magufuli madarakani, CCM inawaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono katika dhamira yake safi ya kuwaondolea kero, kuboresha huduma za jamii na kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Imetolewa na;-
                                                CHRISTOPHER OLE SENDEKA
MJUMBE WA NEC NA MSEMAJI WA CCM
28/10/2016.

No comments: