MKURUGENZI wa Extra Bongo Ally Chocky ametoa kauli nzito
kuhusu waajiri wake wa zamani, Asha Baraka na Baraka Msilwa.
Katika mahojiano yake maaalum na mtandao nambari moja kwa
habari za muziki na wanamuziki nchini, Saluti5, Chocky alisema katika watu
asiowapenda duniani ni Asha Baraka (Mkurugenzi wa ASET) na Baraka Msilwa
(Mwenyekiti wa ASET). Asha Baraka na Baraka Msilwa ni mtu na kaka yake.
Kiongozi huyo wa Extra Bongo akaenda mbali zaidi kwa kusema:
“Nikifa leo hii Asha Baraka na Baraka Msilwa wasije kwenye mazishi yangu, na
kama watanitangulia wao na mimi sitakwenda kwenye mazishi yao.
“Nina uhakika leo hii nikipata matatizo au nikifa Asha na
Msilwa watafurahi, sasa kuna haja gani ya watu kama hao kuja kwenye mazishi
yangu.
“ASET ni kama simba wako tayari kukutafuna hadi macho,
nimetafakari kwa muda mrefu sana nimevumilia mengi sana lakini nimeshindwa na
sasa natamka rasmi, Nikifa wasinizike.”
Chocky ameorodhesha sababu nyingi sana za kufikia hatua hiyo
lakini miongoni mwa sababu zake ni hizi tatu:
Kwanza kitendo cha Aset kumpeleka mahakamani kumdai gari,
pili Aset kukataa kurudisha pesa za Miraji Shakashia na tatu ni ASET
kutothamini michango ya wasanii walioizalishia pesa nyingi.
Chocky ansema kitendo cha Aset kumpeleka mahakamani kumdai
gari ambalo walimpa mwenyewe kilimkera sana.
“Mtu anapokupeleka mahakamani maana yake ni kwamba yupo
tayari hata ufungwe, ukifungwa maana yake ni kila kitu kwenye maisha yako
kinaharibika.
“Gari walinipa wenyewe na maandishi yapo kwamba nikimaliza
mkataba wangu gari litakuwa la kwangu.
Lakini badala yake wakanigeuzia kibao na kwenda kunidai
mahakamani kwamba nimeiba gari.
Kuhusu Shakashia, Chocky amesema mwanamuziki huyo alichukua
shilingi milioni tano za Extra Bongo ili ajiunge nayo na akasaini mkataba wake.
“Lakini badala yake Shakashia akaingia mitini na pesa zetu,
Aset wakasema watazirudisha wao na sasa wanakuja na hadithi mpya.
“Wanasema hawawezi kurudisha hizo pesa eti kwa vile
wananidai, wanasahau kuwa mkataba wa Shakashia ni kati yeke na Extra Bongo na
sio Ally Chocky.
“Hata kama kipo wanachonidai hiyo ni kati ya Chocky na Aset
na haiingii akilini kuliingiza suala la Shakashia ndani yake.
“Huu ni utapeli na inatoa picha kuwa Aset walimtumia
Shakashia kufanya utapeli huu, lakini wajue kuwa mwisho wa siku atakayeathirika
ni Shakashia mwenyewe,” alisema Chocky.
Kuhusu kutothamini wasanii waliozalishia pesa nyingi kampuni,
Chocky anasema wasanii walipota ASET na kuizalishia pesa hawana chochote
walichopewa kulingana na thamani ya kile walichokizalisha. “Sio pesa tu bali
hata heshima pia hakuna,” alifafanua Chocky.
Chocky akazama zaidi na kuwataja wakongwe kama Shem Karenga
na Kasongo Mpinda ambao waliwahi kufanya kazi katika familia ya kina Asha
Baraka kupitia bendi za MK Group na MK Beats.
“Wako wapi Kasongo Mpinda na Shem Karenga, Kasongo
aliwatengenezea pesa nyingi kupitia MK Group “Ngoma za Magorofani” huku Shem
Karenga akiwatengenezea utajiri katika MK Beats “Tukunyema”.
“Lakini hebu tujiulize wako wapi hawa wazee na wana kipi cha
kujivunia?” alihoji Chocky.
Saluti5 haikuishia hapo, iliamua kumpigia Asha Baraka ambaye
naye alikuwa na yake ya kujibu kuhusu mapigo ya Chocky.
Asha Baraka amesema hayo ni mambo ya kike na kwamba kuzikana
si tija.
Asha Baraka akasema: “Hata mimi sina mpango wa kwenda kwenye
mazishi yake na yeye pia asije kwenye mazishi yangu.
“Hivi kuzikana ni nini? Wazazi wangu walifariki na Chocky
hakuja kuzika, kilipungua nini? Halafu mi nikifa sitaona na yeye akifa sitaona
kwahiyo hiyo siyo ishu, wamanyema wenzangu watatosha kunizika hata wasanii wote
wasipokuja achilia mbali huyo Chocky.
“Nilimzikia wazazi wake na hakuliona hilo kwahiyo hata
tusipozikana hakipungui kitu.
“Chokcy tunamdai gari na pesa shilingi milioni 13, kwenda
mahakamani ni sehemu ya kudai haki na yeye kama anaona amedhulumiwa kuhusu pesa
za Shakashia basi aende mahakamani.”
Asha Baraka alimtaka Chocky aelewe kuwa baadhi ya wasanii wa
Twanga ni virusi na watammalizia pesa zake bure.
“Wako wasanii wamelelewa vizuri, wamefanyiwa mengi na Twanga
na wanaelewa utu kwahiyo akijipendekeza kwao atapoteza pesa zake bure.
“Hao ni virusi wetu, wanatuletea taarifa zote za kila mtu
anapotaka kuwachukua.
Asha Baraka amesema kama ni roho mbaya Chocky ndio anaoongoza
kwa roho mbaya.
“Alikaa yeye na kamati yake yenye wakiwemo mpaka wafanyakazi
wa umma na kuzoa wanamuziki wa Twanga”
Anawataja wasanii wa Twanga waliowahi kuchukuliwa na Extra
Bongo ni pamoja na Ferguson, Rogart Hegga, Hosea, Otilya, Nyamwela, Danger Boy,
Aisha Madinda, Maria Soloma, Subrina pamoja na Kanuti ambaye baadae alirudisha
pesa zao na kubakia Twanga.
Asha Baraka anawataja wasanii wengine wenye damu ya Aset
ambao wako Extra Bongo ni Ephraim Joshua, Martin Kibosho, Athanas, Banza Stone
na yeye mwenyewe Chocky.
“Kwa mfumo huo utaona wazi
kuwa Extra Bongo inapumua kwa nguvu ya Aset lakini sisi hatujasema kitu, kama
ni kutoa kauli ya kutozikana basi sisi ndio tulipaswa kuwa wa kwanza,”
alifafanua Asha.
“Tunajua pia kuwa Chocky alihusika kushawishi usajili wa Chaz
Baba Mashujaa Band akiamini kuwa kwa kuondoka Chaz Twanga itakufa,” aliongeza
Asha Baraka amemtaka Chocky aonyeshe mfano wa namna ya kulea
wasanii kwa kuwapa maisha mazuri wanamuziki waandamizi kama Banza na Rogart.
“Asiangalie mambo ya Aset, ajitazame yeye anaishi vipi na
Banza anaishi vipi, badala ya kutoa milioni tano kumnunua Shakashia,
angemnunulia japo Corola Banza au Rogart.
“Chocky aitishe mkutano wa waandishi wa habari halafu mimi na
yeye twende na mikataba ya wasanii inayoonyesha mishahara na marupurupu tuone
nani analea vizuri wasanii.
“Mimi nilifanya kazi Bima na sijajengewa nyumba wala
kununuliwa gari, silalamiki kwa kuwa haikuwa sehemu ya makubaliano yetu.
“Kama Chocky anadhani
muziki unalipa kiasi cha kumnunulia kila mtu gari na nyumba basi atuonyeshe
mfano kupitia Extra Bongo.
“Kila baya linalomfika basi mchawi ni Aset, mbona mimi naumwa
mguu na sijawahi kusema ni Chocky?
“Chocky akapime afya yake
apate ukweli, tunajua rekodi ya sehemu alizopita, sasa asije akadondoka akasema
ni Aset …akapime kwanza” alimaliza Asha Baraka.