HISTORIA HALISI YA WASABATO: AIBU TUPU
Imeandikwa na Padri Titus Amigu
Ndugu zanguni nitaendelea na mada yetu ya “viboko hamsa wa ishirini”
lakini naomba nikatishe kidogo nipate kujibu swali moja linalojirudia
rudia sana. Swali lenyewe naulizwa kwa namna nyingi mno. Mtu wa mwisho
ameniuliza akisema hivi: “ Asante sana baba gombera mstaafu, hivi huyu
Bi Ellen G. White ni nani katika Kanisa Katoliki? Mbona amekuwa
akishambulia sana Kanisa Katoliki au kuna makanisa mengine huanzishwa na
misingi yao ni lazima kushambulia Kanisa Katoliki?
Jibu fupi: Bi Ellen G. White ni mmojawapo wa waanzilishi wa kanisa la
Wasabato lakini fundi sana wa kulitukana Kanisa Katoliki. Yeye hakuwamo
ndani ya Kanisa Katoliki na wala hakujihusisha nalo kwa nia njema
isipokuwa aliondokea kuongoza kulitukana.
Wala si siri yapo makanisa ambayo huanzishwa na misingi yao ni lazima
kulishambulia Kanisa Katoliki kwa sababu zao mbalimbali. Kanisa mojawapo
kati ya hayo ndilo kanisa aliloshiriki Bi. Ellen White kulianzisha
yaani kanisa la Sabato. Inasikitisha sana na kukera sana, lakini
tutafanyaje. Ndiyo hivyo tena, kisera, kanisa la Sabato limepania
kulibomoa Kanisa Katoliki. Sisi hatuwezi kuwachukulia hatua ya kiuhalifu
isipokuwa kufahamishana kama ninavyokusudia kufanya ili tukae chonjo
nalo tu. Kumbe kwa busara ya maisha, anayekuwinda walau mjue tu kusudi
ujue namna ya kumkwepa. Wala si lazima upigane naye.
Sasa kusudi vijana mmwelewe vizuri mtu huyo aheri nikupeni historia
nzima ya kuanzishwa kwa kanisa la Wasabato. Katika historia hiyo mtaona
aibu ya kushindwa utabiri wa mwisho wa dunia. Cha kushangaza
waliposhindwa kutabiri mwisho wa dunia kama walivyojinasibu kuweza,
wakageukia kulitukana Kanisa Katoliki ambalo halina kosa lolote na
halikuwafanya chochote.
Hivi acheni niitumie fursa ya kujibu swali hili kwa kuwaleteen historia
halisi ya Kanisa la Wasabato. Nawaanikieni hadharani aibu yao, aibu
inayowatia hasira na hasira yenyewe kuilekeza kwa Kanisa Katoliki ambalo
halijawakosea.
Jibu hili nimewahi kuliandika kwenye Gazeti la Kiongozi na vile vile
kulirusha hewani kwa njia ya radio. Lakini kwa kuwa bado naendelea
kuulizwa, kwa mitindo mbalimbali, kila uchao napenda nilijibu tena sasa
kwa kupitia ukurasa wangu wa Facebook. Sina nia ya kuleta uchochezi.
Najibu swali kwa kadiri inavyostahili tu.
Jibu refu: Wakatoliki tunatukanwa kwa sababu Wasabato wanajaribu
kufunika aibu yao ya kihistoria na wanadhani matusi ndiyo njia ya kuliua
Kanisa Katoliki. Hawajui kwamba matusi hayawezi kumharibu mtu isipokuwa
kumfedhesha mtukanaji tu. Waungwana hawatukani. Kumbe, aheri tuielewe
historia ya dhehebu la Wasabato au S.D.A tupate kuwapuuza wanaotutukana
huku wakijiabisha wenyewe. Basi, historia hiyo ya aibu inayofichwa ndiyo
hii ifuatayo:
Ni hivi ndugu zanguni, kwa kuiweka bayana historia ya Wasabato,
tuambatane katika kuwaelewa watu wanne ambao hutajwa kama watangulizi au
waasisi wa dhehebu la Wasabato. Mwishoni nitayapembua waliyofundisha
kibiblia na kisaikolojia.
Mtu wa kwanza ni William Miller, wa pili ni Hiram Edson, wa tatu ni Joseph Bates na wa nne na wa mwisho awe Bi Ellen G. White.
Tukianza na Bw. William Miller, yeye alizaliwa mwaka wa 1782 katika mji
wa Pittsfield, Massachusetts, huko Marekani. Ingawa alizaliwa katika
familia ya Kikristo, aliuacha Ukristo alipokuwa kijana mbichi. Kwa
kweli hakuiamini Biblia kuwa neno la Mungu. Basi, akajiunga na jeshi.
Baada ya kutumika kama mwanajeshi kwa muda mfupi, akaishi kama mkulima.
Kumbe, mwaka wa 1816, akaongoka na kuurudia Ukristo wake kwa kasi
mpya. Kwa kweli, tangu mwaka huo wa kuongoka kwake, Bw. William Miller
alisoma unabii kwa kina na hasa unabii uliohusu kurudi kwa Yesu Kristo,
Bwana wetu.
Kumbe, kutokana na kujifunza huko, Bw. William Miller akashawishiwa
kwamba mwisho wa dunia ungetimia mwaka 1843. Kifupi, Bw. William Miller
alishawishiwa kufundisha jinsi hiyo na unabii wa kitabu cha Danieli
9:24-27, unabii unaohusu majuma sabini yaliyowekwa kwa ajili ya watu wa
Mungu, taifa la Israeli.
Zaidi ya hayo, katika Danieli 8:13-14, kuna unabii wa watakatifu wawili
wanaoulizana lini patakatifu patatakaswa. Mintarafu unabii huo, Bw.
William Miller alitafsiri kwamba patakatifu patakapotakaswa, ni dunia
hii iliyochafuliwa na dhambi za kila sampuli. Kwa maoni yake, mwaka wa
1843 B.K., ndio mwaka ambao Yesu Kristo angerudi katika dunia
iliyonajisiwa kupita kiasi na dhambi na hivyo kuitakasa kabisa kwa
kuwapo kwake.
Msimamo huu ulimfanya awe maarufu sana katika sehemu nyingi za Marekani,
na hatimaye akawa mhubiri mkubwa wa dhehebu la Kibaptisti. Kwa kuwa
mwisho wa dunia ulikuwa unaambatana na kurudi kwa Yesu Kristo, ambako
kwa Kiingereza huitwa “Christ’s Advent”, wafuasi wake walianza
kujulikana kama “Adventists” au kwa Kiswahili “Waadventisti”, yaani
“Watu watarajiao kurudi kwa Kristo”. Ijapokuwa mwanzoni hakutaja tarehe
bayana ya kurudi kwa Yesu, punde si punde alisema kurudi kwa Yesu
kungekuwa kati ya tarehe 21 Machi, 1843 na 21 Machi, 1844.
Baada ya mambo kufikia hapo, mfuasi mmoja wa Bw. William Miller
aliyeitwa Samwel Snow, akawa jasiri zaidi na kutaja kwamba Kristo
angerudi tarehe 22 Oktoba, 1844 saa 6.00 usiku; yaani ndipo parapanda
litakapopulizwa, mbingu kukunjwa kama kurasa, na Yesu Kristo kufika kwa
utukufu mwingi. Lakini mambo hayakutukia hivyo walivyohubiri. Basi,
kwa vile Kristo hakurudi kama walivyotarajia, Bw. Miller akakiri kukosea
kwake, lakini akawaonya wafuasi wake wasisahau kwamba Kristo atarudi
upesi.
Kwa bahati mbaya, Bw. William Miller alifariki mnamo mwaka 1849 ndoto
yake ya kumwona Yesu akirudi upesi ikiwa bado haijatimia. Hadi hapo,
ieleweke kwamba Bw. William Miller, hakuwahi kuwa Msabato. Hivyo kama
Mbaptisti, alikuwa anasali siku ya Bwana, yaani Jumapili au Dominika.
Kutokana na kutokutumia kwa utabiri wa Bw. William Miller wafuasi wake
wengi wakarejea nyuma.
Basi, tumwachie Bw. William Miller hapo, nasi tusonge mbele
tukamwangalie mtu wa pili, yanii Bw. Hiram Edson. Kwa bahati, bwana
huyu alikuwa kati ya Waadventisti wachache waliobaki baada ya kuvunjika
moyo kwa wafuasi wengine wa William Miller kutokana na kutorudi kwa
Kristo kama ilivyotazamiwa. Kwa upande wake kwa kusudi la kuwafariji
wenzake kwenye huzuni yao, yeye alidai kwamba Mungu alikuwa ametoa jibu
kwa aibu yao kwani alipata mafunuo juu ya kile kilichofanyika siku hiyo
ya tarehe 22 Oktoba, 1844.
Kwa jinsi gani? Sikiliza. Alifundisha kwamba alioneshwa kulikuwa na
hekalu mbinguni mfano wa hekalu la duniani. Akadai hekalu hilo lilikuwa
na sehemu mbili: patakatifu na patakatifu pa patakatifu, yaani sawa na
lilivyokuwa hekalu la Kiyahudi zamani zile. Kumbe, kilichofanyika siku
hiyo ya tarehe 22 Oktoba, ni kwamba Kristo alitoka patakatifu na
kuingia patakatifu pa patakatifu. Akasema kwisha Yesu kuingia
patakatifu pa patakatifu atabaki humo mpaka siku atakapokuja duniani
mara ya pili.
Mintarafu swali, Yesu anafanya nini siku zote hizo? Akasema Yesu
anafanya ‘hukumu ya upelelezi’ kwa Kiingereza “investigative
judgement”. Kwa maelezo hayo mapya akadai kwamba kitu alichokuwa
amekosea Bw. William Miller kilikuwa tafsiri tu, kwa maana kwamba
utakaso uliofanywa tangu siku ile ya tarehe 22 Oktoba haukuwa wa dunia
hii, bali wa patakatifu pa patakatifu katika hekalu hilo la mbinguni.
Kwa namna hii, Bw. Hiram Edson akawa Mwadventista wa kwanza, hata kabla
hajawa Msabato, kuleta duniani maelezo ya kuwafariji wenzake kwa
kutorudi kwa Kristo siku ya tarehe 22 Oktoba 1844. Hivi basi, mchango
wake mkubwa kwa teolojia ya Wakristo ambao baadaye walijiita Wasabato ni
suala hilo la ‘hukumu ya upelelezi’. Kifupi, kwa maelezo hayo,
Wasabato wanafundisha kwamba Yesu Kristo, tangu 22, Oktoba 1844 yuko
huko mbinguni, katika patakatifu pa patakatifu akichunguza kwa kina
maisha ya Wakristo wote ambao majina yao yapo katika kitabu cha uzima wa
milele na kuamua nani anastahili kufutiwa dhambi zake zilizosamehewa
wakati alipoamini. Hivyo, kila mtu anayeonekana kurudi nyuma, naye
hakutubu dhambi zake zote, anafutwa jina lake kutoka katika kitabu cha
uzima na hivyo huko, mwishoni mwa historia, atakosa nafasi katika ufufuo
wa kwanza. Kinyume chake, kwa upande wao, wote ambao walitubu dhambi
zao, majina yao yanabaki kitabuni pasipo kufutwa, nao watafufuliwa
katika ufufuo wa kwanza.
Ndugu zangu, hadi hapa umeshagundua mafundisho ya uongo. Mbinguni hakuna
hekalu. Huo ndio ukweli wa kibiblia maana mwandishi wa kitabu cha
Ufunuo anatuandikia habari za maono yake matakatifu mintarafu Yerusalemu
ya mbinguni akisema “Nami sikuona hekalu ndani yake, kwa maana Bwana
Mungu Mwenyezi na Mwanakondoo, ndio hekalu lake” (Ufu 21:22). Sasa iweje
Bw. Hiram Edson amzungumzie Yesu anayetoka patakatifu kuingia
patakatifu pa patakatifu? Zaidi ya hayo, mafundisho ya hukumu ya
upelelezi ni uzushi kwa sababu ni matokeo dhahiri ya tafsiri potofu ya
neno la Mungu.
Haya tuachane naye, nasi twende tukamwangalie mtu wa tatu, ambaye ni Bw.
Joseph Bates. Kikazi, Bw. Joseph Bates alikuwa baharia. Bada ya
kustaafu kwake alihamia Fair Haven, katika jimboni Massachusetts, huko
huko Marekani. Kwa kweli, Bw. Joseph Bates ni mmoja wa viongozi
maarufu wa Waadventisti. Yeye aliposoma maandishi ya Thomas Prebble
kuhusu Sabato, alishawishiwa kuamini kwamba Sabato ya Wayahudi ilikuwa
siku halali kwa watu wote wa Mungu kuabudu. Basi, akaandika kijitabu
chake kilichoitwa, “The Seventh Day Sabbath, a Perpetual Sign””.
Baada ya kitabu hicho Bw. Joseph Bates aliendelea kuandika vijitabu
kuhusu Sabato. Hivi bwana huyu anakumbukwa sana na Wasabato kwa mchango
mkubwa katika kuirudisha Sabato ya Agano la Kale. Kwa kweli, ni yeye
aliyekuwa wa kwanza kutafsiri siku ya Jumapili kama siku ya alama ya
mnyama; na kwamba siku ya Sabato ndiyo muhuri wa Mungu kwa watu wake
walio waaminifu, yaani Waadventisti Wasabato 144,000 (rej. Ufu 7:4).
Kutokana na ushawishi wake huu, kuabudu siku ya Jumamosi, kukaanza
kupata nguvu nyingi, zilizoambatana na vitisho vya hukumu kali kwa
wanadamu wote wasioishika Sabato ya Agano la Kale. Kifupi, miongoni mwa
Waadventisti waliomfuata Bw. Joseph Bates kwa karibu, walikuwa ni James
na mkewe Ellen White. Kumbe, Bi Ellen White ndiye aliyeuendeleza
usabato, kwa motomoto zaidi kuliko watu wengine wote naye anaheshimiwa
na Wasabato kama nabii wao. Kwa hali hii ya mambo, yafaa tumalizie
historia hii fupi kwa kumwangalia mwanamama huyo hata kama ikiwa kwa
kifupi sana.
Ndugu zanguni, Bi Ellen G. White, anafahamika pia kwa jina la Bi Ellen
Gould Harmon. Ni kwamba kabla hajaolewa alikuwa anaitwa Ellen Gould
Harmon na baada ya kuolewa kwake na mpenziwe James White, aliyekuwa
mhubiri wa kibaptisti aliyekuwa muadventisti hapo tarehe 30 Agosti, 1846
akajulikana kama Bi Ellen Gould White.
Kwa kufupisha mambo, Bi Ellen Gould Harmon alizaliwa mwaka 1827 huko
Goharm, jimboni Maine, maili kumi hivi toka Portland. Akiwa mtoto mdogo
bado, wazazi wake walihamia Portland kwenyewe. Hapo mwanzoni, yeye
pamoja na familia yake walikuwa wafuasi wa dhehebu la Methodisti.
Kumbe, familia ya akina Ellen ilijiunga na uadventisti baada ya Bw.
William Miller kuhubiri mjini Portland katika mwaka wa 1840 na 1842.
Lakini kwa kuwa familia hiyo ilisadiki maneno ya Bw. William Miller,
kanisa lao la Methodisti liliitenga familia hiyo. Familia nzima
ilitengwa kwa sababu ya kuyapokea mafundisho ya Kiadventisti. Kwa
ujumla, mchango wa Bi Ellen White ulianza kama alivyodai mwenyewe kwamba
alipokea maono mengi nyakati mbalimbali, maono ambayo baadaye
yalimfanya ajulikane kama nabii wa Waadventisti. Inasemekana maono yake
ya kwanza yalimjia mwezi Desemba, 1844, yaani si muda mrefu sana baada
ya watu kukatishwa tamaa na kutokurudi kwa Yesu Kristo.
Bi Ellen White aliingia ulingoni akidai kuliona kundi la Waadventisti
wakisafiri katika njia yenye mwanga wa utukufu, huku wakiongozwa ya Yesu
hadi walipoufikia mji wa Mungu. Bi Ellen akadai kwamba baada ya
kuonywa katika maono ya pili asikae kimya juu ya yale aliyooneshwa,
alilazimika kutangaza na kuyahubiri maono yake wazi mahali pengi.
Kuanzia hapo, Waadventisti wa Portland na Maine wakaanza kumtambua Bi
Ellen White kama nabii wao na kusisitiza kwamba Roho Mtakatifu alikuwa
juu yake na kwamba ilikuwa ni lazima unabii wake ufuatwe na Waadventisti
wote popote pale walipokuwa.
Kama jambo hilo halitoshi, mwezi Februari 1845, Bi Ellen White alidai
kupata maono yaliyothibitisha maono ya Bw. Hiram Edson mintarafu kitu
kilichotokea hapo tarehe 22 Oktoba 1844, yaani kwamba Yesu alikuwa
ameingia patakatifu pa patakatifu katika hekalu la mbinguni. Zaidi ya
hapo alidai kwamba miaka miwili baadaye, alipata maono mengine ambapo
alidai kwamba alichukuliwa na kupelekwa katika hekalu la mbinguni.
Alisema kwisha kufikishwa mbinguni, kwanza kabisa aliingizwa patakatifu
na baadaye patakatifu pa patakatifu ambapo aliona amri kumi zikiwa ndani
ya sanduku la agano.
Tukiwa tayari kusonga mbele, tunaweza kujiuliza swali dogo la
kuchangamsha bongo zetu. Hebu tujiulize, hivi, humo patakatifu pa
patakatifu Bi Ellen White alikumta Yesu akifanya hukumu ya kipelelezi?
Tukikijibu wenyewe, ndugu yangu, jibu ni kwamba suala hilo haligusiwi
ilivyotarajiwa. Basi, acha tuzidi kumfuatilia katika madai ya maono
yake. Bi Ellen White anasema alipong’aza macho yake kwenye sanduku la
agano la humo hekaluni, aliona amri ya sabato ikiwa imezungukwa na
utukufu na hapo eti akang’amua kwamba amri ya kushika Sabato ilikuwa
kubwa zaidi.
Ndugu yangu, hadi hapo, tukimpima Bi Ellen White kibiblia, anaongeza
uongo mwingine mbaya. Uongo wa kwanza ni ule wa kuliona hekalu mbinguni
wakati mbinguni, Maandiko Matakatifu yanasema hakuna hekalu (rejea tena
Ufu 21:22). Uongo wa pili ni huu wa kuhesabu amri ya kushika Sabato kama
amri kuu kwani amri ya kwanza na kubwa kupita zote, kadiri ya Yesu
Kristo mwenyewe, ni ile ya kumpenda Mungu huku ikifuatiwa na ya pili
yake, yaani ile ya kumpenda jirani kama tunavyojipenda sisi wenyewe
(rej. Mt 22:34-40).
Lakini basi, ndugu zanguni, maono aliyopata Bi Ellen White yakawa, kwake
na hatimaye kwa Wasabato wote, kurunzi la kutafsiria Maandiko
Matakatifu yote. Ndipo, kwa njia ya vitabu vingi alivyoandika,
mafundisho ya Kiadventisti yakasambazwa. Hivyo, tangu wakati huo,
Waadventisti Wasabato, huitafrisi Biblia kwa vipimo vya maono ya White,
na siyo kuyatafsiri maono ya Bi White kwa vipimo vya Biblia. Je, si
ajabu ya mwaka hiyo? Basi, ndugu yangu, fumbuka macho ya roho yako,
uyaone na kuyapima mambo haya sawa sawa pasipo kiwi cha macho! Usitoe
hoja ya uongo!
Basi, kwa kukata maneno, Bi Ellen White ndiye aliyewapandikiza chuki
Wasabato dhidi ya Kanisa Katoliki. Amelifanya hilo kwa kupitia vitabu
vyake vingi vyenye chuki ambavyo vinasomwa na kutumiwa na Wasabato
karibu kama misahafu. Kwa taarifa yako, baadhi ya vitabu hivyo ni, kama
vile, Vita Kuu, Afya na Raha na Siri ya Ushindaji. Ndani ya vitabu hivi
Kanisa Katoliki linatukanwa na kushtakiwa kuhusika na maovu mengi. Kwa
mfano, wanashtakiwa kuondoa amri ya kuabudu Sabato. Wanashtakiwa kuabudu
sanamu. Wanashtakiwa kumwabudu Bikira Maria. Wanashtakiwa kumwabudu
Baba Mtakatifu (Papa) ambaye eti ndiye mnyama anayetajwa katika kitabu
cha Ufu 13:1-18. Wanashtakiwa kufundisha mambo ya kidunia badala ya
ufalme wa Mungu. Wanashtakiwa kuongeza vitabu kwenye Biblia na mengine
mengi ya namna hiyo yanayosikika mitaani na katika mahubiri yao. Mungu
utuhurumie!
Ndugu zanguni, kwa ujumla, kanisa la Wasabato likawa muungano wa vikundi
vitatu vya Waadventisti: mosi, kikundi cha Bw. Hiram Edson,
kilichosisitiza zaidi mafundisho ya huduma ya Yesu patakatifu pa
patakatifu mbinguni; pili, kikundi cha Bw. Joseph Bates, kilichosisitiza
zaidi kufuata Sabato ya Agano la Kale; na tatu kikundi cha Bi Ellen G.
White, kilichomwona Bi Ellen kama nabii ambaye unabii wake ni lazima
ufuatwe na Waadventisti wote duniani.
Vikundi hivi vilipoungana Waadventisti Wasabato wakapata kujichipusha
duniani. Mwaka 1860, jina la Seventh Day Adventist lilichaguliwa nalo
likawa jina rasmi la Waadventisti hao. Kishapo, mwezi Mei, 1863, katika
mkutano mkuu wa kwanza, uliokuwa na wawakilishi kutoka majimbo yote
Marekani, isipokuwa jimbo la Vermont, kanisa la Wasabato likazaliwa
rasmi duniani.
Basi, tukipiga muhtasari wa historia ya Wasabato, tuseme tu kwamba
mwasisi wa Waadventisti Bw. William Miller alikuwa ni Mbaptisti lakini
mwanzilishi wa Wasabato yaani Bi Ellen G. White alikuwa ni Mmethodisti.
Hata hivyo, kwa kuhitimisha sehemu hii, yafaa sote tukumbuke kwamba
makanisa hayo mawili, yaani Wabaptisti na Wamethodisti si chochote
isipokuwa matawi ya kanisa la Anglikana, kanisa lililoanzishwa na Mfalme
Henry VIII wa Uingereza hapo mwaka 1534 baada ya kukasirika kukataliwa
na Kanisa Katoliki kumwacha mkewe aliyeshindwa kumzalia mtoto wa kiume.
WASABATO MITUME WA MATUSI DHIDI YA KANISA LA KWELI
Msomaji wangu bila shaka umeiona historia ya aibu na ya zigzaga ya
Wasabato. Wasabato wenyewe huificha sana historia hiyo, hasa kwa wafuasi
wao wanaoingia katika kanisa lao putaputa. Hufichwa ukweli kama paka
wanaosafirishwa katika gunia. Kwa nini? Wanafichwa ili wasiujue ukweli
walikotokea wasije wakajua kwamba wamekosea njia kiimani.
Kifupi, madai yao kwamba Baba Mtakatifu, Kanisa Katoliki au Mfalme
Constantino ndio waliobadili Sabato kwenda Jumapili ni mojawapo ya
matusi ya Wasabato. Wenyewe wanahubiri hayo kwa jasho jingi kabisa
wakati ni kusepetuka kwa uelewa na fichio la aibu yao katika kushindwa
kwao katika utabiri wa tarehe ya mwisho wa dunia, tarehe ambayo Yesu
Kristo, Bwana wetu na Maandiko yanatuambia kwamba haitabiri kabisa. Kwa
maneno mengine, ndiyo matawi ya chuki iliyokosewa mwelekeo na uongo wa
binadamu dhidi ya wanadamu wenzake.
Tusisahau, kutokana kushindwa hoja na aibu kubwa waliyoipata mbele ya
ukweli unaoshikiliwa na kufundishwa na Baba Mtakatifu na Kanisa
Katoliki, Wasabato na makanisa mengine wameamua kutumia mbinu ya
kujikosha kwa matusi makali. Wameamua kujitwika utume wa matusi wakati
mwingine hata matusi ya nguoni. Kwa vyovyote, Wakatoliki hawana namna
rahisi ya kukabiliana na madai hayo ya kimatusi. Usistaajabu haya
kufanyika hivi. Kwa mtindo wa vijijini, ukishindwa hoja kwa mtu fulani
unaanza kumtukania wazazi wake, nyumba yao na kadhalika.
KUITUNZA SABATO NI KUSHEREKEA MKESHA WA SIKU YA UHURU
Kuitunza Sabato mbele ya Dominika ingelingana na kusherekea mkesha wa
siku ya uhuru badala ya siku ya uhuru yenyewe. Taifa litakalofanya hivyo
litachekesha na labda litakuwa la watu punguani. Aidha mtu kupita huko
na huko kuwahimiza watu washerehekee mkesha wa uhuru badala ya siku ya
uhuru wenyewe ingelikuwa sawa na kucheza Ze Comedy.
Nani amegeuka mkondo wa mambo hata kugeukia tena Sabato wakati Wakristo
wa kwanza kwa kumwelewa vyema Yesu Kristo walishaitupilia mbali? Jibu
ni wazi. Ni mmoja wa waanzilishi wa dhehebu la Wasabato, yule mama
anayejulikana kama nabii. Kwa taarifa yako waanzilishi wa dhehebu la
Wasabato ni akina Hiram Edson, Joseph Bates, E.G. Harmon na Hellen
White. Katika hawa aliyekuja na moto wa kurudisha Sabato ni huyo mama
ambaye alikuwa mke wa E.G. Harmon. Mwanamke huyo anaheshimiwa na
Wasabato kama nabii na vitabu vyake , kama vile Vita Kuu, Afya na Raha
na Ushindaji, vinasomwa na Wasabato karibu kama misahafu.
WASABATO WASIMNYANYASE YEYOTE
Maono ya uwongo ya Bi Hellen yasiwe sababu ya kuwanyanyasia Wakristo
wasio Wasabato. Wala si siri, makanisa yanayofuata mabadiliko
yaliyoletwa na Mungu mwenyewe kutoka Sabato kwenda Dominika
yananyanyaswa kweli kweli na kauli za Wasabato wanaomfuasa Bi Hellen
White. Lakini, hivi unabii wa mama huyo ni wa kweli hata tutishik
e nao?
Hapana, wala si wa kweli. Unabii wa mama huyu lazima tuukatae. Kwa nini
tuukatae?
TUHIMIZANE TUMKATAE BI HELLEN NA MAONO YAKE
Ni kwa sababu kuna sababu tatu zinazotuhalalisha tumkatae Bi Hellen
White kama nabii. Mosi, kitabu cha Ufunuo kinaonesha kufungwa kwa
unabii, yaani kwamba baada ya mambo yaliyoandikwa humo kusingekuwa na
ufunuo wowote wa pekee. Ukamilifu wa ufunuo ulitokea katika ujio wa Yesu
Kristo. Alichosema yeye ndicho kitu cha kilele. Sasa Bi Hellen
anakujaje na mapya kumpikua Yesu Kristo? Tunasoma, “Mungu ambaye alisema
zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia
nyingi, mwisho wa siku hizi, amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka
kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni
mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akavichukua vyote kwa
amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa
kuume wa Ukuu huko juu, amefanyika bora kupita malaika kwa kadiri jina
alilorithi liliyo tukufu kuliko lao” (Ebr 4:1-4).
Si hivyo tu hata mintarafu ufunuo wa zamani mihuri yake imevunjwa na
Yesu Kristo mwenyewe, sasa unabii wa Hellen White unaanzia wapi?
Tunasoma, “Kisha nikaona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu
ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa
muhuri saba. Nikaona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa sauti kuu, Ni
nani astahiliye kukifungua kitabu na kuzivunja muhuri zake. Wala
hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya nchi, wala chini ya nchi,
aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Nami nikalia sana
kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kikifungua hicho kitabu, wala
kukitazama. Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama Simba
aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua
kile kitabu, na zile muhuri zake saba.
Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi wale wenye uhai wanne, na
katikati ya wale wazee, Mwanakondoo amesimama, alikuwa kana kwamba
amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za
Mungu zilizotumwa katika dunia yote. Akaja , akakitwaa kile kitabu
katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi.
Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee
ishirini na wanne wakaanguka mbele ya Mwanakondoo, kila mmoja wao ana
kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya
wakatakatifu, nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaaa
hicho kitabu na kizifungua muhuri zake, kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia
Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa,
ukawafanya kuwa ufalme wa makuhani, kwa Mungu wetu, nao wanamiliki juu
ya nchi” (Ufu 5:1-10).
Mintarafu kusasambua ovyo ufunuo wa Mungu, mwandishi wa kitabu cha
Ufunuo alishakatazwa, sasa Bi Hellen White anapata wapi nguvu ya kuja na
ufunuo mpya? Kuhusu marufuku hiyo tunasoma, “Hata ngurumo saba
zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti
kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo
ngurumo saba, usiyaandike” (Ufu 10:4). Hatimaye, maneno ya ufunuo
yaliachwa wazi bila muhuri kwa vile yalivyokuwa njiani kutimia. Juu ya
jambo hili, tunasoma hivi: “Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii
wa kitabu hiki kwa maana wakati huo umekaribia” (Ufu 22:10). Sasa Bi
Hellen White anaongezaje maneno ya ufunuo mpya?
Pili, tuukatae unabii wake kwa vile zile anazoziita njozi, kama elfu
mbili hivi, ni batili kwani zinaonesha jinsi alivyojaa chuki kwa Baba
Mtakatifu na Kanisa Katoliki nasi tunajua kwamba si kazi ya Mungu Roho
Mtakatifu kumjaza mtu chuki kali hivyo dhidi ya mwanadamu mwingine. Kazi
hiyo hufanywa na Shetani nayo huonesha kwamba moyo wa mtu umejaa uovu
kwani kilichomjaa mtu moyoni ndicho kimtokacho. Tunasoma, “Kwa maana
hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda
mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana katika
miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. Mtu
mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu
katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu,
kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake” (rej. Lk 6:43-45). Hakika
chuki dhidi ya Baba Mtakatifu na Kanisa Katoliki inatoka katika moyo
uliofurika uovu. Na kwa jinsi hii maono yake hayawezi kutoka kwa Roho
Mtakatifu.
Tatu, tuukatae unabii wake kwa sababu mafundisho yake yanaonesha kwamba
haijui Biblia. Hoja hii ya tatu nimeshaishuhudia tayari. Nimesema ameota
ndoto akaona huko mbinguni kuna hekalu wakati Maandiko yanatakaa jambo
kama hilo (rej. tena Ufu 22:22-24). Kisha nimeshashuhudia kwamba kule
kusisitiza kwamba Sabato ndiyo amri kuu kunapingana na kile
alichotuambia Bwana wetu Yesu Kristo aliyesisitiza kwamba amri kuu ni
upendo (rej. tena Mt 22: 34-40). Naomba itoshe nilivyokuambia nawe
uyapuuze maono ya Mrs. Harmon tunayemchambua hapa.
MAJIBU KWA MASHTAKA YA ZIADA
Nikiendelea kidogo, naomba ruksa nijibu mashtaka mawili sambamba
wanayotoa Wasabato dhidi ya Wakatoliki: mosi kwamba ndio mnyama yule
Shetani aliyejipa jukumu la kubadili majira na pili kwamba Kanisa
lenyewe linakiri kufanya hivyo katika Katekisimu zake na katika vitabu
vya waandishi fulani fulani wa Kanisa Katoliki.
Mintarafu hoja ya kwanza ni hivi mnyama ni Bi Hellen White aliyethubutu
kumpinga Mungu. Mungu aliibadili siku ya Sabato yeye akijipa jukumu la
kuirudisha kwa maelezo ya maono yake batili kabisa. Tumeshaonesha jinsi
yalivyo batili kwa kadiri ya mizani na darubini ya Maandiko Matakatifu.
Halafu mintarafu hoja ya pili ni hivi Kanisa linajihusisha na mabadiliko
hayo si kama ‘mtendaji’ kwani hakuna mkutano mkuu (mtaguso) wowote wa
Kanisa Katoliki uliojadili hoja ya Sabato na kuamua kuibadili kwenda
Dominika ila kwamba Mungu aliibadilisha Sabato pale alipoanzisha enzi ya
Israeli mpya yaani Kanisa. Natumaini wasomaji wangu hoja hii si ya
kitaalamu mno kiasi cha kutonielewa ninachosema. Ninasema hivi Kanisa
linajisikia kuhusika na ubadilishaji wa Sabato kwenda Dominika kwa vile
Mungu aliufanya kuanzia pale lilipoanza kuwako nalo kwa mamlaka
uliyopata kutoka kwa Mungu ikayasimamia na kuyaendeleza mabadiliko hayo.
MALUMBANO SASA YAKOME
Naomba hadi hapa shtaka la kwamba Kanisa Katoliki limebadili majira,
yaani kutoka Sabato kwenda Dominika (Jumapili), lififie kabisa. Si
unajua kwamba hoja yenyewe hukokotolewa kutoka Dan 7:25 mahali
palipoandikwa, “Naye atanena maneno kinyume chake Aliye Juu, naye
atawadhoofisha watakatifu wake Aliye Juu, naye ataazimu kubadili majira
na sheria”.
Kama unavyoisoma sasa, hoja hii haitaji Kanisa Katoliki bali kwa kinyume
chake inawataja Wasabato wenyewe. Ndugu zangu Wasabato haliwafahamu
jambo hili kwa sababu ndivyo ilivyo, “Jambo usilolifahamu ni sawa na
usiku wa giza.” Kwa vipi? Ni hivi, kama Yesu kwa maneno na matendo yake
alisema Sabato si lolote na wala si chochote “maana mtu hakuuumbwa kwa
ajili ya Sabato”, mtu anayesema Sabato ndiyo yote katika yote ndiye
anayeazimu kubadili majira na sheria. Na moja kwa moja mtu huyo anakuwa
ndiye mpinga Kristo kwa sababu anapingana na kauli ya Kristo mwenyewe.
Hilo ndilo alilofanya nabii Hellen na kuwasadikisha maelfu ya watu kauli
yake kengeufu.
Aidha, kama Yesu alisema kwamba amri kuu ni upendo (rej. Mt 22:37) na
akataka iwatambulishe wafuasi wake popote watakapokuwa (rej. Yn 13:35),
anapokuja nabii Hellen na kusema eti amri kuu ni Sabato ni upinga Kristo
wa wazi wazi na kumfuasa mpinga Kristo kama huyo ni kuwa wapinga Kristo
wadogo wadogo nyuma ya huyo mkubwa. Ona ushuhuda wa Maandiko
Matakatifu. Bila shaka, hata wewe unakumbuka Yesu aliulizwa swali juu ya
amri ya kwanza na kuu naye akatoa jibu mwafaka hata wasomi na walimu wa
enzi zake wakamvulia kofia.
Tunasoma, “Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale
Masadukayo, walifanya shauri pamoja. Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza,
akimjaribu: Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia,
Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na
kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya
pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako.
Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii” na wakati
akiwaaga wanafunzi wake jioni iliyotangulia kifo chake alisema na
kuagiza, “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi
wangu mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yn 13:35). Sasa Nabii Hellen
anathubutuje kusema kinyume cha maneno hayo ya Kristo ambaye tumepewa
tumsikilize? Kama huo si upinga Kristo wenyewe ni nini tena? Hukumu
mwenyewe; wewe ni mtu mzima. Hivi wewe na mimi na sisi sote hatukumbuki
maneno ya Maandiko Matakatifu, “Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu,
msikieni yeye” (Mk 9:7)? Na kwa upande wetu, kwa nini, tunamsikiliza
binadamu tena? “Tumechanganyikiwa” au “tumerogwa”?
UCHAMBUZI WA KISAIKOLOJIA WA WALIOHUSIKA NA HISTORIA HII YA AIBU
Jina Ugonjwa Tunaoweza Kumtuhumu Upinga Kristo Wake Ulipo
William Miller Megalomania – kujidai kujua kuliko Yesu Kristo kwa
kujaribu kuitaja tarehe ya mwisho wa dunia Kukokotoa tarehe ya mwisho wa
dunia kinyume na Mk 13:32.
Samwel Snow Megalomania – kujidai kujua kuliko Yesu Kristo kwa kujaribu
kuitaja tarehe ya mwisho wa dunia Kukokotoa tarehe ya mwisho wa dunia
kinyume na Mk 13:32.
Hiram Edson Schizophrenia – kuona hekalu ambalo halipo mbinguni na kudai
mwisho wa ulimwengu umeshatokea. Kuota ndoto ya kuliona hekalu
mbinguni ni kinyume cha Ufu 21:22-23.
Joseph Bates Megalomania – kujidai kujua kuliko Yesu Kristo kwa kuunga
mkono uongo kwamba mwisho wa ulimwengu umeshatokea. Kuidharau Jumapili,
siku aliyoitumia Bwana kufanya mambo yote makubwa.
Hellen White Schizophrenia – kuona hekalu ambalo halipo Kuota ndoto ya
kuliona hekalu mbinguni ni kinyume cha Ufu 21:22-23 na kudai Sabato
ndiyo amri kuu kinyume na Mt 22:34-40.
MASWALI NA MASHTAKA 12 MAARUFU YA WASABATO KWA WAKATOLIKI
i. Sabato ndiyo siku ya kuabudu iliyoamriwa. Wakatoliki ndio walioifuta Sabato na kuweka Jumapili.
ii. Wakatoliki wanafuata mapokeo ya binadamu, hawajui na wala hawafuati Maandiko Matakatifu.
iii. Baba Mtakatifu ndiye mnyama yule anayewakilishwa na namba 666. Namba hiyo imeandikwa kwenye kofia na mavazi yake.
iv. Wakatoliki wameifuta amri ya pili ya Mungu. Wamefanya hivyo ili waabudu sanamu.
v. Wakatoliki wanaabudu sanamu. Tazama sanamu makanisani mwao!
vi. Kwa nini Wakatoliki wanakunywa pombe wakati imekatazwa kwenye Biblia?
vii. Wakatoliki wanamwabudu Bikira Maria. Kwa nini wanamfanyia heshima kubwa isivyostahili?
viii. Je, Bikira Maria alikuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu Kristo?
ix. Kanisa Katoliki linafanya makosa kuwatangaza wanadamu kuwa
watakatifu. Mwanadamu ana uwezo gani wa kumtangaza mtu mwingine kuwa
mtakatifu?
x. Wakatoliki wana sakramenti saba. Wana makosa kwa sababu hazijaandikwa kwenye Biblia.
xi. Kuungama ni kwa Mungu moja kwa moja. Kuna uhalali gani kwenda kuungama kwa mapadri wakati wenyewe wana dhambi?
xii. Wakatoliki wana hatia kubwa kwa sababu hawataki kuokoka. Kwa nini Wakatoliki ni wabishi hivyo?
Ndugu yangu Mkatoliki
jaribu kuwa na majibu ya maswali haya, hutahangaishwa na Wasabato wowote
katika imani yako na maisha yako yote. Kumbe, usipokuwa nayo siku zote
utayumbishwa kama wimbi la baharini wakati ulipaswa kutulia tuli kama
maji kwenye mtungi.
HATIMA: TUSIHANGAISHANE TENA JUU YA SABATO KWANI ILIKUWA KIVULI TU
Kwa sasa Wakatoliki wote tuhitimisha fikra zetu kwa nukuu hii: “Basi,
mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya
sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO; mambo hayo ni KIVULI cha mambo
yajayo; bali mwili ni wa Kristo” (Kol 2:16-17).
Ndugu zanguni, kama inavyosomeka katika aya hizi, Sabato ilikuwa kivuli
na kivuli hakishonewi suti. Sisi ni watu wazima tuachane na Sabato. Nina
hakika tutaadhibiwa na Mungu kwa hatia ya kukipa hadhi kitu kisicho na
uzito wa kimani.
Imeandikwa na
Pd. Titus Amigu (2016)