Saturday, November 19, 2011

Mwenyekiti wa CCM Awasili Dodoma Kwa Vikao Vya Chama






Na Mwandishi Maalum, Dodoma, Jumamosi Nov. 19, 2011



Mwenyekiti wa CCM Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete Jumamosi (Nov 19) jioni amewasili mjini Dodoma tayari kwa vikao muhimu vya chama hicho tawala vitavyofanyika kwa siku nne katika ukumbi wa Makao Makuu ya CCM maarufu kama White House.


Katika Uwanja wa ndege wa Dodoma Dkt Kikwete amepokewa na viongozi pamoja na wana CCM wengi wakiongozwa na Makamu wa Rais Dkt Mohamed Ghalib Bilal na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye ni Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM.

Baada ya mapumziko mafupi katika Ikulu ndogo ya Dodoma Dkt Kikwete alielekea ukumbi wa St. Gaspers ambako aliongea na wabunge wa CCM na kupata nao chakula cha usiku.

Katika hotuba yake, Dkt Kikwete aliwapa changamoto wabunge hao wa CCM waende kwa wapiga kura wao na kuwaelemisha kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya uliopitishwa Jumamosi Bungeni Dodoma.

Dkt Kikwete aliwasisistizia wabunge hao umuhimu wa kupeleka elimu hiyo ya mchakato wa kupata katiba mpya kwani hivi karibuni kumekuwepo na upotoshaji mkubwa wa nini kinachoendelea, na kusema kuwa wakiwa wabunge wa chama tawala ni wajibu wao kuelimisha umma kwamba kanuni na sheria zote zimefuatwa katika kupitisha muswada huo ambao umesomwa kwa mara ya pili, baada ya kusomwa mara ya kwanza kwa mujibu wa sheria.

Rais Kikwete aliwakumbusha wabunge hao kwamba mchakato huo si jambo geni na kwamba ndio uliofuatwa na Marais wote toka wa awamu ya Kwanza hadi ya tatu, akisisitiza kwamba ni muhimu wanancho wote wakaelewa hilo, ikizingatiwa kwamba kuna baadhi ya watu wachache wanaotaka kupotosha umma kwamba hatua hiyo ni batili wakati sio kweli, ikizingatiwa kwamba kila lililo katika katiba ya sasa limezingatiwa.

Pia aliwasihi Watanzania kujitokeza kutoa maoni yao ya ni katiba gani wanayoitaka pindi muda wa kufanya hivyo utapowadia, na wasikubali kughiribiwa na wachache waliopania kupindisha ukweli.

Kwa mujibu wa ratiba leo Jumapili kutakuwa na Kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili ukumbi wa White House kitachofanyika kutwa nzima, kitachofuatiwa na kikao cha Kamati kuu ya CCM Jumatatu na Jumanne. Halmashauri kuu ya CCM itakutana kuanzia Jumatano hadi Ijumaa.

1 comment:

Anonymous said...

Hao wabunge walikuwa na njaa kweli kweli. Wamemaliza buffet yote!