Sunday, January 15, 2012

Utaratibu wa Mazishi wa Marehemu Mh. Regia Mtema

 Sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imefanya kikao cha dharura leo, Januari 15, 2012, chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu, Dkt. Wilbrod Slaa, pamoja na mambo mengine, kupanga utaratibu wa chama na viongozi wake wakuu, wakiongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Mheshimiwa Freeman Mbowe kuendelea kushiriki kikamilifu kwenye maombolezo, heshima za mwisho na hatimaye maziko yaliyopangwa kufanyika Ifakara.

Wakati huo huo, Kamati ya Uogozi ya Wabunge wa CHADEMA, imefanya kikao cha dharura, kufuatia kifo cha Mbunge wa Viti Maalum, Regia Estelatus Mtema, Pamoja na mambo mengine kamati imezingatia, uzito msiba uliotokea na kupitisha azimio kwamba wabunge wote wa CHADEMA watashiriki katika kutoa heshima ya mwisho kwa marehemu Januari 17, 2012.
Aidha, wabunge wote watasindikiza mwili wa marehemu wa marehemu hadi Ifakara na kushiriki mazito yaliyopangwa kufanyika Januari 18, 2012. Viongozi wakuu wa chama, wabunge wa CHADEMA, hivi sasa wanaendelea kujumuika nyumbani kwa Baba wa Marehemu Regia Mtema, eneo la Tabata Chang'ombe, pamoja na familia, viongozi wakuu wa serikali na bunge katika kuwafariji wafiwa.

Pia pamoja na heshima za mwisho kibunge na kichama kutolewa Jumanne, Januari 17, 2012, familia imeandaa ibada Januari 16, 2012, katika Kanisa la Parokia ya Segerea, kuanzia saa 9, alasiri, ambapo mwili utaagwa na ndugu, jamaa na marafiki.

Taarifa zaidi zitaendelea kutolewa, kutokana na mashauriano kati ya familia, chama na Ofisi ya Bunge.


Imetolewa, Januari 15, 2012
John Mnyika
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

No comments: