Wednesday, August 15, 2007

Rais Kikwete azungumzia Muafaka kati ya CUF na CCM


TAARIFA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KUHUSU MAZUNGUMZO YA MUAFAKA KATI YA CUF NA CCM

Tarehe 7 Agosti, 2007, Mwenyekiti wa Chama cha Civic United Front (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alitoa tamko la kuelezea kukwama kwa mazungumzo ya muafaka kati ya Chama chake na Chama cha Mapinduzi (CCM). Katika tamko hilo, Profesa Lipumba alielezea nia yake na ya Chama chake ya kujiondoa katika mazungumzo hayo ifikapo tarehe 15 Agosti 2007.

Napenda kukumbusha kwamba chimbuko la mazungumzo yanayoendelea sasa ni ahadi niliyoitoa kwa Watanzania wakati nilipohutubia Bunge tarehe 30 Desemba, 2005. Niliahidi kuwa nitakuwa tayari kuchukua hatua za kutafuta ufumbuzi wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Kwa ajili hiyo, nilielezea nia yangu ya kusaidia kuanzisha na kuwezesha mjadala juu ya mustakabali wa kisiasa Zanzibar.

Ahadi hiyo niliitoa kwa dhati ya moyo wangu nikiamini kwamba hakuna tofauti zozote za kisiasa na kijamii katika nchi yetu au baina yetu au katika jamii zetu ambazo haziwezi kumalizwa kwa njia ya mazungumzo. Imani hiyo bado ninayo leo na nitaendelea kuwa nayo daima.Ilichukua muda kwa mazungumzo baina ya CCM na CUF kuanza. Hii ilisababishwa na haja ya kufanya mashauriano mapana baina na miongoni mwa wadau wa pande zote husika ndani ya Chama cha Mapinduzi na wenzetu wa CUF.

Mashauriano haya yalichukua muda kidogo zaidi ndani ya CCM kwa sababu utamaduni na mfumo wetu wa demokrasia ndani ya Chama cha Mapinduzi unatuwajibisha kuwa na mashauriano mapana na ya kina katika ngazi mbalimbali za uongozi na vikao vya Chama.

Nafurahi kuwa kazi hiyo ilikamilika vizuri na tukafikia maelewano ya dhati kuwa CCM ifanye mazungumzo na CUF.Baada ya hapo, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ilimuagiza Katibu Mkuu wa CCM kuwasiliana na Katibu Mkuu wa CUF na kumuomba akubali kushiriki katika mazungumzo baina ya vyama vyetu. Tulifarijika sana kwamba baada ya maombi hayo ya CCM wenzetu wa CUF walikubali kukaa pamoja nasi katika meza ya mazungumzo.Tarehe 17 Januari, 2007, Makatibu Wakuu wa vyama vya CUF na CCM wakakutana na mchakato wa mazungumzo ukaanza. Baada ya kikao hicho cha mwanzo, kila upande ukaunda timu yake ya kushiriki katika mazungumzo hayo.

Tarehe 01 Februari, 2007 Kamati yetu ya Pamoja ilifanya mkutano wake wa kwanza ambapo walikubaliana kuwa jambo la mwanzo la kufanya ni kwa kila upande kutengeneza mapendekezo yake ya mambo unayotaka yazungumzwe, yaani yawe kwenye Ajenda ya Mazungumzo. Baada ya hapo yalifanyika majadiliano mazuri na katika mazingira ya kidugu, ajenda ya pamoja ya mazungumzo ikatengenezwa.
Ajenda hiyo ilikuwa na mambo matano makubwa kama ifuatavyo:
1. Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30, 2005 na taathira zake;
2. Usawa na haki katika kuendesha siasa;
3. Masuala ya utawala ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
4. Njia za kuimarisha mazingira ya maelewano ya kisiasa na uendeshaji wa uchaguzi huru na wa haki Zanzibar; na,
5. Utaratibu wa kutekeleza Programu ya Utekelezaji wa Makubaliano yatakayofikiwa katika mazungumzo haya.

Tangu mazungumzo haya yaanze mwezi Januari mwaka huu, Kamati yetu ya Pamoja imefanya vikao 12 na wametumia siku 43 za mazungumzo. Pia Makatibu Wakuu nao wamekutana mara mbili kutafuta ufumbuzi wa yale mambo yaliyohitaji kufanywa nao. Tulikubaliana kuwa mazungumzo ya msingi yatafanywa na Kamati lakini pale ambapo Kamati itakwama Makatibu Wakuu waingilie kati kutoa mwongozo. Ukweli kwamba wamekutana mara mbili tu ni dalili kwamba mambo yanakwenda vizuri.

Hatua kubwa imefikiwa na mafanikio ya kuridhisha yamepatikana. Kuna mambo kadhaa makubwa na ya msingi ambayo pande hizi mbili zimekwishakubaliana. Katika ajenda tano za mazungumzo, ajenda tatu, yaani ajenda ya Usawa na Haki katika Kuendesha Siasa, Masuala ya Utawala ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na Njia za Kuimarisha Mazingira ya Maelewano ya Kisiasa na Uendeshaji wa Uchaguzi Huru na wa Haki Zanzibar, zimejadiliwa na pande zote mbili zimefikia maelewano mazuri.Kwa upande wa ajenda ya kwanza inayohusu Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30, 2005 na Taathira Zake, mazungumzo yamefanyika na maelewano yamepatikana kwa mambo kadhaa.

Yapo mambo mawili matatu ambayo bado maelewano hayajafikiwa. Hatuna budi tuendelee kuyazungumza mpaka tutakapopata maelewano ya pamoja. Jambo moja kubwa ambalo wawakilishi wa vyama vyetu bado wanaendelea kujadiliana na ambalo bado halijakamilika ni lile linalohusu namna ya kutengeneza mazingira yatakayowezesha vyama vya siasa Zanzibar, hususan CUF na CCM, kuishi na kuendesha shughuli zao kwa pamoja katika hali ya maelewano na mazingira ya amani na utulivu.

Mazungumzo kuhusu kipengele hiki yamechukua muda na muafaka bado haujafikiwa. Kwa maoni yangu imekuwa hivyo kwa sababu ya umuhimu wake na umakini unaotakiwa katika uchambuzi wa hoja na kufikia uamuzi. Katika mazungumzo kuna mambo rahisi yanayochukua muda mfupi kujadiliwa na kufikiwa makubaliano na kuna mambo magumu yanayochukua muda mrefu. Huu ndiyo uzoefu wa vyama vyetu katika mazungumzo tuliyofanya huko nyuma na hata kwa mazungumzo haya.

Kwa sababu hiyo, sisi wa upande wa CCM, hatudhani kama tumefikia mahali pa kusema kuwa mambo yameshindikana na hivyo mazungumzo yavunjike. Hatujafikia hatua hiyo hata kidogo. Ni maoni yangu na ya Chama cha Mapinduzi kuwa tuendelee kuzungumza na kila upande uboreshe hoja zake za kuushawishi upande mwingine. Tupo kwenye mazungumzo kwa ajili hiyo. Tupo kufanya hivyo. Naamini kwamba, kama ambavyo tumepata maelewano katika maeneo mengine ambayo yalikuwa magumu, hata kwa haya yaliyobakia hatimaye tutaafikiana.

Wahenga walisema: “Penye nia pana njia”. Maadam sote nia tunayo, jawabu muafaka kwetu sote na kwa nchi yetu tutalipata.Nawasihi wenzetu wa CUF wasijiondoe kwenye mazungumzo haya na badala yake tuendelee kuzungumza. Tunazungumza kwa sababu tuna tatizo tunalolitafutia ufumbuzi. Kuacha kuzungumza si jawabu kwani tutakuwa tunaacha kulipatia ufumbuzi tatizo linalotusibu sote.

Tutarudi kule tulikokuwa, yaani kwenye uhasama, shutuma zisizoisha, kubaguana, kutozikana na hata kutosalimiana au kuchekeana. Tutaendelea na utamaduni mbaya wa kuzifanya tofauti zetu za kisiasa kuwa ni chanzo cha uadui, chuki na hivyo kuhatarisha amani, utulivu na umoja wa taifa letu na watu wake.Ni kweli, mazungumzo ni lazima yawe na ukomo. Na sisi wote tungependa yafikie mwisho wake mapema inavyowezekana.
Lakini, ukomo wa mazungumzo ni lazima utokane na ridhaa ya pamoja ya pande zote na hasa kwamba ajenda zote zimepata nafasi ya kujadiliwa kwa kina na maelewano yamefikiwa. Ukomo wa mazungumzo usiotokana na hayo ni kuahirisha tatizo litakalokuja kujitokeza na kutudhuru wote siku za usoni. Shabaha yetu katika mazungumzo haya ni kupata ufumbuzi wa kudumu na endelevu kwa matatizo yanayotukabili katika uwanja wa kisiasa nchini.

Tunafanya yote hayo ili kujihakikishia amani, utulivu, mshikamano na umoja wa taifa letu na watu wake vinaendelea kuwepo daima dumu.Napenda kumaliza kama nilivyoanza kwa kukumbusha kwamba mazungumzo haya yametokana na ahadi yangu na ya CCM. Ahadi hiyo ni ya dhati na niliitoa kwa kujiamini na kwa kuamini kuwa hii ndiyo njia pekee iliyo bora kuliko zote ya kushughulikia tofauti zetu.

Kwa msingi huo, ningependa na CCM ingependa kuona mazungumzo haya yanaendelea na yanazaa matunda tunayoyatarajia sote. Nawasihi wenzetu wa CUF tuungane kuhakikisha tunafanikiwa. Tusikubali mazungumzo yavunjike kwani gharama ya kuvunjika kwa mazungumzo haya ni mbaya na haina maslahi kwa taifa letu na watu wake. Itahatarisha amani na utulivu wa nchi yetu.
Ikulu, Dar es Salaam.
14 Agosti, 2007

No comments: