Thursday, August 11, 2011

MBunge Adai Naibu Spika Mhe. Job Ndugai Ameshindwa Kuendesha vikao vya Bunge
Nimepata kwa email:

(Pichani: Mh. John Mynika Mb. Ubungo)


Leo tarehe 11 Agosti 2011 katika kikao cha 48 cha Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi nilitaka kuomba muongozo wa Spika kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la 2007 ) kifungu cha 68 (7) kuhusu maswali na majibu ya Waziri Mkuu na nikarejea pia kanuni ya 133 (1).

Hata hivyo, kabla hata ya kutoa maelezo kamili ya kuomba muongozo wa Spika nilizuiwa na Naibu Spika Mheshimiwa Job Ndugai (Mb) bila hata ya kusikilizwa muongozo ambao nilitaka kuomba kinyume na kanuni ya 5 (1) inayotaka Spika kuongoza Bunge kwa kuzingatia kanuni na pale ambapo kanuni hazijatoa muongozo Spika anapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia katiba, sheria nyingine za nchi, kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali na desturi za kibunge.

Naomba kutoa taarifa kwa umma kwamba sijaridhika na uamuzi uliofanywa na Naibu Spika Mheshimiwa Job Ndugai hivyo nawajulisha kwamba ninakusudia kuwasilisha malalamiko kwa mujibu wa kanuni za Bunge kifungu 5 (4) na 7 (3) mara baada ya kupata nakala ya kumbukumbu rasmi ya Bunge (Hansard) ya kikao husika.

Mara baada ya kunukuu kanuni husika nilipoanza tu kuzungumza kwamba katika kipindi cha Maswali na Majibu kwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amekuwa akitoa majibu yenye upotoshaji yasiyokuwa ya kweli; baada ya kauli hiyo kabla hata ya kumaliza maelezo niweze kuomba muongozo kwa Spika; Naibu Spika alinikatisha na kuninyima fursa ya kuomba muongozo kinyume na kifungu 68 (7) na 5 (1).

Naomba umma uelewe kwamba nilikuwa naelewa kwa kina mahitaji ya kanuni za bunge kifungu cha 133 na vipengele vyake kuanzia cha kwanza mpaka cha sita; ndio maana katika kuanza kuomba muongozo nikasoma kifungu cha 133(1).

Napenda umma ufahamu kwamba muongozo ambao nilitaka kuomba kwa Spika ni kwamba kumekuwa na kawaida ya Waziri Mkuu wakati akijibu maswali ya papo kwa papo kutoa maelezo yasiyokuwa ya kweli yenye upotoshaji ambayo ni kinyume cha katiba ya nchi, sheria mbalimbali pamoja na kanuni ikiwemo kanuni za bunge hivyo nilitaka Spika atoe muongozo wenye kumpa nafasi nyingine Waziri Mkuu kutoa ufafanuzi wa kweli kuhusu masuala husika ili kuepusha uwezekano wa wabunge kupoteza imani na Waziri Mkuu kwa mujibu wa kanuni za bunge kifungu cha 133.

Katika maelezo yangu ya kuomba muongozo huo nilikusudia kutaja mifano miwili mikubwa ya majibu ya Waziri Mkuu kwenye maswali ya papo kwa papo yasiyokuwa ya kweli yenye upotoshaji kuhusu kashfa ya Meremeta na kuhusu mgogoro katika Manispaa ya Arusha.

Ikumbukwe kwamba tarehe 14 Aprili 2011 wakati wa kikao cha saba cha mkutano wa tatu wa Bunge la Tanzania wakati wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, nilimuuliza Mheshimiwa Mizengo Pinda kuwa “Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye vile vile ni Mwenyekiti wa CCM amenukuliwa akizungumzia kuhusu haja ya Chama kinachotawala kujivua gamba. Kati ya mambo aliyoyazungumza ni pamoja na kuondokana na watuhumiwa wa ufisadi. Mheshimiwa Mkuu uliwahi kulieleza Bunge hili tukufu kwamba usingetaka kabisa kuzungumzia masuala ya Meremeta kwa sababu ni siri za Jeshi. Baada ya kauli hii ya Rais na dhamira hii ya kujivua gamba kuhusiana na masuala ya ufisadi. Je, uko tayari Mheshimiwa Waziri Mkuu kutaja wahusika wa Kampuni ya Meremeta na kuelekeza Serikali kuchukua hatua zinazostahili kuhusiana na tuhuma hizo? . Waziri Mkuu katika majibu yake Mheshimiwa Mizengo Pinda hakuitumia nafasi hiyo kurekebisha kauli zake zisizokuwa za kweli zenye upotoshaji alizozitoa kwa nyakati mbalimbali katika Bunge la Tisa kuhusu kashfa ya Meremeta.

Ikumbukwe pia kwamba tarehe 10 Februari 2011 katika kikao cha tatu cha mkutano wa pili wa Bunge la kumi Waziri Mkuu Mizengo Pinda akijibu maswali ya papo kwa papo ya Mheshimiwa Freeman Mbowe (Mb) kuhusu matukio yaliyojitokeza Arusha wakati na baada ya uchaguzi batili wa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha. Tarehe 11 Agosti 2011 katika kipindi cha Maswali ya papo kwa papo ya Waziri Mkuu kuliulizwa maswali kuhusu maamuzi ya kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA ya tarehe 6 na 7 Agosti 2011 kwa kurejea pia mazungumzo baina ya Waziri Mkuu na viongozi wa taifa CHADEMA kuhusu muafaka batili juu ya mgogoro katika Halmashauri ya Jiji la Arusha na uamuzi wa kuwafukuza uanachama madiwani watano kutokana na kukiuka maagizo ya kamati kuu. Badala ya Waziri Mkuu kuitumia nafasi hiyo kutoa majibu yenye kulenga kutoa ufafanuzi wa kurekebisha upotoshaji uliofanyika awali Waziri Mkuu Mizengo Pinda akatoa majibu mengine yasiyokuwa ya kweli kuhusu mazungumzo yake na viongozi wa CHADEMA pamoja na uamuzi wa chama wa kuwafukuza uanachama madiwani waliokiuka maamuzi ya kamati kuu ya chama.

Majibu ya Waziri Mkuu kuhusu ufisadi wa Meremeta, matukio katika halmashauri ya Jiji la Arusha na masuala mengine ya kitaifa katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo yenye uhusiano na utekelezaji wa majukumu ya Waziri Mkuu yaliyoanishwa katika ibara ya 52 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yana mwelekeo wa kuvunja sheria ya maadili ya viongozi wa umma, sheria nyingine za nchi yetu pamoja na misingi muhimu ya utawala bora kama ambavyo nitafafanua katika hatua zinazofuata. Naomba umma upuuze upotoshaji uliofanywa na Naibu Spika Job Ndugai kuhusu muongozo nilioomba mpaka pale maamuzi yatakapofanywa na Kamati ya Kanuni za Bunge kwa mujibu wa kifungu 5(5) na Bunge kujulishwa.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)

Bungeni-Dodoma

11/08/2011

1 comment:

Anonymous said...

Nilisikiliza na kuangalia kwenye luninga tukio lote...Mh Nyika aliomba "ruksa aombe Mwongozo" kwa kupitia Kanuni ya Bunge akitaka ufafanuzi juu ya kipengele cha Katiba ya Nchi...Lakini Naibu Spika hakumpa ruksa kuomba Mwongozo badala yake akajifanya aliisha jua Mh Nyika alitaka kuomba Mwongozo gani anakajitolea eti kutoa maelezo juu ya matakwa ya kipengele cha Katiba...Huu ulikuwa upotoshaji wa lengo la Mh. Nyika kwa makusudi ili hasipate ruksa ya kuomba Mwongozo.

Pale Mh Ndugahi alionyesha wazi wazi kuwa hakutaka Mh Waziri Mkuu abanwe kuhusu msimamo wake kuhusu sakata la umeya wa Arusha na kuhusu alichozungumza na viongozi wa Kitaifa wa Chadema. Leo kwa mara ya kwanza nimeshuhudia Ndugu Ndugahi na Ndugu Pindi wakicheza karata ya ushabiki na ubabe wa chama cha CCM kama nilivyozoea kuona Ndugu Nape na Mh Chatanda yule Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Tanga wanavyofanya siku zote..Inaelekea Mh Pinda ameamua kurudi nyuma na kucheza mchezo wa akina Nape na Chatanda wa kudhani sakata la umeya litaisha kwa ubabe ukipokezana na kuwaonga kwa vyeo wasio na uadilifu ndani ya Chadema Arusha mjini.

Mh. Pinda alinisononesha kujiingiza kwenye siasa uchwara kama akina Nape na Chatanda. Nilimuonea huruma sana. Labda mtoto wa mkulima na yeye anaanza kuota ndoto za kuwa ngombea wa kiti cha urais 2015 na anabidi akubalike kwa watetezi wa siasa uchwara nadni ya chama chake masikini!! Kama kinachoitwa uchanguzi wa meya Arusha haukuwa na utata sasa maridhiano na wale madiwani wa Chema waliofukuzwa yalikuwa ya nini, yarabhi? Na kama Chadema wamekosea katika kuwafukuza wale madiwani wao waliopewa uongozi katika halmashauri kama zawadi na CCM sasa CCM si isherehekee kuvipata viti hivi vya umeya kiulaini kwa kuwasimamisha hao hao madiwani waliofukuzwa na Chadema, au siyo?

Hivi chama cha siasa kikimfukuza diwani au mbunge si yuko huru kuamia chama kingine na kama bado anapendwa si atashinda kiti husika kwa kishindo?Mbona sasa Waziri Mkuu anawashauri madiwani wale waliofukuzwa eti waende mahakamani kudai haki? Haki gani tena? Si angewashauri wajiunge na CCM na CCM iwateue kugombea na watashinda bila wasiwasi kama kweli wananchi husika wanaona Chadema iliwafukuza kwa kuwaonea? Mh Pinda leo amejisogeza karibu na wakina Ndugahi, Nape na Chatanda wa CCM ambao bila shaka yoyote Mh Rostam Aziz , licha ya madhambi yake yote, aliwapatia aliposema ni watetezi wa "siasa uchwara" ndani ya CCM.