Thursday, September 06, 2012

Rais Kikwete Atuma Salamu za Rambirambi Kwa Kifo cha Lt. Col. Adam Makwaia

Lt. Colonel  (ret.) Adam  Hussein Makwaia

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Luteni Kanali (mst) Adam Hussein Mwandu Makwaia, aliyekuwa Mpambe wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais Ali Hassan Mwinyi.

Katika salamu zake, Rais Kikwete amemwambia Jenerali Mwamunyange: “Nimepokea kwa majonzi na masikitiko taarifa za kifo cha Luteni Kanali Makwaia ambaye nimejulishwa kuwa alipoteza maisha Jumanne, Septemba 4, mwaka huu, 2012, katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo mjini Dar es Salaam.”

“Katika miaka yote ya utumishi wa Jeshi na utumishi wa umma, Luteni Kanali Makwaia alikuwa mwadilifu na mwaminifu kwa nchi yake, alikuwa na weledi wa kiwango cha juu katika taaluma yake ya kijeshi na alikuwa mtiifu kwa viongozi wake. Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi salamu zangu za rambirambi kufuatia kifo hiki,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Aidha, kupitia kwako natuma salamu za pole nyingi kwa familia ya marehemu Makwaia ambao wamempoteza baba na mhimili wa familia. Pia, kupitia kwako, natuma salamu za rambirambi kwa maofisa na wapiganaji wote wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao wamempoteza ofisa na mpiganaji mwenzao.”

Luteni Kanali (mst) Makwaia alijiunga na Jeshi Machi 24, mwaka 1974, na alilitumikia kwa miaka 23 na miezi tisa kabla ya kustaafu. Alikuwa Msaidizi wa Mpambe wa Rais kati ya mwaka 1978 na 1981 na kuwa Mpambe wa Rais kwa miaka sita hadi 1987. Amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 62.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
6 Septemba, 2012
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ndugu jamaa na marafiki wa Hayati Luteni Kanali (mst) Adam Hussein Mwandu Makwaia leo Septemba 6, 2012 Keko, jijini Dar es salaam.


Hayati Luteni Kanali (mst) Adam Hussein Mwandu Makwaia, akiwa kazini kama  Mpambe wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na baadaye  Rais wa pili wa Tanzania Alhaj  Ali Hassan Mwinyi.


2 comments:

emu-three said...

Mungu aliaze mahala pema peponi roho ya marehemu huyo na poleni sana ndugu na jamaa zake! Yote ni mapenzi ya Mungu

Anonymous said...

Rest in peace Adam. Condolences to family and friends of the Makwaia family.