Sunday, January 02, 2011

Oscar Kambona, James Mapalala, Augustine Mrema na Siasa

Vijana wengi hawajawahi kusikia jina la Oscar Kambona na James Mapalala. Hao walikuwa wazito katika siasa za Tanzania kipindi fulani. Mimi nilikuwepo Uwanja wa Ndege Dar siku Mzee Kambona alivyorejea kutoka kwenye Exile Uiingereza. Mamia ya wakazi wa Dar walienda kumpokea. Airport walimnyanganya Fax machine aliyokuja nayo kama hand luggage. Mbu walijaa kibao pale uwanjani na nyumbani na jirani kwa Mzee Kambona.

Kuhusu James Mapalala na CUF, yule Mzee ni kweli alipotea kipindi fulani.

Soma Alivyoandika Kaka Maggid Mjengwa.
***********************************************
Ndugu Zangu,

Historia ni mwalimu mzuri. Bado kuna umuhimu wa kukumbushana tulikotoka. Huko nyuma nimeuliza kama kuna wanaokumbuka alichotamka Bw. Augustino Mrema. Ni mrema huyu aliyepata kuwa Waziri wa Mambo ya ndani katika kipindi cha Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi.

Katikati la vuguvugu lile la mageuzi ya kisiasa miaka ya 90 mwanzoni, Watanzania zikatufikia habari; kuwa Oscar Kambona, aliyekosana na Nyerere na aliyekimbila uhamishoni Uingereza alikuwa njiani kurudi nyumbani. Ujio wa Oscar Kambona ukawa gumzo la mjini na nje ya jiji. Kuna waliojiandaa kwenda uwanjani kumpokea.

Usiku mmoja ikasikika sauti ya Bw. Mrema redioni. Sauti ya Waziri wa Mambo ya ndani. Mrema alitamka, kuwa kama Kambona angekanyaga mguu wake Dar es Salaam, basi, angekamatwa kujibu mashtaka ya uhaini.

Ni hofu ile ile ya Serikali hata wakati huo. Hofu ya kuimarika kwa fikra za upinzani na kukua kwa upinzani. Mrema akatumika au akajituma kuwatisha Watanzania. Kambona alikanyaga Dar, hakuwa na mashtaka ya kujibu. Ulikuwa ’ mkwara’ tu, kama wanavyosema mitaani.

Na Mrema, akiwa Waziri wa Mambo ya ndani, alifanya kweli kazi ya kuwa ’ Mbwa wa Serikali’. Na alibwaka kweli. Nakumbuka usiku mmoja mwanzoni mwa miaka ya tisini nilimsikia Mrema akitoa ’ mkwara’ redioni kutishia maandamano ya CUF. Maandamano yale yalikuwa yahitimishwe kwa mkutano viwanja vya Mnazi Mmoja. Mwenyekiti wa CUF, ( Tanzania Bara) Bw. James Mapalala ndiye alikuwa aongoze maandamano hayo na kuhutubia.

Augustino Lyatonga Mrema akaaunguruma redioni usiku ule. Alirusha ’ mkwara’ mzito. Kuwa maandamano hayo si halali na yangekutana na nguvu za dola. Kesho yake CUF waliingia mitaani. Ndio, Ungangari wa CUF ulianza siku nyingi.

Pale mnazi mmoja FFU wakamwagwa, na farasi wao pia. Virungu vilitembea. James Mapalala, Mwenyekiti wa CUF hakuonekana. Kukawa na taarifa kuwa anatafutwa na polisi.

Dar ilikuwa ndogo wakati huo, lakini James Mapalala hakupatikana siku hiyo.
Ninazo taarifa za kuaminika za kibalozi, kuwa James Mapalala alikuwa amejificha kwenye moja ya makazi ya rafiki yake, balozi wa nchi moja ya Kimagharibi. Ni balozi gani huyo? Na nini hasa kilitokea miaka 20 iliyopita?

James Mapalala yungali hai. Huu ni wakati kwa waandishi vijana kuwatafuta wazee veterani wa harakati za mageuzi ya kisiasa hapa nchini kama akina Mzee James Mapalala.

Hawa ni watu muhimu sana watakaotusaidia kupokea simulizi zao. Kisha ziwekwe kwenye maandishi na iwe kumbukumbu za kihistoria. Ni historia yetu, tusiionee aibu. Ni urithi tutakaowaachia wajukuu zetu ili nao waweze kujitambua na kujenga mioyo ya uzalendo.
Huu wangu ni mchango mdogo tu.
Maggid

http://mjengwa.blogspot.com

1 comment:

emu-three said...

Kweli hawa ni watu muhimu sana katika historia ya nchi yetu,