Friday, July 01, 2011

Ziara Mbili za Ughaibuni Zolizovunja Urafiki wa Nyerere na Kambona

Ziara mbili za ughaibuni zilizovunja urafiki wa Nyerere na Kambona

Na Maggid Mjengwa

KUNA wakati nilimsikia Ahmad Rashid akitoa hoja bungeni. Wakati huo mbunge huyo wa CUF alikuwa kiongozi wa upinzani bungeni. Ahmad Rashid aliomba kambi ya upinzani bungeni ibadilishwe jina na badala yake iitwe kambi ya ushindani bungeni. Ni kwa vile neno ‘upinzani’ linatafsiriwa vibaya na wananchi. Spika Samwel Sitta alisimama na kutamka; “ Mtaendelea kuitwa hivyo hivyo kambi ya upinzani, kwa vile nyinyi ni watu wa kupingapinga tu!”


Na maneno haya ya Samwel Sitta yanatokana na historia yetu. Maana, haya ni makosa ya kihistoria yaliyofanywa na waliojenga msingi wa taifa letu. Na ndio tunayoyaona hata katika mfarakano wa miaka hamsini iliyopita kati ya Julius Nyerere na Oscar Kambona.

Na mara ile, mwaka 1965, TANU ilipoaachana na mfumo wa vyama vingi na kuasisi mfumo wa Chama kimoja Kambona alipata kutamka; ” Kwanini tupige marufuku ya vyama vingine vya siasa wakati tunajua wananchi walio wengi wanaipigia kura TANU?” Kambona akaongeza kusema; ” Bila shaka, umaarufu wa TANU utabaki kwa muda mrefu, lakini, je, pale umaarufu wa TANU utakapopungua, ina maana tuwe madikteta?” Alihoji Kambona.

Nimepata kukumbushia mara kadhaa, kuwa historia ni mwalimu mzuri. Na wanadamu hatupaswi kuwa vipofu wa historia yetu wenyewe. Kuifumbia macho historia yako ni kujiandalia njia ya kutumbukia korongoni, kwa kujitakia. Tunapoadhimisha miaka hamsini ya uhuru wa Tanganyika tuna lazima ya kuipitia na kuitafakari historia yetu. Kwa macho makavu na maangavu, tuangalie nyuma tulikotoka. Tuangalie tulipo sasa. Ndio, tufanye hivyo ili tuutafute mwelekeo mwema wa nchi yetu hata kwa miaka mingine hamsini ijayo.


Tuna maswali mengi ya kujiuliza, moja kuu ni hili; Je, ni nchi ya namna gani tutayotaka kuijenga na hata kuvirithisha vizazi vijavyo? Kwa maneno mengine; ni jamii gani tunayotaka kuijenga? Sisi wa ’ Kizazi Cha Azimio’ tulikuwa wadogo sana katika miaka kumi ya mwanzo ya uhuru na hata utekelezaji wa Azimio la Arusha. Nimezaliwa Ilala, Dar es Salaam, Machi 11, 1966.


Ndio, kuna mema mengi tuliyoyaona, lakini, tukitafakari sasa, kuna mabaya mengi pia tuliyoyashuhudia. Tuna wajibu wa kusimulia mema na mabaya hayo kwa manufaa ya Watanzania wa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Kati ya kumbukumbu zangu mbaya za wakati huo ni jinsi tulivyowaona wazazi wetu wakiishi kwa hofu. Waliogopa kushutumu mamlaka hadharani na kwa sauti. Waliishutumu Serikali na hata kiongozi mkuu wa nchi kwa kunong’ona. Wazazi wetu walimwogopa hata mjumbe wa nyumba kumi.

Ni ukweli, kuwa kwa wakati ule, Serikali na chama tawala havikuwa na uvumilivu wa sauti za upinzani.

Na siku zote, mamlaka bila upinzani huzaa kiburi na majigambo. Huzaa hali ya kutokujali na kukosa usikivu. Taratibu, huzaa hali ya kujisikia u-bwana mkubwa. Hali hii ikiachwa ikaendelea, basi, husababisha madhara makubwa kwa nchi. Huleta hasara kubwa kwa nchi, kiuchumi na kijamii.

Juma la jana nilimalizia kwa kuandika, kuwa makala haya ni jaribio la kuvunja ukimya wa juu ya nini kilitokea takribani miaka hamsini iliyopita. Ni mmoja tu wa mfano , wa jinsi umma ulivyofichwa ukweli wa juu ya nini hasa kilitokea kikasababisha mfarakano wa waliopata kuwa viongozi wa mstari wa mbele kwenye harakati za kuanzishwa kwa TANU na kudai uhuru wa Tanganyika; Julius Kambarage Nyerere na Oscar Salathiel Kambona.


Kuna aliyesoma makala yangu ya juma la jana na kuniuliza; ” Maggid, hivi wewe huogopi?” Ni kweli, kama ningeandika haya mwaka 1976 nilipokuwa mtoto wa umri wa miaka kumi tu, basi, vyombo vya dola vingenishukia mithili ya mwewe anayekishukia kifaranga cha kuku. Sio tu mimi ningeswekwa rumande ya watoto, bali hata mama na baba yangu wangetikiswa na dola kwa ’ dhambi’ ya kumzaa mtoto mwenye fikra za ’ kipinzanipinzani ’ na ’ kihainihaini’. Mtoto ’ anayepingapinga’ tu!


Na hapa ndipo kwenye moja ya mapungufu makubwa ya waliojenga msingi wa taifa letu; kuchukia wenye kufikiri tofauti na watawala. Na zaidi kuwachukia wenye ’ akili’ ya kufikiri na kuutumia vema welewa wao- hostility towards execelency. Si tunajua, kuwa utotoni tulisikia kuna maadui wa nchi wa aina mbili; maadui wa nje na wa ndani. Wapinzani ama wenye kufikiri tofauti ndimo walimowekwa wanaoitwa ’maadui wa ndani!’


Niseme tu, mfulilizo wa makala haya ni moja ya makala zangu muhimu tangu nianze kushika kalamu na kuandika makala magazetini. Na naandika nikiwa sina hata chembe ya hofu. Ni kwa sababu moja kuu; kuwa yanahusu historia yetu na mustakabali wa nchi yetu. Sote tuna wajibu wa kuandika historia yetu.


Hii ni nchi yetu. Hatuna sababu za kuionea aibu historia yetu, badala yake, tujivunie, kuwa tuna historia. Na ni unyonge na utumwa kusubiri wasomi kutoka Marekani na Ulaya waje kutafiti na kutuandikia historia yetu. Historia yako isimulie mwenyewe. Hivyo basi, tuna wajibu wa kuifanya kazi hiyo. historia itusaidie kutukumbusha machungu na furaha ya tuliyoyapitia kama taifa. Si kwa kuandika tu, hata kwa kusimulia machache tuliyoyashuhudia.


Niliahidi kuchambua zaidi juu ya marafiki hawa watatu; Kambona, Nyerere na Kawawa. Nitafanya hivyo sasa.

Naam. Julius na Oscar walikuwa viongozi vijana sana katika Tanganyika huru ya wakati huo. Ikumbukwe, wakati tukipata uhuru, Nyerere alikuwa na miaka 39 na Oscar alikuwa na miaka 36. Hawa walikuwa ni vijana waliokabidhiwa dhamana kubwa ya kuingoza nchi kubwa ya Tanganyika. Naamini, walikuwa ni wenye dhamira njema kwa taifa hili; Julius, Oscar, Rashid na wenzao wengine katika TANU.
Ukweli unabaki, kuwa Oscar Kambona hakuikimbia nchi yake kwa kashfa ya kuiba fedha ya Serikali au ufisadi mwingine. Na kwa utafiti mdogo tu niliofanya, nilichobaini, ni ukweli kuwa marafiki hawa wawili; Oscar na Julius walikuwa na mgongano wa tofauti ya kimaono ya kisiasa yaliyoathiri hata urafiki wao.

Maana, haiyumkini Kambona aliyeaminiwa na Nyerere akaja kuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa TANU, akawa Waziri wa kwanza wa Elimu wa Tanganyika huru, akaja kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na hata kwa wakati mmoja kushika wizara mbili; Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Mambo ya Nje. Kwamba, aje tena baadae kutuhumiwa uhaini na hata kushukiwa uraia wake.


Ndio, kwangu mimi, ya Kambona na Nyerere ilihusu zaidi mgongano wa tofauti za kimaono ya kisiasa . Na ukiingia kwa undani kwenye maandiko na simulizi utaupata ushahidi wa haya. Na kwa hakika, ili siasa ya nchi istawi, basi, inahitaji uwepo wa migongano ya kifikra. Hivyo basi, siasa ni migongano ya kifikra yenye kuhitaji majadiliano endelevu.


Tunaona, kuwa migongano ya kifikra kati ya Oscar na Julius ilianza kuonekana dhahiri katika ziara mbili walizozifanya kwa pamoja katika mataifa mawili tofauti. Ziara ya Marekani mwaka 1963 na ziara ya Uchina mwaka 1965. Na hapo katikati kuna jambo lililoopelekea uwepo wa mahusiano ya mashaka kati ya Julius na Oscar. Ni uasi wa jeshi wa Janauri 20, 1964.


Uasi ule ulipelekea Nyerere na Kawawa waende mafichoni, inasimuliwa walijihifadhi eneo la Kigamboni. Mjini alibaki Oscar Kambona aliyeshiriki kikamilifu kuwatuliza wanajeshi wale. Kimsingi, katika kipindi kile cha maasi, Kambona, kama angetaka, alikuwa na fursa ya kutwaa mamlaka ya nchi akisaidiwa na jeshi. Inasemwa, kuwa akiwa Waziri wa Ulinzi, Kambona alikubalika sana jeshini.


Baada ya ziara ya Marekani akiwa na Oscar Kambona mwaka 1963 ambako Rais John Kennedy alimsifia sana Nyerere kwa kuonyesha uwezo wa kiungozi , miaka miwili baadae, mwaka 1965, Nyerere na msafara wake akiwamo Oscar Kambona walikwenda China kwa mara ya kwanza na kulakiwa na Mwenyekiti Mao Tse Tung. Nyerere akiwa kwenye gari la wazi na mwenyeji wake Mao , alishangiliwa na Wachina wapatao milioni moja waliojipanga barabarani.

Pale Ilala tulikoishi, nakumbuka nikiwa na umri wa miaka sita tu, usiku mmoja pale viwanja vya shule ya msingi Boma tuliangalia sinema ya ziara ya Julius Nyerere Uchina . Nyerere aliiona China na alivutiwa sana. ” What we have seen in China is relevant to us”. Nimemsikia Nyerere akiongea hayo kwenye kipande cha filamu ya zamani kilichopo mtandaoni . ” Ana maana, walichokiona China kinaweza kikafanyika kwetu. Na Julius alianza kwa kubadilisha hata staili yake ya mavazi, yakafanana na ya Mwenyekiti Mao, na wengine katika TANU wakamwiga.

Ni nini kilitokea kwenye Mkutano wa TANU wa Januari, mwaka 1967 na kabla ya hapo. Mkutano uliopelekea kumalizika kabisa kwa urafiki wa Nyerere na Kambona. Fuatilia toleo lijalo.
http://mjengwa.blogspot.com

No comments: