Sunday, July 31, 2011

Serikali Iombe Wananchi Msamaha - Mgao wa Umeme

Nimepata hii kwenye email.

*******************************************************************

Imeripotiwa kuwa Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ameitaka serikali iwaombe radhi wananchi kwa mgao wa umeme unaoendelea. Kauli hiyo ya Sitta imewafanya maadui wake ndani ya serikali, CCM na baadhi ya vyombo vya habari vinavyotumiwa kuibuka na kumuita waziri huyo kuwa ni msaliti na lazima afukuzwe kazi.Lazima tukubali kuwa tuna tatizo kubwa sana la uwajibikaji katika nchi hii. Ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata umeme kwa ajili ya kuhakikisha ukuaji wa uchumi, upatikanaji wa huduma za jamii na maisha ya kila siku ya wananchi.

Leo hii, wastani wa asilimia 15 tu ya Watanzania milioni 44 wanapata umeme. Na serikali imeshindwa kuhakikisha kuwa asilimia hiyo ndogo ya wanaopata umeme wanapata huduma ya uhakika. Hapa ndipo dhana ya uwajibikaji inapokuja.

Kitendo cha serikali yenyewe kulazimika kuitoa bajeti ya wizara ya nishati na madini Bungeni ili
wakajipange upya ni ishara nyingine kuwa serikali haiko makini kwenye kutatua mgao wa umeme. Ni baada tu ya kuona kuwa Wabunge wamekuja juu na huenda hawatapitisha bajeti hiyo ndiyo serikali ikashituka usingizini na kusema wanahitaji muda wa kujipanga zaidi.

Wakati serikali imeongeza bajeti ya miundombinu kwa asilimia 85 na kufikia shilingi trilioni 2.78 ($1.73 billion), ilitenga shilingi bilioni 402.4 ($250m) tu kwa wizara ya nishati na madini katika kipindi hiki ambacho taifa liko kwenye janga kubwa la umeme. Ni kweli tunahitaji barabara, bandari, reli na airport, lakini ni lazima tuweke vipaumbele sawa. Kama pesa hazitoshi kufanya vyote kwa wakati mmoja, serikali makini ingetatua tatizo la umeme kwanza ndipo ijenge barabara.

Narudia tena, tatizo la umeme nchini si ukame. Ni matokeo ya serikali kutotoa kipaumbele kwa suala hili tangu ilipoingia madarakani. Ndiyo maana serikali imekiri yenyewe kuwa katika kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano, imeongeza megawati 145 tu kwenye gridi ya taifa. Lazima kuwe na hatua za dharura, muda mfupi na muda mrefu (immediate, medium-term na long-term) za kukabiliana na tatizo hili. Serikali inabidi isimamishe safari za nje, posho, semina, manunuzi ya Landruiser VX, na matumizi mengine ya anasa ili pesa zote ziende kwenye umeme. Na ikibidi hata ikope pesa nje ili kuwekeza kwenye umeme. Kwenye global financial crisis, serikali ilitoa 1.7 trillion shillings (over $1 billion) na kugawa pesa hizi kwa kampuni zenye utata. Leo hii serikali inasemaje haina pesa za kuzalisha umeme na kutoa $250m tu? Athari za mgao wa umeme ni kubwa mara dufu kuliko zile za global financial crisis.

Serikali inabidi ifanye budget re-allocation kubwa na kutoa pesa kwenye wizara na mufungu mengine na kuzipeleka kwenye umeme.

Huko Afrika Kusini mwaka 2008 wakati nchi hiyo ilipokutwa na tatizo la umeme, aliyekuwa Rais wa wakati huo, Thabo Mbeki, alikuwa na uungwana wa kwenda mbele ya Bunge la nchi hiyo na kuwaomba radhi wananchi kwa mgao wa umeme. Sijaona mkuu wa nchi yetu akichukua hatua kama hii.

Thabo Mbeki alisema kuwa Eskom (TANESCO ya Afrika Kusini) ilikuwa inaomba pesa serikalini kila siku iwekeze kwenye umeme serikali ikakataa na kuwambia wasubiri mpaka baadae. Mbeki akakiri kuwa Eskom ilikuwa sahihi na serikali ilikosea. Na akaomba radhi. Wataalamu wa TANESCO waliikataa Richmond, vigogo serikalini wakalazimisha wapewe mkataba na matokeo yake tumeyaona. Hakuna aliyeomba radhi, na mhusika kuu akabaki kusema hajutii maamuzi yake na kujisifu kuwa yeye ni hodari wa kufanya maamuzi magumu. TANESCO kila siku imekuwa ikiomba pesa za miradi mikubwa ya umeme lakini serikali imekuwa ikiwaambia waendelee kusubiri tu. Hakuna aliyekiri kosa, kuomba radhi wala
kuwajibika.

Angalia:
http://www.news24.com/SouthAfrica/Politics/Mbeki-apologises-for-power-cuts-20080208-2
http://www.iol.co.za/news/politics/mbeki-apologises-for-sa-power-cuts-1.382421
http://www.southafrica.info/about/government/stateofnation2008-electricity.htm

Idara ya hali ya hewa iko pale kufanya utabiri wa hali ya hewa. Hivyo basi, tangu mwaka 2005 walitabiri kuwa 2010/11 kutakuwa na upungufu wa mvua. Hata hii leo wanaweza kutoa utabiri wa hali ya hewa ya mwaka 2015/16 itakuwaje. Serikali ilikuwa na taarifa tangu miaka mitano au hata kumi iliyopita kuwa mwaka huu kutakuwa na mvua chache na hii itaathiri uzalishaji wa umeme, upatikanaji wa chakula, mfumuko wa bei, nk. Serikali iache kusingizia ukame. Iombe radhi kwa taifa kuwa mgao huu wa umeme unatokana na serikali yenyewe kutotoa kipaumbele kwa tatizo hili na kutojipanga kukabiliana nalo. Na iseme ukweli chanzo cha mgao ni nini, umeleta athari gani kwa taifa, serikali inafanya nini na tatizo hili litaisha lini. Serikali sikivu ingewaomba radhi wananchi wake. Na wananchi makini na wazalendo wangedai uwajibikaji kutoka serikalini, si visingizio vya ukame!

Mdau

1 comment:

Anonymous said...

Richmond ilikuzwa kwa maslahi ya watu binafsi, kwanini haiandikwi ukweli kuwa waliokuwa kwenye tume walikuwa na vested interest? Kwanini yule mwekezaji wa Richmond kesi yake imefutwa kwa kukosekana ushahidi?

KWANINI WATU HAWAAIMBIWI UKWELI KUWA KINA MWAKYEMBE WALIKUWA NA KAMPUNI YAO WALIYOTAKA KUIUZIA UMEME TANESCO, YEYE NA WENZIWE WAKATI HUO HUO AKAKUBALI KUWA KWENYE TUME ILIYOSEMA RICHMOND INA MATATIZO?

Na hata Zitto Kabwe wakati huo alikuwa kwenye kamati ya Bunge ya Nishati alipotoa ushauri kuwa mitambo ya Dowans inunuliwe na Tanesco kutokana na mapendekezo ya Tanesco huyo Sitta na wenzie walisema heri nchi iwe kizani, sasa leo wanaleta unafiki wao? Hao kwa maslahi yao binafsi kupitia mgongo wa vita vya ufisadi na kwa mambo ya kisiasa ndio wamesababisha mgao kuwa mgumu na mkali, kila kitu walikuwa wanapinga kumbe wana kampuni yao mfukoni, mwe watu wamuogope mungu sasa, na wajue kuwa duniani hakuna siri.