Rais Jakaya Kikwete |
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo ada naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenye
Rehema, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuzungumza kwa mara
nyingine kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri wa mawasiliano baina ya
Rais na wananchi wa Tanzania kila mwisho wa mwezi. Siku ya leo
nitazungumzia safari yangu ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia. Pia
nitazungumzia ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara
kuja Dar es Salaam.
Safari za Kikazi Nje ya Nchi
Ndugu Wananchi;
Safari yangu ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia ilikuwa na
manufaa makubwa kwa nchi yetu. Nchini Ufaransa licha ya kuimarisha
uhusiano wa kirafiki baina ya nchi zetu, tumepata wawekezaji wengi
wakubwa wenye nia thabiti ya kuja kuwekeza hapa nchini. Pia
tumekubaliana kuanza mazungumzo ya kuwa na mpango mwingine wa
ushirikiano. Mpango wetu wa sasa ulioanza mwaka 2006 uliisha mwaka
2010. Mpango ule ulitusaidia sana kuboresha huduma za maji katika
miji ya Utete mkoani Pwani na Mpwapwa mkoani Dodoma.
Katika mkutano wa Kongamano la Uchumi wa Dunia uliofanyika
Davos, Uswizi, tumehakikishiwa ushirikiano katika kuendeleza juhudi
zetu za kuleta mapinduzi ya kijani ili tujihakikishie usalama wa
chakula na kupunguza umaskini vijijini na kukuza uchumi wa nchi yetu.
Aidha, tulipata bahati ya kushirikishwa katika mjadala wa kuanzishwa
kwa programu kubwa ya kuzisaidia nchi za Afrika kutatua matatizo ya
upatikanaji wa umeme. Naamini programu hiyo ikitekelezwa na wakubwa
kuheshimu kauli na ahadi zao itakuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya
nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ndugu Wananchi;
Nchini Ethiopia tulishiriki katika mkutano wa Wakuu wa Nchi
na Serikali wa Umoja wa Afrika na katika kikao cha African Peer Review
Mechanism (APRM) ambapo taarifa ya tathmini ya utawala bora ya
Tanzania na Zambia iliyofanywa na APRM ilijadiliwa. Kwa jumla hatuna
mahali tuliponyooshewa kidole kuwa tunafanya vibaya. Tumepongezwa
katika mambo mengi na tumepewa ushauri kwa baadhi ya maeneo waliyoona
hatuna budi kuyaboresha. Nilipata nafasi ya kusema ambayo niliitumia
kufafanua baadhi ya mambo yaliyokuwamo kwenye taarifa. Niliwashukuru
na kuahidi kuufanyia kazi ushauri uliotolewa. Tathmini ya nchi yetu
ilipitishwa kwa kauli moja.
Vurugu za Kupinga Gesi Kusafirishwa Kutoka Mtwara
Ndugu wananchi;
Kama mtakavyokumbuka tarehe 8 Novemba, 2012 kule Kinyerezi, Wilaya ya
Ilala hapa Dar es Salaam, niliweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba
la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara na Songosongo kuja Dar es
Salaam. Karibu na mwishoni mwa Desemba, 2012 kukafanyika maandamano
mjini Mtwara kupinga ujenzi wa bomba hilo. Katika
maandamano yale na baadaye kwenye kauli za wanasiasa na wanaharakati
yakatolewa madai kuwa gesi hiyo itumike kwa maendeleo ya Mtwara na
kwamba yale yanayotakiwa kufanyika Dar es Salaam yafanyike Mtwara.
Pia, zilitolewa shutuma nyingine dhidi ya Serikali eti kuwa kwa miaka
mingi imewasahau na haiwajali wananchi wa Mikoa ya Kusini na ujenzi wa
bomba hilo ni muendelezo wa hayo. Kauli mbalimbali za wanasiasa na
wanaharakati ni kama vile ziliongeza mafuta kwenye kaa la moto na
kuuchochea mpaka kukatokea matukio yaliyotusikitisha na kutshtua
sote. Baadhi ya ndugu zetu wamepoteza maisha na mali za watu na
Serikali kuharibiwa.
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya kuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka 2013,
tarehe 31 Desemba, 2012, nililisemea jambo hili. Leo mwezi mmoja
baadae, napenda kusisitiza mambo mawili. Kwanza kwamba, si kweli kuwa
Serikali inapuuza Mikoa ya Kusini. Na pili, kwamba kujenga bomba la
kuipeleka gesi Dar es Salaam hakuinyimi Mikoa ya Mtwara na Lindi fursa
ya kunufaika na gesi iliyopo Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Serikali imefanya, inafanya na ina mipango ya kufanya mambo
mengi mazuri kwa ajili ya kuleta maendeleo katika Mikoa ya Mtwara na
Lindi. Ipo mipango ya kuboresha miundombinu, huduma za kiuchumi na
kijamii pamoja na kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda
vikubwa na vidogo. Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Rais
Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, ilijenga daraja katika Mto Rufiji
maarufu kama Daraja la Mkapa. Hii ilikuwa ni hatua kubwa ya awali
katika safari ya kutatua matatizo ya usafiri ya Mikoa ya Kusini.
Serikali ninayoiongoza mie iliachiwa kazi ya kukamilisha ujenzi wa
barabara za lami kufikia darajani na kuunanisha Mkoa wa Mtwara na Mkoa
wa Ruvuma. Kazi hiyo, tumeitekeleza vizuri na sasa tunakaribia
kuimaliza. Tulikamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Mnazi-Mmoja
hadi Nangurukuru. Mwaka 2009 tukaanza ujenzi wa barabara ya kilomita
56kutoka Somanga hadi Ndundu (darajani). Ujenzi wakilometa 36 za
mwanzo ulienda vizuri. Bahati mbaya ujenzi wa kilomieta 20 za mwisho
umechelewa sana kwa sababu ya mmiliki wa kampuni iliyokabidhiwa
kufanya kazi hiyo kufariki. Kwa sababu hiyo, kampuni ilipata
mtikisiko kiasi na kusababisha kazi kutotekelezwa kwa kasi
tuliyoitarajia. Sasa mambo yametengemaa na kazi inaendelea kwa kasi
nzuri. Matumaini yetu ni kuwa ifikapo mwezi Desemba, 2013 kazi hiyo
itakuwa imekamilika.
Hali kadhalika, Rais Mstaafu, Mzee Benjamin Mkapa alituachia jukumu la
kumaliza ujenzi wa Daraja la Umoja katika mto Ruvuma na ujenzi wa
barabara ya lami kuanzia Mikoa ya Mtwara na Ruvuma. Tumelikamilisha
Daraja hilo na ujenzi wa barabara ya lami kutoka Masasi hadi Mangaka
umekamilika. Mchakato wa kujenga barabara ya kwenda Songea na kwenda
Darajani umefikia mahala pazuri. Tenda ya ujenzi wa barabara kutoka
Tunduru hadi Mangaka mpaka Darajani imeshatangazwa. Kama mambo
yataenda sawa miezi mitatu ijayo mjenzi atapatikana. Wakati huo huo
ujenzi wa barabara kutoka Namtumbo hadi Songea – Mbinga na Namtumbo –
Tunduru unaendelea. Hivyo basi, kwa barabara ya “Mtwara Corridor”
kazi iliyobaki ni kutoka Mbinga kwenda Mbambabay ambayo tutaifanya
wenyewe kama tulivyofanya kwa Mnazi Mmoja – Nangurukuru na Somanga –
Ndudu na Daraja la Umoja.
Ndugu Wananchi;
Ipo pia mipango ya kuipanua na kuijenga upya bandari ya Mtwara ili
iweze kuhudumia mahitaji ya utafutaji na uchimbaji wa gesi baharini,
kuhudumia na kuvifanyia matengenezo vyombo vinavyotumika katika
utafiti, uchimbaji na uendelezaji wa gesi. Pia iweze kuhudumia
shughuli za kiuchumi zitakazotokana na uchumi wa gesi pamoja na
zilizopo sasa. Nilipozungumza na makampuni ya utafutaji gesi pale
Mtwara tarehe 25 Julai, 2011 waliomba nikubali bandari ya Mtwara iwe
mahali pa kuhudumia vyombo vyote vinavyofanya shughuli ya utafutaji na
uchimbaji wa gesi na mafuta katika pwani ya Afrika ya Bahari Kuu ya
Hindi. Pia waliomba kuwa sehemu hiyo ya bandari iwe bandari huru.
Niliwakubalia bila ya kusita na tayari eneo la hekta 110 zimeshatengwa
na kutangazwa rasmi kuwa bandari huru. Vile vile waliomba wapewe
sehemu ya bandari ya sasa kuendeshea shughuli na eneo la kujenga kituo
cha mitambo ya kuchakata gesi na kusafirisha nje.
Ndugu Wananchi;
Baada ya kuzungumza na makampuni ya utafutaji gesi na mafuta na
kuelezwa mahitaji yao nilibaini kuwa bandari ya Mtwara inahitaji
kupanuliwa na kujengwa upya. Bahati nzuri viongozi wa Mamlaka ya
Bandari walikuwepo na walinihakikishia kuwa watafanya hivyo.
Tayari eneo la bandari limeongezwa kutoka hekta 70.68 hadi 2,693.68.
Eneo la bandari huru limeshatengwa hivyo hivyo na eneo la kampuni ya
Dangote na makampuni ya gesi yaliyopo. Aidha, mchakato wa kupanua
bandari iliyopo, kujenga gati mpya na kuendelea na ujenzi hadi maeneo
ya Msanga Mkuu ipo katika hatua mbalimbali za matayarisho na
utekelezaji.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Mkoa wa Lindi mipango ya kupanua na kuijenga
upya bandari ya Lindi imefikia hatua nzuri. Naibu Waziri wa Uchukuzi,
Mhe. Dkt. Charles Tizeba alithibitisha hayo tarehe 1 Desemba, 2012
nilipotembelea bandari hiyo wakati wa ziara yangu ya Mkoa wa Lindi ya
tarehe 1 mpaka 5 Desemba, 2012. Hali kadhalika mipango ya kujenga
bandari ya Kilwa iko mbioni. Tena kwa upande wa Mkoa wa Lindi moja ya
makampuni yaliyogundua gesi baharini wameamua kujenga bandari na kituo
cha kuchakata na kusarifisha gesi nje ya mkoa huo kama ilivyo kwa
Mtwara. Naambiwa wametambua maeneo matatu, kilichobakia ni kuamua
mojawapo ili ujenzi uanze.
Ndugu Wananchi;
Nilipotoka bandari ya Mtwara, siku ile nilitembelea Chuo cha
VETA na kuzungumza na viongozi wa VETA taifa na wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi kuhusu kuwa na mitaala ya kutoa mafunzo mahsusi
yanayohitajika na sekta ya gesi na mafuta. Nilisisitiza kwamba
tuwapatie vijana wetu mafunzo yatakayowawezsha kuajiriwa na makampuni
ya gesi na yale yatakayokuwa yanatoa huduma kwa makampuni hayo.
Nilisema tusipofanya hivyo, makampuni hayo yataajiri watu kutoka nje
na hatutakuwa na sababu ya kuwalaumu wala kulalamika.
Nafurahi kwamba agizo langu hilo limefanyiwa kazi ipasavyo. Hivi sasa
katika chuo cha VETA Mtwara mafunzo hayo yanatolewa. Kampuni ya
PetroBrass ya Brazil inaendesha mafunzo ya sekta ya gesi kwa vijana 25
kutoka mkoani Mtwara. Aidha, chuo cha VETA kwa kushirikiana na
Kampuni ya Gesi ya Uingereza (British Gas) na Volunteers Service
Overseas ya Uingereza, kinatekeleza programu ya miaka mitatu iitwayo
Enhancing Employerbility Through Vocational Training. Programu hii
inalenga kutoa kozi zitakazowafanya wahitimu kuweza kuajiriwa katika
sekta ya gesi. Programu hii ilifunguliwa na Makamu wa Rais,
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, tarehe 26 Novemba, 2012.
Ndugu Wananchi;
Chini ya programu hii, walimu wa masomo yanayohusiana na gesi
wanaongezewa ujuzi ili waweze kufikia viwango vya kimataifa. Vile
vile, Wizara ya Nishati na Madini imetoa upendeleo maalum wa
kudhaminiwanafunzi 50 kutoka mkoa wa Mtwara kusoma chuoni hapo ambao
tayari wameshahitimu mafunzo ya msingi ya uunganishaji vyuma
viwandani. Mchakato wa kuwapatawanafunzi 50 kwa ajili ya mafunzo kama
hayo kutoka mkoa wa Lindi unaendelea. Nimeambiwa mpaka wameshawapata
vijana 25 bado 25.
Hali kadhalika, Wizara ya Nishati na Madini inadhamini
wanafunzi 10 kupata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambako kozi
za mafuta na gesi zinatolewa. Kipaumbele kwa udhamini huu unatolewa
kwa wanafunzi wa mikoa ya Mtwara na Lindi wenye sifa za kudahiliwa
katika mafunzo haya. Wamepatikana watatu. Wataalamu hawa na wengine
wa fani mbalimbali za gesi na mafuta watafundishwa kwa kiwango cha
shahada ya kwanza na baadae uzamili na uzamivu ili nchi yetu
ijitosheleze kwa wataalamu wa sekta hii.
Kupanga Mji wa Mtwara
Ndugu Wananchi;
Baada ya kutembelea bandari ya Mtwara na Chuo cha VETA,
nilikaa na kuzungumza na viongozi wa Serikali na Manispaa ya Mtwara.
Katika mazungumzo yangu nao niliwasisitizia umuhimu wa kuwa na mpango
kabambe wa kuendeleza mji wa Mtwara – (Mtwara Masterplan) Mpango ambao
utawezesha kujengwa mji mkubwa wa kisasa unaokidhi mahitaji ya mji wa
uchumi wa gesi. Niliwataka wahakikishe kuwa kuna maeneo ya viwanda,
biashara, makazi, mahoteli, huduma za afya, elimu, mapumziko na
burudani, viwanja vya michezo na kadhalika. Kazi ya kutayarisha
Masterplan hiyo imeanza na Manispaa ya Mtwara inashirikiana na Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Makazi.
Kwa upande wa uwekezaji nafahamu kuwa mpaka sasa makampuni 51
yameonyesha nia ya kuwekeza Mtwara katika viwanda, hoteli, shughuli za
uchukuzi na huduma hasa kwa sekta ya gesi. Wanachosubiri ni kutengewa
maeneo ya kujenga, waanze. Hivyo kukamilika mapema kwa Masterplan ya
mji wa Mtwara kutasaidia kuongeza kasi ya uwekezaji huu kufanyika.
Viwanda hivi vyote vitasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Mtwara na
Watanzania kwa jumla. Nimeambiwa kwa mfano, wakati wa ujenzi wa
kiwanda cha saruji watu zaidi ya 7,000 wataajiriwa.
Ndugu Wananchi;
Kabla hata ya ugunduzi wa gesi iliyoko baharini, tulikuwa na
mipango ya kutumia gesi ya Msimbati (Mnazi Bay) kwa ajili ya kuzalisha
umeme, kuzalisha mbolea na kutumika katika kiwanda cha saruji. Kwa
upande wa umeme kulikuwa na mpango wa kujenga mtambo wa kuzalisha
Megawati 300 kwa kushirikiana na mwekezaji binafsi. Bahati mbaya
wakati wa matatizo ya kifedha ya dunia mwaka 2009 mwekezaji huyo
akashindwa kupata mkopo, hivyo mradi ukasimama kutekelezwa. Haukufa
wala haukuhamishiwa Dar es Salaam au Bagamoyo kama ambavyo imekuwa
inapotoshwa kwa makusudi. Mradi huo bado upo, tena mpango wa sasa ni
kujenga Megawati 600zitumike Mtwara na zingine kuziingiza kwenye gridi
ya taifa kupitia Songea.
NduguWananchi;
Kwa upande wa kiwanda cha mbolea, wawekezaji wengi wameshajitokeza
tangu mwaka 2008 mpaka sasa. Mchakato umefanyika wa kuchambua
wawekezaji wenye sifa na kutambuliwa. Mambo mawili yamechelewesha
utekelezaji kuanza. Jambo la kwanza ni wawekezaji na kampuni ya
Artumas iliyokuwa mbia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(T.P.D.C) wakati ule, kushindwa kukubaliana nao juu ya bei ya kuwauzia
gesi. Wawekezaji walitaka bei ya gesi ipunguzwe, lakini kampuni ya
Artumas na T.P.D.C. hawakuwa tayari kupunguza zaidi ya kiasi
walichopunguza, ambacho wawekezaji bado waliona hailipi kwa kuzalisha
mbolea.
Sababu ya pili ni matatizo ya kifedha yaliyoikumba kampuni ya Artumas
katika kipindi hicho. Kufuatia machafuko ya masoko ya fedha na
mdororo wa uchumi wa dunia mwaka 2008/2009 kampuni ya Artumas
iliathirika na kulazimika kuuza hisa zake kwa wawekezaji wengine.
Katika kipindi hicho ilichopitia kampuni, mazungumzo na uwekezaji wa
kiwanda cha mbolea hayakuweza kupewa kipaumbele. Mtazamo wa sasa wa
wabia wapya na T.P.D.C. ni kuwa wao wenyewe sasa wawekeze katika
ujenzi wa kiwanda cha mbolea. Serikali imekubali rai yao hiyo na
wanaendelea na matayarisho.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kiwanda cha Saruji kitakachojengwa na kampuni
ya Dangote ucheleweshaji ulikuwa kwa sababu mbili. Kwanza, kampuni ya
Dangote iliomba eneo zaidi ya ililokuwa imeomba na kupewa. Hoja yao
ilikuwa kwamba eneo la ziada walilokuwa wanaliomba ndilo lenye
malighafi nyingi na bora kwa utengenezaji wa saruji. Hivyo, waliamua
kusubiri mpaka watakapopewa eneo hilo.
Bahati mbaya eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na mtu mwingine na
alikuwa na hati miliki nalo. Halmashauri ya Mtwara iliomba Serikali
eneo hilo litwaliwe na baadaye ipewe kampuni ya Dangote. Serikali
ilikubali. Hata hivyo, mchakato ulichukua muda na hata pale
ulipokamilika mwenye eneo aliupinga uamuzi wa Serikali Mahakamani.
Kesi ilichukua muda kusikilizwa na kumalizika. Bahati nzuri Serikali
ikashinda na mara baada ya uamuzi wa Mahakama ndipo kampuni ya Dangote
ikamilikishwa eneo hilo.
Kampuni nayo ilichukua muda kuanza. Hivi sasa, timu yake ipo kwenye
eneo na mradi uko tayari kuanza kutekelezwa. Niliambiwa kuwa katika
magari yaliyopigwa mawe katika fujo za Mtwara ni pamoja na lile la
mradi huu. Huo ndiyo ukweli kuhusu ujenzi wa kiwanda cha saruji cha
Dangote. Madai kuwa kiwanda hicho kimehamishiwa Bagamoyo si ya
kweli. Ni uzushi wa makusudi wa watu wenye nia mbaya na Serikali.
Huwezi kudai kuwa mtetezi wa wananchi wa Mtwara kwa hoja za uongo na
kufanya upotoshaji wa makusudi kabisa.
Ndugu Wananchi;
Ujenzi wa bomba la gesi ndiyo uliozua mzozo wote huu.
Zilijengwa hisia kuwa gesi yote inapelekwa Dar es Salaam na kwamba
Mtwara itakosa gesi na maendeleo yatayotokana na gesi hiyo. Na,
wengine wakasema gesi inapalekwa Bagamoyo ili kuzidisha chumvi na
kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali kwamba Rais anapeleka
gesi kwao. Kwanza, Kinyerezi iko Ilala na siyo Bagamoyo. Pili, ukweli
ni kwamba pale Mtwara kuna gesi nyingi ya kutosheleza mahitaji ya
Mtwara, Lindi na Dar es Salaam na kubaki. Gesi itakayoletwa Dar es
Salaam niasilimia 16 tu ya gesi yote iliyoko Mtwara kwa miaka ishirini
ijayo. Hivyo asilimia 84 ya gesi itabaki Mtwara kwa ajili ya kuuzwa
nje ya nchi na kupelekwa kwingineko nchini.
Kwa sababu hiyo, ndugu zetu wa Mtwara hawana sababu ya kuwa
na wasiwasi. Ipo gesi ya kutosha kwa mahitaji ya sasa na ya miaka
mingi ijayo. Viwanda vinavyotumia gesi kama mali ghafi na vile
vinavyohitaji gesi kama nishati vyote vitapata gesi ya kutosha. Kwa
upande wa uzalishaji umeme hali kadhalika ipo gesi ya kutosha
kuzalisha umeme mwingi zaidi. Hivi sasa tunacho kituo kinachozalisha
umeme wa megawati 15 unaotumika Mtwara, Lindi, Tandahimba, Newala,
Masasi, Nachingwea, Ruangwa, na Mtama. Bado umeme huo hautumiki wote
hivi sasa.
Ndugu Wananchi;
Nayaeleza yote haya kuwathibitishia wananchi wa Mtwara kuwa
tunawathamini sana na kuwajali. Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuwapuuza
na kuwatupa mkono wananchi wa Mikoa ya Kusini. Aidha, sitakuwa tayari
kuwaruhusu watu au mtu ye yote Serikalini kuwapuuza wananchi wa Mikoa
ya Kusini au mkoa wo wote hapa nchini. Hiyo haitakuwa sawa.
Nilishasema siku za nyuma na napenda kurudia tena leo kuwa kwangu mimi
hakuna mkoa ulio bora kuliko mwingine. Ni kutokana na msimamo wangu
huo ndiyo maana tumeelekeza nguvu na rasilimali nyingi za Serikali
katika mikoa iliyokuwa inadaiwa kuwa imesahauliwa. Kazi ya ujenzi wa
barabara za lami iliyofanyika na inayoendelea kufanyika katika mikoa
ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Kagera inajieleza yenyewe.
Mipango ya kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Mtwara kufikia hadhi ya
kimataifa na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Lindi na Kilwa ni
ushahidi mwingine kati ya mambo mengi tunayoweza kuyataja.
Ndugu Wananchi;
Haya niliyoyasema ni sehemu ndogo tu ya yale yaliyofafanuliwa
na kuelezwa kwa kina na Mawaziri na Wakuu wa Idara husika za Serikali
na Mashirika ya Umma pale Mtwara katika mkutano wa Waziri Mkuu na
viongozi wa Serikali, dini, vyama vya siasa na wazee wa Mkoa wa Mtwara
tarehe 29 Januari, 2013.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Waziri Mkuu,
Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya kule
Mtwara. Uvumilivu wake, usikivu wake na utulivu wake vimesaidia sana
kulivusha taifa katika moja ya mitihani mikubwa ambayo ingeikuta nchi
yetu tangu Uhuru. Nawapongeza Mawaziri na Wakuu wa Mashirika ya Umma
na Idara za Serikali kwa mchango wao muhimu walioutoa, uliosaidia
kufafanua masuala ambayo yalikuwa hayaeleweki vizuri. Kwa wao
nawasisitiza na kuwakumbusha wajibu wao wa kuelimisha jamii kuhusu
shughuli wazifanyazo. Wakifanya hivyo mara kwa mara migongano
haitakuwepo na wapotoshaji hawatapata nafasi.
Ndugu Wananchi;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawashukuru viongozi wa
Serikali, vyama vya siasa, madhehebu ya dini, viongozi wa jamii,
wazee, wana-Mtwara na makundi mbalimbali ya jamii, kwa muda waliotumia
kuzungumza na Waziri Mkuu na kuwasikiliza wasaidizi wake wakifafanua
masuala mbalimbali. Uvumilivu wao na uelewa wao ndivyo vilivyosaidia
kurejesha hali kuwa ya kawaida. Nawaomba nao sasa, wote kwa pamoja
washirikiane na Serikali kuelimisha umma kuhusu ukweli wa mambo. Pia
watumie nafasi hiyo kutahadharisha jamii na kuwataka watu kuwa
waangalifu na kupima maneno wanayoambiwa na watu. Wajiepushe na
maneno au vitendo vinavyofarakanisha, kuchonganisha na kupandikiza
chuki dhidi ya watu au Serikali. Waambieni kuwa ghasia hukimbiza
wawekezaji kwani wakipata hofu kuwa hali ya amani na usalama ni ya
mashaka, watatoka kwenda kuwekeza kwingine. Vyema iwe hapa hapa
nchini, lakini wanaweza kwenda nchi nyingine na sisi kupoteza kabisa.
Ndugu Wananchi;
Nawapa pole wananchi wa Mtwara na Masasi kwa usumbufu
walioupata kutokana na ghasia zilizofanywa. Nawapa pole waliofiwa na
kujeruhiwa. Nawapa pole waliopoteza au kuharibiwa mali zao. Kwa
kweli inasikitisha na kufadhaisha kuona watu wanafanya vitendo vya
kuua, kuchoma moto nyumba za watu na majengo ya Serikali pamoja na ,
kuharibu na kuiba mali za watu. Huu ni uhalifu ambao hauna maelezo na
haukubaliki. Tunaviachia vyombo husika vya dola na sheria kutimiza
wajibu wao. Kwa waliohusika iwe fundisho kwao na kwa wengineo
kutokubali kutumika kwa maslahi ya watu wengine siku zijazo. Sasa
wameachwa pekee yao wakati wenzao wako huru na kufaidi maisha
Ndugu Wananchi;
Hili sakata la bomba la gesi limefika mahali pazuri. Yaliyopita si
ndwele tugange yajayo.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni Sana kwa Kunisikiliza!
Source: http://www.wavuti.com/4/post/2013/02/hotuba-ya-rais-kikwete-ya-mwisho-wa-mwezi-wa-januari-2013.html#ixzz2JkbkOTwJ
No comments:
Post a Comment