Sunday, November 13, 2016

Mazishi ya Marehemu Mzee Richard Binagi Yafanyika Jijini Dar es Salaam

Mazishi ya Mzee Richard Binagi (88) aliyefariki dunia Jumanne Novemba 08,2016 Jijini Dar es salaam baada ya kuugua, yamefanyika jana Jumamosi Novemba 12,2016 nyumbani kwake Kipunguni Jijini Dar es salaam. Alikuwa askari mstaafu wa JWTZ.
Na BMG
Taratibu za kuuaga mwili wa Mzee Binagi zikifanyika
Askari wa JWTZ wakitoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Mzee Richard Binagi
Askari wa JWTZ wakiusindikiza malaloni mwili wa Mzee Richard Binagi
Gwaride la heshima
Gwaride la heshima
Askari wa JWTZ wakitoa heshima zao 
Wanafamilia (Profesa Lloyd Binagi na mkewe) wakiweka shada la maua
Wanafamilia (Mzee Chacha Binagi na mkewe) wakiweka shada la maua
Wanafamilia (Mama Binagi) akiweka shada la maua
Wanafamilia (Zakari Binagi na mkewe) wakiweka shada la maua
Wanafamilia wakiweka shada la maua
Wanafamilia wakiweka shada la maua
Wanafamilia wakiweka shada la maua
Wanafamilia
Wanafamilia
Wanafamilia
Ndugu, jamaa na marafiki
Bonyeza HAPA Kuhusu Msiba

Saturday, November 12, 2016

Kumbukumbu - Mh. Samuel Sitta Alipokutana na WaTanzania Cambridge, MA Mwaka 2014

Mh. Samuel Sitta akiwa nyumbani kwangu Cambridge, MA, USA
Siku ya jumamosi, 6/15/14 jioni, Mheshimiwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba na Waziri wa Afrika Mashariki​​, Mheshimiwa Samweli Sitta alikutana na baadhi ya viongozi wa Jumuiya za waTanzania wa New York na Massachusetts. Mkutano ulifanyika Cambridge, Massachusetts.  Katika mkutano huo Mh. Sitta aliongea kuhusu maswala ya Katiba na Uraia Pacha.  Pia aliongea kuhusu jinsi waTanzania wa diaspora watakavyoweza kusaidia kuijenga Tanzania. Mh. Sitta alikuwa Boston kwa ajili kozi fupi katika Chuo Kikuu cha Harvard.

Kwa picha na habari zaidi tembelea VIJIMAMBO BLOG. 


Kutoka Kushoto - Mr. Sangiwa, Mr. Temba, Dr. Malima, Mh. Sitta, Mr. Sangiwa, Mr. Tome, Mr. Mhellla, Chemi
Mh. Sitta akiwa mwingi wa furaha baadaya kuongea na WaTanzania mjini Cambridge, MA


Wananchi Wajeruhiwa Katika Ajali Iliyohusisha Magari Manne Kongowe Temeke jijini Dar es Salaam Leo

div class="separator" style="clear: both; text-align: center;">
 Wananchi wakiangalia ajali iliyohusisha magari manne na pikipiki iliyotokea daraja la Mzinga Kongowe, Temeke jijini Dar es Salaam leo mchana. Katika ajali hiyo watu kadhaa walijeruhiwa.
 Wananchi wakiangali basi dogo aina ya Coster ya abiria namba T 415 DCC ikiwa imeharibika vibaya baada ya kugongwa.
 Wananchi wakiwa eneo la ajali
 Wananchi wakiwa eneo la ajali.
 Ofisa wa Jeshi la Polisi akiwa eneo la ajali akichukua taarifa.
Prado yenye namba  T 177 AHH iliyohusika katika ajali hiyo.

Na  Dotto Mwaibale

WATU kadhaa wamejeruhiwa vibaya katika ajali iliyohusisha magari manne na pikipiki iliyotokea daraja la Mzinga Kongowe Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Ajali hiyo ilitokea saa sita mchana na kuhusisha magari hayo lori la mafuta aina ya Scania lenye namba T 617 AQQ, Coster ya abiria namba T 415 DCC inayofanya safari zake kati ya Kilwa Masoko na Mbagala, Prado yenye namba  T 177 AHH, pikipiki na lori jingine. 

Ofisa wa Polisi aliyekuwepo eneo la ajali ambaye alitambulika kwa jina moja la Emanuel alisema chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika.

"Nimefika sasa hivi bado hatujajua chanzo cha ajali wala watu waliopoteza maisha na kujeruhiwa" alisema ofisa huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Gilles Muroto alipopigiwa simu ili kuthibitisha ajali hiyo alikiri kutokea  hata hivyo alisema alikuwa hajapata taarifa kamili kutoka kwa Mkuu wa Kikosi cha Usalama wa Wilaya hiyo ambaye alikuwepo eneo la tukio.

Kwa mujibu wa mashuhuda walioshuhudia ajali hiyo walisema majeruhi walikimbizwa Hospitali ya Manispaa ya Temeke kwa matibabu.

The great escape.

Wimbo Mpya wa Kabago Akiwa na Harmad Tanzania Watoka Rasmi

Mkongwe wa Hip Hop nchini Kabago ameachia rasmi hii leo wimbo wake uitwao Tanzania akiwa na mkongwe mwenzake Hardmad, wimbo unaitwa Tanzania. 
Kupitia BMG sikiliza wimbo huo maana ni wimbo bora.
Bonyeza HAPA Kuupakua au bonyeza Play hapo chini kusikiliza.

Mh. Zitto Kabwe Amkumbuka Marehemu Mh. Samuel Sitta

Mh. Zitto Kabwe akiongea na Mh. Samuel Sitta nje ya Karimjee Hall Miaka ya Nyuma

Makala hii imeandikwa na Zitto Zuberi Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo

ALFAJIRI ya Novemba 7, 2016, tuliamka na kukutana na habari za kusikitisha ya kwamba mzee Samwel John Sitta, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametangulia mbele ya haki.

Mimi, kwa sababu ya heshima zangu kwake, nilikuwa nikimwita Babu. Ninafahamu kwamba alikuwa mgonjwa kwa kitambo kidogo akisumbuliwa na saratani ya tezi dume. Habari hizi zilisambaa kwa kasi kubwa kupitia mitandao ya kijamii. 

Hatimaye taarifa rasmi ikatoka kuthibitisha habari hizo.
Sitta aliitumikia nchi yetu kwa muda mrefu na kwa uadilifu mkubwa sana. Sisi wengine pia kwa kiasi fulani kukua kwetu kisiasa kumetokana na utumishi wake uliotukuka kwa nchi yetu alipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Babu yangu huyu ananigusa mimi binafsi moja kwa moja. Alikuwa mtu wangu wa karibu. Tukiwa bungeni akiniandikia kitu alikuwa akitumia neno hilo “babu” kwa mwandiko wake mzuri usiotoka kwenye kumbukumbu zangu kabisa.
Labda siku zijazo, ‘vi- note’ hivi vinaweza kuchapishwa pindi watafiti watakapokuwa wakiandika historia ya nchi yetu na Bunge letu.

Aliniapisha kiapo cha ubunge tarehe 29/12/2005. Maneno ambayo aliniambia baada ya kunikabidhi Kanuni za Bunge na Katiba ya Nchi niliyaandika kwenye daftari langu la kumbukumbu siku hiyohiyo jioni.

Baada ya kula kiapo cha Utii na cha Uaminifu, kawaida wabunge hupewa mkono na mwapishaji na kupewa nyaraka za kazi. Kwa upande wangu, Sitta alinikumbatia na kuniambia “ utakuwa kiongozi muhimu sana kwa nchi yetu. You have a bright future”.

Maneno haya hayajawahi kutoka katika kumbukumbu zangu na kila nikipata misukosuko yangu kisiasa huyakumbuka na wakati mwengine yeye mwenyewe alikuwa akinipigia na kunikumbusha na kunitia moyo. Babu alikuwa mlezi wa wanasiasa vijana.

Sitta pia naweza kusema amenilea kwa kunisomesha. Mwaka 1996 nilikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Galanos jijini Tanga nikisomea mchepuo wa Historia, Jiografia na Uchumi (HGE).
Hali ya hewa ya Tanga haikunipenda, hivyo nikawa naumwa umwa sana. Pia nilitaka kusoma Hesabu badala ya Historia.

Wakati wa likizo ya mwezi Disemba mwaka 1996, nilitoka Tanga nikaenda Dar es Salaam, Wizara ya Elimu kuomba uhamisho kwenda shule yenye Somo la Hesabu, kidato cha Tano na Sita.
Nikakataliwa. Lakini nikaambiwa kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari wakati ule, Alexander Ndeki, alisoma na Sitta. Kipindi hicho Sitta akiwa Mkurugenzi wa Investments Promotion Centre (IPC) kabla haijabadilishwa jina kuwa Tanzania Investments Centre (TIC).

Nikaenda ofisi za IPC mahala ambapo leo ni CRDB Tawi la Azikiwe. Nilipofika Katibu Muhtasi wake akaniuliza kama nina miadi na bosi wake, nikasema hapana. Akaniambia hawezi kukuona. Nikasisitiza sana na kumlilia dada yule aniruhusu dakika chache tu. Akaniruhusu.

Nilipofika Sitta aliniuliza shida zangu kwa heshima kubwa. Nikamwambia kwamba ninataka kuhama shule. Akaniomba matokeo yangu ya Kidato cha Nne, nikampa maana nilikuwa natembea nayo.
Alipoyasoma akaniambia, “ wewe hupaswi kuhangaika kutafuta shule maana kwa matokeo yako unaweza kusoma shule yeyote nchini ya chaguo lako”.

Akainua simu akampigia Ndeki. Kisha akaniandikia kikaratasi niende wizarani muda uleule. Nilipofika wizarani nikapewa uhamisho kwenda Shule ya Sekondari Mazengo.

Nilipotoka nje ya wizara, nikakutana na kijana mwengine anaomba uhamisho, yeye anatoka Mazengo anataka kwenda Tosamaganga, Iringa. Akaniambia, achana na Mazengo hakuna Mwalimu wa Uchumi na hali ya vyoo ni mbaya sana. Nikarudi kwa Mkurugenzi.

Mzee aliyenipa uhamisho aliponiona narudi na kumwambia sitaki Mazengo akachukua fomu zangu za uhamisho na akachukua ‘whiteout’ akafuta Mazengo na kuweka Tosamaganga huku akisema kwa hasira “ nyie watoto wa wakubwa bwana”.

Sikujali nikaenda zangu Tosa kusoma Uchumi, Jiografia na Hesabu (EGM). Tangu wakati huo, Sitta akaendelea kufuatilia maendeleo yangu shuleni hapo, kisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Taasisi ya InWent nchini Ujerumani.

Nilipotoka Ujerumani kusoma masomo ya Juu ya Biashara ya Kimataifa mwaka 2004, ilipaswa niwe na mradi wa kitaaluma. Nikachagua kuunganisha kampuni za Kijerumani na zile za Tanzania kwa kuandika mradi wa kuchukua wafanyabishiara 20 kutoka Tanzania na kuwaunganisha na wengine 20 kutoka nchi za Jumuiya ya Ulaya.

Ilibidi kupata Taasisi ya Tanzania kwa ajili mradi huo na Sitta akawa mstari wa mbele kuhakikisha mradi unafanikiwa na tukautekeleza kwa umakini kwa msaada wa afisa wa TIC aitwaye Phina Lyimo.

Mwaka mmoja baadaye, tukakutana na Sitta bungeni, yeye akiwa Mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki na mimi nikiwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini. Ulezi wake ukaendelea mpaka mauti yalipomkuta wiki hii. Nimempoteza Babu mlezi.
Sitta alikuwa mwana mageuzi (reformer) na kupitia uanamageuzi wake alifanya mabadiliko makubwa sana katika uendeshaji wa Shughuli za Bunge.

Sisi tuliohudumu kwenye Bunge la Tisa, tukimwita Spika wa Kasi na Viwango, tuliona wenyewe juhudi zake za kuliweka Bunge katika nafasi yake ya Kikatiba. Licha ya kuhakikisha kuwa maslahi ya wabunge yanakuwa yanayolingana na hadhi ya Bunge, alihakikisha pia kuwa Bunge linaisimamia Serikali sawasawa.

Haikuwa kazi rahisi sana kwani kulikuwa na mvutano mkubwa sana kati ya Spika Sitta na Waziri Mkuu, Edward Lowasa, katika kuleta mabadiliko hayo.

Tulikuwa tunaambiwa kuwa mvutano ule ulitokana na tetesi kwamba Sitta ndiye alipaswa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na hivyo kuwa na msuguano na aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo.
Sio Sitta wala Lowasa ambaye alithibitisha ama kukanusha tetesi zile. Sitta ametangulia mbele ya haki, labda Lowasa ataweza kusemea hili siku za usoni.

Sitta alitumia fursa ya msuguano huo kufanya mabadiliko makubwa ya kanuni za Bunge na kutoa uhuru mpana wa mawazo ndani ya Bunge na kuhakikisha kuwa Taarifa za Kamati za Bunge na hususan Kamati za Usimamizi wa Serikali zinakuwa zinasomwa na kujadiliwa ndani ya Bunge kwa mujibu wa Kanuni.

Wakati wa Bunge la Nane, taarifa za CAG hazikuwahi kusomwa hata mara moja. Ni kutokana na mabadiliko haya ya kanuni ndipo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC ) ilianzishwa mwezi Machi, mwaka 2008. Nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Kamati ile na kuingia kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo kipindi hicho tuliiona kama Kamati ya wabunge wazee.

Namna nilivyoingia kuwa Mwenyekiti wa POAC nayo ni hadithi nyengine ya namna ya malezi ya kiuongozi yaliyofanywa na Spika Sitta.

Sikuwa nimejaza fomu kuomba Kamati ya POAC. Wakati huo ulikuwa ni wakati wa vuguvugu la Buzwagi (Mkataba wa Madini uliosainiwa kwa siri na Waziri wa Nishati Hotelini nchini Uingereza ).
Nilikuwa mjini Bagamoyo kwenye kazi za Kamati ya Bomani nikiwa na Harrison Mwakyembe na Ezekiel Maige. Spika wa Bunge akanipigia simu, akaniambia “ Babu, kesho kuna uchaguzi wa Kamati za Bunge.

“Nimekuteua Kamati ya POAC ambayo ni kamati mpya itakayokuwa chini ya Kambi ya Upinzani. Najua hukuomba kuwa mjumbe wa kamati hii, lakini nahitaji damu changa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge.

“Naomba unikubalie na kesho uwepo Dar es Salaam kwa ajili ya uchaguzi na ugombee. Utashinda maana nimeshafanya kazi yangu”. Sikuwa na namna ya kukataa japo nilitaka sana kuendelea kuwa Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya Dk. Abdallah Kigoda, ama Kamati ya Nishati na Madini chini ya William Shelukindo.

Ombi la mzee ni amri. Nikawa Mwenyekiti wa POAC na kuwa mmoja wa washauri wakuu wa Spika wa Bunge. Kamati ya PAC ikawa chini ya John Cheyo na Kamati ya LAAC ikawa chini ya Dk. Willibrod Slaa. Ilikuwa ni Bunge lenye meno kwelikweli.

Sitta alikuwa mbabe. Ubabe wake ulimpelekea kufanya maamuzi ambayo wakati mwingine yalimweka kwenye matatizo na wananchi. Mfano mzuri ni suala la Hoja Binafsi ya Buzwagi na Hoja ya Wizi wa Fedha Benki Kuu ( EPA).

Mwanzoni, Spika alikuwa upande wa wabunge wenye hoja hiyo, mimi na Slaa kiasi cha kuziboresha hoja zile kwa kalamu yake mwenyewe. Wabunge wa chama chake hawakuwa wanapenda hoja hizi na hivyo Lowasa akamweka kwenye wakati mgumu sana wa kuegemea upande wa serikali.
Hoja ya Slaa akaitupa kuwa ‘ ni makaratasi ya kuokoteza’. Hoja yangu akaiingiza bungeni na akasimamia kusimamishwa kwangu Bunge.

Wananchi walimkasirikia sana. Siku moja usiku, nikiwa nyumbani kwa Freeman Mbowe Mikocheni, Samwel Sitta, akanipigia simu kulalamika kuwa wafuasi wangu wanamtukana kwa sms. Akaniambia niwakataze. Nilimkubalia tu, lakini sikuwa na uwezo huo.

Spika Samwel Sitta akawa ni Spika pekee wa nchi yetu aliyeshuhudia uundwaji wa Serikali mbili ndani ya miaka mitano ya Uspika wake. Mzee Msekwa yeye alikaa miaka 10 na Waziri Mkuu mmoja, ingawa mwaka 1993-1995 naye aliona mabadiliko ya Mwaziri Wakuu, kutoka John Malecela kwenda kwa Msuya.

Baada ya kujiuzulu kwa Lowasa, Sitta hakurudi nyuma tena. Aliendelea kuwa Spika wa viwango mpaka alipomaliza muda wake katika Bunge la Tisa.
Spika Sitta alikuwa mwepesi kuomba msamaha alipokosea.

Nakumbuka siku moja mwaka 2009 alimfukuza bungeni Cheyo kwa makosa ambayo mzee Cheyo hakufanya. Baadhi yetu tukakasirishwa na kitendo kile.

Nikaenda kumwona Sitta ofisini kumwuliza kulikoni amdhalilishe mwenzake namna ile. Akanieleza kuwa hakuwa sawa na atamwomba radhi Cheyo.

Tukiwa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge, kwa ajenda zake za kawaida tu, Sitta akamwomba radhi Cheyo. Nikikumbuka kisa hiki nacheka sana maana Jaji Frederick Werema aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alicheka mpaka kuanguka chini. Sababu?

Sitta aliketi kwenye kiti chake, wenyeviti wote wa Kamati tukiwa tumetulia tuanze kikao. Mzee Sitta akasema “ John, naomba radhi kwa tukio lililotokea bungeni wiki iliyopita.
“Sijui nilikuwa nina nini siku hiyo, nadhani nilisumbuliwa na watu wanaopitapita jimboni kutaka kunitoa, nisamehe mzee mwenzangu”.

Baada ya maneno hayo ukumbi mzima ulitawaliwa na vicheko na Cheyo akamkubalia radhi yake huku naye akicheka na yakaishia hapo. Wazee hawa wawili wameandika pamoja kitabu “ Bunge lenye Meno”. 

Nimwelezeje zaidi Babu? Nimwelezeje zaidi Spika huyu wa Kasi na Viwango? Mwanasiasa shupavu, jasiri, mwenye ngozi ngumu, mbabe, mnyenyekevu inapobidi na mwenye uthubutu.
Tangulia Babu. Tangulia Mtemi wa Unyanyembe Samwel John Sitta. 

Raia Mwema

Miss Tanzania 2010, Genevieve Mpangala Kusaidia Kurejesha Heshima ya Elimu Tabora

Mrembo wa taji la Miss Tanzania 2010 Genevieve Mpangala amejitosa kusaidia kurejesha heshima ya mkoa wa Tabora katika elimu hasa kwa wasichana ambao ndio nguzo kubwa kwa familia na maendeleo ya taifa.

Mrembo huyo ameamua kufanya hivyo kwa kutembelea shule mbili za Tabora Girls na Isevya kuongea na wanafunzi, kuwapa moyo na kuangalia matatizo yanayowasumbua katika kujipatia elimu.

Akizungumza na Moblog amesema kwamba amekuwa na masikitiko makubwa na matokeo ya mitihani ya kitaifa ya sekondari kwa miaka mitatu ilhali simulizi za Tabora miaka iliyopita ni za kufurahisha sana uikionesha kwamba mkoa huo ndio kitovu hasa cha elimu.

Anasema ukisoma nyaraka mbalimbali unaona jinsi Tabora ilivyokuwa ngome ya elimu huku watanzania wengi wakifika hapo pia kupata elimu ya sekondari.

Mrembo wa taji la Miss Tanzania 2010, Genevieve Mpangala akizungumza wa shule ya sekondari Tabora Girls hivi karibuni.

“Kwa kweli pamoja na masimulizi mazuri kuhusu elimu Tabora miaka ya 80 na 90 ,nilichagua Tabora girls kwa sababu ni shule aliyosoma mama yangu mzazi form 1 mwaka 1977 mpaka 1980 mpaka na aliisifia sana shule yake hiyo na nikapenda niweze kuwa karibu nao kuhakikisha wanafunzi wote wanamaliza,na Isevya ilikua chaguo la pili kwasababu ilikua ni shule ya kutwa (day) na nilipendelea kuongea na wanafunzi hao” alisema Genevieve.

Mkoa wa Tabora ambao unapatikana kati ya Magharibi ya Tanzania kwenye uwanda wa latitudo 40-70 Kusini na longitudo 310 - 340 mashariki ukipakana na mikoa ya Shinyanga, Katavi, Singida, Kigoma na Dodoma ni mji ulioanzishwa na wafanyabiashara wa Kiarabu kwenye miaka ya 1850 ukijulikana kama Kazeh .

Kihistoria Kazeh ambayo ilikuwa kitovu cha biashara ya utumwa, mwaka 1871 robo ya mji ilichomwa moto na kuvurugwa na mtawala wa wanyamwezi Mirambo .

Ingawa mwaka 1885 hadi 1891 wajerumani walijaribu kutawala, historia zinasema kwamba mji huo ulikuwa na vurugu kubwa lakini baadae ukatawaliwa na wajerumani wakafanya mji wa utawala kabla ya vita kuu ya kwanza kuingia na wao kung’olewa.
Mrembo wa taji la Miss Tanzania 2010 Genevieve Mpangala akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi na mwalimu wao alipofanya ziara shuleni hapo.

Pamoja na historia yenye misukosuko ya Mkoa wa Tabora ambao ni moja ya mikoa yenye eneo kubwa unategemea sana kilimo kufanikisha maisha lakini kwa miaka mingi mkoa umekuwa ukididimia kimaendeleo na kijamii.

Mkoa wa Tabora ambao umekua wa mwisho kwa miaka mitatu mfululizo mwaka 2013,2014 na 2015 unahitaji nguvu kubwa ya kujiondoa katika shida ya kuporomoka katika elimu

Mrembo Genevieve anasema ziara yake katika shule hizo imemfumbua macho na kuona haja kubwa ya kuendelea na programu za kufufua matumaini.

Pamoja na kuwashukuru walimu kwa ushirikiano waliompa aliwataka wanafunzi kuweka mkazo katika imani, matumaini na kutekeleza ndoto zao katika uwanda mkubwa zaidi.
Aidha pamoja na kuzungumza "HAVE FAITH,HOPE FOR MORE AND DREAM EVEN BIGGER", pia aliwaasa kuwa elimu ni msingi mzuri wa maisha na kuwa wasiharakishe na kupotoshwa na mambo ya kidunia kwani haya maisha yapo.

Akiwa na wasichana wa shule ya Tabora Girls walimweleza changamoto wanazokutana nazo ikiwa ni pamoja na kutokuwepo na uzio kwenye shule yao hiyo, uhaba wa vitabu, upungufu wa walimu, uhaba wa upatikanaji wa habari mubashara, kwa wanafunzi kwamba hawana king'amuzi,kwa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi wanauhitaji wa msaada wa kofia pamoja na mafuta ya kuwakinga na jua.

Matatizo hayo yanatokana zaidi na kwamba wengi wao wanatoka kwenye mazingira duni. Changamoto nyingine ni pamoja na kuwa na zahanati ambayo ina uhaba wa vifaa mfano:vyandarua vya kutosha pamoja na vitanda,pia kwa wanafunzi ambao wanaulemavu wa macho ambao ni hafifu na vipofu kabisa hivyo kuna uhaba wa brail paper.

Ziara fupi ya Mrembo wa Tanzania 2010 Genevieve Mpangala kwa shule mbili za jijini Tabora za Isevya Secondary School na shule ya vipaji maalum ya wanawake Tabora girls.

Amesema katika mazungumzo yake na wanafunzi hao amebaini pia kwamba kutofanya vyema kwa wanafunzi pia kunasababishwa na wanafunzi hao kutumia madawa ya kulevya, utoro, mimba za shuleni na wazazi kuozesha mabinti katika umri mdogo kabla ya wao kumaliza shule.

Saturday, November 05, 2016

Shamba la Miti Lunguza Wazipiga Jeki Shule ya Msingi Muheza Wakabidhi Madawati 200

SHAMBA LA MITI LUNGUZA WAZIPIGA JEKI SHULE ZA MSINGI MUHEZA WAKABIDHI MADAWATI 200.

Mkuu wa wilaya ya Muheza,Hajat,Mhandisi Mwanasha Tumbo kulia akipokea madawati 200 kutoka kwa Meneja wa Shamba la Miti Lunguza, yaliyotolewa na wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) Abdallah Mchomvu katika halfa iliyofanyika leo

 Mkuu wa wilaya ya Muheza,Hajat,Mhandisi Mwanasha Tumbo wa kwanza kulia mwenye hijabu akikagua madawati hayo kabla ya kuyapokea anayefuata ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Muheza,Kahoza Joseph ambaye ni Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri hiyo
 Mkuu wa wilaya ya Muheza,Hajat,Mhandisi Mwanasha Tumbo wa kwanza kulia mwenye hijabu akitazama baadhi ya madawati hayo kabla ya kuyapokea anayefuata ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Muheza,Kahoza Joseph ambaye ni Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri hiyo
 Meneja wa Shamba la Miti Lunguza,Abdallah Mchomvu akizungumza katika halfa hiyo ya kukabidhi madawati kwa Mkuu wa wilaya ya Muheza,Hajat,Mhandisi Mwanasha Tumbo wa kwanza kushoto aliyekaa ambayo yaliyotolewa na wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS)
 Kaimu Katibu Tawala wa wilaya ya Muheza ambaye ni Afisa Tarafa ya Muheza Khatibu Omari wakati wa halfa hiyo wa pili kutoka kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Muheza,Hajat,Mhandisi Mwanasha Tumbo
 Baadhi ya wafanyakazi wa shamba la miti la Lunguza ambalo ni la serikali linalojishughulisha na uhifadhi wa misitu ya asili na ustawishaji wa miti ya misaji (Teak)
Baadhi ya madawati yaliyokabidhiwa leo kwa Mkuu wa wilaya ya MuhezaHajat,Mhandisi Mwanasha Tumbo ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na upungufu wa madawati kwenye shule za msingi wilayani humo. Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha.

FIlamu na Tamthilia za Kitanzania Zazinduliwa Jijini Dar es Salaam - Zitarushwa na DSTV

Mwenyekiti wa Bodi ya DSTV, Balozi Ali Mpungwe akizungumza wakati wa uzinduzi wa Filamu na Tamthilia za Kitanzania zitakazorushwa na DSTV kupitia Chaneli yao kuanzia Maisha Magic Bongo Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam jana.
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza wakati wa uzinduzi huo.
 Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fissoo akizungumza katika uzinduzi huo kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Mtendaji Mkuu wa Multchoice, Chande Maharage, akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Mkuu wa Chaneli ya Maisha  Magic Bongo, Barbara Kambogi akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Mkurugenzi Mkuu MNET, Yalisa Phawe akitoa hutuba fupi katika uzinduzi huo. Kulia ni Mkuu wa Chaneli ya Maisha  Magic Bongo, Barbara Kambogi.
Wadau wa filamu wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Viongozi mbalimbali walioshiriki uzinduzi huo.
Wasanii wa filamu na wadau mbalimbali wakiwa kwenye 
uzinduzi huo.
Taswira katika uzinduzi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (katikati) na viongozi wengine wakizindua Filamu na Tamthilia za Kitanzania.

Na Dotto Mwaibale

TANZANIA imeingia katika mapinduzi makubwa ya tasnia ya filamu baada ya Maisha Magic Bongo kwa kushirikiana na Multchoice Tanzania pamoja na maprodyusa kuzindua rasmi chaneli yao (160) Maisha Magic Bongo itakayo kuwa ilirusha filamu na tamthilia za kitanzania.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa filamu na Tamthilia za kitanzania kwa niaba ya Waziri  wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambaye alikuwa mgeni rasmi, Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fissoo alisema mpango wa kurusha filamu za kitanzania kupitia mtandao wa DSTV utasaidia sana kutangaza filamu zetu na kuleta ushindani katika ulimwengu wa kimataifa.

"Serikali tunaona hili ni jambo muhimu sana litakalowafanya wadau wa kazi za kitanzania kutabasamu tena kwani sote tunafahamu umaarufu wa chaneli zilizopo DSTV na jinsi zinavyoweza kuwafikia watu wengi duniani" alisema Fissoo.

Aliongeza kuwa uzinduzi huo uliohusisha filamu sita, tamthilia mbili na kazi nyingine mbili DSTV wametoa mtaji wa dola za kimarekani 450,000.

Mkuu wa Chaneli ya Maisha  Magic Bongo, Barbara Kambogi alisema uzinduzi huo umelenga kusherehekea kazi nzito za maprodyusa wa filamu hapa nchini na utambulisho rasmi wa chaneli yetu yenye maudhui ya kitanzania.

Alisema chaneli hiyo imelenga kuburudisha na kuelimisha watamazaji wa kitanzania kupitia filamu, tamthilia na maigizo mbalimbali ya kiswahili.

Aliongeza kuwa chaneli hiyo itapatikana kwenye kifurushi cha huduma za DSTV (160).


Mwenyekiti wa Bodi ya DSTV, Balozi Ali Mpungwe alisema DSTV Tanzania imetoa ajira 80 hivyo kusaidia katika maendeleo ya nchi.

Mtendaji Mkuu wa Multchoice, Chande Maharage alisema mpango huo utasaidia kukuza lugha ya kiswahili kama alivyokuwa akifanya mtunzi wa mashairi hayati marehemu Shabani Robert katika kukuza lugha hiyo.


Mh. Pinda Atembelea Makao Makuu ya CCM, Lumumba

 Wazuri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara, Rajab Luhwavi alipotembelea Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, jana.  Kushoto ni Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka.
 Wazuri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda akisisitiza jambo wakati akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara, Rajab Luhwavi alipotembelea Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam
Wazuri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara, Rajab Luhwavi alipotembelea Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, Kushoto ni Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, na kulia ni Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Pindi Chana. (Picha zote na Bashir Nkoromo).