Monday, February 26, 2007

Sinema ya 'Maangamizi' itaonyeshwa Toronto, Canada March 9th


Mimi na-acti katika hiyo sinema kama Nurse Malika. Karibuni Kwa habari zaidi kuhusu sinema ya Maangamizi: the Ancient One, bonyeza hapa. http://www.grisgrisfilms.com

***********************************************************************************

Friends of Alternative and Complementary Therapies presents a special screening of Maangamizi: The Ancient One on Friday March 9th, 2007.


This multi-award-winning film about healing trauma from a traditionalAfrican perspective is a Tanzanian-U.S. co-production (2001), co-directed by Martin Mhando and Ron Mulvihill and executive produced by Jonathan Demme.According to American author Alice Walker, "MAANGAMIZI - The AncientOne...is more than a movie. It is a look at how we've been torn at our roots; severed from nourishment at the source...Those of us who can remember and honor who we have been over eons of time, will be able to inspire the whole world to greater heights of compassion."


This powerful film about the role ancestor spirits play in healing will be followed by a panel discussion , moderated by Cameron Bailey, film critic and programmer of Planet Africa for the Toronto International Film Festival.


Panel members include: Ainajugoh Taylor is a traditional African healer from Sierra Leone who is currently helping the government of her home country draft legislation to formally recognize and register traditional healers there according to WHO criteria. She is also a recipient of the Michael Clemons Community Leadership Award for such activities as introducing live African music to Toronto and establishing the health-care team that lobbied the College of Physicians and Surgeons to acknowledge the credentials of foreign graduates in medicine and nursing.


Rebecca Rogerson, born in Toronto, was trained in Soweto, South Africa and is a registered sangoma. After 10 years of work in Southern Africa, she returned to Toronto where she continues her practice as a traditional healer and pursues graduate studies in medical anthropology.


Dr. Ted Lo is a community psychiatrist, Assistant Professor consulting to the Culture, Community and Health Studies Program at the University of Toronto.


When: Friday, March 9th at 7:30 p.m.


Where: Workman Theatre, CAMH 1001 Queen St. W. at OssingtonTickets: $10 (book early to reserve a seat)


Advance Tickets: Send cheque to FACT, 375 Bay Mills Road, # 516, TorontoOn M1T 2G6Payment must be received by Friday, Feb. 23, 2007.


Same day Tickets go on sale at the Workman theatre 30 minutes prior to the screening.For more information, call FACT 416-299-5113 or see http://www.the/ facts.orgFor further details, please see the attached poster. And thanks for passing this on to anyone else who might be interested.FACT is a non-profit

Tuesday, February 20, 2007

Marudio - Wapenzi wa Matako Makubwa



Naona blog ya 'Matako Makubwa' ilikuwa na hits nyingi sana, nilibandika kwanza 12/2005. Hivyo nimeamua kuirudia.

Nimesikia wazungu wakisema hiyo kupenda matako makubwa eti ni 'cultural thing' kwa watu weusi, na hawajakosea. Ni mila na desturi ya mwafrika kupenda matako makubwa. Na kuyasifia. Hata wengi wa waMarekani weusi wanapenda mpaka kutunga nyimbo za 'bootylicious'. Huwa nacheka nikiona mzungu anasifia mwanamke ambaye huko nyuma kapigwa pasi. Yaani fleti. Lakini kuna wesui ambao wamekuwa 'zungunized' na wanapenda matako fleti. Shauri zao!

Matako Makubwa Oyee!



************************************************************************

From my 12/2005 Blog:


Wapenzi wasomaji, leo nimeamua kuzungumzia suala ya matako makubwa. Tafadhali msione kama ni matusi lakini hapa USA ni issue kubwa, maana watu wanayachukia!

Nimeona nizungumzie suala ya matako makubwa kwa vile jana kazini, mzungu aliyekondeana mno kasema ni mnene na akila keki eti yote itaenda matakoni. Nilishangaa na kusikitika sana.Uzuri kwa wazungu ni kuwa na matako fleti kama vile yamepigwa pasi. Sijui kwa nini. Mtu anashepu ya mbao, mwanamke hana hips kakaa kama dume vile eti ndo uzuri. Kumbe ni kwa sababu hao models na wacheza sinema wako hivyo!

Basi wasichana na akina mama wanajinyima chakula kusudi wakonde na eti wapendeze. Ndo maana magonjwa kama Bulimia na Anorexia zimeshamiri hapa. Lakini ukitazama sinema za miaka ya nyuma kama za 1930's na 1940's, wanawake walikuwa na shepu na walikuwa wamejaa na hata wanaume wa kizungu walikuwa wanasifia. Mpaka 1950's kulikuwa na mcheza sinema Marilyn Monroe, alikuwa na zinga la figure 8, na wanaume wote walikuwa wanampapatikia. Ama kweli mambo yanabadilika. Hivi sasa wanasema eti walikuwa ni obese yaani wanene!

Mbona mimi naona matako fleti kama chapati ni mabaya na hayapendezi? Au ni kwa sababu nimekulia Africa? Brothas (waMarekani Weusi) wanapenda mwanamke awe na matako ya maana! Akipita mwanamke mwenye mbarikio utasikia brothas wakisifia, "umm, umm umm!" Kuna siku nilisikia wanaume wa kizungu wakijadili sababu ya wanaume weusi kupenda matako makubwa, walisema ni "cultural thing". Kwa kweli ni culture yaani utamaduni! Kama umekulia katika mazingara ya kupenda kitu utakipenda. Na ndo maana kuna weusi USA wanataka kuwa na shepu iliyokondeana kama mzungu kumbe haiko katika 'genes' zake. Wajitahidi kupunguza mzigo lakini wapi, iko pale pale.

Sisi wanawake wenye asili ya Afrika tumebarikiwa huko nyuma. Yaani boxi, siha, wowowo, booty, na nasikia waGhana wanaita yokohama, matako makubwa yana majina mengi. Waafrika tunaona kama ni urembo, lakini wazungu na waliokulia uzunguni wanaona kinyaa. Wanasema eti ni dalili ya ulafi na uvivu! Lakini kama ni dalili ya ulafi mbona hata mwanamke mwembamba mwafrika anaweza kuwa na kamzigo huko nyuma?

Ubaya mwenye matako makubwa anaweza kubaguliwa kwa vile bosi anaweza kuona kuwa ni 'ugly' (mbay) na mwenye nacho anachafua mazingira ya ofisi. Kweli kabisa!Hayo matako makubwa ni 'genes' za sisi waafrika. Lakini ajabu kuna siku nilisikia wazungu wakisema eti waafrika tuna matako makubwa kwa sababu ya utumwa. Eti mabibi zetu walinyimwa chakula hivyo matako ndo ilikuwa 'godown' ya mafuta ya akiba. Nadhani ni uzushi kama ile ya ngamia kuweka maji kwenye nundu zake!

Mimi mara nyingi nimeambiwa nina matako makubwa, niyapunguze kwa kwenda gym kufanya mazoezi. Hayo mazoezi haisadii kitu ni makubwa vile vile! Lakini msione kama naona haya, wala! Mtu akiniambia nina matako makubwa namwambia mbona kama ni madogo, na ningependa yawe makubwa zaidi! Wanabakia kushangaa hasa nikiwaambia kuwa Afrika, matako makubwa ni uzuri.Na amini usiamini kuna opresheni ya kuyapunguza inaitwa Liposuction. Wanawake wengi weusi na wazungu wamefanya hiyo liposuction ya matako, akiwemo mwimbaji Janet Jackson. Ubaya, ni kuwa ukishafanya hiyo liposuction, mafuta yataenda kwingine mwilini, hivyo utakuwa na shepu ya ajabu!

Sisi waafrika tunapenda kuringia huo mbarikio wa matako makubwa. Nilipokuwa nacheza ngoma shuleni na jeshini, tulikuwa tunatia nguo ndani ya bukta kusudi tuonekana na matako makubwa kweli kweli! Lakini, mara nyingi mitaani hapa USA, nimesikia akina dada wakifokewa, "You got a big a-s!" Kuna siku nilikuwa kwenye kituo cha Subway hapa Boston, kapita mama fualni Mganda, aisei alikuwa amejaliwa kweli huko nyuma, mpaka nikaona wivu. Basi ungeona wazungu walivyokuwa wanamtazama kwa mshangao ungecheka. Ila nilishuhudia baba fulani Mmarekani Mweusi akimtazama kwa furaha na kawa kama vile anamezea mate.

Nampenda sana mecheza sinema, Whoopi Goldberg. Nilikuwa nasoma jinsi akienda kwenye audition au akiwa kwenye movie shoot, wazungu wanamwambia kuwa ana matako makubwa au avae nguo ya kuzificha. Yeye alichoka, na mwishowe kusema, " Mimi ni mwanamke mweusi, nina matako makubwa niache kama nilivyo!" Wanawake wote tungedai heshima kama Whoopi nadhani wazungu wangeheshimu matako yetu makubwa.

Tatizo linigine la kuwa na matako makubwa USA ni kupata nguo. Ukienda kununua sketi au gauni uanweza kukuta mbele refu nyuma umepanda. Au unavaa hiyo nguo lakini kwenye hips na matako haipiti! Hii ni kwa sababu nguo imeshonwa kwa ajili ya wazungu wenye matako fleti. Na kupata Jeans inayofiti ni vigumu. Mtu ambaye atatengeneza nguo 'molded for the black woman' atapata wateja kweli kweli, maana tunalilia nguo kama hizo.

Pamoja na yote haya sasa wazungu wameibuka na staili ya kuwa ka ka-butt. Yaani jeans inakuwa na pedi ndani kusudi mtu aonekana ana matako. Loh! Watu hawaridhiki! Sijui tuseme asante J-Lo (mwimbaji Jennfier Lopez) au nini. Kwanza walikuwa wanamcheka J-Lo na matako yake makubwa lakini naona watu wanaanza kuyapenda. Mpaka kuna opresheni sasa ya kuongeza matako. Wacha wafanye haitapendeza kama matako natural tulyiozaliwa nayo waafrika.

Matako Makubwa Oyee!

Sunday, February 04, 2007

Leo ni SuperBowl - Wanaume wanakuwa Wajinga!

Leo ni siku ya SuperBowl. Yaani msimu wa mchezo wa football unaisha leo. Wanaocheza ni timu za Chicago Bears na IndianapolisColts. SuperBowl inachezwa mji ambayo haina uhusiano na timu wanazoshindana, maana lazima watu wangeuana. Mwaka huu inachezwa Miami, Florida.

Mimi siyo mshabiki wa football wa Marekani. Naona kama wanaumizana, kazi kuangushana. Mara unaona mtu kazolewa kavunjika mguu, mkono au mgongo!

Lakini wanaume hapa USA wanaipenda kweli. Mpaka wasichana wanaotafuta wapenzi, mume wanaambiwa wajifunze kuelewa huo mchezo na itakuwa rahisi kumpata!

Lakini nacho shangaa ni hivi, wanaume wanakuwa wajinga hawajali nini zaidi ya mambo ya hiyo SuperBowl. Wengine wananua tiketi za kwenda huko na mshahara wa miezi kadhaa, mradi wanaenda. Pia TV Kubwa kubwa zinauzwa sana kipindihiki, wanunuzi wakuu wanaume wanaotaka kuangalia Superbowl.

Magazeti, na TV wanaongea habari ya SuperBowl tu mpaka inachosha. Ukienda Grocery store, (dukani) unakuta wanaume wamejaa huko wananunua vyakula vya party kama potato chips, nachos, salsa, chicken wings, cold cuts platters, vinywaji kama soda na bia na nyama za kufanyia barbecue. Hata kwenye baridi unakuta wanaume wako nje wanafanya barbecue. Kwenye football wanita ‘tailgating’

Ajabu wikiendi ya SuperBowl kunakuwa na seli nzuri ya chakula. Mameneja huko Corporate Offices wanakuwa na huruma na kuwapunguzia bei nini? Halafu kila sehemu utasikia kuna SuperBowl party hata majumbani mwa watu. Mabaa zenye TV zinafanya kazi nzuri kweli siku ya SuperBowl.

Niliuliza akina mama wa kizungu kwa nini wanaume wanapenda sana SuperBowl na kupika wao wenyewe siku hiyo. Wakasema ni siku ya mwanaume kuonyesha kuwa ni mwanaume bila kujali wanawake. Haya SuperBowl ikisha watatukumbuka sisi wanawake.

Mama moja kaniambia habari ya chakula fulani wanachopika hao tailgaters, inaitwa jambalaya. Hicho chakula kina wali, sausage, nyanya, vitunguu, pilipili hoho, na viungo kadhaa. Halafu wanatia vipande vya nyama ya kaa. Eti hiyo kaa inaongeza ladhaa. Ukweli eti ina harufu kwa uke wa mwanamke, ndo maana wanaishangalia. Unaona wanaume wananusa halafu wanshangalia. Fikiria mbuzi beberu anvayotanua tanua pua akitaka mambo. LOH!

Hapa Boston timu yetu New England Patriots, hawakufanikwa kwenda. Mbona wanaume walilia machozi walivyoshindwa! Haya tuone nani atashinda Colts au Bears. Na kwa mara ya kwanza timu zote mbili zina kocha mweusi.

UPDATE- Washindi ni INDIANAPOLIS COLTS

Score ilikuwa 29-17.


Huwezi kujua ajali itatokea lini

Ajali ni ajali. Hupangi itatokea lini au itatokea nini. Ukweli ukiamka huwezi kujua Mungu au shetani amekupangia nini siku hiyo.

Zaidi ya wiki mbili zilizopita nikiwa nakwenda kazini nilianguka kwenye ngazi za subway Central Square hapa Cambridge. Hata sikumbuki vizuri ilikuaje, sikuwa nakimbia wala kuwa na haraka, mwendo wa kawaida tu. Nilikuwa nateremka kwenda kwenye geti kusudi nisubiri treni. Ghalfla nilianguka, kwa bahati kuna ile sehemu pana ya katikati ndo nikaishia hapo na sikwenda chini kabisa. Ngazi zenyewe zimechongwa na mawe. Loh, magumu! Baada ya kuanguka nilishindwa kuinuka. Nikasema hayo ni malipo kwa ajili ya kucheka uile tangazo ya bi kizee akisema, “I’ve fallen and I can’t get up!) (nimeanguka na siwezi kuinuka), japo sijaiona miaka mingi. Mzungu mwanaume aliyekuwa anapanda zile ngazi alinisaidia kuinuka. Alivyokuwa ananinsaidia nikasikia maumivu makali kwenye mguu na kushindwa kutembea kabisa. Nikamwambia nadhani nimevunjika mguu. Huyo mzungu alipiga simu polisi, na polisi kaja, halafu wakaamua kuniitia ambulance.

Wale EMT (Emergency Medical Technicians) walinipakia kwenye kiti maalum ya wagonjwa na kunibeba mpaka kwenye stretcher barabarani ndo wakanipakia kwenye ambulance. Nikapelekwa hospitalini donidoni ikiwa inalia.

Basi mle ndani nikawa nalia. Niliamka mzima, sasa nimevunjika mguu! Nikawaza je, ningechelewa kidogo ningeanguka, je, ninegwahi kidogo ningeanguka? Je, nitakuwa mzima tena, je, nitaweza kucheza densi tena? Nikasema nina bahati lakini maana kuna wengine wanapata ajali ya gari na wanakufa. Au wanakatika kiungo. Fkiria mtu unaagana na mpenzi wako mtaonana au mtapigiana simu baada ya muda kadhaa, halafu simu inapigwa, mwenzako kapata ajali. Nilikuwa na mawzao mengi lakini nilishukuru kuwa sikumia kiasi cha kupoteza fahamu.

Hospitalini walinihudumia mara moja. Nilikuwa nimevaa suruali, walivyopandisha wakaona kuwa ngozi imechunwa kwenye gotii. Nilibakia kushangaa maana suruali haikuchanika. Baadaye walinipeleka X-ray. Bahati nzuri hakuna mfupa iliyovunjuika lakini nilikuwa nimeumia misuli tu kwenye goti. Wakanipa magongo, na madawa ya kupunguza maumivu na nikaenda zangu nyumbani kwa teksi. Nilikosa kazi siku mbili na bahati nzuri wikiendi ikaja. Nikapata nafasi nzuri ya kumpumzika. Baada ya hapo ikabidi nirudi kazini na magongo. Na mjue huko kwenye treni hakuna aliyenipisha kiti hata waliokaa viti maalum vya wagonjwa. Wengine wanakuaona halafu wanajidai wanasoma gazeti.

Lakini nashukuru sikuumia zaidi, na daktari kasema baada ya wiki kadhaa maumivu yatakwisha kabisa. Namshukuru Mungu kuwa sikuumia zaidi.

Tuesday, January 16, 2007

Ndoto inaweza kutokea Kweli!




Mimi nimewahi kuota kuwa natuzwa Oscar. Nilivyoamka ilibidi nicheke. Nikasema haiwezekani nituzwe hiyo Oscar, kwanza weusi huwa hawatuzwi, na pili nani atanipa nafasi ya kuigiza kwenye sinema itakayonipa nafasi hiyo.

Lakini jana nimeamini kuwa ndoto huwa inaweza kutokea kweli. Baada ya kuona, Jennifer Hudson, kashinda Golden Globe Award kama Best Supporting Actress. Ijumaa alishinda Critics Choice Awards na sasa watu wanasema anastahili Oscar. Mwaka jana saa hizi nani alitegemea kuwa leo, Jennifer angekuwa Superstar? Ni sinema yake ya kwanza kuigiza, na pia mwaka 2004, alishindwa kwenye mashindano ya American Idol….kama utakumbuka Fantasia Barrino alishinda mwaka ule. Jaji Simon Cowell, alimwambia kuwa hata fika mbali na uimbaji. Kwa kweli nilisikitika sana siku hiyo alivyotolewa kwena AI, maana nilijua Jennifer ana kipaji.

Mungu ni mwema. Akifunga dirisha anafungua mlango. Jennifer kapata nafasi ya kuwa kwenye sinema ya Dreamgirls. Jennifer alichaguliwa kutoka kwenye waigizaji 781 waliofanya audition. Kama hujaiona Dreamgirls nakushauri ukaione. Nilienda kuiona juzi na kwa kweli ni sinema nzuri mno, yaani mno. Sijawahi kuona sinema nzuri kiasi hicho miaka mingi, tena waigizaji wakuu ni weusi. Na waMarekani wametokea kuipenda hiyo sinema. Soundtrack ya sinema ni namba one sasa hivi! Na kila mtu anamsifia Jennifer Hudson na kuigiza na kuimba kwake.

Kwa ufupi, Jennifer anaigiza kama Effie White, ambaye ni mwimbaji mkuu wa Kikundi cha The Dreams. Meneja wa Kikundi (Jamie Foxx) anamshusha na kumweka, Deena Jones, (Beyonce) kuwa mwimbaji mkuu kwa vile ni mzuri wa sura kuliko Effie. Effie anatupwa na kikundi cha chake na anasota na maisha. Sitaki kuwaeleza mengi lakini kuna mapenzi mle. Beyonce naye aliteuliwa kwa ajili ya tuzo ya Best Actress, lakini hakupata.

Eddie Murphy anaigiza kama James ‘Thunder’ Early, ambaye ni mwimbaji mwenye staili ya pekee ya kuimba. Anatokea kupendana na moja wa hao Dreams. Naye alituzwa Golden Globe kama Best Supporting actor. Kama hamkuona show, walivyomtangaza mshindi, alionekana kuwa na mshangao. Sishangai maana alishateuliwa mara kadhaa kwa ajili ya sinema kana The Nutty Professor, na hajashinda hata siku moja. Na huko kwenye Oscars ndo hawajamjua kabisa.

Kwa hiyo ndoto huwa zinatokea kweli. Jennifer Hudson, ametuonyesha kuwa inawezakana.

Tuesday, January 09, 2007

Oprah ajenga shule ya kifahari ya Wasichana Afrika Kusini

Bila shaka mmesikia habari ya Oprah Winfrey kufungua shule ya wasichana huko Afrika Kusini. Shule enyewe inaitwa ‘The Oprah Winfrey Leadership Academy’. Kwa kweli nampongeza kwa kitendo chake cha kukumbuka Afrika na kusaidia wasichana huko. Wanafunzi waliochaguliwa wanatoka kwenye familia zenye kipato cha chini. Na walichaguliwa kutoka kwa maelfu ya wasichana walioomba nafasi ya kuingia huko.

Oprah alijenga shule hiyo kwa gharama ya dola za kimarekani $40 milioni. Kwa sasa ina wanafunzi 145. Bila shaka tutasikia waliosoma hapo watapata mafanikio mazuri kimasomo na kwenda kusoma vyuo vikuu maarufu duniani kama Harvard, Stanford, Cambridge, Oxford etc.

Shule enyewe ni ya kifahari hasa. Hata wanaosoma shule za Ivy League na ma Prep school duniani wanaweza kuwaonea wivu has wasichana. Nikisema ni ya kifahari, nina maana ni ya kifahari hasa. Oprah mwenyewe ni bilionea na kazoea maisha ya kifahari na alitaka hao wasichana wajue ufahari manake nini. Mfano, shule ina saloni kwa ajili ya kutengeneza wasichana nywele, wanalalia mashuka enye nyuzi 200 count (Duh…kama wanalala hoteli ya Waldorf Astoria) sahani zilichaguliwa na Oprah na si ajabu sahani moja ina gharama ya dola mia, ina theatre za ndani na nje, ina ma fireplace tele (Afrika unahitaji fireplace ya nini?) na mengine mengi. Walimu wameletwa kutoka nchi za nje.

Je, wakirudi majumbani mwao kwa ajili ya likizo wataishi namna gani? Si wamezoea ufahari. Si uwongo kuna watu ambao baada ya kukosa maisha ya kifahari waliozoea, walirukwa na akili na wengine kujiua. Natumaini Oprah ana mpango wa kuhakikiisha hao wasichana wanaendelea kuishi maisha ya kifahari wakimaliza masomo yao.

Lakini najiuliza kama hizo pesa katumia vizuri kweli? Nakubali kuwa ni hela yake na anaweza kufanya anachoaka nazo. Lakini jamani hiyo hela ingeweza kusomesha maelfu ya wasichana huko Afrika Kusini na Afrika kwa ujumla. Kuna faida gani ya mtu kula chakula kwenye sahani enye thamani ya dola mia, wakati huko nyumbani kwake huenda hakuna chakula. Pia watoto wengi Afrika wanashindwa kusoma vizuri shauri ya kukosa mlo wa kutosha. Na kisa cha kulalia shuka enye 200 thread count wakati huko majumbani mwao wanashukuru kuwa na sehemu safi ya kulala. Au wanalala wane kwenye Kitanda kimoja. Kuhusu hiyo saloni si bora wangekuwa wanasukana wenyewe kwa wenyewe, ili wajue sanaa ya kutengeneza nywele.

Samahani lakini navyoona kuna watoto Afrika ambao wangeshukuru kuwa na unifomu na viatu vya kuvaa kwenda shule. Wangeshukuru kuwa na vitabu, na madaftari. Wangeshukuru kama wanakuwa na uhakika wakulipwa ada ya shule, na kuwa na njia ya kufika shule bila bugudha, kama vile school buses. Yaani hiyo dola milioni $40 zingeweza kutumiwa kujenga hata shule kumi bora Afrika na kusaidia wengi zaidi.Hayo ni maoni yangu tu. Wapendwa wasomaji, mnaonaje?

Saturday, January 06, 2007

Hongera Dada Asha Rose Mtengeti-Migiro



Nachukua nafasi hii kumpongeza Dada Asha Rose Mtengeti-Migiro, kwa kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (United Nations). Kwa kweli ni jambo sisi WaTanzania lazima tujivunie.

Namfahamu Dada Asha Rose, tangu alivyokuwa anasoma UDSM. Mimi wakati huo bado nilikuwa nasoma Secondary School. Kwa kweli huwezi kujua Mungu amempangia mtu nini. Nikikumbuka enzi zile, yaani tusingeweza kutegemea kuwa atakuwa kiongozi anayeheshimika dunia nzima. Alikuwa hana makuu. Lakini miaka ilivyoenda tuliona alivyoonyesha meno kuwa anaweza kuongoza na kuongoza vizuri.

Pia kuteuliwa kwake unaonyesha jinsi Tanzania inavyoheshimika duniani. Hatujawa na migogoro mingi ya kisiasa kama nchi zingine barani Afrika. Na nasikia ilikuwa kila mkutano wa kimataifa akienda anapata washabiki kwa uongozi wake mzuri. Watu wengine wamekuwa wakishangaa alipataje kuteuliwa katika nafasi nzito hivyo. Nawambia ameteuliwa kwa sababu ameonyesha watu wengi Tanzania na nje ya Tanzania kuwa ni mtu mzuri mwenye moyo na kipaji cha uongozi.

Jambo lingine ni kuwa mwanamke kutoka Third World amekababidhiwa uongozi mzito. Lazima Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Ban Ki-Moon, kamwona Dada Asha Rose ni mwanamke jasiri atakayeweza hiyo kazi.

Dada Asha Rose amekuwa ni mfano mzuri kwa wasichana wote wa Tanzania na Afrika kwa ujumla!

Akina Mama Oyee!

Wednesday, January 03, 2007

Poleni Wafiwa


Kwanza naomba mnisamehe kwa kuongea kuhusu kifo. Najua si jambo la kufurahisha.

Leo nimekwenda kwenda 'Wake' (kilio) ya Mama Anastazia Rupia. Alifariki hapa Boston siku chache kabla ya Krismasi. Alikuwa amekuja kwenye mahafali ya mwanae, Septemba na kwa bahati mbaya alianza kuumwa muda mfupi baada ya hapo.

Kwa kweli waBongo walitokea wengi kuwafariji wenzao waliofiwa na mama yao. Mchungaji mzungu alisoma misa mzuri sana. Watu walikuwa na majonzi hasa mtoto wa marehemu John Rupia, alivyosimulia habari ya maisha ya mama yake na alivyougua. Alivyomaliza naye, John alianza kulia ndo hapo chumba chote tuliishia kulia.

Maiti anawasili Dar Jumamosi na ndege ya SwissAir, naomba muwepokea vyema huko. Poleni.

Lakini jamani ukweli uchungu wa kufiwa unaujua wewe uliyofiwa. Hata tukikupa pole ngapi, marehemu ni marehemu, hatarudi. Watu wataenda zao kwenye shughuli zao na wewe mfiwa utabakia na majonzi yako.

Watu wengi wanajua uchungu wa kufiwa na mtu wa karibu. Nilivyofiwa na mume wangu wa kwanza, mwaka 1995 hata sikumbuki nilifikaje Tanzania. Nilikuwa nasoma hapa Boston, nikapata taarifa, nikakatiwa tiketi na nikashutukiwa niko Dar uwanja wa ndege na wafanyakazi pale walinipa pole na kuniuliza kama nina mtu wa kunipokea. Ile safari yaani ilikuwa kama vile ndoto mbaya na niseme miezi kadhaa baada ya kufiwa si kuwa mzima maana nilijisikia kama sijui niko wapi. Wakati mwingine nilikuwa najiona kama niko kwenye wingu, mara naona mwili mzito kutembea shida. Mungu alinisaidia kipindi kile. Amini usiamini, miaka zaidi ya kumi imepita na bado nina omboleza ila siku hadi siku uchungu unapungua. Unapungua lakini haushi kabisa.

Lakini sisi tuliyobaki inabidi tuendelee kuishi na kujenga maisha yetu na kusimulia kwa wanaetu kuhusu ndugu zao waliowatangulia hapa dunia.

Kwa kila mtu aliyefiwa na ndugu au rafiki yake nasema, pole. Poleni wafiwa wote popote mlipo, na Mungu awape nguvu katika kipindi hiki kigumu. AMEN.

Saturday, December 30, 2006

Heri ya Mwaka Mpya!


Ninawatakia heri ya mwaka mpya! Mbarikiwe wote katika mwaka mpya 2007! Nashukuru Mungu kuwa wote tumefika na nawaombea wote uzima na mafanikio mema katika huu mwaka mpya. Naomba pia tuwe pamoja mingi mingi zijazo, Inshallah!

Pia nawaoba msherekee mwaka mpya kwa amani na usalama kwani kipindi hiki kuna kuwa na ajali nyingi shauri ya ulevi.

HAPPY NEW YEAR!

Tuesday, December 26, 2006

Marehemu James Brown







REST IN PEACE JAMES BROWN

1933 - 2006

Jamani nilisikitika kusikia habari ya kifo cha Godfather of Soul, James Brown! Alifariki jana asubuhi, Krismasi, akiwa anaumwa Pneumonia. Lakini jamani Ijumaa mbona alionekana mzima, ana-sign autographs na kutoa zawadi za Krismasi kwa watoto!

Ukweli, mimi ni mmoja wa washabiki wake wakuu. Yaani kila nikisimikia animba 'funk' lazima niinuke na kucheza! Nyimbo zake, 'Say it Loud, I'm Black and Proud!', 'Hot Pants, 'Sex Machine', Get Up, na zingine nyingi haziwezi kusahaulika. Sasa kwa vile ni marehemu bei ya CD's zake zitaongezeka bei.

Nisiseme habari ya jinsi nilivyokuwa nashangalia akicheza na kutia madoido ya 'splits'! Nina mpaka mDoli wa James Brown, una bonyeza mahala na anaanza kucheza na kuimba ule waimbo wake wa 'I Feel Good!' (Najisikia vizuri). Tangu mdogo yaani miaka minne hivi nakumbuka kucheza na kupiga kelele kila nikisikia anaimba, eti najaribu kumwiga!

Mungu amlaze mahali pema mbinguni. Amen.


Saturday, December 23, 2006

Nawatakia Krimasi Njema!


Wapendwa Wasomaji, ninachukua nafasi hii kuwatakia wote Krismasi Njema! Japo ni sikukuu ya kusherekea kwa kupeana zawadi, kula mlo mzuri na wa fahari, kukutana na familia na marafiki, kunywa pombe etc., tusisahau kuwa ni siku ya kukumbuka kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo.

Napenda sana kipindi hiki Marekani, maana watu wanakuwa na roho nzuri na kusalimiana na watu ambao kawaida wasingewasalimia. Pia watu wanatoa misaada mingi kwa wasiojiweza na maskini kwa vile wameingiliwa na 'Christmas Spirit'. Hata bosi mwenye roho mbaya anaweza kuwa na roho nzuri japo kwa siku moja!

Wengine wataenda kwenye mikesha kanisani, wengine wataenda kwenye party, wengine watalala na kupumzika, wengine hawatasherekea kabisa hasa wasio waKristo.

Bila kujali dini, ninawatakia wote Krismasi Njema, na mapumziko mema.

Mungu Awabariki Wote!

Friday, December 15, 2006

Niliuliwa na Mzungu mwenye Hasira (Aftershock:Beyond the Civil War)




Jamani msishangae sana. Huu ni mguu wangu! Na bado niko hai. Nilikuwa naigiza katika sinema ya 'Aftershock:Beyond the Civil War' kama Field Hand. Hao field Hands walikuwa ni watumwa walioachiwa huru lakini bado walikuwa wanaishi katika hali ya kitumwa baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe (Civil War) 1865. Wakati wa filiming tulikuwa peku kwenye matope! Sinema ilipigwa mwezi wa sita na wa saba hapa Massachusetts.

Hiyo make-up ya damu feki ilipakwa kwenye mguu baada ya kulala chini! Nakumbuka Director David Padrusch anamwambia make-up lady, ongeza, ongeza damu haitoshi! Ai! Walinipaka mwili mzima. Niliona kinyaa maana hiyo damu feki inaonekana kama damu kweli. Na usoni pia nilipakwa madamu na majeraha, ilikuwa tuonekana kama tumepigwa risasi nyingi. Ni kwamba weusi wengi waliuliwa na wazungu wenye hasira baada ya hiyo vita.

Sinema ya Aftershock itaonyeshwa History Channel, Saturday December 30, 3:00PM (Eastern).

Cheki website yao kwa maelezo zaidi.

http://www.history.com/shows.do?episodeId=203497&action=detail

Pia unaweza kusoma habari zaidi ya experience yangu kwenye seti ya Aftershock hapa:

http://chemiche.blogspot.com/2006_06_01_chemiche_archive.html

Unaweza kuona Trailer kwenye You Tube.

Thursday, December 14, 2006

Kariakoo = Carrier Corps





Hapo zamani za kale kabla ya magari, lori, petroli, basikeli, wazungu walitegemea binadamu na wanyama kubeba mizigo yao. Hao waafrika walioajiriwa waliona sifa kubwa kufanya kazi na mzungu na kulipwa.

Hao wabebaji wlaikuwa wanaitwa Carrier Corps, na baada ya 'kuswahililize' ndo ikawa jina la Kariakoo tunaoijua leo.

Kabla ya hao wa kulipwa waafrika walilazimshwa kubeba hiyo mizigo wakiwa kama watumwa. Historia ya mwafrika jamani.

Jamani cheki hiyo mizigo ilivyo mizito halafu fikiria unabeba kuanzia Dar hadi Mwanza, na wakati huo hakuna barabara. Lazima mizigo ilipotea, hasa kama mtu anaanguka nayo kutoka mlimani. Mtu unatembea nayo unatazama mbele huko nyoka anakuuma! Na, kama wabebabaji walikufa njiani nani alibeba mzigo wake?

Kama mmewahi kuona sinema za Tarzan na zingine zilizohusu Afrika, utaona mzungu alivyobebwa kwenye kiti na waafrika huko ana wabebabaji mizigo yake. Tena waafrika wakionekana wavivu wanachapwa kama punda! Ama kweli tumetoka mbali.

Wednesday, December 13, 2006

Nilitolewa Ushamba Dar - Text Messaging


Haya nimezungumza habari ya watu wengi kuwa na cell phone Dar. Sasa kuna hiyo kitu 'text messaging'. Naona ndo mawasiliano ya bei rahisi kuliko voice call. Kila mtu anajua kutuma text message, isipokuwa mimi!

Niliazima simu ya mama yangu. Watu walikuwa wananitumia text message. Doh, niliweza kuzisoma, lakini nilishindwa kutuma jibu! Niliona aibu kweli. Dada moja kanipigia na kusema, 'Nilivyona hujajibu niijua hujui kutumia texting!"

Ni kweli nilikuwa najibu watu kwa kuwapigia simu na of course ni ghali. Japo nina cell phone miaka mingi na nimeona hiyo text feature, huwa nasoma message na kuinua phone na kupiga kama inabidi nijibu. Nimeona vijana na watoto wadogo wanajua kutumia lakini haikuniingia kuwa nami nitumie. Na mara nyingi kwenye TV utasikia, send a Text message to halafu wanakupa namba. Lakini hata siku moja sijajaribu! Jamani USHAMBA! Ni kama vile compyuta. Mtu unaona lakini unaogopa kutumia! Ukianza kutumia unasema, Kumbe ni rahisi hivyo!

Sasa nimerudi Boston, na natazama cell phone yangu. Na ndo nimekuwa na-explore jinsi ya kutumia hiyo text message. Nimeanza kupatia. Lakini naomba mnieleza jinsi ya kuweka space kati ya maneno! Kwa sasa naweka period kati ya maneno.

Kumbe ni simple na mawasiliano rahisi. Nimeanza kupenda text messaging. Ushamba wa text messaging umenitoka.

Thursday, December 07, 2006

Dar es Salaam kuna Joto!


Jamani Dar kuna joto! Loh! Unapigwa nayo ukishuka tu kwenye ndege. Siku mbili za mwanzo nilivyokuwa huko niliona joto kweli. Ni kweli kuwa Novemba/Desemba joto unazidi Dar, lakini kwa kweli nilikipata. Kwa siku nilikuwa na kunywa maji mengi kweli, na vinywaji vingine. Jamani nilitoka jasho zile siku za mwanzo.

Halafu mara nyingi umeme ulikatika kwa hiyo feni na Air Conditioning hazifanyi kazi, kwa hiyo unaendelea kuchemka. Unakwenda ofisini mwa mtu halafu unabakia kujipepea na gazeti shauri ya joto. Asubuhi, umeme ulikuwa unakatika saa 12 kamili. Basi unaamka kwa sababu feni chumbani unazimika na joto unaanza kuzidi. Hata hivyo siku zilivyopita nilianza kuzoea joto.

Haya nilivyondoka nilianza kusikia baridi kwenye ndege. Nilitamani ningebaki Bongo nifaidi joto. Na kufika Boston nilikaribishwa na snow (theluji)! Unatoka kwenye joto kuingia kwenye snow.

Basi nimerudi Boston na ka-tan. Nilikuwa navaa sleveless Dar, basi unaona kabisa mikono umekuwa Dark. Sehemu zilizokuwa zimefunikwa zilikuwa light. Wazungu kazini waliniuliza kama nimepata 'sunburn'. Nikawaambia hapana ni tan, na sisi weusi tunapata tan pia. Lakini wacha nifaidi hiyo Vitamin E ya jua, maana kipindi hiki cha winter jua unaliona tu. Mambo ya kukaa nje na mwili kuganda shauri ya baridi hatutaki.

Monday, December 04, 2006

Aftershock itaonyeshwa History Channel 12/19 and 12/20/06


Habari zenu wapendwa wasomaji. Ile sinema ya 'Aftershock: Beyond the Civil War' itaonyeshwa kwenye History Channel, siku ya jumanne 12/19/06 saa mbili usiku (8:00pm Eastern) na pia itaonyeshwa tena 12/20/06 saa sita usiku (12:00am Eastern midnight). Mimi naigiza humo kama mfanyakazi wa mzungu mbaguzi mno mwenye uchungu shauri ya Confederates kushindwa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe Marekani miaka ya 1860's.

Kwa habari zaidi soma hapa:

http://www.history.com/schedule.do

Pia nimewahi kuandika kwa kirefu kuhusu hiyo sinema hapa:

http://swahilitime.blogspot.com/2006_06_01_swahilitime_archive.html

Thursday, November 30, 2006

Kila Mtu ana cell Phone Dar

Jamani, mawasiliano ya simu ni rahisi sana Dar. Cell phone nyingi, makampuni yanashindana kupata wateja, phone cards zinauzwa kila mahala, tena bei si mbaya hata shilingi 500/- unapata! Watu wengi wanazo! Mbona cell phone USA ni ghali sana, tena ukiweka kwenye credit kadi ndo unalaguliwa kabisa! USA wanaweza kujifunza kutoka Bongo!

Lakini jamani barabara mbovu sana Dar, tena sana! MAVUMBI!

Baadaye!

Sunday, November 26, 2006

Diary from Dar es Salaam

Haya, ni siku yangu ya tano Dar. Malalamiko yangu makuu ni:

Ukosefu wa umeme
Barabara mbovu
Maji shida
Mbu!

Nimetafunwa na mbu! Na nimetumia mosquito repellent. Labda wamekuwa sugu. Lakini wamekunywa damu ya Boston!

Niko Mbezi kwenye cafe iliyoko barabarani kabisa. Kwa kweli computer zao ni safi sana, kuliko cafe iliyoko karibu na nyumbani. Wale wana computer nzee na slow.

Vumbi na michanga!

Lakini jana nilikuwa kwenye sherehe ya arusi. Jamani kuna catering companies siku hizi! Juzi nilikuwa kwenye Graduation party, ilikuwa kama arusi Ama kweli Tanzania kumekuwa Party Culture!

Friday, November 24, 2006

Niko Bongo!

Habari zenu wasomaji wapendwa. Niko Bongo Dar es Salaam. Nimetua juzi, kwa kweli ni joto sana lakini naona naanza kuzoea. Nimefurahi kufika nyumbani baada ya muda mrefu. Leo nimeenda mjini na kwa bahati nimegongana na watu wengi tu ambao nilikuwa nawafahamu. Naweza kuwa natembea halafu nasikia 'Che-Mponda!' Na cheki ni mtu nilimfahamu toka zamani.

Sasa jamani ile jengo la Daily News la zamani wanaifanyia nini? Naona Maktaba wamekarabati kwa nje. Maji ya kunywa ya chupa na phone cards ziko kila mahala, mawasiliano ni rahisi. Lakini barabara nyingi mbovu, na traffic jams ni mbaya! Yaani kutoka mjini kwenda Mbezi Beach ni two hours!

Nimepapenda Slipway! Ice Cream yako safi na ile Mashua Bar pale Beachfront safi sana. Halafu kuna ATM's kila mahala siku izi hakuna kwenda benki kusimama kwenye foleni ndefu. Nimshangaa kuona kuna hata Casino pale karibu na Greek Cub ya zamani karibu na Red Cross. Bongo kumeendelea hata hii internet nayo tumia ni nzuri sana na up to date!

Jamani nisiendelee maana umeme shida!

Mengine baadaye!

Thursday, November 16, 2006

Huyu ni Emmitt Smith na patna wake, Cheryl Burke wlioshinda mashindano ya 'Dancing with the Stars' jana. Alishinda baada ya watazamaji wengi kumpigia kura kama vile American Idol. Kila wiki wachezaji walipunguzwa mpaka kupata wachezaji bora.

Emmitt ni mcheza football na pia bonge la baba, lakini alishangaza watazamaji kwa 'moves' zake ambazo usingeweza kutegemea mtu na mwili kama wake kufanya.

Wacha wazungu wanune lakini weusi wamejaliwa na 'rhythm'! Kucheza iko katika damu yetu!

Navyosikia wanaume wengi sasa wanachukua Dance Lessons! Haya sasa Dancing ni' in' kwa wanaume!