Tuesday, November 06, 2007

Maoni - Falsafa za Watawala wetu na ulinzi wa kikatiba


Falsafa za Watawala wetu na ulinzi wa kikatiba

Imeandikwa na msomaji Ipyana MwakamelaNi mambo mengi sana yamejiri tangu Serikali ya awamu ya nne iingie madarakani dhidi ya ile ya awamu tatu juu ya uborongaji uliotawala katika uongozi wa kipindi cha miaka kumi cha Rais Benjamini William Mkapa.

Mengi yamesemwa na tuhuma kedekede dhidi ya Mkapa sasa zimeanikwa wazi juani kwa kila mwenye uchu wa kutaka kuzijua na afanye hivyo. Ninafurahi binanfsi kwamba kila ambacho kiongozi aliye madarakani alidhani amefanya kwa siri huwa kinakuwa peupe peee amalizapo muhula. Labda huo ndio ule tunaita ukomavu wa kisiasa na demokrasia ama uhuru wa kutoa mawazo kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Imeandikwa magazetini, imeongolewa katika vyombo vyote vya habari na hata katika vikao vya kahawa juu ya ufisadi uliotawala katika kipindi cha serikali ya awamu ya tatu. Kibaya ama kizuri zaidi, itategemea na kila mtu atakavyotafsiri ni kwamba Mzee Ben ameamua kukaa kimya kitu ambacho ama kinafanya uthibitisho wa tuhuma dhidi yake, kuendeleza tafsiri ya ubabe aliyokwishabatizwa nayo, kudharau vilio vya majeraha aliyotuacha nayo ama ni ujivuni wa kinga ambayo viongozi wakuu wastaafu wamewekewa na katiba yetu.

Mzee Ben aliwambia waandishi wa habari waliomtaka kuthibitisha ukweli wa tuhuma dhidi yake kuwa amestaafu siasa aachwe apumzike. Hii naifananisha kabisa na kauli ya Kikwete mwenyewe pale awali aliposema “Muacheni Mzee Mkapa apumzike”

Nashindwa kutafsiri maana halisi ya kauli hiyo ya Kiongozi aliyeshika dola kwa sasa kama ilimtoka kwa bahati mbaya, woga wa kutekleleza majukumu aliyoaminiwa ama ni kuimarisha ulinzi dhidi yake pale atakapokuwa amestaafu.

Ni mkanganyiko mkubwa maana wao pia wote waliona alichokifanya Fredrick Chiluba wa Zambia dhidi ya muasisi wa taifa hilo Kenneth Kaunda na hatimaye Levy Mwanawasa kumbadilishia kibao pale alipokaa nje ya madaraka.

Pengine ingekuwa vyema na busara zaidi kama Viongozi wetu wa Afrika wangejitahidi kuhakikisha macho yao yote mawili yanafanya kazi sawia kwa kuyazungusha kushoto na kulia huku wakiyapima kwa kutazama vitu vilivyo karibu yao na hata vile vya mbali na pale walipo. Hii ingewasaidia kujua yaliyotokea, yaliyopo kuwazunguka wao na hata yale ya baadaye yanayotazamiwa kuwafika. Wangelitekeleza hili hapana shaka hata utekelezaji wa ahadi zao wanazozitoa kwa waajiri wao zingelitimia.

Ninachojifunza kwa viongozi wetu ni kushindwa kabisa kutekeleza usemi wa “Ukila na kipofu msimshike mkono”. Wanatushika mikono yetu huku wakiendelea kusokomeza chakula chote midomoni mwao tena milo yote ya siku….hii ni kasheshe maana kipofu keshagundua kwamba anadhulumiwa na hatimaye atakufa kwa njaa kama akifanya utani.

Kwa mtazamo wangu Rais Mkapa naye alifanya mengi tu ya kukumbukwa tofauti na tunavyoichukulia kwamba ni mmoja kati ya viongozi waliotawala nchi ambao hawakutakiwa kabisa kuingia madarakani.

Baba yetu wa Taifa hili Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifanya mengi sana ya kujivunia katika nchi hii na ndio maana anakumbukwa mpaka leo hii na tungependa viongozi wetu wengine wote wanaofuata waige mfano wake. Lakini kama binadam Mwalimu Nyerere pia hakuyatimiza yote kikamilifu na hata yeye mwenyewe alikubali pale alipojikwaa. Hapa pia tukumbuke kwamba ni ngumu sana kwa viongozi waliofuata kufanya kikamilifu kabisa kama Mwalimu alivyotaka iwe. Wanawe tu wa kuwazaa hawajatimiza matakwa hayo sembuse wa urithi?

Baada ya Mwalimu kuachia madaraka alichukua Mzee wetu Ali Hasan Mwinyi ambaye aliongoza nchi kwa kipindi cha miaka kumi ambacho Hayati Baba wa Taifa alikuwa hai na akikemea kila alipodhani hapakua sawa. Tunakumbuka maneno kama ikulu kuwa pango la walanguzi, mtu kuongoza nchi na mkewe na mengine yafananayo na hayo ambazo ni kauli alizitoa Mwalimu kwa kutoridhishwa na uongozi wa Mzee Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa.

Si muafaka kumuongelea Mzee Ruksa kwa kuwa hakuwahi kujibu hata tuhuma moja dhidi yake katika zile alizotwishwa hata kama zilimdharirisha kiasi gani. Pengine ndiye aliyemshauri kijana wake Mkapa kwa kumuasa kukaa kimya kama alivyofanya yeye inaweza kuwa dawa mbadala.

Ninachojiuliza ni kwamba kama amemsihi hivyo aligeuza macho yake pande zote na kuangalia ni mwanga kiasi gani unamulika kwa viongozi kama wao sasa akilinganisha na wakati alioachia ngazi yeye?. Nadhani hapa panahitaji tafakari ya kutosha kabla hatujapandisha mori.

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Jakaya Mrisho Kikwete yu madarakani sasa, ndiye aliyeshika usukani wa nchi. Kizuri zaidi ni kwamba katika serikali zote mbili kabla yake alikuwamo ndani ya Serikali na hivyo si mgeni sana na mambo yaliyotendeka na pengine yanayoendelea kutendeka.

Labda linalonichanganya mimi sana ni hili: Je Rais atakuwa tayari kuruhusu mabadiliko ya katiba ili vile vipengele vinavyowalinda watu kama yeye waondokapo madarakani vinafutwa ili wakimaliza madaraka yao washitakiwe kwa kila walichotenda kinyume na kiapo walichokula, ama kwa lugha nyingine wahukumiwe sawa na matendo yao?.

Naomba Rais atujibu katika hili ili sasa tuanze kumuona jinsi gani alivyojiandaa kuwa safi katika utawala wake na wala si kufanya mambo kama waliyoyafanya wenziwe waliomtangulia na hivyo kuendeleza Utanzania wa kushupalia mambo wakati muhusika hayupo ama kutoa sifa kwa maiti ambaye hana la kufanya tena kwa wakati huo anapokuwa ndani ya jeneza.

Mheshimiwa Kikwete aliahidi kwamba atafuatailia kwa makini mikataba yote iliyosainiwa ya madini ili kuhakikisha kwamba kila kilichokwenda mrama kinarekebishwa kwa manufaa ya nchi na si kama ilivyofanyika hapo awali. Siwezi kuchimba kiundani kabisa kujua ni kwa kiwango gani mikataba hiyo tayari imekwisha pitiwa na hata kuruhusu kusainiwa kwa mikataba mingine kama ya Buzwagi inayopigiwa kelele kwa sasa na kuiingiza Serikali ya Chama cha Mapinduzi matatani dhidi ya kambi ya upinzani.

Kinacholindwa sana hapa katika mkataba wa Buzwagi hata kupelekea Mh. Zito Kabwe akasimamishwa kuhudhuria vikao vya bunge, Mheshimiwa Lowasa kuiwekea ngao kila anapoulizwa na jeuri ya Karamagi kutojiuzulu kwa kashfa kama alivyofanya Mbilinyi na Mpologomyi enzi za Serikali ya awamu ya tatu ni nini?.

Mheshimiwa Rais alituahidi kwamba Waziri atakayevurunda hataweza kumaliza hata temu ya kwanza ya miaka mitano. Ni nani anathibitisha uvundo wa waziri?, ni mpaka Rais mwenyewe aseme ama kilio cha Wananchi walio wengi ndio chachu ya Rais kujua kiwango ambacho Waziri kavurunda?

Yupo Mheshimiwa Kapuya aliyetumia ndege ya Jeshi kwa safari binafsi na watu wakapiga kelele sana mpaka kwenye vyombo vya habari lakini sisi kama waajiri wakuu wa viongozi hao hatujafahamu hasa nini kilifuata baada ya pale na kelele za vyombo vya habari zilichukuliwa vipi na mkuu wa kaya hii.

Palikuwa na suala la Richmond ambalo lilifukuta na kufuka moshi mzito lakini hatimaye ikaja eksitigwisha ya Dowans ambayo ikauzima moto huo huku na yenyewe ikiwa bado na madhara na inaendelea kutafuna kama kutu inavyokula chuma.

Profesa Maghembe na Wizara yake ya Maliasili, macho yake hayakuzungushwa pande zote na sasa amefanikiwa kupandisha mbao kwa asilimia 700. Hakutazama mlaji mdogo anawezaje kununua ubao mmoja kwa shilingi 9000 kutoka bei ya awali ya shilingi 2000.

Bajeti ya Serikali ya 2007/2008 imepitishwa kwa mabavu pasipo kuzingatia maisha halisi ya Mtanzania na mfumuko wa bei ya vitu wakati tungali na mahubiri ya Maisha bora kwa kila mtanzania. Hakuna asiyejua gharama ya maisha imepanda kwa kiasi gani mpaka hivi sasa na huku mshahara wa kima cha chini wa serikali ukiwa chini ya shilingi laki moja kwa mwezi.

Pamekuja suala la malipo ya wafanyakazi wa majumbani maarufu kama House Girls na House Boys kwamba wanatakiwa kulipwa kima cha chini kabisa shilingi 65000 kutoka katika mfuko wa mfanyakazi anayelipwa shilingi 85000 kwa mwezi. Mahubiri yetu yangali “ maisha bora kwa kila mtanzania.

Kuna mradi wa ugawaji wa viwanja wa Serikali unaitwa viwanja vya bei nafuu lakini unaongelea kwenye malaki kama si mamilioni ya shilingi. Saruji imefikia kiasi cha shilingi 16000 kwenda juu kwa hapa jijini Dar es Salaam kwa mfuko mmoja wa kilogram 50. Tunavyo viwanda vitatu nchini Twiga Cement kilichopo Wazo jijini Dar es Salaam, Tanga Cement kinachozalisha Cement ya Simba na Mbeya Cement kinachozalisha Cement ya Tembo. Nani atajenga hapa ni kila Mtanzania ama tabaka fulani tu la watu?.

Nimeona katika vyombo vya habari matangazo ya Tanga Cement juu ya bei halali ya kununulia Cement yao kwa mikoa yote nchini. Najiuliza utekelezaji wake utakuwa vipi na ni nani atatutetea kuhakikisha bidhaa zinapatikana kwa bei inayotambulika. Sitamani hata kidogo kurudi katika enzi za “Duka la kaya”, nani atakuwa Sokoine wetu wa leo kupambana na uhujumu uchumi unaokuja kwa kasi ya ajabu.

Kikubwa katika haya yote ni kwanini tunawaangalia panya, mende, mchwa, dumizi, nzige na wadudu wengine wanaoingia kwenye boksi la mheshimiwa Kikwete huku wakifanya uharibifu kwa uhuru na viburi tena katika boksi jipya tulilolinunua jana kwa bei ghali zaidi na badala yake tunalishughulikia boksi la Mkapa ambalo tayari limekwisha chanika na hatuna jinsi ya kuliokoa leo.

Ufisadi unaotangazwa leo katika nchi yetu hautaisha kama hatutaacha unafiki wetu kwa wanaokalia madaraka leo ili tuwasubiri kesho watakapokuwa wametoka. Nani atakuwa Raisi wetu jasiri atakayetekeleza kwa dhati kila anayoahidi kuyafanya?.

Wapi Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na kwa nini imebakia nadharia tu na hakuna ukweli halisi wa kwa nini vitendo vyake vimebaki kuwa ndoto. Cha ajabu na kinachotia kichefuchefu ni kwamba kila panapotajwa jina la muasisi wake Wasomi, Wanadiplomasia, Viongozi mashuhuri hawaishi kutaja Azimio la Arusha na mengine mengi yaliyoasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kuna sababu gani ya msingi inayofanya kila mtawala aje na falsafa yake ikiwa falsafa zilizotumiwa na watawala waliotangulia hazina matatizo yoyote. Hapana shaka hapa nitapata waliobobea katika tafakari wanisaidie kupata uchambuzi wa hili tena ulio yakinifu.

Najuliza sana ni wapi “Fagio la chuma” lilikopotelea baada ya Mzee Ali Hassan Mwinyi kuondoka madarakani. Ni kwa nini falsafa yake haikutekelezeka kivitendo hata kwake yeye mwenyewe ikaendelea kubaki kinadharia peke yake na hatimaye kuzikwa kabisa baada ya Serikali ya awamu ya tatu kuingia madarakani. Kama ilikuwa ni falsafa nzuri yenye matunda kwanini haikurithiwa ama hata kuzungumziwa katika Serikali zilizofuata.

Kama pangekuwa na “Ukweli na Uwazi” aliotuletea Mzee Benjamin William Mkapa na ukatekelezeka kama ulivyokusudiwa na kupokelewa na umma wa watanzania walio wengi sidhani Mkapa angekuwa na jina baya machoni na masikioni mwa Wananchi aliowaoongoza kwa miaka kumi. Lakini hali kadhalika mazingira ya nadharia katika falsafa za watawala wetu yameendelea kutukuka na hii pia ilimshinda aliyeiasisi. Leo hii amekalia kaa la moto.

Kibaya zaidi ni kwamba kila inapokuwa mchana na usiku jina la tarehe, siku, mwezi na mwaka hubadilika. Sasa leo kuna mashindano ya viongozi bora wa Afrika wanaopata tuzo za heshima na kuvuna donge kubwa la fedha. Mfanyabiashara Mo Ibrahim amejitolea kutoa tuzo hiyo katika kuonyesha ama kutafuta njia mbadala ya kuwafunda watawala wa Afrika jinsi ya kuwatawala Waafrika wenzao.

Mzee Ben akadondoka kama kiongozi wa Tanzania na huku Joaqim Chissano akivuna alichopanda katika utawala wake. Hata hivyo mimi sikushutumu sana kwa hili kwani angalau ulimkaribia Chissano ukilinganisha na wenzio kumi na mmoja. Kumbuka unashutumiwa tu kwa kuwa tulihitaji kuwa na furaha waliyonayo Msumbiji leo hii…..pole sana mzee Ben labda Kikwete atajifunza kutoka kwako ili aje atutoe kimasomaso siku za mbele katika “ishu” kama hiyo.

Imeshika hatamu kubwa sasa “Kasi mpya, Nguvu mpya na Ari mpya” kwa kuwa ndiyo iliyo madarakani sasa. Ewe Mweny-enzi Mungu tunusuru na hili lisije bakia nadharia kama yaliyopita. Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete tunaona utekelezaji hafifu wa falsafa yako hasa ukizingatia kuwa bado upo katika hatua za awali za uongozi wa nchi ambayo ina kiu kubwa kabisa ya kuona mabadiliko ya kimaisha ili kauli mbiu yako “Maisha bora kwa kila Mtanzania” iweze kufikia lengo.

Hii habari ya badilisha huku kwenda kule kwa watendaji wako inakuharibia kabisa na inazidi kutia giza katika juhudi za kutekeleza kwa vitendo falsafa yako. Hii kwa kukuibia siri tu ndio chanzo cha kuanguka kwa falsafa za wenzi wako waliotangulia. Ikiwa huwa mnafanya hayo kwa makusudi yenu binafsi basi lipa fadhila ama ua nyani kwa kumtazama usoni kisha uone haya.

Boksi la uliyempokea kijiti li tafrani kabisa, limeliwa na wale wadudu aliowafuga kwa muda mrefu na kuwaacha wazaliane huko. Tayari boksi lako limeingia wadudu wale wale kwa kuwa hukulichoma moto boksi la Mkapa bali umeliweka karibu na hilo la kwako jipya na wameanza mapema kulitoboa lakini halahala maana sasa hivi madawa ya kuwaangamiza wadudu hao ni mengi tu ni wewe kwenda sokoni na kununua. Ukiwa mvivu dawa yake itakuwa ni kuchoma nyumba nzima ili hata wale walijificha katika kenchi na kona zisizo fikika waweze kuteketea.

Hatuhitaji mbwembwe na ujuvi wa kuibua falsafa zaidi kinachohitajika na Watanzania wote ni “Utekelezaji kwa vitendo wa falsafa zenu”. Nakumbushia tu, tumeyafumbua macho yetu kwa ung`avu kabisa na hatutalala tena.

Ipyana Mwakamela
P.O. Box 17132
Dar es Salaam
Barua pepe: nakumbushia_tu@yahoo.com

1 comment:

Anonymous said...

Ipyana,
Maoni yako nimeyasoma.Na kama kawaida ya watu ambao ni wavivu kusoma na kuchambua mambo umeamua ku-copy na ku-paste maoni ya wenzako waliowahi kuandika juu ya Serikali na Mkapa.

Hata hivyo bwana impyana makushukuru kwa jinsi ulivyoandika kuhusu serikali ya awamu ya Nne,ila nakuonea huruma kwa jinsi ulivyofikiria pafupi na kumhusisha Mkapa katika uozo.

Mimi ningekuwa Mkapa,KAMWE NISINGETHUBUTU HATA HIYO KUWAAMBIA WATU KUWA NIMESTAAFU SIASA.Ningekaa kimya tu na hilo nafikiri ndo jibu zuri.Unajua mjinga akikufanya wewe mwelevu useme yeye anachotaka basi werevu wenzio watakuona wewe nimjinga zaidi za yule mjinga.Sasa Mkapa aseme ili iweje???Ok akishasema inakuwaje sasa??Yani aende pale Mnazi mmoja na kuita wayu na kuanza kusema jamani leo naongelea watu wanavyonituhumu????Hivi wewe ni kichaa eeh!!!Big up Mkapa.Hawakujui nafikiri.

Chuki yote hii kwa Mkapa ni kwa sababu aliwaambia waandishi wa habari kuwa "Yeye ahukumiwi na vijigazeti uchwara"waandishi waliendekeza njaa kwa Mkapa wakapiga chini.Mkapa hajui kutoa wala kufikiria rushwa.Sasa vijigazeti vinamfuata eti mzee tupe chochote ili tukuandike vizuri"Ahaaaaaaaaaaa!amuoni aibu???Akawatosa na wao wakamchukia.
Athari za serikali ya kutaka sifa ndo kama hii ya sasa.Mavyombo ya habari chungu mzima yamenunuliwa na mnaowahita wazuri.Nafikiri wewe mwenyewe unajua magazeti mangapi yamenunuliwa.Mimi siku hizi kuna baadhi ya magazeti hata vichwa vya habari sisomi.Mfano RAI.

Ktk maoni yako acha ama punguza kila kitu kusema nyerere,nyerere.Yani unataka kuniambia hujui ni mambo mangapi machafu yalifanywa na Nyerere ukilinganisha na Mkapa????Nakushauri mtafute Mtikila atakwambia vizuri kwani kuna maoni yake humu kwenye mtandao alihojiwa na akamweleza Nyerere vizuri jinsi alivyokuwa mbaya na mbinafsi tena katili.
Unadiliki hadi kunukuu baadhi ya maneno ya Nyerere ya ubaguzi,mfano "Nchi inaongozwa na mwanamke" kwa mwinyi.Hivi ingekuwa sasa/leo nyerere angewambia nini wanawake??? kwani mwanamke hawezi kuongoza???unaona hadi marekani wanataka kumpa mwanamke urais ijekuwa Tanzania.

Kimsingi umeboa sana.Nakushauri jipange upya toa hoja zako na si kila kitu urejee kwa Nyerere.Usifikiri wote tunampenda huyo baba yako wa taifa lako.Mimi namdai mambo mengi sana hasa wakati anatuhamisha kwetu na kupoteza mali yetu wakati wa operation yake ya vijiji.Umasikini wangu na familia yangu siku zote huwa tunalia tu na nyerere.ilifikia hadi kipindi ng'ombe wetu maksai aliyekuwa anatulimia tukampa jina la nyerere ili atulimie kurudisha tunayomdai.Ni ng'ombe aliyechapwa mijeredi mingi sana tukifikiri ni nyerere.Sasa wewe leo tena unatukumbushia shida za nyerere???alaaaa.
Wanzagi