Tuesday, October 16, 2012

Waziri Mkuu Pinda Kuunguruma London!


Waziri Mkuu, Mh. Peter Mizengo Pinda

WAZIRI MKUU PINDA KUUNGURUMA LONDON.


*Ni siku chache baada ya uadilifu wake kumuokoa kupigiwa kura ya Imani Bungeni.

*Kuainisha mafanikio ya serikali kuhusu Uraia Pacha na Ardhi kwa wanadiaspora.

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Peter Kayanda Mizengo Pinda (Mtoto wa Mkulima) leo Alasiri ya Jumanne tarehe 16 Oktoba, 2012 anatarajiwa kuunguruma Jijini London katika mkutano wake na Watanzania waishio hapa Uingereza.

Mheshimiwa Pinda ambaye yuko katika ziara fupi ya kibinafsi hapa London amerudia utaratibu wa kupenda kusemezana na Watanzania hata anapokuwa kwenye itifaki ya ziara fupi na ya binafsi, tabia ambayo imekuwa ikisifiwa na watanzania waishio nje ya nchi.

Aidha mkutano huu ni wa kwanza kwa Mheshimiwa Pinda hapa London tangu jaribio liloongozwa na wabunge wa Upinzani na wachache wa CCM kutaka kumng’oa madarakani liliposhindwa vibaya kwa kupata saini 70 tu kati ya 357 kupinga Ufisadi uliokithiri miongoni mwa watumishi vigogo ndani ya Serikali. Mkutano huu wa Waziri Mkuu unakuja katika kipindi ambacho Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania (CHADEMA) kimebadili ghafla mtazamo wake kwa watanzania nje ya nchi na kuanza kufungua utitiri wa matawi, kumwaga Ruzuku na kufanya ziara ya mara kwa mara kwenye matawi yao ili kuwapika makada wake kwa ajili ya uchaguzi wa 2015. Waziri kivuli wa Mambo ya Nje (CDM) Mhe. Dibogo Wenje ndiyo kwanza amemaliza ziara yake hapa London akiwa ameacha ahadi lukuki kwa wafuasi wao akiwataka wajiandae kushika majimbo ya Ubunge na nyadhifa mbalimbali serikalini kunako baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015. Awali, tofauti na CCM, CHADEMA walipinga sana uhusishwaji wa watanzania nje ya nchi katika miradi ya kisiasa na maendeleo ya kitaifa.

Katika hoja za msingi, Waziri Mkuu Pinda anategemewa kuainisha bayana msimamo wa serikali na hatua madhubuti ambazo imezichukua kutafsiri kwa vitendo Sera na Ahadi ya Chama cha Mapinduzi ya kujumuisha suala la Uraia Pacha katika marekebisho mapya ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa uwakilishi wake wa awali ulipokelewa kwa hofu miongoni mwa wabunge, baadhi ya wananchi, wanahabari na wafinyanzi wa Sera katika chelezo mbalimbali za kijamii.

Mashauri mengine yanayotarajiwa katika mkutano huu ni pamoja na maombi ya awali ya CCM UK ya kutaka Serikali iandae utaratibu maalum wa kuwasaidia watanzania waishiao nje ya nchi kupata na kuwekeza katika hazina ya ardhi nchini Tanzania kuliko ugumu uliopo sasa hivi. Aidha Serikali kuhamasisha sekta binafsi za kifedha na mitaji ya jamii kuwafikia watanzania ughaibuni ili kuhamisha teknolojia, ubunifu na uwezo wa kuwekeza katika maeneo kama Kilimo Kwanza na Ujasiria mali wa mizania ya kati.

Pamoja na mahudhurio kutarajiwa kuwa makubwa lakini watanzania wengi wanasemezana kuwa na imani na CCM lakini wanahisi Serikali na mamlaka zake bado hazija chukua hatua madhubuti kupunguza ufisadi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kitaifa.

Na Clement Mbawala

Tanzania Now: Freelance Observers Slough. St.Marys Road. SL3

No comments: