Thursday, March 28, 2013

Mbunge Salim Hemed Khamis Akimbizwa Muhimbili

WADAU NINA SWALI.  Hivi huko Bungeni, hakuna Stretcher ya kubeba wagonjwa?  Je, hakuna watu wa First Aid?   Hii ni mwaka 2013, wanatakiwa wawe na wahudumu wa afya, ambulance, wahudumu onsite yaani pale pale kwenye ofisi za Bunge. Watu wawepo wanaoelewa jinsi ya kubeba wagonjwa. Na hasa huko Bungeni waBunge wengi wana umri mkubwa na matatatizo ya kiafya.  - Chemi

KUTOKA GAZETI LA NIPASHE



Mbunge wa Jimbo la Chambani, Salim Hemed Khamis (CUF), ameugua ghafla wakati akihudhuria kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).


Mbunge huyo alikutwa na masahibu hayo jana na alikimbizwa hospitalini kwa matibabu ambako alilazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU).

Wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Edward Lowassa, na Makamu Mwenyekiti, Mussa Hassan Zungu na baadhi ya wajumbe walimtoa nje ya ukumbi na kumpepea kwa kutumia magazeti na majarida.

Hata hivyo, hali yake ilizidi kuwa mbaya huku akizungumza kwa tabu kuwa alikunywa dawa za shinikizo la damu (BP) kabla hajala chochote na hivyo kuzidiwa.

Wabunge hao na maofisa wa Bunge, waliendelea kumpepea ili apate ahueni, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na kushindwa kuongea kila alipoulizwa jambo.

Walimbeba na baada ya muda waliomba msaada kwa wanahabari waliokuwapo eneo hilo huku wakiwazuia wasipige picha za tukio hilo kwa maelezo kuwa si kila kitu ni habari.

Waandishi watano walisaidiana na wabunge hao kumbeba kwa kupitia mlango wa dharura na alipakizwa kwenye gari la ofisi ya Bunge lenye namba za usajili STK 2178 likiongozwa na pikipiki ya polisi yenye namba za usajili PT 2591.

Gari iliyombeba Mbunge huyo iliondoka kwenye ofisi hizo saa 5:15 asubuhi na habari zilizopatikana baadaye zilieleza kuwa alipelekwa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Baadhi ya wabunge walisema kuwa Khamis akiwa amekaa, ghafla alianza kutapika huku akilalamika kuwa hajisikii vizuri baada ya kunywa dawa za BP na hali yake kubadilika na walisaidiana kumtoa nje ya chumba cha mkutano.

Pamoja na wabunge hao pia, alikuwapo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi.

Waliomsindikiza hospitalini ni Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Amour Arfi (Chadema) na Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF).

Aizungumza na waandishi wa habari baada ya kurejea kutoka Muhimbili, Khalifa alisema Khamis alipokewa na alikuwa anaendelea kupatiwa matibabu.

Khalifa alifafanua kuwa Khamis anasumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Edward Lowassa, alisema hali yake ilikuwa inaendelea vizuri na kuthibitisha kuwa amelazwa ICU. Lowassa alisema kuwa miezi mitatu iliyopita Khamis alikuwa India kwa matibabu. Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Eligaesha, alipoulizwa kwa njia ya simu, alithibitisha kuwa mbunge huyo kupokewa hospitalini hapo na kuongeza kuwa alipatiwa matibabu na anaendelea vizuri. Hata hivyo, alisema taarifa kamili itatolewa na ofisi za Bunge.

Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema hadi jana jioni mbunge huyo alikuwa bado ICU chini ya uangalizi wa madaktari. “Bado yuko ICU. Wanamwangalia. Presure (shinikizo la damu) iko juu, tunampumzisha kidogo,” alisema Joel akijibu swali la NIPASHE kuhusu maendeleo ya afya ya mbunge huyo. Akijibu swali iwapo kuna mpango wowote wa kumpeleka mbunge huyo kupatiwa matibabu zaidi nje ya nchi, alisema: “Tunasubiri ushauri wa madaktari.”

CHANZO: Nipashe

No comments: