Wednesday, March 27, 2013

Siri ya Kuuawa Zitto - Sio Kweli

PRESS RELEASE: 'SIRI YA KUUAWA ZITTO'-SIO KWELI




SIRI YA KUUWAWA ZITTO

Katika gazeti la Mtanzania toleo na. 7269 la Jumatano Machi 27, 2013 kuna habari yenye kichwa chenye maneno ‘ SIRI YA KUUWAWA ZITTO YAFICHUKA’ na vichwa vidogo ‘yadaiwa ilipangwa anyweshwe sumu hotelini’ dk. Slaa atajwa kumtuma Saanane kummaliza’. Habari hii imeniletea usumbufu mkubwa kwani ndugu, jamaa, marafiki na wapiga kura wangu, wamejazwa na wasiwasi mkubwa sana kwamba ninaweza kuuwawa. Napenda kusema yafuatayo:

Moja, sijawahi katika maisha yangu yote kukutana na mtu anayeitwa Ben Saanane na hivyo hicho kikao ambacho inasemekana nilikuwa naye na akajaribu kunipa sumu hakijawahi kutokea. Imetajwa Hoteli ya Lunch Time ambayo sio tu sijawahi kufika, pia hata siijui ipo wapi. Haijawahi kutokea mimi kufanya kikao cha pamoja na Ben Saanane, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba. Hivyo habari iliyoandikwa ni ya kufikirika na hivyo naomba mwandishi ahakikishe kuwa vyanzo vyake vya habari vimempa habari sahihi.

Pili, Siamini kamwe kuwa Katibu Mkuu wa chama changu anaweza kupanga kuniua maana hana sababu ya kufanya hivyo. Napenda kurudia kusema kwamba mimi ninaamini kuwa kila nafsi itaonja mauti. Kila mtu atakufa. Kama nitakufa kwa kuuwawa na mtu mwingine ndio itakuwa nimeandikiwa hivyo na Mungu. Ndio maana hata siku moja silalamiki kuhusu vitisho vya kuuwawa nk. Kama kuna mtu anafikiria kuwa kumuua Zitto ndio furaha ya maisha yake atakuwa anajidanganya tu maana Zitto anaweza kufa kimwili lakini mawazo, fikra na maono ya Zitto yataishi tu. Siogopi kufa maana maisha niliyoyachagua ndio haya ambayo yamejaa vitisho. Muhimu kwangu ni kufanya kazi zangu kwa bidii, uhodari na uaminifu. Siku zote nitasimamia ukweli bila kujali uchungu wa ukweli huo.

Tatu, nawashauri watu ambao wamehama CHADEMA na kuhamia vyama vingine watumie muda wao kujenga vyama vyao badala ya kila siku kuzungumzia masuala ya chama ambacho wao sio wanachama tena. Kama mtu kaamua kuhama CHADEMA anapoteza haki ya kujadili masuala ya CHADEMA maana kama angekuwa anapenda kuyajadili asingehama. Naonya mtu yeyote ambaye anatumia jina langu ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa. CHADEMA sio pango la watesaji wala wauaji. Kama kuna mwanachama wa chama kingine cha siasa anayedhani kuna mtu ndani ya CHADEMA anapanga mipango ovu aende kwenye vyombo vya sheria kumshtaki. Matendo ya mtu mmoja yasifanyiwe propaganda kama ni malengo ya taasisi.

Nne, Nawashauri viongozi wa CHADEMA na hasa wanachama tutumie muda wetu kujenga mshikamano ndani ya chama. Fitna, majungu, uongo, uzandiki nk kamwe havijengi chama. Chama chetu lazima kiwe mfano bora wa kuheshimu demokrasia na haki za binaadamu. Wananchi hawawezi kutoa dola kwa chama chenye mifarakano. Tusiruhusu kugawanywa kwa matakwa ya watu wachache. Tusimamie misingi ya kuanzishwa chama chetu.

--

Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Dar-es-Salaam
Jumatano, Machi 27, 2013

2 comments:

Anonymous said...

Leo anayasema aliyotokanayo Chadema,kesho atayasema atakayotokanayo CCM na vivyo hivyo atayasema atakayotoka nayo serikalini,hawa si watu wa kufanya nao kazi,iwe serikalini,ktk vyama vya siasa,ama ktk biashara.
labda nimweleze jambo moja huyo kijana,si alama hata hapo alipo,maana hata hao alionao hawataweza mwamini kwa lolote lile maana ni mwepesi kusema chochote kile kwa jinsi atakavyo jisikia.
Vijana acheni kutumika,jitafutieni ridhiki kwa nguvu zenu,anayekutumia leo kesho hatafanya hivyo tena,maana dhamani yako itakuwa ni kama toilet paper.

Mh. Zitto Kabwe said...

NINAVYOMFAHAMU ZITTO ZUBER KABWE - KILIO CHA USALITI (Sehemu ya Tatu)

Mimi nilaumiwe kwa lipi?

Nimesema hicho kikao wanachosema mie nilikuwa nipewe sumu hakijawahi kutokea. Hakipo. Huyo mtu athibitishe kuwa kilikuwepo.

Mwandishi anasema Saanane alipewa sumu aniuwe, Mwampamba athibitishe kuwa ameshawahi kukutana na mimi, yeye na Saanane kwa pamoja.

I am too senior kukaa na watoto kama kina Mwampamba kujadili mikakati ya kisiasa. Kuna jambo siwezi kufanya katika maisha yangu ie kusaliti chama changu ambacho nimekijenga kwa jasho na damu. Walioingia chadema baada ya kuona tumaini jipya, kama wanaona maslahi yao hafikiwi waondoke kama Mwampamba lakini sisi tuliowekeza muda wetu na akili zetu kwenye chama hiki cha chadema kamwe hatutaondoka. Tofauti zetu tutazimaliza kwa vikao vya chama na sio kwa kukimbilia CCM.