Tuesday, March 12, 2013

Poleni Kwa Baridi Huko London!


Kaka Freddy Macha huko London, Uingereza ameleta taarifa hii.
BARIDI KALI LEO LONDON

by Kitoto

Wamesema mara ya mwisho baridi kali namna hii kutokea visiwa vya Uingereza ilikuwa miaka 30 iliyopita.

Leo kila mtu nliyekutana naye jijini: mzee, mtoto, mwanaume, mwanamke, alilalama na kulaani baridi.Hata "maglovu" nliyovaa mkononi hayasaidii. Ngumi haikunjiki sawasawa. Miti kule nyuma imepukutika matawi- zimebaki tu kuni kavu. Ndevu zangu zimenyaushwa. Upepo wa kutoboa kisindano sindano ulikuwa ukisaidia baridi kuwa kali zaidi.

Aliyewazidi wote kwa malalamishi alikua ajuza mmoja mzawa wa visiwa vya Karibian. Alihamia hapa miaka 55 iliyopita.

"Nlikuja kusoma na kutafuta ajira. Sipendi na siizoei baridi hata kidogo."

Nkamuuliza kama haipendi baridi kwanini harudi tu kwao kwenye ujoto joto?

Basi linapitisha abiria waliojikunyata ndani.

Ajuza akajibu keshapazoea; lakini asichokiweza baridi.

Rudi basi kwenu.

Ajuza akacheka.

"Baridi kama hii ya leo sijapata kuona." Nilikisia umri wake ushapita miaka 70 na kitu.

Tulikua katika foleni posta. Foleni ndefu kidogo.Foleni za Ulaya, hizo; kila mtu kimya; nje baridi kali.

"Nkishaondoka hapa nakwenda kulala," akatangaza.

Kweli nje palikua kiama.

Kawaida hii sehemu ya kuchezea watoto katika mtaa ninaoishi -huwa imejazana vijana wakicheza kila aina ya utoto, lakini leo palikuwa patupu kama jangwa la Sahara.

Kawaida barafu inapodondoka baridi hupungua, watoto wanacheza; lakini ya leo ilikua na matone machache tu ya barafu. Imeongozana na upepo mkali - wanasema toka Siberia.

No comments: