Monday, March 18, 2013

Utekaji watu Tanzania: Baada ya Kibanda Nani Atafuata?


Wadau,  hivi karibuni yametokea matendo ambayo hatjuazaoea kusikia Tanzania. Waandishi wa Habari, Viongozi wa Dini kutekwa, kuteswa na kuuawa!  Gazeti la Mwanachi inachambua.

************************
Kutoka Gazeti la Mwananchi

Posted Jumatatu, Marchi18 2013

Kwa ufupi

Ni matukio ambayo yameacha maswali mengi zaidi ya majibu, huku wengine katika jamii wakisaka mchawi. Polisi na hata vyama vya kijamii, kila mmoja akiibuka na msimamo wake. Hata hivyo, si rahisi kusema ni lini jibu litapatikana!

Padri Auawa Zanzibar kwa Risasi

Tukio lingine ambalo lilishtua wengi ni la kuawa kwa Padri Evarist Mushi, Paroko wa Parokia ya Minara Miwili , Zanzibar. Yeye, aliuawa kwa kupigwa risasi kichwani na kufa papo hapo na watu wasiojulikana asubuhi akielekea kanisani.

Msemaji wa Polisi Zanzibar, Inspekta Mohamed Mhina alithibitisha tukio hilo huku akisisitiza kuwa uchunguzi wa kina zaidi ungefanyika kuhakikisha waliofanya hilo wanachukuliwa hatua.

Mwingine Apigwa Risasi

Awali, Kabla ya kuuawa padri Mushi, padri mwingine, Ambrose Mkenda naye alipigwa risasi na watu wasiofahamika kwenye lango la nyumba yake maeneo ya Kitomondo mjini Zanzibar, ambako ndiko makazi yake yalipo akiwa ndani ya gari aliyokuwa akiendesha pekee yake.

Hali yake siyo nzuri kwani risasi aliyopigwa imemdhuru maeneo ya mdomoni na hadi sasa bado hajaweza kuwa imara. Waliompiga risasi padri huyo inasemekana ni watu waliokuwa kwenye pikipiki, ambao walimvamia akisubiria afunguliwe geti kuingia nyumbani kwake.

Katibu wa Mufti Amwagiwa Tindikali

Pia Zanzibar ilikumbwa na tukio la linalofanana na matukio hayo kwani kiongozi mwingine wa dini aliingia kwenye msukosuko.

Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, alimwagiwa tindikali na watu wasiyojulikana huko Magogoni Msumbiji Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Yussuf Ilembo, alisema Sheikh Soraga alimwagiwa tindikali majira ya alfajiri alipokuwa akifanya mazoezi ya viungo.

Ni kwamba wakati akifanya mazoezi, alimuona mtu akifanya mazoezi akielekea mbele yake na baada ya kukutana uso kwa uso alimmwagia tindikali na kumjeruhi sehemu za usoni na kifua kabla ya mtu huyo kutoweka.

Dk Stephen Ulimboka

Kiongozi wa jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Stephen Ulimboka, saa sita usiku alitekwa, kupigwa na watu watatu wenye silaha na kisha kutupwa maeneo ya mabwepande ambapo aliokotwa na kupelekwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI) jijini Dar es Salaam.

Wengi wanahoji sababu ya kutekwa Dk Ulimboka, hasa kutokana na ukweli kwamba si mfanyabiashara…Nani alimteka kwa lipi? Ni swali lisilo na jibu.

Dk Ulimboka aliwahi kuwaambia waandishi wa habari na baadaye akasisitiza kauli hiyo kupitia wanasheria wake, Oktoba 2012, kuwa aliyehusika na mipango ya kutekwa na kuteswa kwake ni Ofisa wa Ikulu. Kama ni kweli, je, ofisa huyo alitumwa au alijituma ? Na je, aliwahi kuhojiwa polisi ili Ikulu ijisafishe kutoka katika madai haya ya Dk Ulimboka?

Waandishi wa Habari Wauawa

Baadhi ya waandishi wa habari waliouawa katika mazingira ya utata ni pamoja na wa Kituo cha Redio Kwizera wilayani Kakonko mkoani Kigoma, Issa Ngumba (45) ambaye aliuawa kwa kunyongwa na kisha kupigwa risasi mkono wa kushoto.

Mwili wake ulipatikana katika pori la Mlima Kajuluheta Kijiji cha Muhange, wilayani humo asubuhi baada ya wananchi kufanya msako wa siku tatu mfululizo bila mafanikio.


Lakini, pia vitendo kama hivyo vinawakuta wenye ulemavu wa ngozi ambao wengi wameathirika , lakini waliohukumiwa kunyongwa tangu mwaka juzi mpaka sasa hawajanyongwa.

Richard Masatu Auawa

Richard Masatu aliuawa Agosti 2011. Yeye, alikuwa Mkurugenzi wa gazeti la KASI MPYA, alifia Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure mjini Mwanza, akipatiwa matibabu. Taarifa za awali zinaonyesha kuwa marehemu alifariki kutokana na majeraha ya kushambuliwa na watu wasiojulikana.

1 comment:

Anonymous said...

Jana Machi 22, 2013 kwenye kipindi cha kipima joto cha ITV mtakumbuka
kuwa mwanamabadiliko mwenzetu Marcossy Albanie alikuwa kwenye kipindi
ITV kujadili mada iliyo kuwa inahusu Rushwa.

Pamoja na michango mingine alidadavua kwa kina mamlaka makubwa aliyo
kuwa nayo DPP na kushauri kuwa ni miongoni mwa mamlaka zinazo takiwa
kuwa huru bila kuingiliwa kimamuzi na mamlaka zingine za juu, alitaja
pia taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa kuwa inatakiwa kuwa huru,
tume ya taifa ya uchaguzi pamoja na mhimili wa mahakama.

Kilicho nishangaza leo kwenye tahariri ya the guardian on sunday
wamechukua maoni yaliyo semwa na Marcossy kwenye kipima joto bila hata
ku- acknowledge source. Naamini haikuwa coincidence kwa sababu mengi
yaliyo zungumzwa jana ndio yameandikwa kwenye gazeti la leo.

Hili ndio limenifanya kujiuliza, je The Guardian nao wameanza kuwa
beba beba kama gazeti fulani lililo wahi kuandika kuhusu vijana
mapacha wa kitanzania wanao soma (ambao hawasomi) Havard?.