Thursday, December 27, 2007

Mbwa waua Dar

Nimeandika kuhusu Tiger kuua huko California. Naingia ippmedia.com na kusoma habari ya mbwa kuua mlinzi huko Mbweni, Dar. Mauji yalitokea kwenye mradi ya kufuga kuku wa Idel Chicks.

Kwanza kwa nini wanafuga mbwa wengi hivyo? Je, huyo mbwa wanalishwa vizuri?
Je, ni mbwa wa aina gani? Maana kuna aina ya mbwa kama Rottweiler, German Shepard, Doberman, Pit Bull, ambao ni hatari kwa binadamu kama hawatunzwi vizuri.

Huko Bongo nimesikia watu wakisema kuwa ni vizuri kuwa na mbwa kama mlinzi kuliko binadamu na hata hapa Marekani wanasema hivyo hivyo. Lakini mbwa lazima atunzwe kusudi aweze kukaa na binadamu.

Je, hiyo kampuni iliona ni bora kuwa na mbwa kuliko walinzi binadamu kwa vile ni bei rahisi kuliko kulipa mishahara ya walinzi? Na hao mbwa wengi hivyo wangeshikwa na njaa wangeweza kuvunja mabanda na kula hao kuku!

Hata hivyo ukifuga mbwa wengi wanakuwa na 'pack mentality'. Hiyo ni tabia yao ya asili ya kuwinda pamoja. Ni kama binadamu wakiwa wengi wanapata 'mob mentality' na kufanya maajabu bila kujali matokeo yake, japo kwe muda mfupi.

Mungu ailaze roho ya huyo mlinzi, Muhidin Said, mahali pema peponi. Amin.

****************************************************************

Kutoka ippmedia.com

Mbwa waua mtu Dar

2007-12-27

Na Mwanaidi Swedi, Jijini

Mlinzi aliyefahamika kwa jina la Muhidin Said, anayefanya kazi kwenye shamba kubwa la mradi wa kuku la Idel Chicks, amefariki dunia baada ya kujeruhiwa vibaya na mbwa wanaomsaidia katika kazi yake ya ulinzi.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi, Jamal Rwambow, amesema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa 4:30 usiku huko Mbweni, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam kwenye shamba la mradi huo linalomilikiwa na Bw. Mohamed Hamduni.

Amesema kuwa mlinzi huyo alikumbwa na mkasa huo wakati anawafungulia mbwa hao wapatao 30. Amesema kuwa wakati anawafungulia, mbwa 15 kati ya hao walimvamia na kuanza kumjeruhi vibaya kabla ya kumuua.

Aidha, amesema kuwa mlinzi huyo ni wa kila siku na aliajiriwa kwa kazi hiyo. Akasema, cha kushangaza, siku hiyo mbwa wale walimbadilikia na kumletea maafa hayo. Amesema mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mwananyamala.

No comments: