Friday, August 27, 2010

Hii Itasaidia Wasanii Tanzania Kweli?

Naona kutukuwa na kazi hapo. Je, BASATA itaweza kukidhi mahitaji ya wasanii wa Tanzania nzima? Na hayo mambo ya vibali, watu watapata kwa urahisi au mpaka utoe bahasha. Ina maana ukitaka kuunda kikundi kijijini kwako na kufanya onyesho, ndo mpaka upate kibali kutoka Dar? Hebu nisaidie kuelewa. ila kweli hiyo suala ya haki miliki, residuals, ni muhimu.
**************************
MARUFUKU WASANII WASIOSAJILIWA KUSHIRIKI SANAA NCHINI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

USHIRIKI WA WASANII WASIOSAJILIWA KWENYE TUNZO NA MATUKIO YA SANAA NCHINI


Baada ya BASATA kusimamia na kuratibu uanzishwaji wa Mashirikisho manne ya Sanaa nchini ambayo ni Shirikisho la Sanaa Jongevu (Filamu), Shirikisho la Muziki Tanzania, Shirikisho la Sanaa za Maonyesho na Shirikisho la Sanaa za Ufundi kwa lengo la kuvipa nguvu vyama vya wasanii na kuvipa umoja kitaifa,Baraza linapeleka nguvu kwenye urasimishaji wa sekta ya sanaa ikiwa ni pamoja na wadau wote wanaojihusisha na sekta hiyo hususan wasanii.

Kwa mujibu wa Sheria na. 23 ya Bunge ya mwaka 1984, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limepewa jukumu la kutambua na kusajili wadau wa Sanaa, kumbi zote za burudani Tanzania Bara na wasanii wote ikiwa ni pamoja na kutoa vibali vya kufanya shughuli za Sanaa.

Lengo ni kuzifanya shughuli za sanaa kufanyika katika mazingira rasmi na ya kufuata sheria za nchi pia kuwatambua wasanii wote nchini kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi yetu.Ikumbukwe kwamba, kufanya shughuli za sanaa bila kusajiliwa na kupewa kibali na BASATA ni kuvunja sheria za nchi na hivyo kustahili adhabu.

Faida za kurasimisha sekta ya sanaa hususan kwa wasanii

1. Kuendesha shughuli za sanaa kwa mujibu wa Sheria za nchi ili kuepuka usumbufu.

2. Kutambulika kwa shughuli ya msanii binafsi, kikundi, Chama nk. hivyo kufanya kazi kihalali.

3. BASATA kama shahidi wa Jamhuri hutoa utambulisho/uthibitisho kwa msanii, kikundi au chama halali mahali popote panapohitajika kwa mfano wakati wa kufungua akaunti benki, kupata VISA, pasi ya kusafiria, mikopo kwenye asasi za fedha, msaada au ushahidi mahakamani.

4. Ikihitajika kuweka ulinzi wa kisheria wa kazi za sanaa,kwa mfano wa Hakimiliki na Hakishiriki.

5. Kuingilia kati pale makubaliano/mikataba ya msanii, kikundi, chama nk. inapokiukwa na kuripotiwa katika Baraza.

6. Kushauri na kutoa mafunzo ya sanaa.

7. Kutafutiwa masoko na/au kuunganishwa na masoko, wasanii na fursa mbalimbali zinapojitokeza.

BASATA linawaagiza waandaaji wa matukio ya sanaa nchini (Tunzo za Sanaa/matamasha/maonyesho) kuhakikisha wanafanya kazi na wasanii waliosajiliwa tu na inapotokea kufanya vinginevyo basi muandaaji wa tukio husika na msanii atawajibika moja kwa moja.

BASATA linatoa hadi tarehe 31 Oktoba, 2010 kwa wasanii na wadau wote nchini kujisajili vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwazuia wasanii pia wadau wasiosajiliwa kushiriki tunzo/matamasha/Matukio ya Sanaa.

Ghonche Materego

KATIBU MTENDAJI, BASATA.

2 comments:

Anonymous said...

Njia nyingine ya kupata hela ya chai.

Anonymous said...

Tanzania kila kitu ni mkao wa kula. Sasa mtasikia malalamiko. Au vibali mpaka mhonge fulani. Au kusajiliwa mpaka utoe bahasha enye 50,000/-. Show mpaka upelke 200,000/- kwa fulani!