Tuesday, June 14, 2011

Mchoraji Raza Kufanya Maonyesho LondonHabari Zimeletwa na Mdau Freddy Macha

Mchoraji wa rangi, vitabu na stempu, Raza Mohamed anatazamiwa kufanya maonyesho ya picha zake katika ukumbi wa Mulberry Tea Room, Charlton House, kitongoji cha Greenwich Ijumaa tarehe 17 Juni hadi Jumatano 20, Julai mwaka huu.

Raza Mohamed ambaye ni hazina ya taifa letu amekuwa akichora toka akiwa mtoto wa miaka sita tu mwaka 1952. “Nilianza kwa mkaa...” alisema nilipomhoji nyumbani kwa mwanae, jana.

Michoro yake Raza huonyesha taswira mbalimbali za maisha ya Watanzania, wakiwemo watoto wadogo, wanawake, watu wazima, wavuvi, wafanyakazi mbalimbali, nk. Amewahi kuonyesha michoro hiyo katika majumba mbalimbali ya utamaduni Marekani, Norway, Ujerumani, Kenya, Denmark na pia matamasha ya kimataifa mathalan Festac, mjini Lagos, Nigeria, mwaka 1976.

Raza ambaye ni pia mjumbe katika kamati ya Sanaa katika Ikulu amewahi pia kuwachora Marais wote wanne wa Tanzania yaani, Mwalimu Nyerere( 1965), Ali Mwinyi, Benjamin Mkapa na Rais Jakaya Kikwete.

Mwanae, Eddy Mohamed anatazamiwa pia kushiriki katika maonyesho haya ya Charlton House. Kama babake, Eddy amekuwa pia akisanifu michoro tangu akiwa na umri mbichi wa miaka 6. Alizaliwa Oktoba, 1940, akamalizia shahada ya Sanaa katika chuo cha East London University, Docklands.

Baba na kijana wake wote wameeleza mapenzi yao makubwa katika uzuri wa Tanzania na hutumia fani ya muziki wa Jazz kujihamasisha kazini. Jazz iliyoasisiwa Marekani na wanamuziki weusi mwanzo wa karne ya 20 inayo mizizi katika utamaduni na ngoma za Waafrika. Kati ya picha kubwa zitakazoonyeshwa na Eddy ni ile aliyomchora gwiji maarufu wa jazz , mpiga Saxafoni, Charlie Parker aliyefariki mwaka 1955 akiwa na wenzake.

Mara ya kwanza picha zake Mzee Raza kuonyeshwa hapa London ilikuwa wakati wa mkutano wa Watanzania Ughaibuni (Diaspora) mwezi jana. Ila onyesho hili ni la kwanza la kimataifa na linategemewa kutumbuizwa na mwanamuziki Mtanzania. Freddy Macha.

Tafrija nzima imeandaliwa na shirika la sanaa la Global Fusion Music and Arts (GMFA) lenye makao yake Greenwich. GMFA inayoendeshwa na wasanii toka mataifa mbalimbali mjini London ilianzishwa mwaka 2001 na wanamuziki Louisa Le Marchand (Uingereza), Kaz Kasozi (Uganda), marehem Sukh Saini (India) na Gill Swan Uingereza).

Habari zaidi tembelea www.globalfusionarts.com

Barua pepe: globalfusionarts@yahoo.co.uk

Blog: www.kitoto.wordpress.com

Simu: 0208-858-9497

Mobaili: +44-7976-941-435 begin_of_the_skype_highlighting +44-7976-941-435

1 comment:

SIMON KITURURU said...

Asante kwa taarifa!