Sunday, May 06, 2012

Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU)


Taarifa ya Kuundwa kwa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU)
Tuna furaha kuwatangazia wakereketwa wote  wa Kiswahili duniani, walioko  barani Afrika na kwengineko pia, kuhusu kuundwa  kwa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili  Duniani(CHAUKIDU). Chama hiki kitakuwa na makao yake makuu katika mji anamoishi na kufanya kazi Rais wa chama, na kwa sasa ni katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, Marekani. Madhumuni makuu ya Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) ni: Kuwajumuisha pamoja waendelezaji wa Kiswahili duniani kote kwa lengo la kuchochea kasi ya malengo mahususi yafuatayo:

1.Kukuza Kiswahili katika nyanja zote ambamo lugha hii inatumika au inaweza kutumika na kuongeza ufanisi wa mawasiliano katika ufundishaji na utafiti wa maarifa ya aina zote, uandishi/utangazaji wa habari, uandishi wa vitabu, uchapishaji vitabu na majarida, utayarishaji wa safari za mafunzo katika Afrika ya Mashariki na Kati, nk.

2.Kusambaza habari na matokeo ya utafiti kwa kutumia kijarida, jarida, na teknolojia ya mtandao wa kompyuta juu ya vipengele mbalimbali vya Kiswahili na masuala yanayohusiana na Kiswahili.

3.Kujumuisha pamoja wanachama kwa ajili ya kubadilishana mawazo na tajiriba zao katika masuala mbalimbali yanayohusu Kiswahili (k.v. uboreshaji wa ufundishaji, utangazaji, utafiti, uandishi, nk.) kwa njia ya mkutano wa kila mwaka, warsha au semina au kongamano maalumu, na hata kwa njia ya mtandao.

4.Kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kujivunia, kuendeleza, na kuheshimu Kiswahili.

5.Kushauri ama kushinikiza serikali za nchi ambamo Kiswahili kinazungumzwa kutambua thamani iliyobebwa na maliasili hii ili kuunda sera muafaka za kukiendeleza kadri ya uwezo wake kwa manufaa ya maendeleo ya serikali na watu wake kijamii, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, n.k.

. Chama hiki kimeundwa baada ya miaka mingi ya miito, matayarisho, na majadiliano mbalimbali baina ya wakereketwa kutoka pembe mbalimbali  duniani ambao wote kwa jumla walidhamiria kuwepo chama ambacho kitashirikiana na vyama vingine vya Kiswahili na asasi nyingine mbalimabli kukisukuma mbele Kiswahili kipate hadhi na ukuzaji muafaka ndani na nje ya Afrika.
Chama hiki cha CHAUKIDU kimebuniwa na kuzinduliwa baada ya katiba kupitishwa kwenye kikao maalum kilichofanyika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison mnamo Aprili 26, 2012. Wanachama watarajiwa ni pamoja na walimu, watafiti, wanafunzi, waandishi wa habari, wasanii, waandishi wa vitabu, wachapishaji, maafisa utalii, taasisi, n.k .Tayari Bodi ya Uongozi imechaguliwa na imeshaanza kutekeleza hatua za mwanzo za urasimu kuhusiana na chama.  Bodi imewachagua Dkt.Ken Walibora kuwa Rais wa CHAIUKIDU, Dkt. Leonard Muaka, Mkurugenzi, Bi Zeinab Iddi, mhariri, na Bi Judith Namayengo, katibu.  Washiriki wote wa Bodi ya Uongozi ni kama wafuatao:

1. Bi. Zeinab Iddi (Chuo Kikuu cha Taifa, Zanzibar)
2. Bw. David Kyeu (Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison)
3. Dkt. Clara Momanyi (Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki)
4. Dkt. Lioba Moshi (Chuo Kikuu cha Georgia)
5. Dkt. Leonard Muaka (Chuo Kikuu cha Winston Salem)
6. Dkt. Samuel Kamau Mukoma (Chuo Kikuu cha San Francisco)
7. Bi. Judith Mayanja (Chuo Kikuu cha Wisconsin- Madison)
8. Prof. F.M.K. Senkoro (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam)
9. Dkt. Ken Walibora Waliaula (Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison)

Bodi ya Uongozi inawashukuru waasisi wa chama kama vile Dkt. Katrina Thompson, Dkt. Mahiri Mwita, Dkt. Charles Bwenge, Bwana Deo Tungaraza na Dkt. Alwiya Omar na wengineo ambao wamejitolea kwa hali na mali na kujikusuru vilivyo katika kupanga mikakati  ya kuundwa kwa chama hiki. Kwa niaba ya wanachama wote,  waliomo chamani na watarajiwa, tunafurahi sana kuhusishwa na tukio hilo la kihistoria  hatuna budi kutangaza kujitolea kwetu kutekeleza majukumu ya chama kwa mujibu wa katiba ya chama na kwa kuzingatia matarajio  na maslahi ya wanachama wote. Ni matamanio yetu kwamba kwa ushirikiano wa wote wanaohusika na watakaohusika, CHAUKIDU, kitatoa mchango wake mkubwa katika ukuzaji wa Kiswahili barani Afrika na kwengineko duniani.


Dkt. Ken Walibora Waliaula, Rais wa CHAUKIDU
Profesa Mwandimizi katika Idara ya Fasihi na Lugha za Kiafrika
Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison
Baruapepe: waliaula@wisc.edu
Simu: 608-262-8983

4 comments:

emuthree said...

Duuh, hii imekaa vyema,jamani tusaidie hili ili lugha yetu iwe miongoni mwa lugha za kimataifa, ...maana moja ya kitu kinachopunguza nguvu ya elimu hasa huku kwetu ni lugha....

Kumbuka mtoto ana lugha yake ya asili, anatakiwa ajifunze kiswahili na bado ili aonekane kasoma anatakiwa akijue kiingilishi...kazi kweli kweli

Anonymous said...

Kujiunga unafanyaje nataka sana na niko huku kwa Obama

Anonymous said...

ni suala zuri sana,je kujiunga unafanyaje mimi ni Igira,Frank E.mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar es salaam

Anonymous said...

chama kikubwa kama hiki kina undwa wakati sisi walengwa hatujui,basi si wote hata sisi wasomi wa lugha hii,kingine kwa nini makao makuu ya chama hiki yawe marekani wakati lugha hii ni ya taifa la Tanzania?kuna mambo hapa hayaendi sawa,tunaomba udhibitisho wa swala hili sisi kama wenye lugha hii