Thursday, January 10, 2008

Siku nilivyokamtwa na polisi Dar


februari 14, 1992: waandishi godfrey lutego wa uhuru na mzalendo (shoto) na chemi che mponda wa daily news wakiwa na mwanyekiti wa uwt mkoa wa dar mh. mary kabigi wakitoka kituo cha polisi cha msimbazi walikowekwa chini ya ulinzi kwa kuvamia ofisi za uwt mkoa wa dar na kuhatarisha usalama wa katibu mkuu wa uwt mkoa huo e.h. stima. hapo wanatoka kituoni hapo baada ya kuandika maelezo yao. da'chemi tupe stori nini kilitokea na yaliishaje?
Someni jibu langu kwa Michuzi chini:
************************************************************************************
Hi Michuzi,

Asante kwa hiyo picha. Umenikumbusha mbali! Wakati huo mimi ndo nilikuwa mpigania haki za akina mama hasa na ndio maana nilipangiwa hiyo kazi siku hiyo.

Yalikuwa hivi. Nilienda kazini Daily News kama kawaida. Baada ya post-mortem nilipangiwa kazi UWT kumhoji Mama Mary Kabigi (sasa marehemu) alikuwa na tangazo fulani. Kule nilikutana na na Godfrey Lutego wa gazeti la Uhuru.

Tulikaribishwa vizuri mle ofisini, ilikuwa na deski mbili. Kulikuwa na viti mbele ya deski ya Mama Kabigi na tulikaa hapo. Kwenye deski nyingine kulikuwa na mama mwingine Mama Eshe Stima. Mama Kabigi alilmtambulisha Mama Stima kwetu. Ajabu Mama Stima hakujibu. Mama Kabigi alianza mahojiano huko Mama Stima ana nuna na kuguna. Ghafla aliinuka na kutoka ofisini na kufunga mlango. Tuliendelea na mahojiano na Mama Kabigi. Kukaa kidogo tukasikia mlango unafungwa na ufunguo.

Mama Kabigi aliuliza kama tumesikia mlango unafungwa. Mimi na Godfrey tulibaki tunatazamana na kujibu ndiyo. Basi tulimaliza mahojiano na kutaka kuondoka. Tulishindwa kutoka mle ofisini kwa vile mlango ulikuwa umefungwa kutoka nje.

Basi Mama Kabigi alisema tukae tusibiri. Kulikuwa hakuna simu mle ndani ya ofisi na enzi hizo hakuna cell phone. Tulisubiri kama saa moja hivi, mlango ulifunguliwa.
Ilivyofunguliwa Mama Stima kaingia mle na mwanaume na mwanake waliokuwa serious kweli na kuelekea kwetu kwa hasara. Kumbe walikuwa ni polisi waliovaa kiraia.

Mama Kabigi, mimi na Godfrey tukaambiwa tuko chini ya ulinzi na hao watu! Doh! Tukaanza kuwauliza sababu ya kutuweka chini ya ulinzi.
Hawakusema kitu zaidi ya kuwa tutaelezwa kituoni. Tuliwaambia kuwa sisi ni waandishi wa habari tuko hapo kikazi na tuliwaonyesha vitambulisho vyetu. Hawakutuka kuviona.

Basi tulikamatwa na kutembezwa kwa kushikwa mikono kipolisi barabarani hadi kituoni. Tulivyokuwa tunavuka barabara mhariri wa Daily News na aliyenipangia assignment hiyo, Mkumbwa Ally alipita na gari. Nikafoka, "Mkumbwa!"

Mkumbwa alisimamisha gari huko najaribu kumwelezea kuwa tumekamatwa na polisi. Wale polisi walinifokea ni nyamaze. Mkubwa alitoka kwenye gari alinishika mkono mwingine na kumwambia yule polisi wa kike, “Huyo anakwenda na mimi!” Yule polisi akasema Hapana wanakwenda kituoni wako chini ya ulinzi!” Basi Mkumbwa alikuwa hana la kufanya. Aliwauliza tunapelekwa wapi. Walimwambia na yeye aliondoka.

Kufika kituoni, tulikalishwa kwenye benchi ndani ya kituo kama masaa mawili. Eneo tuliyokalishwa ilikuwa chafu sana halfu ilikuwa giza. Kila tukiuliza sababu ya kukamatwa hatuambiwi!

Basi kama baada ya masaa mawili na nusu hivi, tulipelekwa ofisini kwa mkuu wa kituo. Tuliingizwa mle moja moja na kuulizwa ilikuaje. Nakumbuka nilimwonyesha huyo mkuu wa kituo kitambulisho changu na kumwelezea mambo yalivyokuwa na kurudishwa kwenye hiyo benchi. Baadaye tulikalishwa wote pamoja na huyo Eshe Stima ofisini kwa huyo mkuu wa kituo.

Mama Stima alisema hivi, "Nilikuwa nimekaa ofisini kwangu. Huyo Mama Kabigi kamleta huyo mwanamke na huyo mwaname mle. Walinitishia kuwa wataniua, walianza kunipiga, niliweza kukimbia kwenda kituoni kutafuta msaada!"

Alisema kama mara tatu. Wewe! Mbona tulibakia kushangaa na kusema huyo huyo mama Stima ni mwongo mkubwa. Tukasema yeye ndiye alikuwa mkali kwetu maana tulimsalimia ha hakujibu halafu alitufungia ofisini.

Sasa huko nje, front deski ya kituo kulikuwa na mambo, alikuja Mzee Millinga kutoka Daily News, mwakilishi wa gazeti la Uhuru (jina nimesahau), mtu wa RTD na Lucas Lukumbo wa SHIHATA. Nakuambia habari zilienea haraka kweli. Nje ya kituo kulikuwa na magari ya vyombo vya habari na wananchi nje wanauliza kuna nini mle ndani.

Basi baada ya muda yule Mkuu wa Kituo alisema kuwa tunaruhusiwa kuondoka. Nikamwuliza sababu anaturuhusu kuondoka alisema, kuwa sisi wote tulikuwa na story sawa. Godfrey alimwambia mkuu wa kituo kuwa kwa kweli hajafurahi kunyimwa uhuru wake!

Mimi nililalamika kuwa tumeshikwa kwa upuuzi. Nilisema kuwa ina maana kuwa mtu yeyote anaweza kutunga uwongo na mtu akamtwe hivi hivi! Wale wakilishi wetu walituambia tuchukue vitu vyetu tuondoke.

Mbona ilikuwa raha kutoka nje ya kituo cha polisi ukiwa mtu huru.

Na kesho yake, hiyo habari pamoja na picha ilikuwa FRONT PAGE news kwenye magazeti ya DAILY NEWS na UHURU.

Huyo Mama Stima aliishia kuaibika, hasa kwa vile alituingizia kwenye ugomvi wake na Mama Kabigi. Mpaka sasa sijaelewa hasa ugomvi wao ulikuwa nini, lakini nilivyosikia ni kuwa yule Mama Stima alionywa vikali kuhusu kusema uwongo polisi, na wale polisi walionywa maana walivyotukamata ilikuwa si sahihi. Nadhani aliharibu urafiki wake na yule Rafiki yake polisi siku hiyo maana majina yalitoka kwenye gazeti! Wengine walisema kuwa walikuwa wana ugomvi juu ya nafasi ya uongozi wengine walisema waligombania bwana. Sijui ukweli uko wapi. Ila nilijikutwa nimeingizwa kwenye ugomvi wao.

Siku hiyo naiwrite off kama, "Ajali Kazini! - Adventures of a Journalist!”

Lazima niseme kuwa niliendelea kuwa na uhusiano mzuri na Mama Kabigi. Baadaye alikuja kuwa Mbunge wa akina mama (viti maalum). Na nilimwona kama mtu anayependa kutetea haki za akina mama. Huyo Mama Stima sijui aliishia wapi.
- Chemi

10 comments:

KKMie said...

Eh! Mambo ya wanawake na chuki zao za kizembe eti? Natambua yamepita lakini Pole tena Da' Chemi japo nina hakika ukikumbuka sasa unaishiakucheka tu.

Wakati huo mimi ndio nilikuwa namaliza mwezi toka nimejiunga kidato cha kwanza.

Anonymous said...

Dada Chemi. Kwanza nikupe pole kwa yaliyokupata.

Nakujulisha kuwa Esha Stima yuko CCM NEC viti vya UWT. Mama Kabigi alifariki dunia mwaka 1999.

Asante.

Chemi Che-Mponda said...

Anonymous wa 1:35PM, asante kwa taarifa kuhusu Mama Stima. Ndiyo nilikuwa na habari ya kifo cha Mama Kabigi. Mwanae Agnes Kabigi, alinijulisha.

Anonymous said...

Huyo Godfrey Lutego anafanya kama anaongea na simu...au 1992 kulikuwa na Mitandao...???

Anonymous said...

Sasa huyu mama Esha Stima, tunaweza kupata habari zake kamili, baada ya kufanya vitimbi hivi ?

Je ameweza kuomba msamaha, kwa UWT, CCM na serikali kwa ujumla ?
Kama hajaweza kufanya hivi, inabidi ajiuzulu kutoka NEC ?

Na hata kumchukulia sheria kali, mojawapo Chemi, fungua File upya, tafuta Lawyer Dar, hii itasaidia sana kuibua kesi za ufisadi wa mtu kwa mtu, hata ufisadi mwengine wowote, hali yakua kama vielelezo vipo ?

Ni kweli, Mama Kabigi, amefariki, lakini wewe Chemi na mwenzako mwandishi wa Uhuru kama yuko bado Dar, mshughulikieni huyu bibi.

au munaonaje wanablog, we intend to get rid of ufisadi, whatever shape or form, on whatever the time it might have happen, place or on any circumstances, that they-mafisadi would think will hinder our efforts and convictions to fight those who break the law.

Go Chemi Go Chemi. Get them out of hiding. Last but not least.
if you win this case, Chemi, would on somehow help all the victims of tenuous crimes, jails without proper convictions, rape victms will all be inspired by this case. I know that for sure there are helpless people out there who are not exposed to media like yourself Chemi, who suffer them same fate, and never been able to rid of scars and trauma caused by the perpetrators like Mama Stima.

If personally affected by this, I would have done just that.

Thank you for listening, taking actions will be a prides for other victims.

Chemi Che-Mponda said...

Asanteni waliotoa maoni. Kwa kweli sikutegemea support namna hii.

Mtoto wa fisadi,

Godfrey alikuwa ameshika begi/mfuko.

Anonymous wa 4:12am,

Tulitaka kumfungulia kesi huyo Mama Stima. Shtaka la kwanza kutufungia mle ofisi kwa muda. Pili kusema uwongo juu yetu polisi.Sijui 'statute of limitations' inasemaje kwa Tanzania maana miaka 15 imepita.

Ukweli mambo yaliishia hewani. Hatukuitwa mahakamani wala polisi tena juu ya hilo swala.

Nilikutana na huyo Mama Stima kama mwaka moja baada ya tuko na alinichekea kwa aibu. Huko anajaribu kuongea na mimi kama hajafanya kosa.

Mama Kabigi nilikuwa naongea naye kwa mara alisema kuwa huyo Mama Stima alikuwa na matatizo yake na hakuelewa sababu ya kumfanyia unyama siku hiyo.

Japo habari ilikuwa Front News (na wakati huo Daily Newa na Uhuru ndo yalikuwa magaztei pekee za Daily)sikusikia statement yoyote kutoka UWT Taifa. Maana Mama Kabigi alikuwa Mkuu wa UWT wa Mkoa wa Dar, si wangesema kitu?

KKMie said...

Anony @ 4:12am naungana mkono wazo lako kuwa huyo Mama Esha Stima anapaswa kuomba msamaha kutokana na kitendo chake vingivevyo ajiuzuru as hafai kabisa kuwa Kiongozi sio huko NEC bali hata jukumu lolote Kijamii.

Kwa kufanya hivyo Da' Chemi utakuwa umesaidia sana "victims" wengine navilevile itakuwa changamoto kwa wenye "tuveyo" au nafasi fulani kutodharau na kufisadi raia kama ilivyokuwa wewe na mwenzio.

Aliwatia aibu wanawake wakati huo na kwavile historia huwa haifutiki basi aibu hiyo inendelea kizai hadi kizaizi.

Aombe radhi adhalani (in public)au Ang'atuke.

Anonymous said...

Pole sana Da Chemi kwa yaliyokusibu miaka 15 iliyopita, ningekushauri ibua upya hili suala and shame this woman.
Honourable Esha Hassani Stima [ CCM ]
Special Seat - 2000 to 2005

1.Huyu mama alishawahi kuwa mbuge CCM viti maalum
2. aligombea ujumbe wa NEC akashindwa mwaka 2007

Click link below for more details;

http://64.233.183.104/search?q=cache:EWqWrWhumy0J:www.bunge.go.tz/bunge/Mp_Cv3.asp%3Ffpkey%3D238%26PTerm%3D2000-2005%26frop%3D%2520GENJOBDEPPEREDUMEDTRNSKLHISCRFPAR%26vusername%3DGUEST%2522)+Esha+Stima&hl=en&ct=clnk&cd=7&gl=uk

Chemi Che-Mponda said...

Dinah,

Huyo Mama Stima hajatuomba msamaha hadi leo. Sijui kama aliomba msamaha kwa Mama Kabigi labda nimwulize mwanae. Lakini Mama Stima alitia aibu sana jina la UWT. Watu walisema kazi yao UWT kugombania mabwana.

Kama alifika NEC/CCM heri yake labda alitubu dhambi zake. Pia watu walisahau alivyotufanyia ni Michuzi ndo alifufua hii habari. Lakini bado nauliza UWT Taifa walisemaje juu yaa hii swala maana sikusikia kitu kutoka kwao.

Anonymous said...

Chemi, nakuona na mfuko wako wa TAMWA. Viongozi wote wa TAMWA walikuwa na mifuko kama huo. Ilikuwa poa sana. Mliwatia aibu waandishi wanaume, walikuwa wanatembea na mifuko ya rambo