Tuesday, March 23, 2010

Michuzi Safarini Uingereza


Mwasisi wa habari za jamii mtandaoni (social media) nchini Bw. Muhidin Issa Michuzi (pichani) anaondoka leo Jumatano kuelekea London, Uingereza, kuhudhuria kongamano la pili la Watanzania wanaoishi nchi za nje (Diaspora 2 conference) kwa mwaliko maalumu akiwa kama blogger.

Bw. Michuzi, ambaye ametoa mchango mkubwa katika kupromoti habari za jamii mtandaoni kupitia blog yake maarufu ndani na nje ya nchi iitwayo issamichuzi.blogspot.com, amealikwa huko mkutanoni na ubalozi wetu Uingereza ili kutoa mada inayohusu umuhimu wa habari za jamii mtandaoni katika kujenga daraja kwa walio ndani na nje ya nchi.

Akiongea nasi leo kabla ya kukwaa pipa la shirika la ndege la Emirates, Bw. Michuzi ambaye pia ni maarufu kwa majina kama Mzee wa Libeneke, Mdau na Ankal, amesema amefarijika sana kuona kumbe kuna wanaotambua mchango mkubwa unaoletwa na vyombo vya habari za jamii mtandano, hasa blogs.

Amesema anajisikia mwenye furaha sana kuona azma yake ya kuifanya tasnia hii ya kupashana habari kwa njia ya intaneti kwa waandishi wa hapa nyumbani unatambulika na kukubalika na kupewa heshima stahili kama ilivyo kwa vyombo vya kawaida kama vile magazeti, redio na luninga.

Bw. Michuzi, anayeweka rekodi ya kuwa bloga wa kwanza nchini kualikwa kama bloga kwenye mkutano muhimu kama huo, anaushukuru ubalozi wetu Uingereza chini ya Balozi Mh. Mwanaidi Maajar ambaye naye anakuwa miongoni mwa wazalendo wa kwanza kuutambua hadharani mchango wa wanahabari za jamii mtandaoni kwa kutoa mwaliko huo.

"Nilijua iko siku wanahabari za jamii mtandaoni tutatambulika na mwaliko huu hakika umekuja wakati muafaka kwani msisimkmo na mwitikio wa jamii kuikubali njia hii ya mawasiliano hapa nyumbani umekuwa mkubwa kuliko ilivyotarajiwa.

"siku hizi habari za jamii mtandaoni zinachukua kiti cha mbele katika kusomwa na wenye kuwa na intaneti kutokana sio tu na habari kuwa za uhakika, zisizochujwa na za haraka bali pia kwa kule wasomaji kupata fursa ya kuchangia habari waionayo tofauti na ilivyo kwa magazeti, redio na luninga.

"dunia imezidi kuwa kijiji kimoja kidogo kwa teknohama hii ambayo hata Rais Jakaya kikwete yuko mstari wa mbele kutaka iendelezwe mijini na vijijini ili kuwezesha wananchi wawe na habari za uhakika, za haraka na zenye kutoa fursa ya wasomaji kuchangia maoni" alisema Bw. Michuzi.

Blog ya issamichuzi.blogspot.com ilianza rasmi Septembe 8, mwaka 2005 katika jiji la Helsinki, Finland, ambako alikwenda kuhudhuria mkutano wa Helsinki Conference akiwa kama mwandishi na mpiga picha wa gazeti la Daily News.

Alikuwa ni bloga wa siku nyingi aliyekuwa anaishi Marekani wakati huo, Bw. Ndesanjo Macha, aliyemshawishi Bw. Michuzi kufungua blog yake na kuwa bloga wa kwanza wa Tanzania kuupasha ulimwengu ya kila linalojiri nchini, kazi ambayo ameifanya kwa ustadi mkubwa kiasi ni hivi majuzi tu ameweza kufikisha wasomaji milioni 8, kati ya hao asilimia 30 wakiwa ni wasomaji wa hapa hapa Tanzania.

Bw. Michuzi ameweka wazi kwamba amefurahi na kusisismkwa sio kwa sababu anakwenda ulaya, kwani ameshatembelea karibu miji mikubwa yote duniani, ukiondoa Australia na New Zealand, ila amefarijika kwa sababu hatimaye blog zimeanza kutambuliwa rasmi.

Anatoa masikitiko yake kwamba pamoja na fanaka hiyo, lakini bado hapa nyumbani jamii, hasa ya mahafidhina (conservatives) wasiotaka mabadiliko wamekuwa wazito kukubali kwamba vyombo vya habari za jamii mtandaoni vimeshapata nguvu sawa na vyombo vya kawaida kutokana na wingi wa wasomaji na hata kupelekea kujitokeza kwa wadhamini wanaotangaza biashara zao humo.

Pamoja na mambo mengine, Bw. Michuzi amesema anatamani sana kuanzisha umoja wa wanahabari za jamii mtandaoni ili kutetea na kulinda maslahi yao pamoja na kuindeleza tasnia hii ambayo inakua kwa kasi za ajabu.

Kwa mahesbu ya haraka haraka hivi sasa kuna blog zinazotumia lugha ya kiswahili zipatazo 200 ambapo pia blog takriban 10 zinaanzishwa kila siku, na kuifanya Tanzania kuw nchi zinazoendelea katika tasnia ya habari kwa njia ya mtandao.

11 comments:

Anonymous said...

Kusema kuwa ni muasisi itakuwa ni kutia chumvi mno, huku ukitanabaisha kuwa alipewa ushauri wa kuanzisha blog na watanzania ambao baadhi yao walikuwa tayali wakiblog!

Hongera kwa mafanikio makubwa kwa blog yake na anastahili sifa kubwa kwa kutumia muda wake mkubwa katika kuhabarisha jamii.

Hilo la uhasisi ni vema likatizamwa kwa kina ili kuondoa kupindisha historia ya kublog kwa Tanzania.

Anonymous said...

kila la heri bwana michuzi,sasa uje na mapya si kama viongozi wetu wanakesha kwenye tv wanaangalia ngumi za usiku,na magari yao yenye tinted glasses hawaoni hata mapya fungua macho halafu rusha mapya mapya ambayo tunaweza kujifunza,hongera sana!

Anonymous said...

Yeye ni mwasisi au Ndesanjo?

Anonymous said...

KUFANYA NINI HUKO

Kaka Trio said...

Kwanini Michuzi kuwa mmoja wa uasisi Tanzania kuna ubaya gani kwa sababu huo ndio ukweli wenyewe. Kwanini akina Rashidi na Nyerere kuitwa wasisi wa Tanzania ina maaana akina Sykes na wengineo hawakuwepo?

Ndesanjo ndio chanzo cha Michuzi kublog lakini Ndesanjo hayuko Tanzania, ila walikutana Finaland kama sikosei ndio ndesanjo akamshauri aanzishe na hivyo basi Michuzi kuwa mmoja wa waasisi wa kublog kama tunavokufahamu leo hii.

Mnyonge Mnyongeni lakini haki yake Mpeni, Michuzi ni Muasisi wa blog. hajajitangazia hivyo yeye mwenyewe isipokuwa huo ndio ukweli ni muaisisi.

Fadhy Mtanga said...

Mie namwona Michuzi kama mmoja wa waasisi. Nilianza kublog kwa kuitikia wito wa Ndesanjo Macha, lakini blog za Michuzi, Mjengwa na Chemi ndizo zilizonihamasisha na kujiona ntaweza.
Heshima kubwa sana kwa wanablog. Ahsante sana kaka Michuzi kupeperusha vema bendera ya Bloggers.
Tutafika tu!

Anonymous said...

GO MICHUZI GO..............

Kibunango said...

Sidhani kama hili ni suala la ushindani, zaidi ya kuweka kumbukumbu sawa.

Ni kosa kubwa kusema kwamba Issa Michuzi ni muasisi wa blog za Tanzania. Hii ni maana kwamba yeye ndie mtanzania wa kwanza kublog huku hali halisi ni sivyo.

Bw.Isaa anastahili kupewa heshima ya kublog kupitia njia ya picha na sio venginevyo. Kupitia utoaji wa habari kwa picha ameweza kupata umaarufu mkubwa na kusogeza mbele njia tofauti ya kublog.

Sio sahihi na haitokuwa sahihi kusema kama yeye ndie mwanzilishi aka muasisi wa kublog Tanzania.

Anonymous said...

Kama alipewa ushauri hawezi kuwa muasisi bali ni mmojawapo wa watanzania wa kwanza kupewa ushauri na kuutumia kuanzisha blogu.

Fadhy Mtanga said...

nimerudi tena. Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili inatafsiri neno -asisi kama: weka msingi; anzisha. Na mwasisi, kamusi inasema ni mtu mwenye kuanzisha jambo fulani. Haijalishi yalikuwa ni mawazo yake, ama alipewa ushauri. Jambo la msingi ameanzisha.
Kwa mantiki hiyo, kama tunakubali Michuzi kuwa blogger wa mwanzo kabisa, lazima ukweli ubaki kuwa ukweli, Michuzi ni mmoja wa waasisi. Lazima tukubali hivyo, wengi wamezifahamu blog kwa sababu Michuzi alikuwa tayari anablog. Kwa nini hatupendi kumpa mtu stahili yake? Mchango wa Michuzi kama mwanablog wa mwanzo ndani ya Tanzania ndiyo unaompa credit kama mwasisi.. Ndesanjo aliweka misingi ya kublog, akawa anablog lakini akiwa nje ya nchi. Ni mwasisi mkubwa. Michuzi akaanzisha kublog akiwa anaishi nchini nakuweka misingi ya kublog. Heshima anastahili. Tunapoona leo blog ya Michuzi inapata mafanikio makubwa, ametoka nayo mbali.
Jamani ukweli lazima ubaki ukweli.

Anonymous said...

Bwana Fadhy na Kaka Trio,

Tafadhali tafuta ukweli juu ya unayosema au unayoamini. Si kweli kwamba Michuzi ni muasisi wa bloging miongoni mwa Watanzania. Si kweli hata kidogo. Kama walioanza kublog toka nyumbani Tanzania wapo wengi kabla ya Michuzi. Tafadhali usijipotoshe wala usipotoshe wengine kusema kwamba Michuzi ni muasisi wa blog.

Michuzi amechangia kwa kiasi kikubwa kwa Watanzania wengi kujua ulimwengu wa blog kwa kuingia kwenye blog yake na kuangalia picha, kusoma na kuchangia maoni. Blog yake imekuwa ndiyo chanzo cha habari pevu za matukio yanayowahusu Watanzania waliopo nyumbani na nje ya nchi.

Michuzi pia kachangia katika kupindisha mwelekeo chanya wa majadiliano ya kina kwenye blog za Watanzania.

Asanteni.