Monday, April 12, 2010

Dk. F. Mghanga Akumbuka IlivyokuwaTanzia ya Mh. Edward Sokoine

Asante Da Subi kwa kuleta habari hizi:

Dk. F. Mghanga AKUMBUKA ILIVYOKUWA TANZIA YA EDWARD MORINGE SOKOINE


Pichani -Edward Moringe Sokoine (1938 - 1984)


Ni miaka ishirini na sita iliyopita. Siku ya Alhamisi, majira ya jioni kama saa kumi na moja. Anga la jiji la Dar es Salaam lilikuwa jeusi likihanikizwa na mawingu madogo madogo yaliyojikusanya kuashiria kamvua kalikokuwa kametawala siku hiyo. Hizi ni nyakati za masika katika sehemu kubwa ya nchi.

Ndo kwanza nimerudi toka shule, tayari nimeshajipakia ugali wangu wa njano (Yanga) na maharage ya Iringa.

Nipo mtaani nikicheza na wenzangu chandimu. Hatuna viatu, tupo pekupeku lakini hatujali kitu. Maisha yalikuwa mazuri bila kujua adha na masumbufu ambayo wazazi walikuwa wanayapitia ili kutufanya watoto wao tuweze kwenda chooni.

Nikiangalia pembeni, akina mama walikuwa wamekaa wakisukana na wengine walikuwa kwenye vibustani vyao wakipalilia matuta ya viazi vitamu. Hakika hatukujua lililokuwa limetokea masaa machache yaliyopita hapa nchini kwetu.

Lakini ghafla redio zikaanza kupiga wimbo wa taifa. Si aghalabu kusikia wimbo wa taifa mida kama ile tena kipindi kile kisichokuwa na sikukuu wala mgeni yeyote wa kitaifa. Haiyumkiniki kuna jambo kuu limetkea. Katika utoto wangu, ghafla nikaacha kucheza, akina mama waliokuwa wakisogoa nao wakapigwa na ubaridi wa ghafla. Katika mshawasha wangu wa kitoto nikaijongelea redio kutaka kujua kilichojiri jioni hiyo ya Alhamisi nyeusi. Dakika kadhaa zilipita kabla ya wimbo wa taifa kuisha.

Sauti iliyojaa huzuni ikasikika. Hata katika utoto wangu, naweza kusema kwa hakika kuwa sauti ile ilikuwa katika huzuni na majonzi na ilionesha ni ya mtu aliyekuwa katika kilio muda si mrefu uliopita. Naam, ilikuwa ni sauti ya hayati baba wa Taifa. Nayakumbuka maneno yake mpaka sasa. Hivi ndivyo alivyosema:

"Ndugu wananchi, leo mnamo majira ya saba mchana, ndugu yetu, mwenzetu, Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais, Edward Moringe Sokoine amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea huko Morogoro wakati akilejea Dar es Salaam kutoka Dodoma kwenye mkutano wa Bunge"

Naam, hiyo ndiyo sababu ya kupigwa kwa wimbo wa Taifa jioni ile. Utando mweusi ukatanda. Simanzi ikatawala. Vilio vikasikika, furaha ikatoweka. Giza la mawingu meusi likaongezea upotevu wa furaha. Nikausikia ukelele mkuu kutoka kwa mama mmoja aliyekuwa ameshika jembe akipalilia bustani yake "Mama wee mkombozi wetu amekufa, nani atatutetea sisi wanyonge?" Hakika ndivyo aliomboleza mama yule.

Huzuni kuu ikaniingia ghafla. Nikajiwazia "Sokoine kafa? Hapana, amekufa?" Nafsi ilikataa kuamini, akili ya utoto ikaniambia haiwezekani. Ghafla machozi yakaanza kunitiririka. Naam nililia. Nilimlilia mzalendo wa kweli. Wazazi walilia, wananchi walilia, hata Nyerere alilia tena hadharani, hakulia kiunafiki alilia kweli.

Watanzania wapenda haki tulilia, tulimlilia mpenda haki mwenzetu. Sokione mzalendo wa kweli. Mwana wa Kitanzania asilia, mtetezi wa kweli wa wanyonge, mchapakazi, mpigania mema ya nchi.

Naam, yawezekana kwa wengine ameshafutika lakini kwa wapenda haki, Sokoine atabaki kuwa kioo chetu daima. Huyu ndiye mtu aliyekuwa na sifa nilizozitaja wakati ule kwenye ile ndoto yangu ya "Namuona mtu huyu". Yawezekana alikuwa na kasoro zake kama mwanadamu na hata kiutendaji lakini daima nia yake njema kwa watu wake iliyafunika makosa yake hayo. Alipendwa na wanyonge na kuchukiwa na wezi, wabadhiifu wa mali ya umma na wahujumu uchumi (leo tunawaita mafisadi). Huyu ndiye aina ya mtu tuliyemuhitaji Tanzania ya leo.

Nimemkumbuka Sokoine, mtanzania mzalendo mwana mpenda nchi aliyenifanya nihisi msiba wake kuwa unanihusu kwa ukaribu mno. Naam, wajamaa kama kina Subi lazima watamkumbuka mtu huyu na kumuomboleza daima.Mungu alipenda kumchukua ingawa tuliona amemchukua mapema mno.

Pumzika kwa amani Baba Sokoine, mtanzania na mzalendo wa kweli.

Amina!
Dk. F. Mghanga, MD

*************************************************************************

Na mimi naongezea. Siku hiyo nilikuwa kwenye zamu ya ulinzi wa usiku JKT Masange. Tulijiandaa kwenda zamu, lakini wote kambini tuliambiwa tukusanyike mbele ya ofisi kuu wa kambi. Kwenda huko, tukambiwa kuhusu msiba wa Waziri Mkuu Edward Morine Sokoine. Nadhani kila mtu alipigwa na butwaa kusikia habari hizo huko wengine walisema habari hiyo si kweli.

Wakati huo Masange JKT pori, hata simu hakuna. Kuna afande fulani alikuwa na redio ndo tukathibitisha kuwa habari hiyo ni kweli. Niliendelea na zamu ya ulinzi na wenzangu kama kawaida. Mambo kambini kwa ujumla yaliendelea kama kawaida. Waliobahtika kupata pasi kwenda uraini ndo walisema kulikuwa na vilio kibao. Nawaambia gazeti enye habari hizo zilikuwa kama almasi. Nakumbuka kuona picha ya Mama Gertude Mongella akilia kweli. Wakati huo alikwa Katibu Mkuu katika ofisi ya Waziri Mkuu.

Watu walikuwa wanasema kuwa ajali ya Sokoine haikuwa ajali, bali yule MSoweto alilipwa amwue. Wengine walisema alipigwa risasi na ajali ilikuwa kama cover-up. Eti kuna watu walikchukia kwa vile ilionekana atakuwa rais baada ya Mwalimu, wengine walisema eti kuna watu walichukia maendeleo alikuwa anajaribu kuleta. Lakini nakumbuka Mwalimu na viongozi wengine walisisitiza kuwa ilikuwa ni ajali! - Chemi

9 comments:

Anonymous said...

KWELI DADA KIFO CHA SOKOINE ILIKUWA COVER UP NA SI YEYE TU BALI VIONGOZI WENGI WA TANZANIA WANAKUFA KWA AJALI YA GARI AU UTAAMBIWA HEART ATTACK, FOR EXAMPLE KOLIMBA, CHACHAWANGWE, DR.OMAR, MALIMA NA WENGINE WENGI TU.

Anonymous said...

hadi leo hii siwezi kusahau wakati huo nilikuwa na umri wa miaka kumi na minne, inasikitisha sana bado naikumbuka ile nyimbo aloimba John Komba NI MWAKA WA HUZUNI NI MWAKA WA MATATIZO KWETU WATANZANIA WOTE, MSUMBIJI, ZAMBIA , ANGOLA NA AFRIKA YOTE

Anonymous said...

Jamani nilikuwa na umri wa miaka minne ila nilielewa kila kitu!Mungu amlaze pema peponi!

Kaka Trio said...

COVER UP? Hebu niambia kwanza afya zao ha viongozi wako, sitashangaa kama kweli ili,uwa heart attack, hizo za ajali sina comment.

Wabongo wengi hatucheck afya zetu hata tukicheki hatufuati masharti ya afya, ukiw ana mtumbo mkubwa na kunenepeana ati ndio afya, sas aukipatwa na hati attack na visukari umerogwa kha.

Anonymous said...

Kipindi kile mengi yalisemwa. Mtu ambaye alikuwa na jibu kuhusu ukweli wa kifo cha marehemu Sokoine ni yule Pathologist mlevi kupindukia lakini mwenye akili Dr. Shaba. Alikuwa Muhimbili miaka mingi. Alitaka hata kufungua funeral home Dar serikali walimzuia.

Anonymous said...

Nilikuwa niko Lusaka,mama akanipigia simu na siku iliyofuata akanitumia magazeti mawili tofauti kuhusu kifo cha Sokoine.Ukweli ni kwamba umaarufu wa Sokoine siku hizo ulianza hata kuupita umaarufu wa Mzee Nyerere,kwani Mzee Nyerere alimpa Sokoine madaraka mengi na alimuamini na kumpenda sana.Ndiyo maana Nyerere alihuzunika sana na kifo chake.ASANTE KWA NAKALA NZURI YENYE KUMBUKUMBU NYINGI YA WAKATI HUO.VERY PROFFESSIONALLY WRITTEN!

Anonymous said...

Mungu aendelee kulaza roho yake mahala pema mbinguni. Amen. Nchi yetu ilipata hasara. Na ni kweli alikuwa ameanza kupendwa kuliko Mwalimu!

Anonymous said...

Da Chemi, nilikuwa Msange JKT mwaka 1990/91. Afande Manyilizu alikuwa heshi kukutaja.Unamkumbuka?

Chemi Che-Mponda said...

Anonymous wa 6:54am ndiyo namkumbuka Afande Nestory Manyilizu. Yuko wapi siku hizi? Alikuwa ameonewa kweli na maafande maafisa. Walimshusha cheo toka Staff Sajenti kuwa Corporal halafu baadaye walimrudishia. Alikuwa na roho nzuri sana. Holla at chemiche3@yahoo.com