Thursday, July 08, 2010

Sauti ya Siti - Gazeti la TAMWA

Mwezi Machi, 1988 TAMWA ilizindua gazeti 'Sauti ya Siti'. Mimi ni mmoja wa waanzilishi wa TAMWA. Nakumbuka siku tulipotaarifiwa kuwa serikali imekubali kusajiliwa kwa TAMWA, na siku tuliporuhusiwa kuchapisha Sauti ya Siti. Ilikuwa jambo kubwa mno maana wanaume walitupinga kweli hata baadhi ya wanawake. Walisema TAMWA ni chama cha mashoga. Cha ajabu hao hao waliokuwa wanatusema walikuja kujiunga na TAMWA baada ya kuona mafanikio yetu.

Gazeti ya Sauti ya Siti ilikuwa na nia ya kuelezea habari za akina mama ambazo zilikuwa haziingii katika magazeti ya kawaida. Kumbuka wakati ule magazeti yalikuwa machache, Daily News, Uhuru, Mfanyakazi, Kiongozi. Redio ilikuwa Radio Tanzania tu!

Mzee Ali Hassan Mwinyi (Mzee Ruksa) ndiye alikuwa Rais. Mke wake alikuwa anaitwa Siti. Basi watu walisema eti sisi wanaTAMWA tuliamua kuita gazeti Sauti ya Siti ili kumpendeza Rais. Jamani!

Watu walikuwa wamesahau kuwa kulikuwa na Siti Binti Saad. Nia ya TAMWA ilikuwa kukumbusha watu juu ya mchango wa Bibi Siti katika muziki na pia hasa kuwa Siti ndiye alikuwa mwanamke wa kwanza wenye uwezo wa kufikisha ujumbe kwa Umati. Taarab aliyokuwa anaimba ilikuwa na ujumbe za kisiasa pamoja na mapenzi. Wangapi wanajua kuwaa Bibi Siti ndiye alihamisha watu kufanya mgomo huko Zanzibar miaka ya 1930's? Wanasema Siti alitunga zaidi ya nyimbo 600! Bahati mbaya nyingi zimepotea maana hazikuwa Recorded.

Nitafanya jitihada hivi karibuni za kufufua ile website niliyokuwa nayo iliyokuwa inaelezea mengi kuhusu maisha ya Siti Binti Saad.

Leo tunakukumbuka Bibi Siti Binti Saad.

No comments: