Thursday, February 17, 2011

Sinema 'Shoga' Yafungiwa na Serikali


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeiagiza Kampuni ya kutengeneza filamu ya 'Al-Riyamy Production Company' kuwasilisha Filamu ya 'Shoga' kwa Bodiya Taifa ya Ukaguzi wa Filamu kwa ajili ya ukaguzi.

Aidha Kampuni hiyo pia imeagizwa kutoisambaza Filamu ya 'Shoga' na kusitisha hatua nyingine yoyote kuhusiana na filamu hiyo hadi hapo Bodi ya Taifa ya Ukaguzi wa Filamu itakapojiridhisha kuwa filamu hiyo inakidhi kuonyeshwa hadharani kama ilivyoainshwa katika Sheria ya Filamu na Michezo ya Jukwani Namba 4 ya mwaka 1976.
Kampuni hiyo inatakiwa kuwasilisha kanda hiyo kabla ya tarehe 17 februari, 2011.Kwa mujibu wa Sheria hiyo hairuhusiwi kutengeneza filamu bila kupata kibali cha kutengeneza filamu.

Aidha kifungu cha 4 (1) inaelekezwa bayana kuwa kila anayetengeneza filamu anatakiwa kuwasilisha maombi kwa maandishi kwa Waziri chini ya Sheria hii yakiambatana na mswaada na maelezo ya filamu inayotarajiwa kutengenezwa.

Pamoja na mambo mengine katika kifungu cha 14 (2) Sheria inaipa Bodi ya Filamu mamlaka ya kukagua filamu, picha ya matangazo au maelezo yake kwa makusudi ya kuamua kuonyesha na ikiwa rushusu itatolewa maonyesho yawe kwa namna gani.

Katika Sheria hiyo kifungu cha 15 (1) kinapiga marufuku kwa mtu yoyote kuongoza,kusaidia , kuruhusu au kushiriki katika maonyesho ya filamu bila kuwa na kibali cha Bodi.

Sheria hii ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa waraka Namba 22 wa mwaka 1974.

Imetolewa na
Kitengo cha Habari,Elimu na Mawasiliano,
Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo.
Tarehe 14 februari,2011.

4 comments:

SIMON KITURURU said...

Mmmmh!

Anonymous said...

hapa isiwe swala la sheria tu,hivi jamani watu wamemsahau Mungu wao.sanaa inapoelekea ni kutupotezea wadogo zetu ambao ndo wanaangalia sana hizo filamu na mwisho wa siku wana practise wlichokiona .plz baraza la sanaa uko wapi na sheria ziko wapi.wito wangu watu wamuogope Mungu

Anonymous said...

Hapa Bongo kila kukicha watu wanafyatua filamu na matokeo yake ndio haya. Mara nyingi maadili yanawekwa pembeni katika vita ya kutafuta soko. Sinema nyingi za Bongo huwezi kuziangalia ukiwa na mtu unayemheshimu.

Anonymous said...

Nashangaa imekuwaje hii filamu wameipa jina la Kiswahili maana mtindo wa sasa ni kuzipachika filamu la Kiswahili majina ya Kiingereza. Sinema ina jina la Kiingereza lakini humo ndani wanazungumza Kiswahili mwanzo mpaka mwisho! Ni ajabu na kweli! Wengine wanaweza kudai kuwa pamoja na kwamba lugha inayotumiwa ni Kiswahili, lakini filamu hizo zina ‘subtitles’ za Kiingereza zinazotafsiri kinachozungumzwa. Sawa, lakini ‘subtitles’ hizo huwa zinaandikwa kwa Kiingereza ambacho ni vichekesho vitupu. Najua lengo la wasanii wa filamu wa ‘Bongo’ ni kuuza kazi zao nje ya Tanzania, lakini nadhani sinema hizo zinapotua Kenya, Uganda, Nigeria, Ghana na Afrika Kusini hutumika zaidi kuchekesha watazamaji. Watayarishaji wa filamu za ‘Bongo’ waache kubana matumizi kama wanataka kazi zao ziwe na viwango vinavyokubalika. Hizi ‘subtitles’ wanang’ang’ania kuziandika wenyewe wakati wapo Watanzania wanaojua Kiingereza ambao wangeweza kufanya kazi hiyo kwa malipo nafuu.