Friday, February 18, 2011

Rekodi ya Ajali za JWTZ tangu mwaka 2007

Naomba niwasilishe rekodi ya haraka ya ajali za JWTZ angalau kuanzia mwaka 2007:

DESEMBA 2007
Helikopta ilianguka juu ya Ziwa Natron na watalii wanne, msindikizaji wao mmoja Mtanzania, na maofisa watatu wa JTWZ. Hakuna aliyepoteza maisha lakini ililipuka na kuishilia mbali na moto.

JUNI 2008
Helikopta ya pili ilianguka Oljoro, Arusha, wakati ikianza safari ya kwenda Dar es Salaam. Watu wote sita waliokuwemo ndani walipoteza maisha wakiwemo watoto wawili ambao sijui walibebwa humo kwa minajili gani.

APRILI 2009
Mlipuko mkubwa kwenye kambi ya Mbagala ulitokea na kuua watu 31 na kujeruhi wengine 700. Maelefu walipoteza nyumba zao na serikali ilitumia mamia ya mamilioni kulipa fidia na huenda fedha zilishafika bilioni kadhaa.

SEPTEMBA 2009
Mlipuko mwingine tena ulitokea kwenye kambi ya Mbagala na kuua watoto watatu. Wazazi wao waliishia kulia na kuambiwa kwamba wao ndio waliozisogelea kambi hizo za kijeshi kwani zilipojengwa zamani hakukuwa na nyumba. Majibu rahisi kwa maswali nyeti.

JUNI 2010
Ndege ya jeshi kutoka kambi ya Ngerengere ilianguka kwenye kijiji cha Manga, mpakani mwa mkoa wa Pwani na Tanga, wilayani Handeni, na kuwaua marubani wote wawili. Ndege hiyo ililibatiza lori la watalii ambao waliishia kubwagwa chini na kuporwa mali zao na wahuni na hatimaye kukatisha ziara yao na kurejea kwao Uholanzi wakiwa na simanzi kubwa na mshituko.

OKTOBA 2010
Siku chache kabla ya uchaguzi, Afisa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, ambaye kiutendaji ni ofisa utumishi mkuu, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo, alitangaza jeshi kuingilia siasa pale alipotoa onyo kwamba wanasiasa wapinzani wakubali matokeo ya uchaguzi ingawa ulikuwa haujafanyika bado. Hakusema iwapo kulikuwa na taarifa za kiintelijensia au la. Bahati nzuri jeshi halikuua mtu.

FEBRUARI 2011
Mlipuko mkubwa ulitokea kwenye kambi ya Gongo la Mboto na hadi sasa bado idadi kamili ya waliouawa haijafahamika lakini imeshazidi 23. Angalau kwa uchache watoto 200 wameokotwa wakiwa hawana wazazi wao. Wananchi zaidi ya 4,000 wamepiga kambi kwenye Uwanja wa Uhuru, Temeke. Shule ya sekondari na nyumba kadhaa kwisha habari yake. Maafa bado yataendelea kwani mabomu yametawanyika kwenye eneo lenye nusu kipenyo cha kilomita 11.

TAREHE INAYOFUATIA
Naomba mtabiri aendelee.

Mobhare Matinyi.

3 comments:

malkiory said...

Uchambuzi yakinifu.

Anonymous said...

Waambata wa kijeshi toka nchi marafiki hasa Wachina wako wengi ndani
ya kambi zetu za jeshi.Hivi unadhani kwa kukaa kwao muda mrefu mpaka
kiswahili wanakijua na watoto wamezalisha ndugu zetu,hawajui ghala
sensitive za siraha ziko wapi ndani ya Nchi.Haitoshi baadhi yao ndio
walimu wetu wa mafunzo ya kijeshi na mabomu hayo.

Maazimio yaliyopitishwa na Baraza la Usalama la Taifa yako sawa,wasi
wasi wangu huwa ni utekelezaji tu hapo ndipo kichwa cha mwendawazimu
kinaanzia.Hili la kuleta Nchi marafiki (hasaa marafiki) sio wajinga
watawakimbilia wale wale waliotuuzia hayo mabomu hasa China na Urusi
ambao siku zote hawana shida na sisi.

Anonymous said...

Bado kumbukumbu moja, mwaka 2005 kambi hiyo hiyo ya Gongolamboto mabomu yalilipuka, ingawa hatukupata taarifa za uharibifu wala majeruhi.