Sunday, December 04, 2011

Ni lini tuta sherehekea Uhuru wa Tanganyika?

Bendera ya Tanganyika

Imeandikwa na Mdau VM

Ni lini tuta sherehekea Uhuru wa Tanganyika?
Kila mwaka utasikia sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara!!!!!
Ni lini sasa tutasherehekea Uhuru wa Tanganyika? Hivi kweli huu ni umbumbumbu wa Historia kwa miongoni mwetu watanganyika au ni unyanyapaa wa Tanganyika, na ustaarabu kwa Z'bar? Mimi Sipendi!

Mapinduzi ya Z'bar yapo kila Januari 12 tena kwa mbwembwe zote, sherehe za kumbukumbu ya Muungano zipo kila Aprili 26 kwa kwa kila hamasa, lakini Uhuru wa  Tanganyika ni lini??? Mimi sipendi!!!

Tunaambiwa eti Uhuru wa Tanzania Bara! Sipendi!!!
Ok. Potelea mbali. Sasa hivi Tanzania Bara imefikisha umri gani? Miaka 47 au 50? Hivi Tanzania Bara haikuzaliwa Aprili 26, 1964. Sasa hiyo ni miaka mingapi, 50 au 47? Mi sipendi kabisa kuvuruga na kuchanganya historia.

Sipendi watoto wetu, wadogo zetu, kupotoshwa kwa makusudi kuhusu Uhuru wa Tanganyika! Tunawadanganya ili iweje? Sipendi kabisa!!!.
Siendi kwenye sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara wala siangalii televisheni kuhusu uhuru huo, hadi ntakapo sikia tunaazimisha miaka kadhaa ya Uhuru wa Tanganyika! Labda mnisaidie kuelewa, vinginevyo hakuna. Asante.

Vins

5 comments:

Mwl. Lwaitama said...

Utanganyika na Utanzania ni dhana si maneno tu ndugu zangu. Kunamitizamo imejificha nyuma ya maneno haya jamani! Nadhani mimi labda sijaelewa nieleimisheni, kipande kilichokuwa kinaitwa Tanganyika sasa kinaitwa Tanzania Bara na kina miaka 50 tangu kijitawale kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza; Kipande kilicho kuwa Zanzibar kinasherehekea miaka 50 ya uhuru ya Kipande kilicho kuwa Tanganyika amabcho sasa kinaitwa Tanzania Bara.. Ebu nieleimisheni ugomvu huu kuhusu eti lazima tusiseme Tanzania Bara ni ugumvi kuhusu nini hasa yalabhi! Watawala wetu wa CCM wameacha kabisa kutetea Uafrika wetu uliotukutanisha katika African Association na Afracan Congress za kila sehemu ya Africa na baadaye kuzaa Tanu, ASP na baadaye zaidi CCM: watawala wetu wako mbioni kutufanya tuichukie Tanzania na kuwa na hulka kama ya wale wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam cha mwaka 1966 waliomkasirisha Mwalimu Nyerere kwa kusema eti afadhali wakati wa mkoloni....Hasira zetu kwa mafisadi hawa wanaotawala kwa mgogo wa chama kitukufu cha CCM leo wametufikisha hapa ambapo tunachukia kuitwa Watanzania Bara. Mungu amurehemu Mwalimu Nyerere masikini aliyepambana peke yake dhidi ya G55 ambao nao wakati huo walifikishwa mahali wakatamani kufufua serikali ya Tanganyika kwa vile walikasirishwa na utwala mbovu uliokuwa umeleta ufa kwenye muungano wa awamu ya pili ya urais. ...Mwalimu Nyerere hana tena mtetezi ndani ya chama alichokianzisha cha CCM. Mswada wa Mchakato wa Katiba Mpya wa CCM tayari unasambaza sumu ya dhana ya serikali tatu kinyemela ndiyo maana hasira hizi na kushabikia kufufuliwa eti utambulishio wa Tanganyika badala ya kujivunia kuitwa Tanzania Bara! Hii ni sababu nyingine kwa nini CCM hakistahili kuendelea kutawala Tanzania, iwe hiyo Tanganyika yenu au Zanzibar...Sasa kwisha kabisa, hakuna mtetezi wa Utanzania ndani ya CCM...Mbona wote tunashserekea Majimaji, na Vita vya Mkwawa kule Kalenga, na nk,nk?....Leo hii kuitwa Mtanzania Bara imekuwa nongwa? Ama kweli tumepoteza dira ya Umajumui wa Kiafrika chini ya utawala wa CCM hii mamboleo ya makuadi wa soko huria waliokiteka chama hiki cha wakulima na wafanyakazi hususani mara baada ya Mwalimu Nyerere kufariki 1999!!! Sitoshangaa wapo akina Yelsin wetu hapa wanajiandaa kutumia pesa nyingi kuwalisha kasumba ya kushabikia utambulisho wa Utanganyika Watanzania Bara waliozaliwa baada ya 1964 ambao ndio walio wengi. CCM legelege itazaa kuibuka tena uzalendo muflisi wa eti Utanganyika na baada ya hapo tutarudi tena kwenye utambulishao muflisi zaidi na zaidi wa vikabila na vikoo kama Rwanda ya 1994 na Somalia ya leo. Ni utambulisho wa Umajui wa Kiafrika tu ndio nguzo ya amani na mshikamano tunaolingia leo hii Tanzania!!!

Mwl. Lwaitama

Simon Kitururu said...

Mmmmh!

Anonymous said...

Kaazi kweli kweli…….binafsi naungana na mh Tundu Lisu katika hoja zake na kupitia mjadala huu nilipata nafasi ya kuitafuta katiba ya Zanzibar na kuipitia ndipo nilipogundua mh Lisu yuko sahihi kwani Katiba hii imefanyiwa mabadiliko kumi tangu ipitishwe, lakini mabadiliko makubwa ni yale ya nane ambayo yaliingiza yale yote yaliyokubalika katika muafaka ya CCM na CUF na ya 1o ya mwaka 2010 yaliyoanzisha aina mpy ya srikali kwa upande wa Zanzibar nayo ni ;Yameitambua Zanzibar kama nchi yenye mipaka bendera na vikosi vyake, Yamempa nguvu rais wa Zanzibar kuigawa Zanzibar katika wilaya na mikoa, Yamempa nguvu ya kuteua wakuu wa wilaya na mikoa, Yameongeza viti maalumu vya wanawake ktk baraza la wawakilishi Zanzibar kutoka 30% hadi 40% yameanzisha makamu wawili wa rais katika nchi ya Zanzibar ambao katiba ya Jamhuri ya muungano ya Tanzania haiwatambui,. Na kibaya zaidi Katiba ya zanzibar imeweka wigo kwa baraza la wawakilishi kutochezea na kubadilisha katiba ya zanzibar kirahisi rahisi…je kwa msimamo huu huoni kuna haja ya kuwa na Tanganyika yetu? Think critically then u may reach to a reasonable decision about this issue.

Anonymous said...

Jamani ndugu zangu, mimi nadhani kuna haja ya kujitahidi kujadili mambo ya muhimu zaidi badala ya kujikita mambo haya yasiyo tija kwa gharama za kujiita wazalendo.

Ingawa bado naheshim uhuru wako wa kimawazo lakini nimeona nami nitumie haki hiho pia kueleza ninavyodhani mimi pia.

Umeuliza kama tuna miaka 47 au 50? Pia umeamua kutambua jina la Tanganyika na sio Tanzania bara. . . Mimi hoja zangu ni kama ifuatavyo;

Kwanza, hebu fikiria hivi, Kijana mmoja alivozaliwa kijijini Geita aliitwa Masanja, miaka mitatu baadae akapata ubatizo na Kuitwa jina la kitakatifu akaitwa Julius. Kijana huyu na wazazi wake wakakubaliana kutumia rasmi jina lake la ubatizo Je Julius atakua na umri gani?

Wakati wa muungano mwasisi wa muungano ule aliamua kutumia jina la ubatizo kua jina rasmi hivi hapa sbida ipo wapi? Sidhani kama Wanzanzibar ambao wao waliamua kubaki na jina lao la asili baada ya ubatizo ni tatizo mpaka ikatupelekea nasi tukadai jina letu.

Ni nini Jina Tanganyika? Nini asili yake? Je kabla ya ukoloni kulikua na tawala inaitwa Tanganyika? Au wakoloni baada ya kuchora mipaka yao waliamua kutuita Tanganyika? Kwa nini tuvombee haki kutoka kwenye jina walilotubatiza wakoloni tukadhau jina tulilojibagiza wenyewe?

Nionavyo mimi hakiwahi kuwa na Tanganyika kabla ya ukoloni, ila kulikia na tawala ya chifu mkwawa, mangi, mirambo and the like kama unataka kugombea historia yako. Baba wa Taifa aliye muasisi wa muungano akishawahi kuhoji kuhusu asilia ya jina Tanganyika, mimi naelewa kwanini alihoji, kwa sababu aliudhika na asili ya jina hili, jina hili lina kumbukumbu ya kuudhi ha watu hawa walivogawana ardhi zetu kama vipande vya samaki?

Anonymous said...

Nadhani kuuita mjadala mzima unaozunguka kero za mungano na kuwepo ama kufutika kwa Zanzibar na au Tanganyika ndani ya Muungano kuwa ni NJAA tu nadhani ni kurahisisha sana mambo.

Zanzibar, inayodaiwa na kudai uwakilishi wa viti sawa katika uandikaji wa katiba nk; Zanzibar ambayo wabunge kutoka huko wanashiriki kupiga kura juu ya mambo ya siyo kuwa ya Muungano ya upande wa Bara, kuihalalishia uhai wake tu kwa vile ni ndogo na 'uchumi wake ni mdogo' nadhani nalo lina hitilafu. Tanganyika/iite hata Tanzania Bara, inaweza kuwa symbol ya ustawi wetu kama vile ambavyo unadai Zanzibar ni symbol

Haya na tukubali tunayodhambi kubwa sisi 'tunaoshambulia Zanzibar' unayoidogosha, unasemaje basi kuhusu Wazanzibar wanaobadili katiba na kuiondosha Zanzibar kuwa sehemu ya nchi moja ya Tanzania bali nchi iliyoungana na (vacuum) kuunda Tanzania? Mwenzake yuko wapi? Mbona hutoi mwito wakapimwe akili?

Bado nadhani kuwa suala la ukabila linalazimishiwa kwenye mjadala huu kuua hoja kwa nguvu. Mrema alishakuwa mbunge wa Temeke, Makongoro Nyerere vivyo Arusha (rare cases though, lakini zipo).

Pia suala la 'Mbeya kujitangazia uhuru' ni la mapambano ya kitabaka zaidi kuliko ya ukabila/ukanda nk. Pale mwanjelwa tuko kina meku kibao, wakinga, wahehe, wanyakyusa, wasafwa, wafipa, na wahaya, na wasukuma wengi tu nk. Hakuna kabila la Mbeya! Pia si sahihi kusema Mbeya walijitangazia uhuru, bali labda kuwa wafanyabiashara ndogo walijitangazia uhuru! ni tabaka mwalimu, sio kabila wala hata kanda, ama mkoa. Si ajabu wafanyabiashara wa mbalizi pale wanamtazamo tofauti. Ukabila usilazimishiwe kwenye hili.