Saturday, December 10, 2011

Barrick Gold Mines Wakwepa Kulipa Kodi!


IMEBAINIKA kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama imepoteza mapato zaidi ya sh milioni 300 kutokana na kampuni 30 zinazofanya kazi migodi ya Kampuni ya African Barrick Gold Mines LTD kukwepa kulipa
ushuru wa huduma za jamii.

Hayo yalibainishwa jana na Ofisa Biashara wa Wilaya ya Kahama, Boniphace Bulali, alipokuwa akitoa
ufafanuzi juu ya msako mkali wa kuzisaka kampuni hizo katika migodi hiyo unaofanywa
na wakala wa kukusanya madeni ya halmashauri hiyo, Mustered Seed International LTD.

Bulali alisema kampuni hizo zimekwepa kulipa ushuru unaopaswa kulipwa wa huduma za jamii kwa kipindi cha miaka mitatu, hali ambayo imezorotesha mapato ya halmashauri na kushindwa kufikia baadhi ya malengo yake katika kuleta maendeleo stahiki kwa wakati wilayani humo.

Alisema katika msako huo tayari baadhi ya kampuni zimekiri kushindwa kulipa fedha hizo kwa madai
jukumu hilo hufanywa na makao makuu ya ofisi zao zilizopo Dar es Salaam kinyume cha utaratibu
wa sheria ndogo za halmashauri zinazoeleza kulipa ushuru huo kwenye eneo wanalofanyia kazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mustered Seed International LTD ambayo ni wakala wa kukusanya madeni hayo, Zacharia Soko, alisema kuna kampuni 15 zinazofanya kazi katika mgodi wa
Buzwagi pekee ambazo hazijapata kulipa ushuru huo kwenye halmashauri hiyo tangu zianze
kuwajibika katika mgodi huo.

Soko alisema pia kuna kampuni 15 katika Mgodi wa Bulyanhulu ulio kilometa 74 kutoka Kahama
mjini ambazo nazo zimebainika hazijalipa ushuru huo na tayari katika msako huo baadhi ya mali zake
zikiwamo magari yanashikiliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kahama.

Chanzo: Tanzaniadaima

1 comment:

Anonymous said...

Tatizo bado lipo bado kwenye serikali kuu ambayo imekuwa ikiziamulia serikali za mitaa ktk mambo mengi ambayo kimsingi yalipaswa yafanyike kati ya wawekezaji na tawala za Halmashauri husika.
Ht katika suala la kodi ya mapato ya dola laki mbili kwa mwaka lilifikiwa na serikali kuu wakati kulikuwepo na nafasi kubwa kwa halmashauri hizo kubargain zaidi ya kiwango hicho.
Hapa ndio tujiulize wao Halmashauri walikuwa wapi muda huo? Ina maana hakuna ufuatiliaji wa karibu kiasi cha kutojua ht makampuni madogo madogo yanayofanya kazi kwenye migodi hii.
Barrick wanalipa kodi kwa mujibu wa mikataba yao na serikali lakini hawawajibiki kuwakumbusha contractors wao.
Hapa kuna tatizo kubwa zaidi ila kwa vile sheria zipo zimesinzia, hakuna anayejali. Ni makampuni haya haya ambayo pamoja na kukwepa hizo kodi bado hayaaply hata sheria za kazi ambapo wengi wa waajiriwa wao wanalipwa km vibarua na hawana ht mikataba ya ajira.
Anapaswa pia awepo wakala wa ufuatiliaji hili.