Saturday, February 18, 2012

Dk. Mwakyembe Amjibu DCI Manumba!


Dr. Harrison Mwakyembe (picha kutoka JamiiForums.com)

           Dk. Harrison G. Mwakyembe (Mb), NW-UJ
Dar es Salaam
18/02/12
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Nimelazimika leo Jumamosi, tarehe 18 Februari, 2012 kutoa taarifa hii kwa vyombo vya habari kufuatia mkutano wa DCI Robert Manumba na waandishi wa habari jana (17/02/12) kuongelea, pamoja na mambo mengine, hali yangu ya afya na kuhitimisha, kienyejienyeji tu kuwa “sikunyweshwa sumu” ila naumwa tu ugonjwa wa ngozi bila kufafanua ugonjwa huo wa ngozi umesababishwa na nini!
Napenda nisisitize mapema kabisa kuwa msimamo huo wa Jeshi la Polisi umenikera sana katika hali niliyonayo ya ugonjwa, kwanza kwa kuingilia mchakato wa matibabu yangu na uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake unaoendelea hospitali ya Apollo nchini India ambako bado sijahitimisha matibabu yangu; pili kwa ufinyu wa uelewa unaojitokeza bayana kwenye tamko la Jeshi la Polisi unaosisitiza kuwa “sikunyweshwa sumu” wakati sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru, inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa tu; na tatu kwa Jeshi la Polisi kujiingiza kwenye suala ambalo kwa takriban mwaka mzima halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.
Itakumbukwa kuwa tarehe 9 Februari, 2011 nilimwandikia barua IGP Said Mwema kumtaarifu kuhusu njama za kuondoa maisha yangu na ya viongozi wengine. Kwa kutambua kuwa Jeshi la Polisi la Tanzania daima husisitiza kuletewa ushahidi kwanza ndipo lifanyekazi, nilihakikisha nimeainisha katika barua  hiyo kila ushahidi nilioupata au kupewa. (Utaratibu huu wa Jeshi la Polisi kusubiri kuletewa ushahidi mezani, kama ambavyo mahakimu wanavyosubiri ushahidi mahakamani, haupo popote pale duniani (ila Tanzania tu) kwani kazi ya msingi ya Polisi si kuletewa, ni kutafuta ushahidi. Polisi wanachohitaji duniani kote ni kupata clue au tetesi tu. Hiyo inatosha kufukua ushahidi wote unaohitajika). Pamoja na kujitahidi kuanika kila aina ya ushahidi niliokuwa nao, mambo manne yalijitokeza ambayo yalionyesha wazi kuwa Polisi hawakuwa na dhamira ya dhati ya kupeleleza suala hilo:
(i)                Siku chache baada ya kumkabidhi IGP barua hiyo, nilitumiwa timu ya “wapelelezi” ofisini kwangu kuja kuchukua maelezo yangu ya ziada. Timu hiyo ilikuwa inaongozwa na ACP Mkumbo, afisa wa polisi ambaye wiki chache zilizokuwa zimepita alikuwa miongoni mwa askari waliotuhumiwa kupokea rushwa kwa lengo la kumbambikizia madawa ya kulevya mtoto wa Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi, suala ambalo mpaka leo hii uongozi wa Polisi umeshindwa kulitolea maelezo ya kuridhisha. Kwa msingi huo, nilikuwa nimeletewa mtuhumiwa wa rushwa/ ujambazi kuendesha uchunguzi wa watuhumiwa wengine wa ujambazi! Nikatambua mara moja kuwa zoezi zima lilikuwa la mzaha, tena mzaha mkubwa!
(ii)              Wiki chache baada ya barua yangu kuwasilishwa kwa IGP na timu ya ACP Mkumbo “kuanza kazi”, Jeshi la Polisi likachukua hatua ya kuwapongeza na kuwazawadia askari niliowatuhumu kushirikiana na majambazi! Huhitaji kuwa profesa wa falsafa kuelewa kuwa huo ulikuwa ujumbe tosha wa kunipuuza.
(iii)            Hivi karibuni tuhuma za askari polisi kujihusisha na vitendo vya ujambazi mkoani Morogoro zilipopamba moto na kuwagusa askari “wale wale” niliowatuhumu kwenye barua yangu, IGP alichukua hatua ya kuwahamishia mikoa mingine!
(iv)           ili kunikatisha tamaa kabisa, barua yangu ya “siri” kwa IGP ikavujishwa kwa makusudi kwenye vyombo vya habari na kuchapishwa kama habari ambayo ilikebehi na kukanusha taarifa nzima niliyotoa, sijui kwa faida ya nani! Lakini huu ni mchezo wa kawaida kwa polisi kwani hivi karibuni Mhe. Waziri Samuel Sitta alipohojiwa na ofisa mwandamizi wa Jeshi la Polisi ofisini kwake, wakiwa wawili tu, taarifa ya kikao hicho ikawa kwenye moja ya magazeti ya mafisadi ikikebehi ushahidi aliotoa Sitta! The integrity of the police force leadership is on the line.
Nimeelezea vizuri katika barua yangu kwa IGP kuwa kundi hilo la mauaji lilikuwa limeelekezwa kuniua kwa kutumia sumu, taarifa ambayo kwa karibu mwaka mzima Polisi hawakutaka kuifuatilia kwa sababu wanazozijua wenyewe.  Sasa huu msukumo mpya wa Jeshi la Polisi kutaka kujua kama nilipewa sumu au la na kukurupuka kutoa tamko hata kabla ya kunichunguza nilivyo, kunihoji mimi na wasaidizi wangu ofisini na hata kuongea na mabingwa wa Kihindi wanaonifanyia uchunguzi, umetokea wapi?  Si ni polisi hawahawa ambao, badala ya kushukuru,  wamekuwa wakikerwa na tahadhari ambazo Waziri Sitta amekuwa akitoa ili suala hili lichunguzwe kwa kina?
Aidha napata taabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matatibabu yangu au walisoma taarifa “nyingine”, na kama waliisoma taarifa hiyo wenyewe au “walisomewa”! Nasema hivyo kwa kuwa alichokisema DCI Manumba kwa wandishi wa habari hakifanani kabisa na picha iliyo kwenye taarifa halisi ya Apollo ambayo inatamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua, kukidhibiti /kukiondoa huku vyombo vyetu vya dola vikipelekeshwa na mafisadi kusema bila msingi wa kisayansi wala aibu: “hakulishwa sumu”, “hakulishwa sumu”!
Nimesoma darasa moja Kitivo cha Sheria Mlimani na DCI Manumba. Baadaye IGP Mwema alikuwa mwanafunzi wangu wa sheria Mlimani. Vigogo hawa wawili wa usalama wa raia nchini hawajanitendea haki, nao wanajua. Wanajua vilevile kuwa sitakaa kimya au kumung’unya maneno come what may pale ambapo haki inakanyagwa.
Tuendelee kuombeana afya na uhai ili tutendeane haki na vilevile tuitendee nchi yetu haki kwa kuvimalizia viporo vinavyokera vya Dowans, EPA, Kagoda n.k. kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
 
Mungu Ibariki Tanzania .

5 comments:

Anonymous said...

Ukweli utajulikana tu.

Anonymous said...

Hivi Tanzania inaelekea wapi jamani? Kama hali ni hii, hivi kuna mtu yeyote aliye salama?

Anonymous said...

DCI ameudanganya umma... Waziri wa Afya aikana ripoti yake kuwa haikotoka wizara ya afya.

Je, polisi nao wameanza kuwa wanatoa taarifa za kutengeneza kama wanasiasa? Kama mkuu wa uchunguzi anadanganya umma, hawa walio chini yake watakuwaje?
Iko wapi moral authority kutoka kwa polisi?

Tanzania tuitakayo ina watu kama akina Manumba watatupeleka wapi kama taarifa za mawaziri zinachakachuliwa, je kwa watu wasio na majina wanafanyaje?

Jason Bourne said...

RIPOTI YA UCHUNGUZI BINAFSI JUU YA UGONJWA WA DR HARISON MWAKYEMBE 12/10/ 2011

JASON BOURNE
TEL:*********
ID************

Hatua ya kwanza:
Niliamua kujua kama ni kweli kalishwa sumu au laa. Na watu nilio
wahusisha katika kujua huko ni TISS.

Katika uchunguzi niliweza kuzungumza na LTK wapatao kumi na tano.
Maboharia wawili
Wapanga mikakati wawili
Mkuu wa LTK
Vijana wa kazi kumi
Wote maelezo yao yalifanana kwa maana ya (walishiriki kupanga na
kutekeleza kumlisha sumu Dr Harison Mwakyembe)

Hatua walizopitia:

Kwa mujibu wa maelezo ya LTK/D00/B1 mkuu wa kitengo hicho ambae kwa
kweli niliongea nae kama rafiki yangu wa karibu ndie aliyenipa
mwangaza wakufanikisha kazi yangu.

Katika misheni hii watu wengi wanatakiwa KUFA, nitawataja wale muhimu tu:
1. Wilblod Slaa
2. Samweli Sitta
3. Harison Mwakyembe
4. Said Kubenea
5. Mark Mwandosya

Mnamo ijumaa ya tarehe 01/10/2010 saa 4:25, kikao kikuu cha mikakati
kilikalika Moven Pick kikihudhuriwa na watu sita,
TISS/A001 XXX
TISS/B1
TISSB32
TISS/B5
TISS/A6
TISS/F5


1 Samweli Sitta
2 Harison Mwakyembe
3 Mark Mwandosya
Hawa wamepangiwa vifo vya aina mbili kwanza ajali na ikishindikana
watalishwa sumu.

1 Said Kubenea

Kumwagiwa tindikali, baada ya kufeli ile ya kwanza imeagizwa nyingine
toka Bulgaria yenye kuua baada ya masaa kumi na mbili tu!

1.Wilblod Slaa

Huyu anatakiwa kufa kwa shabaha ya risasi (snipers) ndio wanao
andaliwa tu kwa sasa.

Waliopewa kipaumbele kufa ni Samweli Sita, Mark Mwandosya na Harison
Mwakyembe ambapo LTK/D00/B10, LTK/D00/B14, LTK/D00/B17 na LTK/D00/B21
walipewa kazi hiyo.

Kikwazo kikuu walichokumbana nacho vijana wa kazi, ni kuwa, Sita,
Mwandosya na Mwakyembe wote ni majasusi na kwapamoja walifanikiwa
kufumbua njama hizo chafu za mauaji kwa siri.

Mitego ya ajari 16 kwa Mwakyembe yote imemkosa, 12 kwa Sita nayo
ikamkosa,7 kwa Mwandosya nae kakoswa.

Walipoona mbinu zote za vifo vya ajali zimefeli wakahamia kwenye aina ya pili ya vifo vya kulishwa sumu:


Katika aina hii ya mauaji kwa muujibu wa vijana wa kazi wanashangaa
uimara wa Samweli Sita na Mwakyembe kwani wameshalishwa aina nyingi za
sumu lakini bado wanadunda tu, kwanza sumu ya kwanza kuwalisha ni
katika kikao cha kwanza cha bunge mwa 2011, hawakupata madhara yoyote.


Baada ya kufika tz bwana Zudrav alitoa mafunzo ya wiki moja jinzi ya kuhifadhi na kutumia kisha akatokomea kurudi kwao na vijana wake wanne.


Baada ya Mrusi kuondoka misheni zikaendelea na mnamo tarehe 24 /7/
2011 wakati afya ya Mwandosya ikiendelea kuzorota mmoja wa LTK/D00/B10
wa kike alifanikiwa kumuwekea Polonium 236 katika chai nyumbani kwake
akiwa ni miongoni mwa watu waliokwenda kumjulia hali,

Na Mwakyembe alikuja kuwekewa ktk maji ya kunywa na kwenye kitambaa
cha kufutia uso LTK/D00/B17 siku ya uzinduzi wa kikao cha
Makandarasi,Wahandisi na Wakadiriaji majenzi pale Mlimani City
kilichohudhuriwa na rais.

Kuonyesha kuwa Mwakyembe ni jasusi aliye kubuhu siku hiyo maji
hakuyanywa wala kugusa kabisa lakini mungu si athumani kitambaa
akakitumia, jambo la kushangaza nikuwa baada ya kama dakika 20
kukitumia kile kitambaa alikitupa wakati anatoka eneo la Mlimani City.


Said Kubenea amekabidhiwa LTK/D00/B21 ambae anasubiri kitendea kazi
toka Bulgaria ambapo jasusi Yugrov Dittzov ndie atakae ileta.





Huu ndio uchunguzi wangu binafsi baada ya kupata taarifa juu ya hali
ya Dr Harison Mwakyembe kuwa ni tete.

Nasema kuwa serikali ya Tanzania inafanya mauaji ya rai wake hasa
viongozi wenye mtazamo tofauti na serikali.

Naiomba serikali ya Mh rais isikilize kilio cha watanzania isisikilize
kilio cha wa kwasi na mafisadi.

Nina waomba watanzania tuungane pamoja bila kujali dini zetu,makabila
yetu wala rangi zetu kulikataa kundi hili la wahalifu lisilozidi watu
30.




Huu ni uchunguzi wangu, unahaki ya kusubiri uchungu wa madaktari wa India

ASANTENI SANA:
JASON BOURNE

Anonymous said...

Mafisadi kweli kiboko.