Monday, February 06, 2012

Aolewa na Wanaume Wawili huko Katavi!

Sijui ilitoka kwenye gazeti gani. Lakini kwa kweli nimependa ushujaa wa huyo Mama Kaela!

********************************************************
MWANAMKE AOLEWA NA WANAUME WAWILI


MWANAMKE mkazi wa kijiji cha Ikandamoyo, wilayani hapa, Veronica Saleh ‘Mama Kaela’ (50), amefanya uamuzi adimu wa kuolewa na wanaume wawili ambao anaishi nao kijijini hapo.

Kijiji hicho kipo umbali wa takribani kilometa 30 kutoka mjini hapa katika Jimbo la Katavi linalowakilishwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Pamoja na ndoa hiyo iliyowezeshwa na mume mkubwa kukubali kuishi na mume mdogo, imeelezwa kuwa mwanamke huyo ndiye ‘aliyewaoa’ wanaume hao kwa zaidi ya miaka saba sasa, huku akiwa na amri kuu katika nyumba, kama ilivyo katika ndoa za kawaida.

Wanaume hao ni Paulo Sabuni ‘Baba Kaela’ (60) ambaye ndiye mume mkubwa na Arcado Mlele (45) ambaye ni mume mdogo.

Taarifa za kuwapo kwa ndoa hiyo ya aina yake, zililifikia gazeti hili na kufanyiwa uchunguzi kwa zaidi ya wiki tatu, na hatimaye katikati ya wiki hii, wahusika walikubali wao wenyewe kuzungumzia suala hilo. Kwa mujibu wa maelezo ya mwanamke huyo ambaye alionekana kuwa msemaji wa familia hiyo, yeye na mumewe mkubwa, walifika kijijini hapo miaka 24 iliyopita, wakitoka kijiji cha Usumbwa mpakani mwa Chunya, Mbeya na Tabora.

Wakiwa kijijini hapo mume wake aliendelea kufanya kazi ya ukulima wakati yeye mama (Veronica), pamoja na kilimo hujihusisha na upishi na uuzaji wa pombe ya kienyeji ya iitwayo kayoga.

Mwanamke huyo ambaye amesema ana watoto wanne, Alfred (20), binti mwenye miaka 16 (ambaye ameolewa) na wengine wawili wa kiume, mmoja akisoma darasa la sita na mdogo ana miaka saba, amesema hana shida na waume wake.

Ingawa wanandoa hao walizungumza kwa hadhari, majirani walikiri kuwa mwanamke huyo anaishi na wanaume hao wawili kwa amani na kwamba mwanamke huyo ndiye mwenye sauti na si waume zake.

“Si siri tena sasa, tumeshawazoea, kwani wanaishi kwa amani ila yule mume mdogo anaishi kwenye nyumba aliyoachiwa na marehemu baba yake, lakini anashinda kwa mume mkubwa, ambapo inajulikana kijijini hapa kuwa ni nyumba kubwa. “Basi pale ni mambo yote, kula na kunywa, mama huyu amewapangia zamu wanaume hao kama afanyavyo mume mwenye wake wengi. Ama kweli ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni,” alisema mkazi mmoja kwa masharti ya jina lake kutoandikwa gazetini. Ilielezwa, kwamba wanaume hao wana akili timamu na hawatumii kilevi cha pombe kama ilivyo kwa mke wao.

Hata hivyo, mume mkubwa anapewa sifa za upole tofauti na mume mdogo anayetajwa kuwa mkorofi kiasi cha mara kadhaa kumchapa makofi mkewe anapomuudhi.

Majirani wanadai kwamba Mama Kaela na mumewe Paulo, walipofika kijijini hapo, walipokewa na kuishi maisha ya kawaida, lakini baadaye mama huyo alianza kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Arcado, ambaye naye alilazimika kuachana na mkewe wa ndoa anayefahamika kijijini hapo kwa jina la Mama Pere.

Ilielezwa na mashuhuda hao kwamba mume mkubwa alipobaini uhusiano huo, alikuja juu, lakini mwanamke huyo inadaiwa alimweleza mumewe huyo, atake asitake lazima wataishi wawili, vinginevyo ataachana naye, ndipo mume mkubwa alipokubali kuishi na mume mwenza.

Katika maisha ya kawaida katika familia hiyo, inaelezwa kwamba katika baadhi ya siku ikitokea kuwa mama huyo amechoka kupika, mume mdogo huchukua jukumu la kupika na kumwandalia chakula na maji ya kuoga mume mkubwa.

“Lakini mara nyingi kwa mfano, ikiwa ni zamu ya mama huyo kulala kwa mumewe mkubwa, basi humfulia nguo zake kisha anakwenda kwa mumewe mdogo nako anamfulia nguo.

“Ndivyo wanavyoishi, nasi sasa tumewazoea ila yule mama ni mkali na ana sauti pale kwake kwa wanaume wale ila tunaona kama ana wivu sana kwa huyu mdogo ambaye naye pia ana wivu kwa mkewe huyo, labda anahofia kuwa mama huyo anaweza kuongeza mwanamume mwingine,” anasema mmoja wa majirani hao.

Hakuna mazuri yasiyokuwa na machungu, japo familia hiyo inaelezwa kuwa na amani, mtoto wao mdogo nusura avuruge uhusiano wa wanandoa hao, baada ya kuibuka mzozo wakati wa maandalizi ya ubatizo wake.

Kwa sababu anazojua mama, ingawa inafahamika kuwa wote ni watoto wa mume mkubwa, mke huyo katika hati za ubatizo aliandikisha ubini wa mtoto huyo kuwa ni Mlele (akimaanisha kuwa mtoto wa mume mdogo), lakini mume mkubwa aliweka pingamizi kanisani akidai yeye ndiye baba halali wa mtoto huyo.

Kwa mujibu wa mwanamke huyo, yeye na Arcado ni waumini wa madhehebu ya Katoliki wakati Paulo ni Mpentekoste. Madai ya mzozo wa uhalali wa `ubaba’ wa mtoto huyo, yalithibitishwa na baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, akiwamo mwalimu wa dini wa Kigango cha Kanisa Katoliki Uruira, Mashaka Abel. Walisema miaka sita iliyopita, mtoto huyo akiwa na umri wa mwaka mmoja, alifanyiwa taratibu za ubatizo, lakini ilishindikana, kutokana na wanaume hao, kila mmoja kudai ndiye baba mzazi wa mtoto.

“Lilikuwa jambo la kustaajabisha sana, kwani familia hiyo ilifanya maandalizi yote ya sherehe ya ubatizo wa mtoto huyo, lakini siku hiyo kanisani wakati huo ilikuwa ni kigango cha Katumba ambacho sasa ni Uruira, sakata lilianzia pale Padri alipomwuliza mama wa mtoto huyo ubini wa mtoto naye akasema ni Mlele.

“Hapo ndipo mume mkubwa alipopinga na kudai kuwa mtoto yule si wa Arcado bali wake na yeye ndiye baba halali. Padri hakuamini, aliuliza tena na tena na majibu yakawa ni yale yale, ndipo ubatizo ukashindikana,” alisema Katekista Abel.

Kazi ya kutafuta undani wa ndoa hiyo haikuwa rahisi kutokana na mazingira ya woga na usiri uliokusudiwa kubaki, ambapo awali mama alisema kwamba mume wake ni Paulo pekee japo siku ambayo mwandishi wa habari hizi alifika kijijini hapo na baadaye nyumbani kwa wanandoa hao na kumkuta mume mdogo (Arcado akimsaidia mkewe kukoroga pombe. Awali katika utambulisho, walidai kuwa ni mtu na mdogo wake na kusita kuzungumzia maisha yao ya kifamilia.

Mke wao ambaye alionekana wazi kuwa ni msemaji mkuu alifoka na kuja juu, akidai kuwa hayuko tayari kuzungumzia uhusiano wake na wanaume hao wawili, ingawa alikiri kuwa wanaishi pamoja.

"Kwa hiyo umefunga safari yote hii kutoka huko ulikotoka ili uje kwangu mie Veronica … nasema sitaki kabisa mtu kuja hapa na kutaka kunivurugia mpangilio wa maisha yangu, kwanza nani alikueleza hayo, wambea wakubwa hao yanawahusu nini watu hao?” alihoji.

“Mie mume wangu ni huyu Paulo basi … sasa leo umeniachia vurugu ndani ya nyumba nitapigwa na huyo mume wangu Paulo, kwani mmenishikisha ugoni?” alifoka Mama Kaela. Hata hivyo, mume mkubwa alidai kuwa hatamwadhibu mkewe huyo na kwamba wataendelea kuishi pamoja na mdogo wake Arcado kwa amani. Hata hivyo, akina mama wengi kijijini hapo wanalaani kitendo cha mama huyo kuishi na wanaume wawili ambapo waliomba uongozi wa Kanisa uingilie kati, ili mama huyo aweze kufunga ndoa na mume mmoja.

Lakini kwa upande mwingine, baadhi walimpongeza mwanamke huyo wakidai kuwa kitendo hicho ni cha kijasiri kwa mwanamke, kumudu kuishi na wanaume wawili na kuwa na mamlaka juu yao.

Ndugu wa Arcado wao wanalaani kitendo cha ndugu yao kuolewa na mama huyo, wakidai kuwa walishamshauri na kumuahidi kuwa endapo ataachana na mama huyo watamwozesha mwanamke mwingine, lakini yeye Arcado, amedai kuwa yuko tayari kufa, lakini si kuachana na mama huyo, kwani ndiye ubavu wake wa maisha.

“Sasa tumebaki tunamwangalia tu huyu ndugu yetu Arcado, tumemshauri, lakini mkaidi, hatusikilizi. Basi nasi hatuna la kufanya zaidi ya kumwangalia,“ alisema mmoja wa ndugu wa karibu wa Arcado. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Florence Katobasho, alikiri kuwa mwanamke huyo anaishi kinyumba na wanaume wawili na wanaishi kwa amani kwani hajawahi kufikishiwa malalamiko yoyote kuhusu wanandoa hao.

“Ni ukweli usiopingika, kwamba Mama Kaela anaishi na wanaume hao wawili … lakini kwa kuwa sijafikishiwa malalamiko yoyote kuhusu maisha ya wanandoa hao, mimi kama kiongozi hapa sina la kufanya na siwezi kuwafukuza, kwa kweli wanaishi kwa amani, mengine ni yao,” alisema Mwenyekiti wa Kijiji

SOMA   ZAIDI http://www.fotobaraza.me/profiles/blogs/mwanamke-aolewa-na-wanaume#ixzz1lVfLAlP4

No comments: