Monday, February 20, 2012

Taarifa ya CHADEMA Kuhusu Ombi la CCM kw Dr. Slaa

  TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KURUGENZI ya Habari na Uenezi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) inapenda kutoa taarifa kuhusu habari zilizoripotiwa kupitia
njia mbalimbali za upashanaji habari, juu ya maombi ambayo Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kimesema kinafanya usiku na mchana ili eti Katibu Mkuu
wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa, agombee ubunge, kwenye uchaguzi mdogo
unaotarajiwa kufanyika Jimbo la Arumeru Mashariki, Aprili 1, 2012.

Ingawa haijajulikana maombi hayo yanafanyika msikiti upi au kanisa
lipi au sehemu ipi yoyote ile nyingine ya kufanyia maombi, Kurugenzi
imeshangazwa sana na mantiki ya kuwepo kwa maombi hayo ya CCM
yakionesha upendo wa kutiliwa mashaka kuwa chama hicho kimefikia
mahali kinaweza kufanyia maombi vyama vingine ili vipate wagombea
makini wa kukibwaga vibaya sana katika uchaguzi.

Kurugenzi inapenda kusema yafuatayo juu ya maombi hayo ya CCM, ambayo
kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye,
kama ilivyoripotiwa katika njia mbalimbali za upashanaji habari,
imedhihirika dhahiri kuwa ni maombi yanayoongozwa zaidi na hila,
husuda kwa CHADEMA na Katibu Mkuu wake, Dkt. Slaa;

Tunapenda CCM wajue kuwa CHADEMA na viongozi wake makini, akiwemo
Katibu Mkuu, Dkt. Slaa, si watu wa kurudi nyuma. Chama hiki daima muda
wote kinapanga mikakati na mipango ya kusonga mbele, kikionesha
utawala mbadala, kikijiandaa kushika dola na kutekeleza malengo ya
Watanzania!

Kwa mantiki hiyo, chama hiki hakiwezi kurudi nyuma, hakiwezi
kumrudisha nyuma Katibu Mkuu wake, Dkt. Slaa kuwania ubunge. Kiongozi
huyu makini, ambaye umma wa Watanzania una imani kubwa naye,
ameshavuka viwango vya ubunge, si mtu wa kuwania nafasi ya ubunge
tena, (is not parliamentary material).

Kwa nafasi yake ndani ya CHADEMA, anao wajibu mkubwa kujenga chama.
Kwa kutimiza wajibu huo, Dkt. Slaa anafanya kazi ya kutengeneza na
kuivisha watu wengine makini zaidi, kuweza kuwa viongozi ndani ya
chama, nafasi za udiwani na ubunge, ili kuendeleza umakini na uimara
wa chama hiki ambacho dhahiri ni tumaini jipya la Watanzania katika
kutoa uongozi mbadala wa nchi.

Kwa umakini wa CHADEMA, uwezo wa Dkt. Slaa na matumaini makubwa ya
Watanzania, ambayo wameendelea kuyaonesha kwa chama hiki tangu mwaka
2007, kilipoanzisha rasmi mapambano dhidi ya ufisadi na mafisadi,
kisha kudhihirika wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, nafasi pekee
inayomstahili Dkt. Slaa ni urais kwa maana ya kuwa ni ‘presidential
material’, si ubunge.

Lakini pia, tunatambua kuwa CCM, wameweza kutoa kauli hiyo ya
kukurupuka baada ya Dkt. Slaa kuwa tayari ametamka wazi tangu awali na
kurudia kauli yake thabiti mara kadhaa kuwa hana nia wala mpango wa
kuwania ubunge mahali popote pale nchini. Hawezi kufanya hivyo kwani
hata ubunge wa Karatu hakushindwa bali aliacha mwenyewe kwa hiari
yake, ili kutekeleza mahitaji ya umma wa Watanzania.

Kurugenzi ya Habari na Uenezi inatumia nafasi hii kuwaambia CCM kuwa
watambue CHADEMA ni chama makini. Kimedhihirisha hivyo mara kadhaa
katika masuala makubwa kwa maslahi ya Watanzania. Kitaendelea
kudhihirisha hivyo pia katika uchaguzi wa Arumeru kwani kina utaratibu
wa kuwapata wagombea wake, kutokana na maamuzi ya wanachama wake.

Tunatambua kuwa kauli hiyo ya CCM pia ni sehemu ya mkakati wa makusudi
kuwakatisha tamaa baadhi ya watu wanaotaka kugombea jimbo hilo kupitia
CHADEMA. Kurugenzi ya Habari na Uenezi inapenda kusisitiza taarifa ya
awali, kuwataka wanachama wetu wajitokeze kwa wingi kuwania uteuzi wa
kugombea ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki.

Tunataka CCM wajue kuwa suala la kuteua mgombea wa CHADEMA ni la
CHADEMA yenyewe, kwa kutumia utaratibu wake, ikiongozwa na katiba,
kanuni na mahitaji ya umma, wala hatuhitaji ushauri wa chama ambacho
kadri siku zinavyokwenda, kinadhihirisha kila dalili ya kuchoka
kujisimamia chenyewe, kusimamia wanachama wake, kusimamia serikali na
maendeleo ya watu, hivyo kupoteza kabisa ushawishi kwa wananchi. Wala
hatujawahi kuomba ushauri kutoka kwao hata siku moja.

Lakini maombi hayo ya CCM, kama ambavyo Nape amenukuliwa katika vyombo
vya habari akisema, yamedhihirisha namna ambavyo chama hicho bado
kinaandamwa na mzimu wa CHADEMA na Dkt. Slaa tangu baada ya uchaguzi
mkuu, kwa kuiba kura na kuvuruga matokeo ya uchaguzi huo.

Kauli ya Nape kuwa iwapo maombi yao yatafanikiwa na Dkt. Slaa akawania
ubunge, CCM watakuwa wamemaliza kazi katika uchaguzi mkuu wa mwaka
2015, inathibitisha tuhuma hizo na namna ambavyo CCM hakikushinda kwa
haki uchaguzi huo.

Kurugenzi ya Habari na Uenezi ya pia inataka CCM waelewe kuwa umaarufu
wa CHADEMA hautokani na umaarufu wa mtu mmoja mmoja wala hausubiri
matukio pekee, bali unatokana na uongozi makini, kuanzia ngazi ya
taifa hadi ya msingi, kikijikita katika kusimamia masuala yenye
maslahi kwa Watanzania na nchi yao muda wote!

Imetolewa leo Februari 18, 2012, Dar es Salaam na

Tumaini Makene
Afisa Habari wa CHADEMA

No comments: