Wednesday, April 03, 2013

Watuhumiwa 11 Kesi ya Kuporomosha Ghorofa Kizimbani

Kutoka Gazeti la Mwananchi


Mtuhumiwa namba moja wa mashtaka 24 ya kuua bila kukusudia, Raza Hussein Ladha (kushoto) akipelekwa chini ya ulinzi wa polisi kuingia katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana.

MFANYABIASHARA Radha Hussein Ladha wa jijini Dar es Salaam, Diwani katika Manispaa ya Kinondoni, Ibrahim Mohamed maarufu kama Kisoki (59) na wenzao 9, jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 24 ya kuua bila ya kukusudia.

Katika kundi hilo pia wamo vigogo wa Manispaa ya Ilala ambao ni Mhandisi Mkuu, Mhandisi Charles Salu (48), Mhandisi wa Majengo Godluck Sylivester (35) Mbaga na Mkurugenzi Mkuu wa Mkaguzi wa Majengo, Willibrod Wilbard (42).

Washtakiwa wengine ni Mhandisi Mohamed Swaburi (61), Mhandisi Mshauri, Zonazea Oushoudada (60), Mkadiriaji Majenzi, Vedasto Nziko (59), Msanifu Majengo, Michael Hema (59), Msajili Msaidizi AQRB, Albert Mnuo na Ofisa Mkuu Mtekelezaji OQRB, Joseph Ringo.

Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Kisoka, Wakili wa Serikali, Tumain Kweka akisaidiana na mawakili wenzake watano, alidai kuwa washtakiwa walifanya makosa kinyume na kifungu cha 195 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho 2002.

Kweka anasadiana na wenzake Benard Kongora, Ladslaus Komanya, Neema Haule, Joseph Maugo na Mutalemwa Kishenyi. Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao kwa pamoja Machi 29, mwaka huu katika Mtaa wa Indira Gandhi, Wilaya ya Ilala waliwaua bila ya kukusudia Yusuph Mohamed, Kulwa Khalfan na Hamada Mussa.

Mbali na watu hao, pia wanadaiwa kuwaua bila ya kukusudia Kessy Manjapa, Khamis Mkomwa, Boniface Benard, Suhail Ally, Salmani Akbar, Seleman Haji, Seleman Mtego, Sikudhani Mohamed, Ahmed Milambo, Salum Mapunda, Suleiman Rashid na John Majewa.

Wengine ni Mussa Mnyamani, David Severin Herman, William Joackim, Abdulrahman Mwiha, Emmanuel Christian, Mmanyi Ngadula, Adivai Desiki, Emmanuel Greyson na Augustino Kasiri. Washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mashtaka yanayowakabili Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza hadi Mahakama Kuu.

Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Wakili wa Kujitegemea, Jerome Msemwa waliiomba mahakama kutoa dhamana kwa wateja wao kwa sababu mashtaka ya kuua bila ya kukusudia yanayowakabili yanadhaminika. Wakili wa Serikali, Kongora alipinga maombi hayo, huku wakili mwenzake Komanya akisema kuwa wakati huu si wa kutoa dhamana kwa kuzingatia mazingira ya tukio lililosababisha kuwepo kwa kesi hiyo.

Kutokana na hoja hizo, Hakimu Kisoka aliiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 16, mwaka huu atakapotoa uamuzi iwapo washtakiwa wapate dhamana ama la. Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ametangaza kiama dhidi ya wamiliki wenye maghorofa yaliyojengwa kinyume cha utaratibu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye Ofisi ndogo ya Bunge, Profesa Tibaijuka alisema kwa kuanzia angesaini hati ya kuamuru kubomolewa kwa jengo lililokuwa karibu na lile lililoanguka wiki iliyopita na kuua idadi kubwa ya watu. Alimwonya mmiliki wa jengo hilo anatakiwa kufanya ubomoaji mara moja tena kwa gharama zake.

“Serikali ikibomoa jengo hilo ina maana atatakiwa kulipia gharama za zoezi hilo,” alionya Profesa Tibaijuka, ambaye aliapa kuanza leo ukaguzi wa maghorofa mbalimbali ya jijini Dar es Salaam.

CHANZO: http://www.mwananchi.co.tz

2 comments:

Anonymous said...

Janga la kuanguka jengo linasemekana ama linaonyesha kwa sehemu ni utamaduni wetu wa rushwa hata kwa jengo linalomilikiwa asilimia 75 na mtu binafsi bado rushwa inaingia!

NHC ndo leo imetangaza kubadili mkataba wake na mwenye jengo! Ilikuwa wapi mapema kujua ubia wake na mmiliki unaweza kuingiwa na dosari hii?

Tunajua rushwa ipo lakini hatuifuatiliii kwa namna ambayo ingetusaidia kuimaliza, lakini tunasubiri mpaka litokee ndipo tuanze kusema na kulalamika.

Kifusi Arusha kwa sehemu ni kushindwa kufuatilia uchimbaji wa aina ambayo umeletea maafa. Inawezekana rushwa ipokatikati, lakini janga limeshatokea, maisha yamesharokea, uyatima umeshaingia, ujane, umasikini nk.

Juzi watoto wetu nchi nzima wameshindwa masomo yao - katika umri ambao mtu anafurahia kujifunza, kudadisi, kuhoji, kutaka kujua zaidi, tumewanyima nafasi hii na hatuhofii rushwa iliyoangamiza kizazi!

naogogopa sana!

Anonymous said...

Hii ya kuanguka majengo Bongo has become so predictable that unaweza kutengeneza ratiba ya kuanguka majengo. Yaani imekuwa ni kitu cha kawaida and yet nobody seems to care. Hata hii kesi ni kiini macho tu. Hakuna atakayefungwa hapo.