Monday, January 04, 2010

Kumbukumbu za Kongamano 2009 - Dar es Salaam

Kumbumbukumbu za Kongamano

Kongamano la Kwanza la Wanataaluma Waishio Ndani na Nje ya Nchi 2009


Mada Kuu: Wanataaluma Na Vipaumbele Vya Taifa na Jinsi Wanavyoweza Kuchangia na Kuchochea Maendeleo ya Nchi na ya Watanzania

Kongamano la Kwanza la Wanataaluma Waishio Ndani na Nje ya Nchi 2009 lililoandaliwa na
Mtandao Wa Wanataaluma Tanzania (Tanzania Professionals Network – TPN ) ikishirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH); Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT); Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mlimani (UDSM); na Serikali (Mambo ya Nje) lililofanyika kwa siku moja Ijumaa; tarehe 18 December 2009 katika Hoteli ya Golden Tulip Dar es Salaam limemalizika kwa mafanikio makubwa.

Kongamano hili lililohudhuriwa na Wanataaluma kutoka Dar Es Salaam; mikoani na nje ya nchi, lilifunguliwa na Mheshimiwa Bernard Kamillius Membe (Mbunge), Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia alitoa mada iliyoanzisha mjadala wa suala la Uraia wa Nchi Mbili (Dual/Smart Citizenship) na masuala mengine yahusuyo Watanzania wanaoishi nje ya nchi.

Majadiliano katika Kongamano hili yaliendeshwa kwa utaratibu wa kuchangia hoja kuu, huku mchangiaji akieleza suala / hoja husika, tatizo au changamoto kama ipo, mapendekezo ya kutatua tatizo na mikakati ya utekelezaji. Baada ya hapo washiriki wengine walichangia hoja hiyo na makubaliano kufikiwa. Mijadala yote ilijikita katika kujadili hoja za msingi na ufumbuzi wa tatizo pale ilipobidi.

Mwishoni mwa Kongamano kulikuwa na Maazimio kadha wa kadha na Mikakati ya Utekelezaji katika kufanikisha maazimio hayo. Yafuatayo ni Kumbukumbu, Maazimio na Mikakati ya yaliyojiri katika Kongamano hilo:

1. Kuhusu ni Namna Gani Wanataaluma Waliopo Nje ya Nchi Wanaweza Kushiriki Kuleta Maendeleo Nchini

Kongamano limechambua na kukubaliana kuwa Watanzania Wanataaluma wengi wanahamia na kuishi nje ya nchi kwa sababu zifuatazo:

• Kupata Elimu ya juu na hasa ya vyuo vikuu huku baadhi wakitafuta uraia wa nchi husika ili kupata unafuu wa maisha yanayotokana na gharama za chini za elimu, matibabu n.k kwa raia ukilinganisha na wageni.
• Kutafuta ajira za kitaaluma katika sekta tofauti kama Afya; Elimu, Sayansi na Teknolojia; na wengine hutafuta ajira zisizo za kitaaluma katika sekta tofauti. Ajira nzuri katika nchi husika huwa rahisi kupata kama tu utapata uraia.
• Kutafuta, kufanya biashara na kuwekeza katika nchi husika
• Kupata uraia wa nchi husika: Sababu zinategemea mhusika mwenyewe na mazingira yake zikiwemo sababu za kindoa; michezo au kupenda tu kupata kibali/uraia wa kuishi huko kwa sababu mbalimbali.
• Sababu nyingine ni kama kupata mikopo; matibabu n.k

Kongamano pia limetambua faida na michango inayotolewa na Wanataaluma wanaoishi nje ya nchi ikiwa ni pamoja na:

• Kutuma pesa nyumbani kwa ndugu jamaa na marafiki kwa ajili ya mahitaji mbalimbali yakiwemo ya kifamilia, ujenzi, biashara n.k.
• Kuunganisha na Kufanikisha shughuli za Kibiashara kati ya Wafanya biashara waTanzania na wa Nchi husika
• Kupata ujuzi wa Kitaaluma na Kisomi kwa baadhi ya fani kutoka kwa Watanzania wa Nje kusaidia nyumbani katika sekta tofauti.

Kongamano pia limetambua changamoto mbalimbali zinazowapata Wanataaluma waliopo nje ya Nchi. Changamoto hizi ni pamoja na:

• Kukosa kutambuliwa, ushirikiano hafifu au kukosa kupata misaada toka kwenye baadhi ya balozi zetu nje na hata serikali kwa baadhi ya mambo kwa sababu mbalimbali; lakini zaidi ni ile dhana ya kuwaona watu walioenda kuishi nje kama wasaliti.
• Kukosekana kwa umoja wa kindugu kwa baadhi ya Watanzania walioko nje ili waweze kusaidiana katika mambo ya kimsingi na ya maendeleo.
• Kukosekana kwa taarifa za msingi za watanzania Wanataaluma waliopo nje ya nchi i.e. idadi; fani, matukio muhimu toka nyumbani, fursa za kazi katika mashirika ya kimataifa huko huko nje ama hata nyumbani nk.
• Kukosekana kwa sheria ya kuruhusu uraia wa Nchi mbili ili kwa wale walio na uraia wa Nchi za Nje wawe wanakubalika kuwa na wao ni raia wa Tanzania.
• Kukosekana kwa mikakati na sera nzuri kwa wale walioamua kurudi nyumbani na kuja kuwekeza ili kuchochea wengi waweze kufanya hivyo kirahisi.
• Kutokuwako mipango na mikakati ya maendeleo ya muda mrefu yanayoweza kuwapa uhakika wa maisha yao endapo watarudi nyumbani.
• Matatizo ya rushwa na usimamizi mbovu wa rasilmali na utawala usio wa uwazi na kuwajibika hapa nchini huwakatisha tamaa ya kurudi nyumbani haswa wakizingatia jinsi maswala ya utawala bora yanavyopewa kipaumbele huko nje wanakoishi.
• Kiwango cha huduma za jamii bado hakiridhishi sana kiasi cha kuwatia wasiwasi kama watoto wao na familia kwa ujumla watapata elimu na huduma za afya bora pamoja na mambo mengine ya ustawi wa jamii. Hii pia inachangiwa na ukweli kuwa viongozi wengi watoto wao wanasoma nje na baadhi wanapata matibabu yao nje ya nchi.

Kutokana na hoja zilizotajwa hapo juu; Kongamano limeazimia yafuatayo:

• TPN iwe ni chombo mahsusi cha kuwaunganisha Wanataaluma walio nje na ndani ya nchi (kupitia vyama na Jumuiya zao, n.k.) na kushughulikia na kufuatilia masuala yao hapa nyumbani na hata yale ya kule nje hususani toka kwa balozi zetu na ofisi za serikali mbalimbali ndani na nje ya nchi.
• TPN iwe ni chombo cha kuwasemea hapa nyumbani katika masuala yao mbalimbali, vipaumbele vyao na mambo mbalimbali kuhusiana na uhamiaji na maendeleo kwa ujumla kwa Serikali ya Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa hapa nyumbani.
• Wanataaluma wa Nje ni ndugu, jamaa na marafiki zetu na hivyo ni sehemu muhimu kwa maendeleo ya nchi. Hivyo basi wito umetolewa kwa madau mbalimbali kuweka mipango ya mbeleni na sera ambazo zitazingatia pia mahitaji ya wanaoishi nje.
• Ni vema wadau na vyombo husika vikaandaa mazingira mazuri kwa wale wenye nia ya kurudi na kuja kuwekeza nyumbani kwa kuweka vivutio na urahisi wa wanaorudi kuanzisha miradi yao.
• Kuhusu uraia wan chi mbili:
a) Kwa kuwa kuna raia wa nchi za nje wanaopewa uraia nchini Tanzania lakini bado ni raia au wanatambulika katika nchi zao walizotoka,
b) Na kwa kuwa tunao wanataaluma Watanzania wengi ambao ni wataalamu katika fani mbalimbali nchi za nje wanakoishi na wamepewa uraia wa nchi husika ingawa walizaliwa huku na ni ndugu na jamaa zetu lakini kwa ajili ya sheria yetu ya uraia wa nchi mbili haiwatambui,
c) Na kwa kuwa wanataaluma hawa wanachangia maendeleo ya nchi yetu kwa namna mbalimbali kama ilivyoainishwa hapo juu

Kongamano linatoa wito kwa Watanzania na vyombo husika kutowaona wanataaluma hawa kama wasaliti au kuwakatalia uraia warudipo nyumbani badala yake tuliangalie suala hili kwa mtazamo wa kimaendeleo na kuweka utaratibu makini wa kukubali kuwa na sheria ya kukubali uraia wa nchi mbili baada ya kuridhika na vigezo Muhimu vitakavyowekwa.

• Kongamano pia limetambua na kuipongeza hatua ya serikali katika kipindi hiki ya kuwatambua wanaoishi nje kama eneo maalumu na hata kuamua kuliundia Idara maalumu ya kushughulikia masuala yao. TPN inaahidi kufanya kazi kwa karibu na idara hii katika kushughulikia masuala ya waliopo nje kama kiungo chao au chombo maalumu katika masuala mbali mbali.
• TPN iendelee kuandaa Kongamano kama hili kila mwaka litakalowakutanisha wanataaluma Watanzania wa ndani, nje, wanazuoni; wafanyabiashara; serikali na wadau wengine kuzungumzia masuala mbalimbali ya Kitaaluma na yanayohusu maendeleo ya nchi.
• TPN ishirikiane na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi kuhusiana na suala zima la utumaji wa pesa nyumbani. TPN ifuatilie bank kuu kuona ni vipi inaweza kupunguza au kuondoa gharama za kutuma pesa na pia kuangalia uwezekano wa kuanzisha Diaspora/Investment Bank.
• TPN kwa kushirikiana na wadau wengine na wanataaluma ianze kuandaa Database ya wanataaluma waliopo nje na ndani ya nchi kwa madhumuni ya kuwatumia walio makini katika kazi za kitaalamu (consultancy and contract works) badala ya kazi hizo kufanywa na wataalamu toka mataifa mengine. Database hii pia itatumika kuunganisha walio nje lakini wanapenda kurudi kufanya kazi au kuwekeza na makampuni mbalimbali nchini.
• TPN iwe kama kiungo cha kusaidia kupata taarifa mbalimbali juu ya Tanzania katika mambo mbalimbali hasa yanayohusu utalii na biashara au uwekezaji.
• Wito umetolewa kwa wale ambao kwa kuishi kwao nje hawana maendeleo yoyote warudi nyumbani na kusaidiana kujenga nchi – Nyumbani ni nyumbani. Imedhihirika wakati wa Kongamano kwa mfano ulio hai kuwa mafanikio pia yanaweza kupatikana hapa nyumbani. Mwanataaluma mmoja wa darasa la saba aliyepata kuwa msaidizi wa fundi wa umeme tu, kwa sasa ana maendeleo makubwa sana ya kiuchumi na maisha kwa ujumla. Kama tukiwa makini na mikakati bora mafanikio yanaweza kupatikana hata nyumbani.
• TPN ifanye jitihada za makusudi za kuanzisha matawi nchi mbalimbali waliko Watanzania Wanataaluma ili kuunganisha nguvu za kimaendeleo

2. Kuhusu ni Namna gani Wataalamu Wanavyoweza Kusaidia Kuleta Maendeleo na Kuboresha maisha ya Watanzania wa Kawaida katika nyanja mbalimbali kama Uchumi; Siasa; Elimu; Jamii nk.

Kongamano limechambua na kukubaliana mambo yafuatayo:

Mambo yanayokwamisha maendeleo yetu hasa ya kiuchumi ni pamoja na:

a) Kukosekana kwa maarifa na ujuzi na hasa wa vitendo katika kufanya mambo mbalimbali yatakayopelekea kupata maendeleo
b) Ugumu wa kupata mitaji na ushauri wa kitaalamu na mafunzo katika kufanikisha azma yoyote ya maendeleo.
c) Kukosekana kwa mazingira bora na ya makusudi ya kuwezesha mafanikio ya kiuchumi katika maeneo ya sera, sheria; taratibu na utawala.
d) Kukosekana kwa mitazamo chanya ya kimaendeleo itakayopelekea kuleta mafanikio bila kuwa na ulazima wa kupata mafanikio ya haraka bila juhudi zozote. Hii pia inachangiwa na baadhi kukosa kujiamini; kushindwa kuwajibikaji kikamilifu; kukosa uaminifu; uadilifu na kupenda maisha ya fahari yasiyoendana na kipato.
e) Uongozi mbovu kwa baadhi na kukosekana kupenda kuthamini rasilimali zilizopo kama muda; ujuzi; maliasili, mitandao nk.
f) Kukosa hamasa ya kujifunza, kuboresha na kuwa wabunifu katika mambo mablimbali ya kimaendeleo
g) Tatizo la kupata wenza (partners) wenye mitazamo inayofanana wa kuweza kufanya nao mambo pamoja katika hali ya kuaminiana.
h) Ugumu wa kupata masoko ya uhakika kwa wakati mwafaka kwa ajili ya mazao au huduma mbalimbali aidha kuwa na uwezo duni wa kukabiliana na soko hata pale masoko yakipatikana.
i) Bado kuna mambo mengi yanapangwa na kuandaliwa na wafadhili, kutolewa fedha na kusimamiwa utekelezaji wake na wafadhili kwa namna fulani huku kukiwa na kuhusishwa kwa kiwango cha chini katika mikakati na umiliki wa mipango hiyo na utekelezaji kwa wananchi walengwa au waliokusudiwa.
j) Kukosekana kwa umakini katika ubunifu wa mikakati itakayokuwa endelevu na kuleta maendeleo mfano: Mabilioni ya JK; SME Guaranteed Fund; Kilimo Kwanza, Shule za Kata n.k. na kushindwa kujifunza vema kutokana na makosa ya nyuma au toka nchi nyingine.
k) Kukosekana kwa uadilifu na umakini wa kiutendaji kwa baadhi ya Wanataaluma waliopo ndani na nje ya serikali.

Maazimio ya Ni Nini Wanataaluma Wanaweza Kufanya Kuleta Mabadiliko ya Kweli

1. Kuanzisha na kutoa uongozi (Leadership) kwa mabadiliko ya mazoea ya Kifikra (Attitude Change) na Kiutamaduni (Culture Change) tukianzia na sisi wenyewe kila mmoja binafsi .
2. Kuhamasisha na kuongoza mikakati yetu wenyewe na miradi yetu huku tukijifunza kutokana na makosa/mafanikio ya nyuma na kutoka nchi nyingine ambayo moja kwa moja yanalenga katika kutatutua changamoto za Kimaendeleo katika nyanja ya uchumi, siasa, jamii, nk.
3. Kuwajibika na kuwa na moyo wa kizalendo huku kila moja wetu akijiuliza ni nini anaweza kuchangia katika kutatua maendeleo ya nchi badala ya kutaka kuona tu Serikali na wadau wengine ndiyo wanaotakiwa wafanye kila kitu.
4. Kubuni mfumo wa Elimu na Mafunzo ambayo itatoa ujuzi wa kiutendaji na mabadiliko ya Kifikra na Utamaduni kutoka ngazi ya chini.
5. Kuanzisha huduma mbalimbali za kifedha zinazoendana na mahitaji na changamoto za Kitanzania mfano wa Muhamad Yunus Grameen Bank Scheme
6. Kubuni na Kuanzisha huduma ambazo zitaendana na mahitaji ya kijasiriamali kwenye miradi ya kilimo, au ofisi/nyumba za biashara, ufugaji, umeme, incubators (Sehemu za kuzalisha au kutoa Wajasiriamali), ushauri nasaha wa kitaalamu kuhusiana na sheria na taratibu, nk.
7. Kuhakikisha kuwa kuna mipango madhubuti ya kuwawezesha wengi kuwa na taarifa na kujua mifumo ya masoko na nini kinatakiwa kifanyike.
8. Kwa wale walofanikiwa kutengeneza nafasi za ajira, Waajiri Watanzania na kuwapatia mafunzo husika.
9. Sisi wenyewe kuwa mfano na kupigania maendeleo kwa nguvu zote na kuelimisha jamii na umma kwa ujumla juu ya changamoto na jinsi ya kukabiliana nazo zikiwemo za ukimwi, uharibifu wa mazingira, nk.
10. Tujitokeze kutetea haki za wenzetu zinapokiukwa, kwa kutumia taaluma zetu za kisheria, na kwakutumia vilevile mahusiano yetu na viongozi wa taasisi na vyombo mbalimbali (Network). k.m. kama kuna masuala yanayohusu taasisi kutowajibika katika jambo au mambo Fulani kiasi cha kuleta madhara kwa wananchi, ama kama kuna idara za serikali, wawekezaji au waajiri wanapokiuka taratibu na kuwanyima haki wafanyakazi wao basi tuwatetee hao wenzetu kwa taaluma zetu na pia kuchukua hatua hasa pale panapokuwa na ushahidi ulio dhahiri.
11. Kujenga Mtandao wa Kibiashara (Business Networking): Watu wengi wana mawazo mazuri ya biashara/miradi lakini hawana sehemu ambayo wanaweza kupeleka mawazo hayo na kuyauza kwa watu wengine ambao kama watavutiwa wanaweza kutoa ushirikiano wa kuafanikisha.
12. TPN iwasiliane na EAC kujitambulisha na kutaka kujua masuala muhimu yanayogusa maslahi ya nchi na kisha kuyatolea msimamo kama taasisi huru na kusaidia kuwaandaa watu wetu katika mchakato wa kuelekea katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
13. Wazalendo Wanataaluma waone uwezekano wa kuokoa rasilimali tulizo nazo kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusindika matunda badala ya kuendelea kutumia Juice kutoka nje ya nchi wakati matunda ya nchi hii mengi yanaharibika, mazao ya mifugo mfano maziwa. Hivyo tuonyeshe uzalendo wetu kwa kutumia taaluma zetu.
14. TPN ianzishe kampeni kubwa za kuhamasisha wadau mbalimbali kutengeneza bidhaa bora zinazozingatia viwango na kisha kuanzisha kampeni za kuwataka Watanzania wajivunie, wathamini na kutumia vinavyotengenezwa ndani na hivyo kuinua uchumi,
15. TPN iwe kituo cha mawazo ya kulinda na kuboresha mambo ya kiuchumi.
16. Kutokana na hali duni ya uchumi wa watanzania, Wanataaluma wazalendo tuwe huru kutoa ushauri /huduma bila kujali utapata au kufaidi nini.
17. Kuitisha mkutano wa Wanataaluma wanaotoa maamuzi na wanaofanya kazi Seriklai za Mitaa kuanzia na Dar Es Salaam katika maeneo ya: ardhi; mazingira; huduma za jamii; usalama katika ngazi zote; uhumi; miundombinu; elimu, teknolojia nk.
18. TPN ianzishe kituo cha Taarifa za Ajira na nyinginezo muhimu: Taarifa za Wanataaluma zinazoonyesha, elimu, sifa, uzoefu, ujuzi, umri, anuani nk.
19. TPN ianzishe mazungumzo na vyombo husika na sekta binafsi katika kubuni na kutekeleza sera zitakazohakikisha kuwa michakato ya ajira inawapendelea.

Kuhusu Vipaumbele vya Taifa (Kilimo) na Dira ya Maendeleo - Tulikotoka; Tulipo, Tunakokwenda: Changamoto na Ufumbuzi

Uchambuzi ulifaofanywa:

1) Kilimo ni sekta inayoongoza ambapo inachangia karibu asilimia 45% ya pato la taifa na karibu aslimia 60% ya mauzo ya nje katika miaka 3 iliyopita. Kilimo ni chanzo cha chakula na pia malighafi kwa baadhi ya viwanda. Kilimo ndicho kinachoendesha maisha ya watu wanaokaribia asilimia 82% ya watu wote. Hivi karibuni, sekta ya Kilimo imeonyesha kukua kwa asilimia 4.8 kwa mwaka ikilinganishwa na asilimia 3.1% katika kipindi cha mwaka 1998 to 2000. Vikwazo vya kuondoa umasikini kwa kiasi kikubwa vinapatikana katika sekta ya Kilimo ambayo kwa ujumla wake inatakiwa ihuhusishe mifugo, uvuvi na ufugaji wa nyuki.

2) Vikwazo katika sekta ya Kilimo ni pamoja na matumizi ya chini ya ardhi, juhudi ndogo za wakulima wenyewe, ukosefu wa pembejeo za uzalishaji; kukosekana kwa miundombinu ya umwagiliaji; ukosekanaji wa mitaji, ukosefu wa huduma za fedha na kibenki; uhaba wa huduma za ushauri wa kifundi; Miundombinu isiyoridhisha inayounganisha vijijini na mijini; magonjwa na wadudu wa kuharibu mazao na mifugo; mmomonyoko wa ardhi na uharibifu wa mazingira. Vikwazo vingine ni pamoja na mahusiano mabaya ya kijinsia katika uzalishaji, uzalishaji mdogo na matumizi ya chini ya teknolojia katika Kilimo.

3) Kama tunahitaji kukuwa kwa haraka kwa GDP, ni dhahiri kuwa kupunguza umasikini maeneo ya vijijini kunatakiwa kupewe kipaumbele. Kukuwa kwa mapato kutategemea kuongezeka kwa uzalishaji na ubora wa Kilimo. Itategemea sana ukubwa wa uwekezaji binafsi katika Kilimo kwa Jumuiya ya wafanyabiashara na wadau wadogo wadogo wenyewe ambao wanatakiwa waunganishwe katika mfumo wa jumla wa uzalishaji unaohusisha upatikanaji wa pembejeo, upanuzi, usafirishaji, michakato na masoko. Mifumo hii ya jumla inaweza ikaimarishwa na kufanywa iwafikie walio wengi na kuwatia moyo waongeze uzalishaji na ubora wa mazao yao.

4) Kuna changamoto za wafugaji hawa kupata mikopo wanayoweza kumudu kulipa na pia kupata dhamana ya mikopo. Na hata wanapofanikiwa bado kunakuwa na shida ya kupata masoko ya uhakika. Viwanda vya kusindika maziwa na hata mazao ya Kilimo ni vichache sana na baadhi ya sehemu hakuna kabisa.

5) Wako wapi Wanataaluma wa kuwekeza katika eneo hili na kuunga mkono jitihada hizi kwa kuanzisha masoko ya uhakika na kuongeza vipato? Tanzania ni nchi ya tatu katika Afrika yenye idadi kubwa ya mifugo. Hata hivyo jirani zetu wa Kenya wanasindika maziwa zaidi kuliko sisi. Botswana wanazalisha na kusindika maziwa zaidi ya Tanzania. Wakati huo huo inakisiwa kuwa kuna Watanzania kama asilimia 85% ya Wanataaluma wote wanaofanya kazi katika sekta hii huko Botswana. Ni kwa nini?

Waraka wa Kilimo Kwanza:

Kongamano lilipitia waraka wa Kilimo Kwanza

1) Kilimo kinachukua takribani nusu ya GDP na robo tatu ya bidhaa zote zinazouzwa nchi za nje. Pamoja na kutoa chakula, kilimo vile vile kinatoa ajira kwa asilimia 80 ya Watanzania. Sehemu kubwa ya kilimo Tanzania ni cha wakulima wadogo-wadogo (small-holder farmers, au peasants) ambao mashamba yao yana ukubwa wa kati ya hekta 0.9 na hekta 3.0 kila moja. Karibu asilimia 70 ya ardhi ya ukulima wa mazao inalimwa kwa kutumia jembe la mkono, asilimia 20 kwa kutumia maksai na asilimia 10 kwa kutumia trekta. Kilimo cha Tanzania ni cha kutegemea mvua. Uzalishaji wa mazao ya chakula ndio unaoongoza katika uchumi wa Kilimo. Hekta milioni 5.1 zinalimwa nchi nzima kila mwaka, na kati ya hizo asimilia 85 ni kwa ajili ya mazao ya chakula tu. Wanawake ndiyo wafanyakazi wakubwa mashambani. Matatizo makubwa yanayokabili Kilimo nchini Tanzania ni upungufu wa nguvu kazi na uzalishaji kutokana na uhaba wa nyenzo za kisasa za ukulima pamoja na kutegemea sana hali ya hewa ambayo haiaminiki. Mazao na wanyama huathirika vibaya sana nyakati za ukame. Kilimo cha umwagiliaji maji ndicho ambacho kinaweza kuinusuru Tanzania katika kuhakikisha uzalishaji usioterereka ili kujenga akiba nzuri ya chakula, pamoja na kuongeza kipato na kuboresha uzalishaji wa mazao kwa mkulima.

2) Mazao makubwa ya chakula ni: mahindi, mtama, mpunga, ngano, maharage, muhogo, viazi na ndizi. Na ya biashara ni:Kahawa, pamba, korosho, tumbaku, katani, alizeti, majani ya chai, karafuu, mazao ya bustani, ufuta, viungo vya chakula na maua.

3) Waraka umeainisha maeneo ya Kilimo; uwezo wa kuendeleza Kilimo cha umwagiliaji na pia maeneo yaliyotengwa ya kuwekeza au kuingia ubia na serikali. Mkazo umewekwa kwenye uzalishaji wa chakula na kupunguza umaskini. Kwa miaka mingi uzalishaji wa chakula nchini umeshindwa kutimiza mahitaji ya chakula, na hivyo kusababisha uagizaji kutoka nje na misaada ili kufidia pengo.

4) Kilimo Kwanza kimeelezwa kuwa kimepangwa kisitegemee misaada ya wafadhili kama jitihada zingine za nyuma za Kilimo. Kinatakiwa kiwe kiungo kati ya wakulima wadogo na wa kati kitu ambacho pia kilikosekana katika mipango ya miaka ya nyuma. Kilimo kwanza kimeelezwa kulenga kuwahamasisha wawekezaji wa ndani kujihusisha na Kilimo kikubwa cha Kibiashara.

5) Hata hivyo bado Kilimo kwanza kinaweza kikashindwa kutatua matatizo ya umasikini ya wakulima wadogo walio wengi ambao kipato chao ni chini ya TZS 700 kwa siku kwa kuwa hakushirikishwa ni vipi na kwa namna gani hatimaye atawezeshwa amudu Kilimo hicho kwa kipato hicho hata kama atapatiwa mkopo. Je pembejeo atapewa bure, atazipata vipi, gharama za awali atamudu vipi nk. Inatakiwa kazi ya ziada ifanyike kuhakikisha kuwa wakulima hawa masikini wanaelewa kwa undani Kilimo kwanza ni nini na wao watahusika vipi ili kufanikiwa ikizingatiwa kuwa wako katika lindi la umasikini. Kama itachukuliwa tu kuwa Kilimo kwanza ni biashara kama dhana ya Kilimo Kwanza inavyotamka sasa, basi inawezekana masikini wengi wa vijijini bado wakapata tabu kujihusisha na biashara hii na kupata faida.

Maazimio kuhusiana na Vipau mbele vya Taifa na hasa Kilimo:
1) Umasikini katika Tanzania umeenea sana na wala hauwezi kumalizwa katika kipindi kifupi. Ni malengo ambayo yatatekelezwa kupitia mikakati ya muda mrefu inayolenga katika ukuaji wa kiwango cha juu, kuboresha nafasi za kiuchumi kwa wasio na uwezo au masikini, kujenga uwezo wa wafanyakazi (human capital) na kuwawezesha masikini washiriki katika mikakati ya maendeleo. Kufikia katika malengo hayo, katika muda huu wa kati inatakiwa tujikite katika mipango madhubuti ya kurekebisha na kukuza uchumi ambayo itahusisha kuimarisha uwezo wa kila mtu, kila familia na kila jamii na kupunguza athari mbalimbali kwa kuwapatia huduma muhimu kwa wale walio katika hali mbaya.

2) Kongamano limeona jitihada kubwa zinatakiwa kwa Wanataaluma wa Tanzania kujipa changamoto ya kutoka katika nadharia na kwenda katika kutenda au utekelezaji. Wanataaluma tumekuwa maarufu katika kuandika na kutoa machapisho na makabrasha mengi mazuri yanayogharimu pesa nyingi katika tafiti na kisha semina na makongamano na hatimaye vyote kuishia katika makabati (Shelves) na kutumika kama rejea tu (reference) badala ya kufanyiwa kazi. Njia pekee ya kuondoa umasikini ni kuyaweka haya yaliyomo katika makabrasha katika vitendo. Inafaa kabisa kuitisha Makabrasha mbalimbali zikiwemo machapisho ya research na thesis za kisomi ili zifanyiwe kazi.

3) Inashauriwa kuwa Kilimo Kwanza ihusishe pia dhana ya kuwa na “incubators au Vituo vya ujasiliamali” huku ikihusisha sekta mbalimbali kama Kilimo, Mifugo, Uvuvi na shughuli nyingine za Kiuchumi katika eneo husika huku mkazo ukiwa katika Kilimo. Vitu vingine muhimu vya kuzingatia na kuhakikisha vinafanyika ni pamoja na kutoa mafunzo,kuweka au kuboresha miundombinu ikiwepo ya umwagiliaji na barabara, huduma za kifedha, masoko ya uhakika, ghala za kuhifadhi chakula; “packing”, uvunaji na usindikaji.

4) Baada ya kupitia taarifa za msingi, Kongamano limeona na kushauri kuwa: pamoja na nguvu kubwa kuwekwa katika Kilimo Kwanza, kulikosekana kwa ushirikishwaji wa Wananchi wa Viijijini katika mipango ya awali kama inavyotakiwa na Katiba na Kitaalamu ili waweze kuwa wamiliki halali wa Kilimo kwanza. Pia yako maeneo mengine kama Ufugaji, Uvuvi, na ufugaji wa Nyuki ambayo yangefaa sana yaingizwe katika Mkakati wa Kilimo Kwanza kwa kuwa ni maeneo yanayowahusu hasa wananchi masikini na walio na kipato cha chini lakini yanakosekana.

5) Wanataaluma wanatakiwa sasa kuhusika katika jitihada hizi na kuunga mkono wazalishaji wadogowadogo kwa kuwapa mafunzo katika ufugaji na Kilimo bora na hata katika Kilimo cha Bustani na usindikaji na kuwapatia misaada mingine na kuwaunganisha na masoko ya ndani na nje. Hili linawezekana hasa ukizingatia kuwa tunazo rasilimali za kutosha katika nchi yetu.

6) TPN kupitia kwa wanachama wake mbalimbali imedhamiria kuhamasisha wanachama wake na Watanzania kwa ujumla kupata ardhi katika kila mkoa kwa ajili ya Kilimo kwanza na mambo mengine ya kimaendeleo.

7) Inashauriwa mikakati ya vijijini inatakiwa pia ihusishe matunzo ya mifugo ya familia na jamii na kuwahusisha na mafunzo ya ufugugaji wa shamba la maziwa na vitu vinavyohusiana na hilo kama ecolojia ya Kilimo na ufugaji. Upo ushahidi kuwa kupitia mafunzo na huduma nasaha kwa wafugaji familia zinaweza kuboresha mabanda ya wanyama, menejiment, uzalishaji, lishe na matibabu.

8) Yako mengi ya kufanya kuwezesha mazingira ya maendeleo yawepo. Wadau wote wanatakiwa wajihusishe katika utekelezaji. Utekelezaji mzuri ungeweza kufanywa na Asasi zisizo za Serikali, CBOs and NGO’s, Vyama vya Uzalishaji, Vyama vya Ushirikana hata Sekta binafsi. Mfano mkakati wa vitendo kama “Ng’ombe moja kwa kila familia masikini” unaoendeshwa katika baadhi ya nchi umefanyiwa tathmini na kugundua kuwa, Mifugo ni ni silaha Muhimu sana ya kumaliza tatizo la njaa na umasikini katika nchi. Sasa hivi wamewapa kazi CSO na NGO katika kutekeleza mpango huo kwa niaba ya serikali.

9) Sambamba na kilimo na mifugo, Ufugaji nyuki na uvuvi wa kibiashara ni maeneo mengine muhimu sana yanayohitaji kuangaliwa vyema na kuungwa mkono.

Je, Ni Wakati Gani Mwafaka Wanataaluma Walazimike Kuchukuka Hatua za Kuleta Mabadiliko Na kwa Vipi?

Yafuatayo yaliangaliwa kama msingi mkuu wa kujihakikishia maendeleo hasa katika muktadha wa sheria kama ilivyo ainishwa katika katiba ya nchi:

1) Binadamu anatakiwa awe mlengwa na kiini cha sheria, na zaidi ya hayo sheria ni kwa ajili ya mtu na lazima imtumikie mtu na si vinginevyo. Hata kabla haijatumikia dola, sheria lazima kwanza imtumikie mtu asilia. Ni sawa kabisa kusema sera zote za maendeleo na michakato yake ikihusisaha kila sheria lazima imuweke mwananchi kama “Mshiriki na Mlengwa” wa maendeleo husika. Leo hii miaka 48 baada ya Uhuru, maendeleo ya kiuchumi bado yamebaki ni ndoto za matumaini kwa Watanzania walio wengi.

2) Tanzania ni nchi inayotajwa kuwa ni masikini kati ya nchi masikini sana katika maeneo ya kukua kwa uchumi. Hata hivyo, ni nchi inayotajwa kama tajiri sana kwa rasilimali za asili. Swali pekeee ambalo wengi wanajiuliza ni “Je, shida yetu ni ni ni hasa?” Je, tunao mfumo wa sheria wa kuunga mkono mchakato wa maendeleo? Je, Katiba yetu inavo vifungu vya kisheria vinavyojitosheleza katika suala zimana muhimu kwa maendeleo? Kitu Muhimu zaidi ni Je, katiba inazo vifungu vinavyoheshimika katika kiwango cha kuweza kuleta maendeleo yunayoyataka?

3) Mfumo wa Sheria unatoa msingi wa uendeshaji ambapo mipango yote na utekelezaji inafanyika. Sheria inaelezea maelekezo yote ya kushughulikia masuala yote Muhimu ikiwa ni pamoja na taratibu, maadili; wajibu na majukumu ya watekelezaji, walengwa na wadau wengine.


Katiba ya Nchi inatambua yafuatayo:

a) Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba;
b) Lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi;
c) Serikali itawajibika kwa wananchi;
d) Wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya Katiba
e) Utu na haki nyinginezo zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa;
f) Sheria za nchi zinalindwa na kutekelezwa;
g) Shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumyonya mtu mwingine;
h) Maendeleo ya uchumi wa Taifa yanakuzwa na kupangwa kwa ulinganifu na kwa pamoja;
i) Kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi, na kazi maana yake ni shughuli yoyote ya halali inayompatia mtu riziki yake;
j) Heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata Kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu Haki za Binadamu;
k) Serikali na vyombo vyake vyote vya umma vinatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wake kwa waume, bila ya kujali rangi, kabila, dini au hali ya mtu;
l) kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini;
m) Matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha umaskini, ujinga na maradhi;
n) Shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache binafsi;
o) Nchi inatawaliwa kwa kufuata misingi ya demokrasia na ujamaa

LAKINI Katiba pia ina Ibara ifuatayo:

• Masharti ya sehemu ya sura hii hayatatiliwa nguvu ya kisheria na Mahakama yoyote.
• Mahakama yoyote nchini haitakuwa na uwezo wa kuamua juu ya suala kama kutenda au kukosa kutenda jambo kwa mtu au mahakama yoyote, au kama sheria, au hukumu yoyote, inaambatana na masharti ya Sehemu hii ya Sura hii 7(2).

Angalizo: Katiba inatoa haki kwa upande mmoja na kunyima haki kwa upande mwingine.

Jukumu la Serikali Kuu:

a) Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi;
b) Lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi;
c) Serikali itawajibika kwa wananchi;
d) Kuiweziwezesha Serikali za Mtaa ziweze kuleta huduma, maendeleo na menejimenti ya Sera na sheria na kusimamimia au kufuatilia utendaji wa Serikali za Mitaa; matumizi na ukaguzi wa fedha na kutoa misaada ya kutosha.

Jukumu la Serikali za Mitaa:

Kuwezesha ushiriki wa watu katika maaamuzi ya mambo yanayowahusu katika maisha yao, kupanga na kutekeleza mipango yao ya maendeleo na kujihusisha na vikundi vya kiraia.

Maelekezo hayo yanatoa uhakikisho wa maendeleo endelevu.Ni jukumu la Wanataaluma kufuatilia.

Haki ya kuwa na mali na maendeleo:

Azimio la Haki za Maendeleo (General Assembly Resolution 41/120 1986 ):

a) Kuwa na mamlaka kamili juu ya rasilimali za asili; kujihakiki; kushiriki katika maendeleo; usawa wa kupata fursa; kuwepo kwa mazingira ya upendeleo katika kufurahia haki za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni.
b) Kwamba kuwe na haki ya Kumiliki inasaidia kufahamu mahusiano ya haki, wajibu; majukumu na kutambuliwa katika jamii.
c) Kwamba kuwe na msingi wa watu kutambuliwa kisheria, kuwa na haki ya kupiga kura na kupata huduma za msingi kama umeme, maji nk.
d) Kwamba kuwe na mfumo kamilifu unaofanya kazi wa haki ya umiliki utakaohakikisha mali inaweza kuhamishwa kutoka kwa mtu moja hadi mwingine na unaoweza kusaidia watu kupata mikopo ya kuanzisha biashara au kununua nyumba nk..
e) Walio masikini lazima walindwe na sheria ili waweze kumiliki, kutumia na kuuza mali zao pindi waonapo inafaa.

Haki za ujumla za Binadamu

• Haki katika maendeleo ya uchumi; siasa; jamii na utamaduni itakayokuwa endelevu na ambayo itatoa haki ya mgawanyo wa haki wa maslahi ya mtu na watu katika jamii inayo ruhusu upatikanaji wa haki za binadamu.
• Haki katika mazingira ya kimataifa ambamo haki ya maendeleo na haki zingine zinaweza kupatikana.
• Haki ya kushiriki kikamilifu na kwa usawa katika mipango na maamuzi ya maendeleo na ya kimazingira na kuweka sera zote zinathiri jamii na hali ya maisha katika ngazi ya anapoishi, taifa na kimataifa.
• Haki ya kupata mafanikio ya maendeleo ya kisayansi.
• Haki ya usawa wa fursa na uhuru kutoka katika ubaguzi wa kijinsia, rangi, dini au hali yoyote.
• Haki ya hali ya maisha inayojitosheleza ikiwepo chakula salama, maji na malazi.
• Haki ya kufanya kazi na kupata ujira ambao utatosheleza kiwango cha maisha ya kawaida.
• Haki ya mazingira salama ya kazi ikiwepo usalama wa wanawake wajawazito.
• Haki ya kupata kwa usawa kwa watu wote rasilimali za uzalishaji zikiwemo ardhi, mikopo na teknolojia.
• Haki ya mazingira salama na ya afya
• Haki ya kufukia kiwango cha juu cha hali ya afya.
• Haki ya mtoto kuishi katika mazingira yanayofaa kwa ajili ya maendeleo ya kimwili na kiakili.
• Haki ya kupata elimu na habari ikiwemo elimu ya uzazi.
• Haki ya usawa kati ya wanaume na wanawake yakiwemo mambo yote yanayohusiana na uzazi na usawa wa ushiriki katika familia.
• Haki ya Amani.
• Haki ya kila mtu na watu kutambuliwa ikiwa ni pamoja na haki ya kuchagua kwa uhuru hali zao za kisiasa, kujiendeleza kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na kuwa na mamlaka kamili juu ya mali na rasilimali zao.

Misimamo ya Serikali

Imekuwa ni kawaida kwa serikali mbalimbali kukata kupitisha sheria zinazotambua haki hizi kwa woga kuwa serikali itajiingiza katika majukumu yasiyotekelezeka. Hata hivyo inapaswa ziwekwe sheria zitakazosaidia kuwekwa kwa mchakato wa upatikanaji wa haki hizi.

Nchini Tanzania

Katiba ina vifungu vifuatavyo:

• 24.-(1) Bila ya kuathiri masharti ya sheria za nchi zinazohusika, kila mtu anayo haki ya kumiliki mali, na haki ya hifadhi kwa mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria.

• (2) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (1), ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang'anywa mali yake kwa madhumuni ya kuitaifisha au madhumuni mengineyo bila ya idhini ya sheria ambayo inaweka masharti ya kutoa fidia inayostahili.

Angalizo: Kwa sasa Watanzania wanamiliki ardhi Tanzania kwa miaka kadhaa huku mmiliki wa kudumu akibaki kuwa Serikali.

Ufumbuzi wa Kisheria wa Kupata Maendeleo

• Mfumo wa kisheria unayo nafasi muhimu wa kusaidia kuondoa umasikini kwa kuwasaidia watu masikini wapate haki na unafuu. Sheria lazima ilinde mali za masikini na waliokatika mazingira hatarishi. Sheria zinazobagua au kutotambua haki na maisha ya masikini zinaweza kuweka vipingamizi katika kuondoa umasikini.

• Kubadilisha sheria katika makaratasi haitoshi wala haimaanishi itabadilisha hali halisi. Watu masikini pia wanahitaji sheria na mfumo wa mahakama ambao utawezesha sheria z ifanye kazi kwa masikini. Hatua za kuboresha upatikanaji wa haki ulenge katika kuleta njia za upatikanaji haki kwa gharama kidogo zikiwepo huduma za msaada wa kisheria.

Angalizo: Wanataaluma wanapaswa kutoa msaada wa kisheria kwa wajasiriamali wadogo kufanikisha maendeleo yao.

Vikwazo katika kuleta maendeleo kwa kutumia sheria zilizopo:
• Kukosekana kwa elimu na ufahamu wa sheria.
• Ufisadi
• Ushiriki mdogo katika mchakato wa demokrasia katika ngazi ya chini, taifa na kimataifa na katika maaeneo yote muhimu kwa maendeleo ya kweli.
• Ukosefu wa ushirikishwaji katika michakato ya serikali kama inavyotakiwa na sheria. Mfano: Kilimo kwanza: Ni wazo la nani? Wananchi au Serikali au Wafanyabiashara? Kwa kiwango gani kulikuwa na ushirikishwaji wa Wananchi katika kupanga mikakati hadi kuanza utekelezaji?
• Mgawanyo usio wa haki wa nguvu za kiuchumi na kisiasa katika sekta zote za jamii na za kitaifa. Mfano: Umiliki halisi au udhibiti wa rasilimali za uzalishaji mali kama ardhi, mitaji na teknolojia.
• Uwajibikaji wa vyombo vya maamuzi, na mgawanyo wa kutoa maamuzi.
• Upatikanaji wa taarifa kwa uma kwa wakati unaofaa na kwa watu husika.
• Na majibu ya maoni ya wananchi kutoka kwa watoa maamuzi.
• Namna yeyote ya uvurugaji wa uchaguzi ni kumyima mwananchi haki ya maendeleo.
• Ukosefu wa maandalizi mazuri na elimu ya kutosha ya uraia na ya upigaji wa kura.
• Kukataliwa kwa watu binafsi kugombea katika chaguzi mbalimbali kama wagombea binafsi.
• Mazoea ya asili na kuwepo kwa sheria amabazo zinazuia maendeleo ya wanawake na kusababisha matatizo yanayoambatana na mambo ya jinsia.

Angalizo: Wanataaluma wanatakiwa wanaelimishe jamii

• Kuendelea kuwepo kwa sheria za dini ambazo zinabagua na kudhalilisha wanawake na wakati mwingine kuvunja katiba. Mfano moja ni tamko la sheria za jadi la mwaka 1963.
• Hali ya mapungufu ya wanawake wa vijijini ambao ni sehemu kubwa ya idadi ya wanawake wa vijijini na hata wafanyakazi wa vijijini.
• Sheria za jadi na za kidini zinatumika na kukubalika zaidi vijijini mara nyingi zinazuia wanawake wasirithi wala kuwa na ardhi na mali.
• Kukosekana kwa miundombinu au miundombinu mibaya
• kukosekana kwa fursa za maendeleo
• Kukosekana kwa majumuiko ya kijamii.

Kukosekana kwa uelewa wa michakato ya kisheria na kisiasa.

Hatua tano za kuleta mageuzi:

1. Tamko la wazi la sera juu ya mabadiliko ambayo itaungwa mkono na uongozi wa juu wa serikali (Baraza la Mawaziri)
2. Utaratibu wa kuwezesha mabadiliko (Mswada, Sheria)
3. Sheria ndogo ndogo za kusaidia mabadiliko (Waziri)
4. Taarifa za mabadiliko (Waziri)
5. Kuanzishwa kwa mfumo wa utawala unaoendana na sheria mpya (Serikali kuu na ya mtaa)

Sababu za Kudai Mageuzi:

a) Mfumo mbovu wa uendeshaji wa serikali za mitaa: Ni wapi serikali za mitaa zinawajibika?
b) Majukumu ya maofisa wa kuteuliwa wa serikali: Wanawajibika kwa nani?
c) Je ni sawa kwa Rais kuteua maofisa katika serikali za mtaa?
d) Je mabadiliko ya msingi yanawezekana au ufanyike mgawanyo wa madaraka kwenda mikoani.

Majukumu ya Kisheria: Haki na Wajibu katika Katiba:

26.-(1) Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii Katiba hii na sheria za Jamhuri ya Muungano.
(2) Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria
kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za nchi.

Wajibu:
(3) Mtu yeyote hatakuwa na haki ya kutia sahihi kwenye mkataba wa kukubali kushindwa vita na kulitoa taifa kwa mshindi, wala kuridhia au kutambua kitendo cha uvamizi au mgawanyiko wa Jamhuri ya Muungano au wa sehemu yoyote ya ardhi ya eneo la taifa na, bila ya kuathiri Katiba hii na sheria zilizowekwa, hakuna mtu atakayekuwa na haki ya kuwazuia raia wa Jamhuri ya Muungano kupigana vita dhidi ya adui yeyote anayeshambulia nchi.

Rais wa Nchi:
46.-(1) Wakati wote Rais atakapokuwa bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii,
itakuwa ni marufuku kumshitaki au kuendesha mashataka ya aina yoyote juu yake mahakamani kwa ajili ya kosa lolote la jinai.

46A.-
(1) Bila ya kujali masharti ya ibara ya 46 ya Katiba hii, Bunge linaweza kupitisha azimio la kumuondoa Rais madarakani endapo itatolewa hoja ya kumshtaki Rais na ikapitishwa kwa mujibu wa masharti ya ibara hii.
(2) Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya ibara hii, hoja yoyote ya kumshtaki Rais haitatolewa isipokuwa tu kama inadaiwa kwamba Rais-
(a) Ametenda vitendo ambavyo kwa jumla vinaivunja Katiba au Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma;
(b) Ametenda vitendo ambavyo vinakiuka maadili yanayohusu uandikishwaji wa vyama vya siasa yaliyotajwa katika ibara ya 20(2) ya Katiba, au
(c) Amekuwa na mwenendo unaodhalilisha kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano, na haitatolewa hoja ya namna hiyo ndani ya miezi kumi na miwili tangu hoja kama hiyo ilipotolewa na ikakataliwa na Bunge.

Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma

132.-(1) Kutakuwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo itakuwa na mamlaka ya kuchunguza tabia na mwenendo wa kiongozi wa umma yeyote kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba masharti ya sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma yanazingatiwa ipasavyo.

Public Leadership Code of Ethics Act [CAP 398]

Kutokana na mambo yote yaliyojitokeza ya Kikatiba Kongamano limekubaliana na Kuazimia mikakati ifuatayo ifanywe kwa kutumia sheria zilizopo huku TPN ikiwa kama mwamvuli wa vyama vyote vya kitaaluma na visivyo vya kiserikali vitakavyokubali kujiunga na TPN kama jukwaa la kuyafanyia kazi.

1) Kupitia katika harakati na mikakati mbalimbali tunahitaji kuwa na uwezo na haki ya Uwezeshaji:

• Uwezo wa kushiriki katika michakato ya maendeleo
• Uwezo wa kubadili maamuzi ya umma
• Uwezo wa kushiriki katika kutoa maamuzi
• Uwezo wa kuelezea masuala mbalimbali katika mijadala ya umma
• Uwezo wa kujadili na kukubaliana juu ya thamani na riba
• Uwezo wa kubadili mila na tamaduni

2) Wanataaluma lazima washiriki na kuhakikisha kuwa sheria zilizopo zinaendana na na mahitaji ya jamii na matarajio yao. Wasinyamaze tu.

3) Kushirikiana na wadau husika kuhakikisha kuwa Sheria ni lazima ziwekwe kufanya mifumo ya taasisi na ya utendaji iwatoe watu katika umasikini. Mifumo hii iliwasaidia Wakoloni; Sasa inabidi tuwekeze rasilimali katika kuondoa mambo yote ya Kikoloni.

4) Kushirikiana na wadau husika kuhakikisha kuwa Sheria za urithi na kupeana zibadilishwe ili kuwahakikishia makundi hatarishi kama wanawake wa vijijini, haki yao ya kurithi na kumiliki ardhi na mali.

5) Kushirikiana na wadau husika kuhakikisha kuwa Sheria iweke wazi ulazima wa kutoa elimu ya uraia na wajibu na haki ya kiraia. Hatua za makusudi zichukuliwe kuondoa mila potofu na za kibaguzi.

6) Kushirikiana na wadau husika kuhakikisha kuwa Wananchi wanapewe fursa zaidi ya kushiriki katika kuzipitia sheria

7) TPN ihakikishe kuwa inakuwa au kushirikiana na kitengo maalumu au wadau wengine Kupigania mabadiliko haya kwa niaba ya jamii.

8) Asasi zisizo za Kiserikali lazima zijihusishe sana na ikiwezekana kuunganisha nguvu katika kuendesha program za elimu ya kiraia; Kampeni za Kudai mabadiliko; Kujihusisha katika kutunga sera na sheria na katika Mikakati ya kufungua madai yanayolenga kuleta mabadiliko.

9) Majukwaa mapya ya harakati za kuleta mabadiliko yaanzishwe. Sheria ya sasa inaruhusu na Serikali imetoa fursa kubwa ya uhuru wa kujumuika.

10) Harakati za mabadiliko na ufahamu lazima ziongezwe kwa wadau ili waweze kuwajibika na kufanya maamuzi sahihi.

Maazimio: Ni Mikakati Gani Watumie Wanataaluma Kupeana Habari na Taarifa Za Uhakika na kwa Muda Muafaka

1) TPN iangalie namna bora ya kuwasiliana na kuwapa changamoto watanzania juu ya mitazamo yao katika jamii, na kuwafanya wafikiri na kufanya mambo kimkakati huku wakilenga maendeleo yao wenyewe kwa kujitegemea bila kungoja kusaidiwa. Swala la umasikini na jinsi ya kuuondoa iwe ni jukumu la klila mmoja. TPN iwe mstari wa mbele kuwaelimisha wanajamii juu ya kutumia rasilmali zilizopo katika miradi mbalimbali ya uzalishaji.
2) Habari na mawasiliano vikitumika sawasawa vitatuondoa katika umasikini, kuuondoa mfumo au sheria mbovu kwa sababu ufahamu na taarifa vinawapa nguvu wananchi ya kuiuliza maswali serikali na kuishinikiza kuleta mageuzi ama kuzingatia uboreshaji wa haki za jamii.
3) Watanzania wanawajibika kushirikiana katika kupeana taarifa muhimu ambazo zitawasaidia kufanya maamuzi muhimu katika maisha yao.
4) Teknolojia ya Kujumuika “Mtandao” – Wanataaluma wote ni vema tujumuike kwa njia ya Mtandao na mifumo mingine ili kuongelea na kujadili mambo Muhimu ya kitaifa kuelekea katika mabadiliko yanayotakiwa.
5) Kuhakikisha kuwa tunazo taarifa katika database kuhusiana na mambo Muhimu.
6) Ubuniwe mfumo wa kupeana taarifa katika ngazi zote ili kuwafikia walengwa waliowengi kwa kutumia vyombo vya Habari kama Radio, Runinga, Simu, barua pepe, tovuti, magazeti, semina nk. Mabadiliko yaanze na Wanataaluma ambao wao wenyewe wanatakiwa wabebe ujumbe wa mabadiliko pia kwa vitendo.
7) Kutoa changamoto kwa vyombo vya Habari ili viwe vinatoa Habari ambazo ni Muhimu kwa wananchi na umma kwa ujumla.
8) Kuwa na taarifa ya mitandao mingine ambayo itasaidia kupatikana kwa Habari na taarifa Muhimu.

Sayansi na Teknolojia

1. Wanataaluma watilie mkazo na kutambua kuwa Sayansi, Teknolojia na Utafiti vinaweza kutupatia taarifa Muhimu kwa ajili ya mipango ya kimaendeleo na hivyo kufanikisha ndoto ya kuwa na “jamii yenye uchumi wa maarifa” “Knowledge Based Economy”.
2. Suala zima la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA) liwekewe mikakati ya kusambazwa nchi nzima. Pia wadau wote wahamasishwe kuwekeza katika sekta ya TEKNOHAMA na kuifanya Tanzania kuendana na utandawazi wa TEKNOHAMA kwa maendeleo ya nchi.

Elimu na mafunzo

1) Kila juhudi zifanywe kwa kiwango cha juu kabisa kutoa Mafunzo Stadi “Vocational training” kwa wale ambao wana elimu ya chini kabisa katika mchakato wa kujenga uwezo wa taifa wa rasilimali watu.
2) Mfumo wa Elimu tulionao hauwasaidii wanafunzi kuwa wabunifu na kufikiri nje ya mfumo wa sasa. Ni vema mfumo unagaliwe upya kukidhi mahitaji ya sasa ya taifa.
3) Vyuo vyetu vikuu mara nyingi vinatoa shahada za ujumla mfano: Computer Science, Public Administration n.k. Hata hivyo wanapohitimu na kuja katika soko la ajira au biashara wanajikuta wanatakiwa kufanya kazi ambazo siyo za ujumla kama walivyojifunza. Ni vema wadau wakaandaa mafunzo ya kistadi na kifani ili kuwawezesha kumudu kazi zao.
4) Wanataaluma wajitolee kuwa wakufunzi na waalimu wa kizazi kinachokuja katika mabadiliko ya nchi.
5) Kuangalia ni jinsi gani tunaweza kutumia maarifa yaliyopo kutoka kwenye vyuo vikuu yaweze kutumika kwa vitendo katika maisha halisi
6) TPN iitishe tafiti Muhimu za Madaktari wa Falfasa (PHd’s ) ambazo ni Muhimu kwa maendeleo ya nchi na kuona ni jinsi gani zinaweza kusaidia badala ya tafiti kama hizi kuishia katika makaratasi tu.
7) Moja ya tatizo kubwa la wahitimu wengi kutoka shuleni na vyuoni ni mawasiliano na hasa kuelezea kile wanachokijua. Hii inatokana kukosekana kwamasomo yanayohusisha ujuzi wa kuwasiliana “communication skills”. Somo hili ni vizuri likiangaliwa upya pamoja na masomo mengine ili yaendane na mahitaji ya hali halisi mara wamalizapo masomo.

Kampeni na bidhaa za ndani

1) TPN ianzishe kampeni za kulinda haki ya mlazi “consumer protection” baada ya kupata taarifa za uhakika ni bidhaa gani au kitu gani kibaya na kwa nini kisitumiwe na ni kipi kinafaa hasa kwa manufaa ya watumiaji na maendeleo ya nchi.

Kukuza Mtandao na Kurejesha Uzalendo

1) TPN ipanue Mtandao wake ufike katika kila manispaa kwa kuanzia na ifanye kila linalowezekana kushirikiana na vyama vingine vya kitaaluma na visivyo vya kiserikali.
2) TPN inahitaji kuwafiikia wanataaluma wengi na kupata mawazo yao ya kimaendeleo na kuyaunganisha na yale ya wasio wanataaluma kwa ajili ya kufanyiwa kazi na wadau wote huku kukiwa na mikakati yake ya utekelezaji.
3) TPN isimamie baadhi ya watu na agenda mbalimbali muhimu za kijamii kama kunyimwa haki za msingi, machafuko ya hali ya hewa na mazingira; wananchi kufa kutokana na kunyimwa haki mbalimbali, nk.
4) TPN inahitajika kukaa pamoja na kuunda kamati mbalimbali ili kukabiliana na matatizo yote ya kitaifa yanayooneka ikiwa ni pamoja na kuyafanyia kazi.
5) TPN, Wanataaluma na Watanzania kwa ujumla yatupasa kutafuta utambulisho wetu kama taifa na kuangalia ni nini kitakachotutambulisha.
6) TPN iendelee kuandaa kongamano kama hili na lifanyike kila mwaka ili tuweze kukua na kuleta mabadiliko makubwa zaidi.
7) TPN ibuni mkakati wa kutafuta fedha za kuendesha shughuli mbalimbali ambao utajiendesha wenyewe na utakookuwa endelevu.
8) Wanataaluma walio katika Mtando wa TPN wasaidiane katika kukuza taaluma zao na katika biashara na kufanikisha malengo mbalimbali.

2 comments:

Anonymous said...

Damn chemi
This is too long for an article.why dont you just write a piece and then kama mtu anataka kuendelea kusoma unaweka kitu kama "more".Mbona yule jamaa wa bongocelebrity.com yeye anafanya hivyo?

Anonymous said...

This has taken the whooooole blog space!! Too much blah blah take the previous advice Sis.