Thursday, January 01, 2015

Kwa Nini Levina Alijiua ? The Case of Levina Mukasa - UDSM

Wadau niliandika habari hii nikiwa mwandishi wa habari Daily News mwaka 1991.  Kesi hii ilikuwa chanzo cha ile Movement ya Kumpambana na Unyanyasaji wa Kijinsia wa Akina Mama Tanzania (Sexual Harassment).  TAMWA iliongoza movement hiyo. Nasikia mmoja waliyomnyanyasa Levina, Omari Saloti ni marehemu. Sijui huyo Mark Victgor yuko wapi, lakini ana damu mikononi mwake.

******************************************************************************
The Late Levina Mukasa
Na Chemi Che-Mponda

 Tarehe kama ya leo mwaka 1990 wakati mwanafunzi wa kike wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alipojiua, watu wengi walifikiri kuwa alifanya hivyo kwa sababu alikuwa na matatizo kwao na kuwa masomo yalikuwa yanamshinda. Hata hivyo, waliposikia kwamba alifanya hivyo kutokana na unyanyawaji wa kijinsia uliofanywa na wanafunzi wawili wa Kitivo cha Uhandisi pamoja na kikundi kilichojukana kama “Punch”, baadhi walikasirika wakati wengine walicheka tu.

Marehemu Levina Mukasa, alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza aliyekuwa akisomea shahada ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kulingana na maelezo ya waliokuwa wakimfahamu wanasema alikuwa mkimya mwenye msaada na ambaye wakati wote alikuwa tayari kutumia vitu vyake na wenzake. Kila aliposoma wakati wote alishika nafasi ya juu darasani.

Mnamo tarehe 7 Februari 1990, Levina alikatisha maisha yake kwa kumeza vidonge vingi vya klorokwini (vinavyotumika kutibu Malaria). Swali linabaki, “kwa nini alifanya hivyo?” Karibu kila mwanafunzi wa kike aliyesoma katika kampasi kuu ya Chuo Kikuu (inayojulikana sana kama Mlimani) atakuwa amenyanyaswa kijinsia katika kipindi cha Miongo miwili iliyopita. Wamekuwa wakidhihakiwa, kutishiwa kijinsia au kuvamiwa papo kwa hapo na kubakwa.

PUNCH

Pamoja na hayo lipo kundi la kisirisiri hapo mlimani linajukana sana kama PUNCH, linafikia hata kiwango cha kuchapisha maandishi na michoro michafu kuhusu habari za kimapenzi za sasa au za zamani za Mhasirika wao. Madhumuni hasa ya PUNCH ni kuwaweka wanawake chini ya wanaume, kuwafanya wanafunzi bora wa kike washindwe masomo yao na hata kulazimika kukatisha masomo. Inatumiwa pia kuwatishia wasichana wakubali kufanya mapenzi na watu wanaowataka ambao wako katika kundi la PUNCH. Kumkataa mtu aliyeko kwenye kundi la PUNCH kunamfanya mhusika“apanchiwe”.

Bahati mbaya, wanawake walio katika kampasi wanaiogopa PUNCH. Wanafungwa na sheria zake kama vile kutokunywa chai ya saa 10.00 katika mgahawa, kutokukaa kwenye high table, kutokuvaa khanga Mgahawani n.k. Wengine wanafurahia hata kumwona mwanamke mwenzao akipanchiwa. Kutokana na maelezo ya shangazi wa marehemu, Dkt. V.K. Masanja, ambaye ni mhadhiri wa hapo Mlimani, matatizo ya Levina yalianza wakati wa dansi ya kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza iliyofanyika kwenye hoteli ya Silversands ambapo alikataa kwenda na mwanafunzi wa mwaka wa nne wa Kitivo cha Uhandisi aitwaye Mark Victor.

FUJO

Levina alienda dansi hiyo na rafiki zake. Victor alipomuona alimtaka warejee pamoja na akalalamika kwa nini alidhubutu kwenda kwenye dansi na watu wengine wakati alikataa kwenda naye. Levina alikataa kuondoka naye na Victor akamvuta gauni, rafiki zake walijaribu kumtetea na papo hapo ugomvi ukaanza. Baadhi ya marafiki wa Victor wanaojita “Engineers” [Wahandisi] [kundi linalofahamika sana kati ya wanafunzi] walimsaidia Victor. Kundi jingine lijulikanalokama “insiders” walimsaidia Levina. Hatimae, baada ya kushindwa Wahandisi waliondoka kwenye dansi, lakini huo haukuwa mwisho wa matatizo ya Levina.

Waliporejea kwenye dansi mgogoro mwingine ulizuka kati ya Victor na kundi lake na Levina na rafiki zake. Walipofika kwenye mabweni yao, Victor alikuwa akimsubiri ndipo ikawa usiku mzima kutupiana matusi. Asubuhi na mapema Levina alipeleka malalamiko MUWATA [Serikali ya wanafunzi] uongozi ambao ulisulihisha tatizo hilo. Victor aliomba radhi na akadai kuwa alikuwa amelewa.

Siku iliyofuatia, tukio la Silversands lilipanchiwa. Michoro ya Punch haikumwonyesha jina lake lakini kwa kutoa namba yake yakusajiliwa ilidhihirisha kuwa michoro inayofuatia angekuwemo. Baadhi ya wanafunzi wa kiume walimwendea Levina na kumwambia kuwa walikuwa kwenye kundi la PUNCH. Walimtishia kumpanchi iwapo angekataa kufanya nao mapenzi. Aliwakatalia na akakosa raha sana. Mmojawapo wa wanafunzi hawa alikuwa Omari Saloti, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Uhandisi.

Dkt. Masanja alisema kuwa yeye (Levina) ndiye alimweleza yaliyotokea. Dkt. Masanja alisema kuwa alimweleza Levina kuhusu uzoefu wake na mambo ya PUNCH alipokuwa mwanafunzi na jinsi alivyoweza kuyapuuza. Alisema kuwa Levina alionyesha kupata ujasiri na akafikiria kuwa mambo yamekwisha. Marafiki wa Levina waliambiwa kuwa wangepanchiwa iwapo wangeonekana wakiandamana naye. Alitengwa. Maelezo machafu yalitolewa na maandishi yaliandikwa dhidi ya jina lake katika kila orodha ya majina ambamo majina yake yalikuwemo.

Usiku wa tarehe 3 Februari mwaka huu kiasi cha saa 7.30 wakati Levina alipokuwa kitandani akijisomea alisikia mlango ukigongwa. Kabla hajajibu, mlango ulifunguliwa na Omari Saloti aliingia kwa nguvu chumbani. Walipigana. Levina alimng’ata mkono naye alimpiga ngumi za mashavuni na kwenye matiti. Levina alikimbia akiwa amevaa gauni ya kulalia tu na akajificha kwenye kichaka kilichoko nje ya bweni wakati Saloti akiwa bado anamnyemelea. Aligonga nyumbani kwa mlinzi, ambaye alimsindikiza hadi chumbani kwake na akasubiri kwa muda nje.

Madhumuni hasa ya PUNCH ni kuwadhalilisha wanawake

Inasemekana kuwa Saloti alitaka kumbaka, wakati wengine wanasema alimbaka. Wanasema Levina alikataa tu kusema. Hata hivyo Saloti alikuwa amemtishia Levina kuwa angembaka na kumwibia vitu vyake. Asubuhi iliyofuatia, mlinzi alisema kuwa alizungumza na saloti na akasema alikuwa “Amelewa” wakati huo. Levina pia aliwona meneja wa bweni, ambaye alizungumza na Saloti. Alisema kuwa Saloti alimwambia kuwa alifunguliwa mlango na Modesta mwenzake Levina ambaye walikuwa wakiishi naye chumba kimoja. Modesta, alikanusha madai hayo kwani yeye ameoloewa na kila mwisho wa juma huwa nyumbani na familia yake.

Dkt. Masanja alisema alimpa barua Levina na kumwelekeza kwa Mshauri wa wanafunzi, Dkt. Biswalo ambaye alikuwa akienda kwenye Mkutano wa Baraza hivyo naye alimelekeza kwa Mama Rajabu. Waliitisha jalada la Meneja wa bweni/Mlinzi lakini halikuwa na chochote. Levina alifariki jioni ya tarehe 7, Februari 1990. Inaonekana kuwa kundi la Punch ni mabingwa wa vita vya kisaikolojia na wamefanikiwa lengo lao kinyume cha matarajio yao kwa kumkatisha tamaa Levina mpaka akaona kuwa maisha yake hayana maana tena. Zaidi ya hayo utu wake ulikuwa umedhalilishwa na jitihada za Saloti za kutaka kumbaka [Maana katika jamii ya Kitanzania inaaminika kuwa mwanamke akibakwa amependa mwenyewe].

Kutokana na Punch kuwalazimisha marafiki wa Levina wamtenge, kumdhihaki mbele ya kadamnasi, kumdhalilisha na kumuonea, kutokana na malalamiko yake kutoshughulikiwa na MUWATA kwa kumwambia kuwa hakuna awezaye kushindana na Punch, wakati wengine walikuwa wakimcheka tuu anavyolalamika na rafiki zake wakimuepuka, yote haya yamemfanya alazimike kukata maisha yake kwani aliamini jamii nzima ilikuwa dhidi yake.

Punch ilifanikiwa kuondoa umoja kati ya wanawake. Saloti alifanikiwa kumkosanisha Levina na Modesta, mtu pekee ambaye ndiye alikuwa akimwamini, kwa kudai kuwa yeye ndiye alimpa ufunguo. Ukweli ni kwamba funguo zote za Hall 7 [alimokuwa akiishi Levina] ziliweza kufungua angalau milango mitano, wakati katika Hall 3 bweni lingine la wanawake ufunguo mmoja unafungua milango yote ya gorofa hiyo. Walimfuatafuata na kumgongea mlango usiku wa manane, walimtupia maneno machafu na kumtishia mlangoni pake, walifanya aonekane kama ‘mwenda wazimu’ na asiyefaa.

Mkutano wa dharura wa wanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu, wahadhiri, wafanyakazi na wakazi wengine kwenye kampasi uliotishwa tarehe 9 Februari ulikubaliana kuwa wanawake walilaumu uongozi kwa kukataa kuchukua hatua za kinidhamu wakati mambo kama hayo yalipotokea. Wanasema iliendelea hivyo hadi kufikia hatua ya kuwakatisha tamaa wahasirika wasichukue hatua za kisherina kushindwa kutoa ushauri unaofaa kwa wanafunzi.

Levina Shujaa

Walisema kuwa Serikali ya wanafunzi [MUWATA] imekuwa kimya ikiangalia tu na mara nyingine ilishirikiana na waovu hao. Walisema kuwa wanafunzi wa kike ambao walijaribu kupata msaada kutoka MUWATA walijikuta katika matatizo makubwa zaidi, maana walihubiriwa kuhusu ukubwa na uwezo wa Punch.

Zaidi ya hayo wakina mama walisema kuwa jumuiya ya wanafunzi wanaichukulia Michoro ya matusi ya Punch kama burudani muhimu na wanafunzi wanaonewa wametumbukia kutokana na mgawanyo na mbinu za utawala za Punch, wakati wasomi na uongozi wamekaa kimya wakihofia visasi kutoka kwa Punch ambayo ilikuwa, inatikisa jamii nzima. Wakina mama walikubiana kuwa, Levina “asipotee hivi hivi, sisi tumtangaze shujaa ambaye hatimae ameikomesha Punch”.

Hata hivyo wanaume wanaposikia haya wanacheka. Wanauliza, “kwa nini mmuite Levina shujaa? Alikuwa malaya! Alikula pesa za watu! Mlitaka ale tu halafu asilipe? Kwani yeye ni wa kwanza kujiua! Ni m.p.u.m.b.a.v.u. Alikuwa mdhaifu. Alikuwa mjamzito! Unyanyaswaji wa kijinsia ni jambo la kawaida, wanawake pia wanayanyasa kijinsia. Mwanafunzi mmoja alirukwa na akili kwa sababu alikataliwa na msichana.” hayo ni baadhi ya maelezo yanayotolewa na wanaume wetu ndani na je ya kampasi.

Hati zenye kuonyesha uso wa levina zilikuwa zimebandikwa fuvu la Punch. Aliyekuwa Waziri wa nchi asiye na Wizara Maalum, Mheshimiwa Getrude Mongella, alipozungumza kwenye mgahawa baada ya kunywa chai katika ‘high table’ alilaani unyanywasaji wa kijinsia huko Mlimani na kusema ni sawa na kitu kilichokuwa kinachemka na sasa kimepasuka baada yua kufikia kikomo. Mapambano ndiyo kwanza yameanza. Walakini mapambano hayo lazima yaenezwe katika asasi kwanza yameanza. Walakini mapambano hayo lazima yaenezwe katika asasi zote za elimu ya juu na sehemu za kazi. Lazima kuwepo na mapambano ya kitaifa dhidi ya uovu huu!

Makala hii iliandikwa na Chemi Che-Mponda.

6 comments:

X B.A. Education UDSM said...

Ooh ! So sad ! Sipendi hata kukumbuka! Siku ya tukio nilitoka na girlfriend wangu (hakuwa mwanafunzi) kwenda kupata chakula cha jioni pale Savei. Tukiwa tunakula, Levina aliingia pale hotelini akaenda moja kwa moja kwenye bomba la maji. Alichukua glass akateka maji bombani. Sikumjali. Mimi na mpenzi wangu tuliendelea na chakula huku tukizungumza, ilikuwa majira ya saa 12 hivi jioni.

Baada ya kama dk 5 hivi niligeuka nikamuona Levina akifungua karatasi ya gazeti iliyofungwa akatoa vidonge na kumeza, akafungua nyingine akafanya hivyo hivyo na nyingine tena. Nilipoconcentrate kumuangalia, yule gf wangu alinigeuza kichwa na kuniuliza kulikoni namwangalia yule dada hivyo. Nikamwambia kuwa tulikuwa tunasoma naye na nilikuwa nashangaa kwa nini anameza vidonge vingi namna ile. Kisha nikatania, isije ikawa anataka kujiua maana nyie wanawake amkawii !!!

Levina alimaliza kumeza dawa, akatoka nje. Alikuwa amevaa khanga na kandambili huku nywele zake nyingi nyeusi zikiwa hazijachanwa vizuri. Jambo hili lilinishangaza kidogo maana Mzee Punch alikuwa haruhusu wanawake kuvaa mvao ule na kwenda mbali na mabweni yao.

Tulimaliza kula, nikarudi chuo nikaenda kujisomea baadaye nikalala. Asubuhi nakwenda cafeteria nakuta wanafunzi wamesimama makundi makundi kuuliza kulikoni naambiwa Levina amefariki kwa kumeza vidonge vingi vya Chloroquine. Nilipata mshituko ambao ulinifanya nikose raha hadi namaliza chuo kwani niliona sikuwa responsible enough kiasi cha kumfuata pale alipokuwa anameza dawa na kumuliza pengine angebadilisha uamuzi wake.

Hata hivyo, pengine ningekuwa peke yangu ningeweza kumfuata lakini kwa vile nilikuwa na gf wangu, kumfuata mwanamke mwingine tukiwa naye ingeweza kuwa issue labda kama ningekuwa na uhakika wa alichokuwa anakifanya Levina.

R.I.P Levina Mukasa, X B.A Ed class UDSM !!!

Anonymous said...

Miaka ya mwishoni mwa 80 na mwanzoni mwa 90 karibu taasisi nyingi za elimu zilikuwa na makundi kama haya.

Wanafunzi wengi haswa wa kiume walikuwa na makundi ya siri au yanayojulikana na lengo kubwa la makundi haya ilikuwa ni kufanya tu vitendo vya kihuni na haswa kwa wasichana au wanawake.

Wengi wanaweza wakawa wanaikumbuka Tambaza(WU-TAMBA CLAN) ya wakati huo kabla wanafunzi wake hawajasambazwa mashule mengine na O-Level kuvunjwa rasmi.

Shule kama Ilboru ilikuwa na makundi ya wanafunzi wavuta bangi ambao walijitenga na kuishi katika bweni moja kiasi kwamba mwanafunzi mgeni ukiingia huko ni kama umepelekwa gereza la Sona na kukutana na kina Theodore Bagwell (T-Bag).

Anonymous said...

Namkumbuka sana huyu dada yangu, Levina Mukasa. Alikuwa Mtanzania kutoka maeneo ya Kyaka, Misenyi. Alikuwa anachukua shahada ya Ualmu. Alikuwa mtulivu sana kwa aiba na kwa matendo.

Nakumbuka siku aliyofika Getruda Mongela akahutubia akiwa amesimama juu ya HIGH TABLE, meza iliyokuwa katika cafeteria ya Manzese, na ilioyotumiwa exclusively na wanafunzi wa Engineering mwaka wa nne. Mama Mongela alisema kuwa alikuwa amekuja kuizika PUNCH.

Jioni yake Profesa Shivji aliweka mdahalo usiokuwa rasmi nje ya cafeteria ya Manzese na kupinga kauli ya Getruda na kumbeza kwamba " You can't declare resolution of what you didn't establish" Wiki iliyofuata PUNCH akatoa toleo lingine likimtukana Getruda matusi yote.

Ndipo baada ya hapo serikali ikatangaza kitita cha Sh Mil 10 kwa yeyote atakayempata mshirika yeyote wa PUNCH. Baada ya hapo ilitoka makala ndogo ya PUNCH iliyotundikwa Hall One. Kisha PUNCH ikafifia kabisa.

Anonymous said...

Huyu Levina Mukasa... ni dada yake na mtunzi mahiri wa nyimbo za kikatoliki bwana... BERNARD MUKASA

Anonymous said...

Huyu dada moja ya sababu iliyofanya ajiuwe inasemekana ni kukosa uvumilivu kulikochangiwa na kutokwenda JKT.

Wengi wanasema kama angelikwenda JKT, basi matusi ya PUNCH yasingelimtisha kabisa maana JKT, wale ma-Coplo Magwegwa, Gumo, Wawa, Wera, Manyilizu, Mandevu, Chacha, Matron Makunyanzi nk kwa kweli walikuwa wanajua kutukana na kunyanyasa.

Kuna Madada wawili sikumbuki walisoma miaka gani, ambao nasikia Mzee Punch alishindwa kabisa kuwanyoosha. Walikuwa wakiwahi kula kama Wanaume na kuvaa suruali, tabia ambayo Punch hawakuipenda. Basi wakaanza kuwashughulikia. Na wao wakaanza ukorofi wa kwenda mapema Cafeteria kuangalia wamechorwa na nguo gani, basi wanarudi chumbani na kuvaa kama walivyochorwa ili kila mtu awafahamu.

Walisumbuana na Punch hadi mwisho jamaa hawa wakakosa nguvu na kuwaacha. Walipowaacha na wao kweli ndipo wakatulia kabisa na kuacha ukorofi wao. Ila hii kama sikosei inaweza kuwa ilitokea miaka ya 70 kwa sababu zote ni story ambazo mie nilisikia na kwa bahati mbaya, sikusoma UDSM.

Halafu kweli dunia imebadilika Bandugu. Siku hizi wanafunzi wanajibandika wenyewe picha za uchi wa Mnyama na siyo za kuchorwa tena. Wengine walienda kabisa na kuanza kujieleza "nimebakwa Meen" na bila wasiwasi wowote huku TV Camera na Radio zinawarekodi. Mzee Puch angelikuwepo basi watu wangelilipa ili wawekwe pale na wajiongezee umaarufu.

Kufa kwa Punch ilikuwa ni lazima hata kama Levina asingelijiuwa. RIP LEVINA

Anonymous said...

Kwa ufupi tu, hawa akina Mark Victor na Omari Saloti wako wapi kwa sasa? Na huyo dada Modesta aliyemsaliti yuko wapi?

Ni vizuri kuwakumbuka wote hawa na upuuzi wao hata kama leo hii wana nafasi muhimu ili jamii ifahamu ushetani uliowalea.