Wednesday, November 19, 2008

Mike Sikawa wa BBC Afariki Dunia

(Mike Sikawa 1982 Dar es Salaam, Tanzania - Mike alinitumia hizi picha nikiwa denti Form Five, Tabora Girls. Mbona nilitamba nazo, kwanza zilikuwa za rangi, halafu pili alikuwa mwandishi wa habari maarufu sana hivyo kujuana naye ilikuwa fahari kweli. Miaka yote hii nimekaa nazo.)

*******************************************************************

Nimepokea habari za kusikitisha sana leo. Mwandishi wa Habari wa BBC, Mike Sikawa, amefariki dunia. Aliwahi kufanya kazi Daily News. Alikuwa na kipaji mkubwa wa kuandika habari mpaka Daily News walimpa 'special privileges'.

Nilikutana naye kwa mara ya kwanza nikiwa nasoma 'A' levels Tabora Girls. Nilikuwa likizo Dar na tuliktana kwenye party Chuo Kikuu cha DSM. Wakati huo Mike Sikawa alikuwa maarufu sana. Nilimwambia kuwa nataka kuwa mwandishi wa habari na yeye alisema kuwa huo kazi haufai mwanamke. Nikamwambia kuwa hata hivyo bado nataka kuwa mwandishi wa habari. Nilianza kazi Daily News Agosti 1984, na baada ya muda mfupi yeye alitoka na kwenda Uingereza. Nilikutana naye tena miaka ya 90 na Mike aliniambia kuwa alijua nitakuwa na mafanikio makubwa katika uandishi wa habari.

Nakumbuka huo ugonjwa wa kisukari ulianza kumsumbua wakati huo na ndo ulimaliza.

Mungu ailaze roho yake mahala pema mbinguni. Amen.

****************************************************
Kutoka Lukwangule Blog:

Mike Sikawa wa BBC afariki dunia

MTANGAZAJI wa idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Mike Sikawa (55) ,amefariki dunia jana mchana baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na ugonjwa wa kisukari.

Sikawa, ambaye pia aliwahi kufanya kazi katika Kampuni ya Tanzania Standard Newspapers (TSN) inayomiliki magazeti ya Daily News na HabariLeo, alifariki dunia juzi majira ya saa 8.47 mchana nyumbani kwake Njiro, nje kidogo ya mji wa Arusha.

Kwa mujibu wa mdogo wake marehemu, Mchungaji Charles Sikawa, ndugu yake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa muda mrefu na kutokewa na kidonda mguuni.
Mchungaji huyo alisema ndugu yake alipata matibabu katika hospitali mbalimbali hapa nchini ikiwamo AICC, KCMC, St. Thomas na Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili iliyoko Dar es Salaam lakini hakupata nafuu yoyote.

Alisema ilifika wakati nusura akatwe mguu uliokuwa na kidonda lakini madaktari walifanikiwa kukwangua nyama ya mguu wa kidonda lakini haikuweza kusaidia.
Mchungaji huyo aliendelea kusema kuwa baada ya kuhangaika kwa muda mrefu katika hospitali mbalimbali hapa nchini na kushindwa kupata nafuu, Sikawa alikuwa akipata matibabu akiwa nyumbani kwake hadi alipofikwa na mauti.

Alizaliwa King’ori wilayani Arumeru mkoani Arusha na kusoma elimu ya msingi katika eneo hilo kabla ya kufaulu na kuendelea na elimu ya sekondari katika shule ya Ilboru na Mzumbe ya mkoani Morogoro.

Katika miaka ya 1970, aliajiriwa katika kampuni ya TSN kama mwandishi wa kawaida na baadaye kujiunga na idhaa ya Kiswahili ya BBC kama mtangazaji. Ameacha mjane na watoto wawili ambao wako Amerika ya Kusini.

Mipango ya maziko inasubiri ndugu, jamaa na marafiki walioko nje ya mkoa wa Arusha na sehemu zote alizofanyia kazi.

Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro ametuma salamu za rambimbi kutokana na kifo cha mwandishi huyo na kuelezea jinsi alivyoguswa na msiba huo.

Dk. Migiro alisema alipoteuliwa kushika wadhifa huo katika UN, Sikawa alikuwa mwandishi wa kwanza kumtafuta kwa ajili ya kumhoji juu ya uteuzi huo.

Kwa habari zaidi soma:

http://dailynews.habarileo.co.tz/home/index.php?id=8536

7 comments:

Anonymous said...

R.I.P. Aisei jamaa alikuwa mwandishi mzuri kweli.

Anonymous said...

Mimi nilikuwa mfuatiliaji mkubwa sana wa BBC World Service Broadcasting from London. Namkumbuka mtangazaji Mike Sikawa. Kwakweli taaluma ya habari imepoteza mtu muhimu ktk uwanja huo wa kupashana habari.
MOLA alitoa, MOLA ametwaa. Amrehemu apumzike kwa Amani,AMEN

Anonymous said...

RIP Mike.Tumepoteza shujaa! nakumbuka ulivyoweza kusimamia ukweli, na umakini katika kazi yako.

Simon Kitururu said...

R.I.P Mike!

Anonymous said...

rip mike.
ila anti chemi na wewe una balaa,sa mjomba alisemaje au hujawahi kumuonyesha?

Anonymous said...

Da Chemi huo msiba umekugusa kweli. Pole sana.

Mungu amlaze mahala pema mbinguni. AMEN.

Anonymous said...

duuuuuuu sister chem nadhani jamaa kwa wakati huo alikuwa nanihii wako nini?maana emekuuma sana.MUNGU AMREHEMU MAREHEMU-AMEN