Friday, May 10, 2013

Polisi Kilosa Wakamatwa na Fuvu la Binadamu - Waliitumia kudai Rushwa


Kutoka Gazeti la Mtanzania!

Mei 10, 2013


JESHI la Polisi mkoani Morogoro limeingia kwenye kashfa nzito baada ya askari wake watatu na raia wanne kukamatwa wakiwa na kichwa cha binadamu. Tukio hilo lilitokea Mei 7 mwaka huu katika eneo la Mgudeni- Dumila wilayani Kilosa.

Inaelezwa kuwa polisi hao kwa kushirikiana na raia hao walikwenda nyumbani kwa mfanyabiashara Samson Mura na kutaka kumbambikizia kesi ya mauaji.

Mbali ya kubambikizia kesi hiyo, polisi hao wanadaiwa kuomba wapewe Sh milioni 25 na mfanyabiashara huyo ili wasimpeleke kituoni.

Wakizungumza na MTANZANIA jana, baadhi ya wananchi walisema wameshangazwa na askari hao ambao wawili ni wa Kituo cha Polisi Dumila na mmoja wa Kituo cha Polisi Mvomero.

Walisema siku ya tukio, polisi hao walifuatana na raia mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa kwa ajili ya masuala ya usalama.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mgudeni,Zaituni Kifutu alisema walishangazwa na tukio hilo.

“Tumeshangazwa mno na askari hawa… sijui walichukulia wapi mafunzo yao? Kama walibaini kuwapo tukio hili kwa nini hawakutaka kulifikisha kituoni?

“Inasikitisha mno, eti wao kwa kushirikiana na mfanyabiashara wanakwenda kudai kwa mwanakijiji mwenzetu wapewe Sh milioni 25… haiingi akilini hata kidogo wakamate mhalifu halafu washirikiane kwenda kuomba fedha.

“Tunaona na mazingira ambayo askari na raia huyo ambao walifika kwenye nyumba ya mfanyabiashara huyo, Samson Mura na kumtuhumu kukutwa na kichwa hicho si mazuri ni ya kutaka kumbambikizia kesi tu. Yaani inasikitisha jeshi kujaa uozo kiasi hiki,”alisema Kifutu.

Naye Musa Magisu alisema polisi hao walifika kwenye nyumba ya Mura na kufanya upekuzi ambao hata hivyo hawakuambulia kitu.

“Pamoja na kupekua kwa nguvu kubwa, hawakukuta kitu. Sisi tunamfahamu Mura ana silaha yake ambayo anamiliki kisheria,”alisema.

Alisema baada ya polisi hao kutoka nje ya nyumba walikwenda moja kwa moja kwenye gari lililokuwa limeegeshwa nje ya nyumba.

“Baada ya kufika kwenye gari, yule raia na wale polisi waliona kuna mfuko wa rambo chini na ghafla wakaanza kuuliza eti mfuko huu una nini na walipofungua wakakuta kuna kichwa cha binadamu.

“Yaani baada ya kukuta kichwa kile, walimuamuru mfanyabiashara yule atoe Sh milioni 25 lakini alikataa katakata akidai hajawahi kufanya tukio la aina hiyo,”alisema.

Alisema mpaka sasa hawajui kwa nini polisi ambao ni walinzi wa raia na mali zao, wamegeuka watu wa kumbambikizia kesi wananchi wasio na hatia.

Ofisa Upelelezi Msaidizi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Morogoro, Asifiwe Ulime alikiri kutokea tukio hilo na kusema mpaka sasa polisi hao wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.

Alisema hata yeye mwenyewe, alifika eneo la tukio na kushuhudia fuvu.

“Tunawashikilia polisi watatu na mwananchi mmoja kwa mahojiano ili watoe maelelezo ya kina juu ya tukio hili,”alisema.

Kutokana na hali hiyo, Ulime amewaomba wananchi wa Dumila kuwa watulivu wakati uchunguzi unaendelea.

1 comment:

emuthree said...

Hiri jeshi rinatakiwa marekebisho, ra sivyo, ritareta kasheshe