Monday, September 22, 2008

Mzee Zephania Musendo aelezea maisha ya Gerezani

Mzee Zephania Musendo (Kushoto) na mke wake na mtoto wao Joseph

Msendo: Kutoka Mhariri hadi Mnyapara Mkuu wa wafungwa

Kutoka ippmedia.com

2008-09-18

Na Mwandishi Wetu


Mhariri Mkuu wa zamani, Zephania Msendo amesema aliteuliwa kuwa mnyapara mkuu wa wafungwa katika Gereza la Mahabusu la Mkuza lililopo Kibaha mkoani Pwani kutokana na ujasiri wake wa kutetea haki za wafungwa.

Msendo ambaye kwa kauli yake hajaridhika na hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, iliyomtia hatiani kwa kosa la kupokea na kuomba rushwa aliyasema hayo nyumbani kwake Kawe jijini Dar es Salaam baada ya kuachiwa juzi kufuatia kumaliza kutumikia kifungo cha miaka mitano jela. Alifungwa Mei 17, 2005.

Anasema anakumbuka alivyopigania haki zake binafsi na kwa wakati huo huo za wafungwa wengine, jambo ambalo lilimfanya mkuu wa gereza hilo kumteua kuwa mnyapara wa kawaida.

Akionekana kuwa na afya njema na furaha, Msendo anasema mara nyingi alikuwa akihoji kwa nini hatendewi haki, licha ya daktari wa gereza hilo kuthibitisha kuwa alikuwa mgonjwa na anatakiwa kupata chakula maalum na kufanya kazi za kawaida.

Vilevile anasema alihoji utaratibu wa kupata msamaha wa Rais, na iwapo anaweza kunufaika nao, lakini alijibiwa kuwa kutokana na kosa lake hawezi kuupata.

Anaongeza kusema kuwa, alihoji kuhusu utendaji wa Bodi ya Parole kwa wafungwa ambao waliotumikia kifungo kwa muda wa miezi 18 na kuonyesha tabia na mwenendo mnzuri, kama wanaweza kunufaika na Bodi hiyo na kupendekezwa kutumikia kifungo cha nje.

Musendo ambaye alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la wiki la Family Mirror la Kiingereza, anasema aliwasilisha malalamiko hayo katika mkutano wa wafungwa mbele ya Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Pwani.

Anaendelea kusema huenda mambo hayo ndiyo yaliyopelekea yeye kuteuliwa kuwa mnyapara mkuu, wadhifa ambao alikuwa nao hadi anamaliza kutumikia kifungo chake.

Kwa mujibu wa Msendo inawezekana pia alichaguliwa kushika wadhifa huo kutokana na kujibu vema maswali mengi yaliyokuwa yakiulizwa na mkuu huyo wa magereza kuhusu matukio mbalimbali yaliyotokea hivi karibuni duniani.

``Mkuu wa Magereza alikuwa anauliza maswali mengi ya current affairs, nikawa najibu ipasavyo, inaweza pia ikawa sababu nyingine ya kuchaguliwa kwangu kuwa mnyapara mkuu wa wafungwa,`` anasisitiza.

Anasema akiwa na wadhifa huo mpya, alipewa mkanda ambao alikuwa akiufunga nje ya shati sehemu ya tumboni na beji yaliyoshonwa katika shati lake iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza, `Convict leader,` yaani mfungwa kiongozi.

Akizungumzia kazi za cheo hicho, Msendo anasema jukumu lake lilikuwa ni kutengeneza orodha ya wafungwa wanaokwenda kufanya kazi nje na ndani ya gereza na kuikabidhi kwa bwana jela kila siku.

Jukumu lingine lilikuwa ni kuhakikisha wafungwa waliopangiwa kazi wanafanya kazi zao kama walivyotakiwa, kukagua usafi wa gereza na kuhakikisha wafungwa hawapigi kelele na kuleta fujo gerezani.

Katika kutekeleza wajibu wake, Msendo anadokeza aliruhusiwa kumpiga kofi moja mgongoni mfungwa anayekaidi kufanya kazi alizopangiwa au kuleta fujo gerezani.

Msendo ambaye anaonyesha matumaini mapya katika maisha yake baada ya kutoka kifungoni, anasema amedhamiria kuandika kitabu kuelezea maisha aliyoyakuta gerezani.

Katika kitabu hicho, Msendo anataka kuishauri serikali kuangalia, kusimamia na kutekeleza kwa msingi haki za binadamu katika magereza.

Anasema wapo wafungwa wengi ambao wapo magerezani sio kwa sababu walifanya makosa, isipokuwa wameingia huko kwa bahati mbaya, kutokana na kubambikizwa kesi za uongo.

SOURCE: Nipashe

No comments: