Monday, September 22, 2008

Mwanamitindo Bora 2008

Kutoka Lukwangule Entertainment:

WALIMBWENDE 13 wamefuzu kutinga kwenye fainali za kinyang’anyiro cha michuano ya kumsaka mwanamitindo bora wa Afrika Mashariki kitakachofanyika Novemba 29 jijini Dar es Salaam.

Mmoja wa waratibu wa kinyang’anyiro hicho Judy Felician alisema leo kuwa walimbwende hao 13 wataingia kambi mwezi ujao pamoja na washindi wengine kutoka nchini za Kenya Uganda, Rwanda na Burundi kupata washindi wanne ambao watakwenda kushiriki kwenye shindano jingine la uanamitindo nchini Ugiriki.

Judy alisema nchi za Kenya Uganda, Rwanda na Burundi zitatoa walimbwende watatu kila moja ambao wataungana kambini na walimbwende 13 wa hapa nchini katika kambi ambayo itaanza Oktoba 25 jijini Dar es Salaam.

Walimbwende 13 waliofuzu kutinga fainali ni Rihama Mohamed, Gloria Emson, Namrata Mandania, Nshoma Mkwabi, Sarah Kazaura, Cynthia Kimasha na Beatrice Wilbard.
Wengine ni Nelly Kamwelu, Doris Godfrey, Evanuru Isaack, Joyce Mbago na Irene Shirima . baadhi ya vigezo vilivyotumika kuwapata washiriki hao ni binti kuwa na umri kati ya miaka 18 hadi 22 na urefu wa sentimita 170-175, kifua cha upana wa sentimita 60.

Kwa mujibu wa Judy walimbwende hao 13 waliofuzu kutinga hatua ya fainali zitakazofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubileee jijini Dar es Salaam walipatikana katika michakato miwili tofauti iliyofanyika Agosti 30 na Septemba 20 na kuhusisha walimbwende kutoka shemu mbalimbali za Tanzania .

Aidha mratibu huyo alisema katika fainali hizo walimbwende wanne watakaoshika nafasi nne za juu watapelekwa nchini Ugiriki na kampuni ya G-Cat ya Uingereza kushiriki katika kinyang’anyiro kingine ambacho kitawakutanisha na wanamitindo wengine kutoka ulaya.
Judy alisema wakiwa Ugiriki wanamitindo hao watachuana kuwania kupata mkataba wa mwaka mmoja kuonyesha mavazi kwa mwaka mzima huko ulaya.

Akizungumzia mustakabali wa walimbwende ambao watashindwa kufuzu kwenda Judy alisema walimbwende hao watakuwa wakitumika katika shughuli mbalimbali za matangazo na masuala mbalimbali ya mitindo hapa nchini.

Shindano hilo linalenga kuwawezesha wanawake na kauli mbiu yake inasema ‘Wasichana wajihadhari na ujauzito katika umri mdogo, umalaya na utumiaji wa dawa za kulevya na Ukimwi’.

No comments: