Monday, December 20, 2010

KUMBUKUMBU ZA REMMY ONGALA


Pichani : Marehemu Remmy Ongala (1947-2010)


KUMBUKUMBU ZA REMMY ONGALA

Na Freddy Macha

Miaka yake ya mwisho ya Remmy Ongala alikuwa Mlokole, tuseme akimsifu Yesu Kikristo. Kutokana na hali hiyo huenda baadhi ya vijana waliozaliwa karibuni wakashindwa kumjua vizuri. Mbali na kubadili dini marehemu alikata nywele zake ndefu na kuacha kuimba nyimbo maarufu tulizozoea mathalan Siku ya Kufa, Nalilia Mwana, Samaki na Mambo Kwa Soksi.

Mwaka 1997 televisheni ya Channel Four, Uingereza ilitoa kipindi (documentary) kilichotayarishwa na Mswidi, Jan Roed, kuhusu Remmy Ongala. Picha na mahojiano zilimwonyesha jijini Dar es Salaam, akifanya shoo zake sehemu kadhaa, akiongea na wananchi, vile vile akielezea dini yake asilia, Kibatala.

Nilifurahishwa sana na maelezo yake Mwanamuziki Ramazani Mtoro Ongala kuhusu imani zetu za jadi kabla ya kuja Wazungu. Leo ni wasanii au viongozi wachache sana bara Afrika wanaothubutu kusema hadharani Uislamu na Ukristo vililetwa na wageni. Mwanamuziki mwingine ni Fela Kuti wa Nigeria aliyekuwa akitambika na kusali kupitia imani za kabila lake la Kiyoruba. Fela Kuti alifariki mwaka 1997 ( kwa UKIMWI) pasina kugeuza imani zake za kijadi; kama alivyofanya marehemu Ongala.

Kimaudhui Waafrika hawa wawili mashuhuri wanatukumbusha kwamba iko haja ya kujichunguza zaidi tunatoka wapi, sisi ni nani na tunakwenda wapi, kiutamaduni.

Nilikuwa na mazoea ya karibu na mwanamuziki Remmy ambaye jina lake Ramazani lina maana “mizimu iko nami” toka nikiwa mwandishi wa habari Uhuru (1976-78). Wakati huo alipiga na bendi ya Mzee Makassy iliyokuwa ikiwika Afrika Mashariki nzima.

Remmy alianza kuitwa Dokta na waandishi wa habari wa Uhuru kutokana na alivyokuwa akivaa kama mchawi. Aliitwa pia mvuta bangi, kichaa hata muhuni. Mwaka 1983 nilianza kumwandika na kumhoji nikiwa na safu yangu ya Utamaduni (Cultural Images) gazeti la Sunday News, baada ya kuchoshwa na dharau kwa msanii huyu aliyekuwa akifungua uwanja mpya wa muziki Tanzania. Mathalan alioanisha muziki wa jadi na wa kisasa (pop) akishirikiana na wacheza ngoma wa Muungano wakiongozwa na Norbert Chenga, manju aliyecheza ngoma ya nyoka na Bugobogobo ya Kisukuma.

Ushirikiano huu ulifikia kilele wakati Remmy alipoanza kuunganisha ngoma maarufu ya “Mdundiko” (ya wenyeji asilia wa Dar es Salaam) na ile Sokous aliyoiimba kwa Kilingala, Kifaransa na Kiswahili. Nilitoa kitabu kuhusu maisha yake kilichochapishwa nikishirikiana na marehemu Stanley Mhando, mwaka 1985.

Kitabu cha Remmy kilifuatiliwa na msururu wa vitabu vingine kimojawapo cha hayati Ben Mtobwa aliyemlinganisha na Bob Marley.

Mwaka 1988 kuna Mzungu (Simon) aliyeituma kanda yake (Nalilia Mwana) kwa kampuni ya “Real World” iliyosajili na kuanza kutoa albam zake Uingereza. Awali Dk Remmy (kama wanamuziki wengine) alitolewa tu Redio Tanzania; hapakuwa na runinga au studio kama leo.

Kati ya 1988 hadi 1998 Remmy aliwaka dunia nzima. Alizunguka na Super Matimila akiimba nyimbo zilizoangalia maisha ya walala hoi, wasifu wa Mwalimu Nyerere (kwa kuondoa ukabila Tanzania) na kuchangia vita dhidi ya Ukimwi (“Mambo kwa Soksi”).

Mara kwa mara niliongea, nikamhoji na kumhoji Remmy alipokuja Uingereza.

Mara ya mwisho alipofanya shoo yake London mwisho wa mwaka wa 1996 katika klabu ya Mean Fiddler alinidokeza anao ugonjwa wa kisukari na kwamba waganga wamemweleza apunguze unene, aache pombe na sigara.

Tulizungumzia pia kuandika kitabu chake kipya katika lugha ya Kiingereza. Mara ya mwisho kuongea naye ilikuwa Oktoba 1997 nyumbani kwake. Wanawe niliowaacha wakiwa wadogo ( Kali, Jessica, Aziza) na Shema (aliyezaliwa karibuni) sasa walikuwa vijana wakakamavu. Mkewe Toni bado aliishi Bongo, akisema Kiswahili fasaha. Na nyumbani kwake palikuwa sasa “Kwa Remmy”, kituo cha basi.

Kifupi alinipa taswira ya mtu aliyeshajijenga; aliyechangia muziki wetu na kutukuza utamaduni wa Bongo ingawa hakuzaliwa hapa. Miaka yote alinisisitizia kuwa yeye ni Mwafrika na kwamba popote alipoishi au kutembea barani palikuwa nyumbani kwake. Mungu ailaze roho yake pema peponi, Amina.

http://www.freddymacha.com/

3 comments:

John Mwaipopo said...

thamani ya mtu huja punde mtu huyo atowekapo. sasa waliokuwa hawajui watajua dk remmy alikuwa mtu wa namna gani. katika nyimbo zake zote huwa nazipenda zaidi Karola na Nalilia Mwana. hakika ni mtu aliyekuza muziki wa tanzania.

Anonymous said...

Muziki wake unauzwa kwenye Itunes na sehemu zingine za kimataifa. Je, familia yake watapata Royalties?

Rest in Peace.

Anonymous said...

nimependa hiyo picha ... na huo mwanya ndio maana yule mama wa kizungu alikubali kubaki nae Afrika maana watu wanasema wanaume wenye mwanya ni mandingo.i.e...(wamefungasha sehemu sehemu)....lala pema peponi dr. remmy