Friday, March 18, 2011

Lowassa Naye Apata Dawa ya Babu Loliondo

Bila shaka mmesikia habari za dawa ya Loliondo. Kuna mchungaji mstaafu ambaye amegundua dawa ya mitishamba inayotibu magonjwa karibu yote. Watu wanahaha kwenda Loliondo, wengine wamekodi hata helikopta! Na serikali ya Tanzania imebariki dawa ya babu! Sasa wagonjwa wanatoroka Muhimbili kwenda kufuata dawa Loliondo!

*****************************************************************************


Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile aka. BABU akipima dozi

Msongamano wa wangonjwa na wananchi wakienda kupata dosi. Dozi ilikuwa shs 500/- tu. Sijui kwa sasa ni bei gani.

Picha na Habari kutoka Michuzi blog:

Lowassa apata kikombe Loliondo, huduma zaimarishwa, bei ya mabasi Ubungo zapanda
Source: Gazeti la Mwananchi

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa juzi alipata tiba ya magonjwa sugu inayotolewa na Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile katika Kijiji cha Samunge, Tarafa ya Sale, Loliondo, mkoani Arusha.

Lowassa alifika katika eneo hilo mchana akiwa na viongozi kadhaa wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na Serikali kisha kupata kikombe kimoja chenye dawa kinachotolewa na mchungaji huyo kwa ajili ya tiba.

Tofauti na viongozi wengine, Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli (CCM), Jimbo linalopakana na Kijiji cha Samunge, alikwenda huko akiwa na viongozi mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini na baadhi ya wapigakura wake.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Lowassa alithibitisha kwenda Loliondo na kuwataja viongozi wa dini alioambatana nao katika msafara wake kuwa ni Askofu Msaidizi wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini, Dk Frederick Shoo na Mkuu wa Jimbo la Masai Kaskazini, Dayosisi ya Kaskazini Kati (Arusha), Mchungaji John Nangole.
Katika ramani ya utendaji kazi ya KKKT, Jimbo la Masai Kaskazini ndipo kilipo Kijiji cha Samunge ambako ni makazi ya Mchungaji Mwasapile.

“Ni kweli, nimekwenda pale na wapigakura wangu pamoja na viongozi wa dini, Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dk Shoo na Mkuu wa Jimbo la Masai Kaskazini, Mchungaji Nangole,” alisema Lowassa na kuuliza: “Kwani hiyo nayo ni habari jamani?”

Baada ya Lowassa kufika katika kijiji hicho akiwa na ujumbe wake, aliongoza moja kwa moja hadi kwa Mchungaji Mwasapile na kuzungumza naye kisha akapata kikombe cha tiba na kuondoka.

Kabla ya Lowassa kwenda kupata tiba, amekuwa akitoa msaada wa nauli kwa wagonjwa mbalimbali wa jimbo lake kwenda kwa mchungaji huyo ambaye dawa yake inadaiwa kutibu magonjwa ya saratani, kisukari, pumu, shinikizo la damu na Ukimwi.

Kwa habari zaidi BOFYA HAPA:

1 comment:

Anonymous said...

Hiyo dawa ya babu imekuwa dili. Kuna wajanja eti ukiwapa laki watakurusha foleni. Lakini ubaya watu wanafariki wakiwa wanasubiri dawa kwenye foleni. Wagonjwa mahutiti wasiende jamani.