Monday, December 15, 2008

Funga Mwaka Arusha


MWANAFA, AY NA C4 DJS UNIT KUFUNGA MWAKA ARUSHA

Wasanii wa muziki wa kizazi kipya Ambwene Yesaya (AY) na Hamis Minyijuma (MwanaFA) wanaotesa katika anga ya muziki kwa sasa, wanatarajia kutoa burudani ya aina yake kwenye uzinduzi wa kundi la C4 DJs linaloundwa na wachezeshaji muziki ambalo linatarajiwa kuzinduliwa rasmi katika mkesha wa sikukuu ya Krismas ndani ya Ukumbi wa Triple ‘A’ jijini Arusha. Kundi hilo linaundwa na Ma-DJ wenye uzoefu wa siku nyingi wakiwemo DJ Joe, DJ Peter, DJ Gerry na DJ A-Plus. Pia kutakuwa na Madj wengine wakali kusindikiza uzinduzi huu wa aina yake.

Aidha maandalizi kwa ajili ya uzinduzi huo na sherehe za funga mwaka yanaendelea vizuri hivyo mashabiki wakae tayari kupata burudani ya aina yake. Uzinduzi huu ndiyo mwanzo wa mfululizo wa burudani ndani ya Ukumbi wa Club Triple ‘A’ hadi mwaka 2009.

MaDJ hao wa kitanzania waliobobea katika fani hiyo wameamua kuzindua umoja huo ili kuonyesha kwamba wapo pamoja na watatoa kipaumbele kwa wahusika wote katika tasnia hii. Baada ya uzinduzi kutakuwa na program ya burudani kabambe ndani ya Ukumbi wa Triple ‘A’.
Siku ya Krismasi kundi la C4 litaandaa onyesho litakalofahamika kama ‘White Party’ambapo wateja watakaopendeza ndani ya mavazi meupe watapewa zawadi kemkem za papo kwa papo.
Na kwa mara ya kwanza katika historia ya burudani katika Ukumbi wa Triple ‘A’ Arusha kutakuwepo na shindano la kumsaka malkia wa Desemba (Miss Desemba). Shoo hiyo itafanyika usiku wa tarehe 26 Desemba. Shoo hii ya aina yake itawahusisha warembo kumi wenye vipaji mbali mbali.

Burudani ya Funga Mwaka katika jiji la Arusha inatarajia kuleta mageuzi makubwa katika fani ya muziki na burudani nchini Tanzania.

Funga mwaka hii itatoa fursa kwa C4 DJs kupata fursa ya kuonyesha umahiri wao katika kupangilia muziki ikiwa ni moja ya lengo la kuendeleza fani hiyo ya muziki ambao ulishika chati zaidi katika miaka ya 80 na 90 kabla muziki wa dansi haujateka soko na watu kuwapa kisogo maDJ.

Katika kuhitimisha Funga Mwaka Kundi la C4 limeandaa bonge la Bethdei party kwa ajili ya kusherehekea mafanikio ya Club Triple ‘A’ zaidi ya miaka kumi.

JOSEPH NAMALOWE (DJ JOE)
MRATIBU

No comments: