Wednesday, December 03, 2008

Waheshimiwa Yona na Mramba watoka jela

Hatimaye mawaziri wa zamani, Mh. Basil Mramba na Mh. Daniel Yona, wamefanikiwa kutoka jela kwa dhamana. Tuone kesi itaishaje.

*******************************************************************
Kutoka ippmedia.com

Mramba, Yona warejea uraiani

2008-12-03
Na Hellen Mwango na Joseph Mwendapole

Mawaziri waandamizi wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona ambao wanakabiliwa na kesi ya kutumia madaraka vibaya jana waliachiwa kwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kutimiza masharti.

Hata hivyo, watuhumiwa hao walizongwa na wananchi wenye hasira baada ya kuachiwa, huku wengine wakitoa maneno ya kuwakejeli na hata kudiriki kuzonga magari yao walikuwa wamepanda.

Umati mkubwa uliokuwa nje ya Mahakama, ulikuwa ukizomea kwa kuwaita `wezi hao...`wezi hao` na kugonga gonga vioo vya magari yaliyowabeba washitakiwa hao, ambayo yaliondolewa kwa kasi kutoka eneo hilo la Mahakama.

Mara baada ya kuachiwa, Mramba alipanda Land Cruizer GX namba T521 AFS ambalo lilikuwa limeegeshwa mbele ya mlango wa kuingia kwenye mahakama hiyo na Yona alipanda gari aina ya Suzuki Vitara T822 ANR lililokuwa limeegeshwa mbele ya gari la Mramba.

Mpaka kufikia jana, washitakiwa hao walikuwa wamekaa gereza la Keko kwa siku saba baada ya shauri lao la dhamana kuwa gumu.

Tafrani hiyo ilitokea nje ya mahakama hiyo mara baada ya Hakimu Mkazi Hezron Mwankenja kukubali hati za dhamana za washtakiwa na kutangaza kuwa, watakuwa nje kwa dhamana mpaka Januari 2, kesi hiyo itakapotajwa.

Mshitakiwa wa kwanza, Mramba alifanikiwa kupata dhamana baada ya kuwasilisha hati za mali zenye thamani ya Sh. bilioni 3.1, na Yona zilikuwa na thamani ya Sh. bilioni 3.063.

Washitakiwa hao walitakiwa kujidhamini kwa kutoa fedha taslim Sh. bilioni 2.9 kila mmoja au mali zenye thamani kama hiyo.

Walifikishwa mahakamani hapo jana saa 1:20 asubuhi, lakini shauri lao lilianza kusikilizwa na Hakimu Hezron Mwankenja saa 5:00 asubuhi katika ukumbi namba mbili wa mahakama hiyo.

Mawakili wanaowatetea washtakiwa, waliwasilisha hati za mali mbele ya hakimu huyo ambaye baada ya kuzipitia, alisema hana shaka nazo.

Hakimu Mwankenja alisema amezipitia hati hizo kwa msaada wa waendesha mashitaka na mawakili na kubaini kuwa hazina kasoro.

Alisema kila mshitakiwa ametekeleza masharti yote ya dhamana aliyopewa na mahakama hiyo na kwamba hati hizo zitatunzwa na mahakama hadi mwisho wa kesi hiyo.

Baada ya kusema hayo, Hakimu Mwankenja aliwaamuru washitakiwa kusimama na waliposimama, alitangaza watakuwa nje kwa dhamana.

Baada ya hakimu kutangaza washitakiwa watakuwa huru, baadhi ya ndugu na jamaa walisikika wakimshukuru Mungu na wengine wakisali.

Baada ya mahakama kumaliza kazi zake, askari Magereza walianza kuwafukuza watu waliokuwa wamefurika katika ukumbi huo ili waweze kuwapitisha washitakiwa kuelekea nje ya Mahakama.

Hata hivyo, watu hao badala ya kwenda nje ya Mahakama kama walivyoamriwa, walibaki katika viambaza vya mahakama hiyo wakisubiri kuwaona washitakiwa kwa karibu zaidi.

Baada ya nusu saa hivi, washitakiwa walitolewa nje ya Mahakama wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Magereza wakiwa wamezungukwa na mawakili wao.

Walipopanda kwenye magari yao, baadhi ya watu waliokuwa nje ya mahakama hiyo, walianza kupiga kelele za `wezi hao`...`wezi haoo`, huku wengine wakigonga gonga vioo vya magari hayo.

Hata hivyo, washitakiwa hao hawakupata madhara yoyote kwani madereva waliyaondoa magari hayo kwa kasi ili kuepusha vurugu zaidi.

Washitakiwa hao wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.

Kusoma story nzima BOFYA HAPA:

No comments: