Wednesday, July 15, 2009

Unapoona Aibu Kuogozana na Mpenzi Wako


Da Flora Wingia Wiki Hii!



Mpenzi msomaji, leo ngoja nikumegee kituko fulani ambacho hata wewe pengine umekishuhudia mtaani kwako, lakini kinaonekana cha kawaida kabisa.

Mtu anapokuwa na mpenzi wake ama mke au pengine mume, huona fahari sana kuandamana pamoja pale wanapokuwa wanakwenda mahali fulani. Iwe ni kwenye mialiko, kazini na kadhalika.

Lakini msomaji wangu ni jambo la kushangaza kwamba wapo baadhi ya watu, ni mara chache sana utaona wanaongozana na wenzi wao(mke, mume au rafiki kutokana na sababu mbalimbali ambazo naweza kusema zimejificha.

Ipo sababu moja nimeigundua ambayo imeniacha hoi, hivyo nikalazimika kuwamegea wasomaji wangu ili nao kama waliwahi kujiuliza niweze kuwapa jibu mojawapo.

Eti wapo watu wanaofahamika kuwa ni marafiki lakini huona aibu kuongozana wanapokuwa barabarani, wakihofia ama kuchekwa au kusemwa vibaya. Kisa ni kwamba eti mmoja ni mtu mzima sana kiumri huku mwingine ni kijana mdogo au wengine huita ‘chekibobu’.

Hivi majuzi jamaa yangu mmoja alinisimulia kisa cha rafiki yake ambaye ni kijana mtanashati aliyefikisha umri wa kuoa lakini amemganda mama mmoja mtu mzima ambaye alishazaa watoto wawili na wanaume tofauti na watoto hao kuchukuliwa na baba zao.

Anasema, kijana huyu mfanyabiashara, amemfungulia grocery ya vinywaji mwanamama huyo na kila inapofika majira ya saa tatu usiku, huenda kumchukua mchuchu wake huyo kwenda zao nyumbani.

“Ajabu ni kwamba, muda wa biashara ukimalizika hapo usiku, bwana huenda kumfuata mwenzake. Ajabu ni kwamba kijana yule siku zote hutangulia mbele kwa umbali fulani, kisha mwanamama humfuata kwa nyuma. Yaani hawataki watu wawaone eti wakiongozana pamoja…sijui wanahofu nini”, anasema jamaa yangu huyo.

“Sababu kubwa niionayo mimi ni utofauti wa umri, kijana ana umri wa miaka 24, mama yule ni mtu mzima anakaribia miaka 48”, anaongeza kusema.

Mpenzi msomaji, ipo misemo mingi inayoweza kuendana na kituko hicho. Kwa mfano, ‘kila shetani na mbuyu wake’…sikio la kufa halisikii dawa… ndege hutua katika mti aupendao…inzi hufia kidondani na kadhalika.

Siku zote, katika mambo ya mahusiano, kila mtu anazo hisia zake katika jambo fulani. Yupo mtu anayempenda mwenzake kwa kuvutiwa na umbile lake, mwingine sura, mwingine namna anavyoongea, tabia yake, ukacharamu wake na kadhalika. Ili mradi kipo kitu kinachouvuta moyo wake na hatimaye kumpenda.

Sasa katika maamuzi ya aina hii, siyo rahisi kumbandua mtu pale alipoukita moyo wake. Yupo anayependa vibinti vidogo vidogo tu.(ndivyo ibilisi wake anavyomtuma). Yupo anayependa mahusiano na watu wenye umri mkubwa kama kijana niliyemzungumzia na yupo anayechagua wanayekaribiana kiumri ili kuweka mizani ya kimaisha sawa. Yote haya ni maisha anayochagua mtu.

Pamoja na yote hayo, bado maamuzi mengine yana athari mbalimbali katika maisha ya kila siku. Tuchukulie kijana niliyemzungumzia. Hajaoa lakini amejichimbia kwa mama mtu mzima ambaye alishazaa watoto wawili kwa wanaume tofauti.

Kijana huyu hajapata mtoto na mama huyo siyo ajabu hana mpango tena wa kuzaa hasa ikizingatia umri nao umesonga mbele. Kijana penzi la utu uzima ndio limemkolea. Je, ataweza tena kuanzisha mahusiano na binti ambaye ni kijana mwenzake na kuachana na mama huyo?

Inanipa shaka kwamba anaweza kujinasua upesi toka kwa mama huyo mtu mzima hasa kwa jinsi baadhi ya kinamama wenye tabia ya kurubuni vijana wadogo walivyo wajanja. Hawa wanajulikana kama mashugamami.

Vijana walioangukia mikononi mwa mashugamami, wengine wameharibikiwa kabisa. Wapo wanaorubuniwa na kinamama wenye uwezo mkubwa, wakiwemo wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo. Huwavuta kwa fedha na wengine wamediriki hata kuwanunulia magari.

Lakini usaliti huu hufanyika kwa siri kwani huwezi kuona warubuniwa wakiambatana na mashugamami hao. Na kwa kuwa hivi sasa kuna simu za viganjani ndiyo kabisa mambo ni kimya kimya. Watendao haya wamuogope sana Mungu. Hukumu iko mbele yao.

Hakika, Maisha Ndivyo Yalivyo. Mimi natoa dokezo tu kwamba tusione watu wanaambatana kwa umbali fulani, kumbe hiyo ni janja tu ya kuficha mambo. Hata hivyo, hebu tujiulize, kama wanayofanya ni halali, kwanini wasishikane hata mikono mashuhuda wakawaona? Au ni yale mapenzi ya wizi tunayoambiwa mitaani?

Mpenzi msomaji, kwa leo niishia hapa nikupe fursa nawe uchangie maoni au kisa chochote unachodhani tunaweza kujadili kwa pamoja. Kila la kheri.

fwingia@yahoo.com

Wasalaam

4 comments:

Fadhy Mtanga said...

Duh! Kwa hiyo huyo mwanamama ni fataki! Kazi kwel kweli!

Kama umemchagua mwenyewe wasiwasi wa nini? Ongozana nae tu watu waone.

Anonymous said...

Basi hawezi kuwa anapenda kweli. Katika mapenzi ya kweli hakuna cha aibu! LOVE IS BLIND!

Anonymous said...

zipo sababu zingine, mfano mwenzie huwa macho juu, au anariga na kumfanya mwezi wake kama kikaragosi hadharani, au wakiwa nyumbani faragha huwa mmojawapo haonyeshi mapendo n.k

Hiyo yaweza ikawa ni kutokana na kujisahau baada ya kumpata mwenzi wake kwa ndoa au urafiki, na hivyo kusahau kuendelea na ubunifu wa kuyapatia chachandu mahusiano yao ya muda mrefu.

Hivyo unapoona mwenzie kajisahau mkumbushe kwa njia ya mawasiliano mazuri ili wajirekebishe.

Mdau
Nguli wa ushauri nasaha ktk mahusiano.

Anonymous said...

huyo kapata mtu wa kumuuzia grocery anamvuna mwenzie wala hampendi