Friday, May 01, 2009

Athari za Mabomu Dar

Picha kutoka Global Publishers

Je, walioathirika watapata fidia gani?

***********************************************
Mabomu Dar: Inatisha!

2009-05-01

Na Waandishi Wetu,Jijini

Hali imekuwa ya kutisha kufuatia taarifa zaidi za athari ya janga la kulipukiwa mabomu na makombora ya kivita pale karibu na Kambi ya Jeshi la Wananchi Mbagala baada ya vifo vya watu kuongezeka maradufu.

Hadi sasa, kuna taarifa kuwa waliokufa kutokana na tukio hilo lililozua hofu kubwa Jijini juzi baada ya milipuko kutokea kwenye ghala la silaha pale Mbagala, wameshafikia zaidi ya watu 13.

Taarifa zinadai kuwa idadi hiyo imetokana na kubainika kuwa kuna raia wengine wamefariki na pia askari sita wa JWTZ wanahofiwa kufa kwa kukatwa vipande vipande na mabomu hayo, hivyo idadi ya wafu kuongezeka toka ile ya jana iliyokuwa chini ya watu 10.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, ndiye aliyebainisha hayo wakati akizungumza na Alasiri leo asubuhi.

Aidha, inadaiwa kuwa majumba ya raia zaidi ya 300, Kanisa la Pentekoste, Misikiti miwili ya Mbagala Kuu na Mbagala kwa Mwanakote yamefumuliwa kwa baadhi ya makombora hayo na kusababisha hasara kubwa.

Pia, taarifa zaidi toka kwenye eneo la tukio zinadai kuwa baadhi ya makaburi ya pale Mbagala kwa Mwanakote, nayo yamefumuliwa vibaya, hasa yale yaliyokuwa yameshajengewa.

Pia kambi hiyo hivi sasa imesalia kama gofu, baada ya majengo karibu yote kambini hapo kusambaratishwa kwa mabomu na makombora.

Kuhusiana na raia aliyeongezeka katika wafu, Kamanda Kova amemuelezea kuwa ni mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa chini ya miaka 12 ambaye mwili wake uliokotwa katika Mto Kizinga.

Naye Brigedia Jenerali Meela wa JWTZ, amekaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa wanajeshi wao sita wanahofiwa kufariki dunia katika mlipuko huo na kwamba hadi sasa bado hawajaonekana tangu baada ya tukio hilo.

Hata hivyo, kuna taarifa kuwa vipande vya miili ya baadhi ya askari vimeshaonekana na kuhisiwa kuwa ni pamoja na hao sita.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi amesema Serikali imeamua kugharimia gharama zote za mazishi ya watu waliopoteza maisha katika tukio hilo.

Akasema leo wanawazika watu wanne, ambao ni wakazi wa Mbagala, kazi ambayo itafanyika leo huko huko Mbagala.

Akasema ndugu wa marehemu hao wameambiwa kusema bajeti ya mazishi ya wapendwa wao ili Serikali itoe fedha hizo.

Akadai kuwa jamaa za watu wanne wanaozikwa leo wameomba shilingi milioni moja kwa kila marehemu mmoja na Serikali imekubali kuwapatia.

``Hadi hivi sasa tunavyoongea ndugu wa marehemu hao wapo ofisini kwa Meya kupewa fedha hizo za kugharimia mazishi,`` akasema Bw. Lukuvi.

Akasema wapo watu wawili ambao walizikwa jana na familia zao tayari zimesema kuwa zimetumia sh. Milioni 2.5 kila moja na Serikali itazirejesha.

``Wenzetu waliozikwa jana walikuwa ni waislamu, kwa imani yao wasingeweza kusubiri hadi fedha zitolewe ndio wazike, hata hivyo wameshasema gharama walizotumia kwa mazishi kuwa ni Mil. 2.5 kila familia na Serikali itazirejesha,`` akasema Bw. Lukuvi.

Aidha akasema ipo miili ya watu wawili ambayo inatarajiwa kusafirishwa kwenda mikoani, mmoja ukisafirishwa kwenda Singida na nyingine mwingine Musoma mkoani Mara.

Akasema jamaa wa marehemu hao pia wameambiwa watamke bajeti ya mazishi na kufika katika Ofisi ya Meya Adam Kimbisa, ili kupewa fedha za mazishi.

Akasema kwa taarifa alizonazo maiti hizo za kwenda mikoani zitasafirshwa kesho ambapo Serikali imeahidi kuwa bega kwa bega na jamaa wa marehemu hao.
Tukio hilo lilitokea juzi na jana, Rais Jakaya Kikwete aliwatembea wahanga katika pale Mbagala na pia katika Hospitali ya Temeke.

SOURCE: Alasiri

2 comments:

Anonymous said...

Fidia! Fidia gani tena! unadhani Bongo Marekani!

Anonymous said...

che mponda omba hisani ya BLOG PUBLISHERS wakupe picha uweke humu. ni hatari nashangaa hakuna chombo cha habari kinachosema ukweli.
hivi habari kama hizo lazima uende kwa mkuu wa mkoa wakati mazishi na maathiriko yanaonekana wazi?
hivi uandishi gani wa habari huu uliooza na kunuka rushwa kiasi cha kushindwa kuandika habari ambazo hata mtoto wa miaka minne atakuambia bila kuhitaji elimu.
INGIA GLOBAL PUBLISHERS UTAONA HATA PICHA ZA MIILI YA WATU WALIOFIA MTONI.
hakuna cha ambulance bali ni mikokoteni ndiyo iliyobeba majeruhi, maiti.
nyumba zimeteketezwa vibaya mnno. wewe najua upo mbali. NDUGU YAKO MICHUZI ANATEMBELEWA NA MAELFU YA WATU AMESHINDWA KUWEKA PICHA BADALA YAKE HABARI ZA MUZIKI WA ASHA BARAKA?
HIVI WATU AU WAPIGA PICHA HUPATA TUZO KWA KURIPOTI HABARI ZA MUZIKI AU MAAFA? HABARI ZINAZOWAGUSA WATU AU ZINAZOWACHENGUA WATU?
WATU WALIOKUFA KWENYE SOKA KULE IVORY COAST, SERIKALI ILITANGAZA MSIBA NA SIKU ZA MAOMBOLEZO. BONGO LALA WAMETANGAZA NINI? WA NADHANI MABOMU NI KITU CHA KAWAIDA TU.
MNATIA AIBU SANA NYIE WAANDISHI WA HABARI. SIJUI KAMA KUNA MTU ANAWEZA KUJIITA MWANDISHI WA HABARI KUANZISHA BLOG NA KUWEKA UOZA WA ASHA BARAKA, KILIMANJARO BEER, JUMA MBIZO, MZIZIMA JULIO. WHAT A RUBBISH! au mkono kinywani?