Sunday, March 27, 2011

Maoni ya Mdau Kuhusu Mjengwa Blog na Dawa za Babu

ndugu mjengwa...

habari za kazi.

kwanza nakupongeza kwa kutumia muda wako mwingi kuelimisha umma wa watanzania ambao kwa bahati mbaya wengi wamo katika giza nene.

nimeshawishika kukuandikia mail hii baada ya kusoma makala zako kadhaa kuhusu dawa ya babu wa loliondo. niliona matusi, kubezwa na kudharauliwa unakokupata kufuatia kuwaambia watanzania ukweli, jamii ambayo kwa miaka kadhaa imezoea kuambiwa uongo, blah blah na kupumbazwa.

kimsingi nakubaliana nawe kuwa dawa ya babu ni abra kadabra. ni pumbazo ambalo limeingia katika jamii yetu kwa wakati huu na kwa bahati mbaya wasomi, wanasiasa na watu mashuhuri wamekuwa ni baadhi ya watu wanaofurika huko loliondo kupata kitu kinachoitwa kikombe.

hivi karibuni televisheni ya kenya ya ntv imetoa documentary kwa lugha ya kiswahili na lugha ya kiingereza kuelezea kile kinachoitwa maajabu ya loliondo. watu wamehojiwa wakiwemo wagonjwa, madaktari na baadhi ya wananchi wa kawaida hasa wa arusha. kuna maoni mchanganyiko kuhusu suala hili lakini ni wazi kuwa watu wamepumbazwa na maelezo kuwa mtaalamu wa dawa hiyo ni mchungaji mstaafu. kwa kuwa ni mchungaji mstaafu basi bila shaka dawa yake ni ya kweli!!!!

suala hili linaendeshwa kidini zaidi badala ya kijamii. wengi wa watu wanaodai kuponywa hisia zao wameziegemeza zaidi katika cheo au hadhi ya uchungaji wa babu. hii ni psychological treatment ambayo kwa vyovyote itaonekana kwa siku kadhaa kama sio miezi lakini baadae itaondoka na ndipo watu watakapojiona kuwa ni wapumbavu na hawakupata nafuu yoyote kutokana na kikombe cha babu.

ingekuwa mtaalamu huyu wa loliondo hakuwa mchungaji mstaafu hwenda hali ingekuwa tofauti kwa wanasiasa wetu na viongozi wa kijamii lkn hili la uchungaji ndilo linalowapumbaza watu na kujiona kuwa kumpinga babu na dawa yake ni sawa na kupinga imani jambo ambalo kwa mtazamo wangu si sahihi na ni kujipotosha wenyewe. dawa ya babu na imani ya dini hapa ni vitu viwili tofauti ambavyo vimewekwa pamoja.

kuna wengi duniani wanaotumia kivuli cha dini kwa maslahi yao na watu kupumbazika kwa kuona kuwa kinachosemwa na mtu husika hakipaswi kupingwa maana ukipinga utakuwa umepinga dini na dini inaogopwa. mtu huogopa kuwa akipinga ataonekana ameasi au atalaaniwa na dini au mungu.

maslahi ya dawa hiyo tunaambiwa yanagaiwa kwa kanisa husika, wasaidizi wake na kiasi kidogo huchukuwa yeye babu. katika hali kama hiyo iwapo kanisa linapata share fulani jee unategemea kuna kiongozi wa kanisa lake atakaemkataza? hilo haliwezekani maana kanisa litakosa mapato ambayo halikutegemea kuwa yangetokea.

mnakumbuka kufukuzwa kwa father NKWERA na waumini wake na kutengwa na kanisa lake? sababu kuu ilikuwa ni kufanya maombi na kuponyesha wagonjwa jambo ambalo lilisemwa kuwa si katika mafundisho ya kanisa. inawezekana kanisa la babu na la father NKWERA ni tofauti lakini hoja ipo pale pale. father NKWERA hakuwa ananufaisha kanisa kwa wakati ule lakini babu analiingizia kanisa fedha za kutosha hivyo watu wanafumba macho.

kwa bahati mbaya wanasiasa nao wamekumbwa na uozo huu. wakati waziri wa afya alitoa tamko awali kabisa la kupiga marufuku dawa hiyo hadi uchunguzi ufanyike, waliibuka wanasiasa uchwara ambao kwa kutaka sifa waliona tamko lile la waziri halina maana. kina SHIRIMA NA LUKUVI wakalivalia njuga jambo hilo na kudai kuwa serikali ipo pamoja na babu. waziri wa afya kwa kuepusha shari ya udini aliamua kukaa pembeni na kujinyamazia kimya.

hawa kina SHIRIMA na LUKUVI wanadai kuwa ni suala la kiimani hivyo serikali isiingilie imani za watu. wamesahau siku chache tu kabla ya uchaguzi mkuu mwaka jana mtu mmoja aliyejipa cheo cha mtabiri maafuru afrika mashariki na kati alitangaza kuwa mgombea mmoja wa uchaguzi angefariki dunia kabla ya uchaguzi mkuu na kupelekea uchaguzi kuahirishwa.

serikali hiyo hiyo wanayoisema kina LUKUVI na SHIRIMA ilitoa tamko kali la kupinga kauli hiyo na kumtaka mtabiri huyo anyamaze kimya au atachukuliwa hatua. serikali haikusema kuwa mambo yake ya utabiri ni maswala ya kiimani anayetaka aamini na asietaka aachane nae. lakini sasa tunaambiwa kuwa masuala ya imani serikali haiwezi kuingilia. hatua ile ya serikali kwa mtabiri yule ilikuwa sahihi kabisa lakini kwa sasa tunaona serikali ikiwa na kigugumizi kuhusu babu huyu.

hivi sasa kina babu wanaongezeka, wengine wakitokea mbeya. si hasha baada ya siku chache tukasikia mwengine ameibuka dar es salaam au mtwara au mwanza au hata pemba akidai nae ameoteshwa kuwa awahudumie watanzania kwa dawa ambayo formula yake haijulikani.

kwa ufupi dawa ya babu ni kanyaboya kwa hoja zifuatazo:

1. maradhi anayosema inatibu ni maradhi yanayosababishwa na vitu tofauti. baadhi husababishwa na virusi, mengine bakteria na mengine ni matatizo ya kutokuwa na uwezo wa homoni fulani mwilini. kwa vyovyote vile dawa ya matatizo haya haiwezi kuwa ni moja kwa sababu hata chanzo chake si kimoja. kwa mfano huwezi kupeleka gari gereji kwa matatizo tofauti kisha ufumbuzi wake kuwa ni huo huo mmoja. tatizo la gear box, chasis au tyre haviwezi kuondoshwa kwa aina moja ya ufumbuzi.

2. kauli za babu anapohojiwa na vyombo mbali mbali vya habari zinatofautiana. kuna sehemu anasema kuwa dawa yake inatibu maradhi matano kama alivyoambiwa na mungu. kuna sehemu anasema kinachotibu sio huo mti bali ni maombi yake na kuna sehemu anadai kuwa kinachotibu ni kikombe hivyo dawa husika isipotekwa kwa kikombe chake (kikitumika cha mtu mwengine) haitamsaidia mgonjwa. hizi ni kauli zenye mgongano. kwa mtu mwenye kutumia akili, hapa babu anajaribu kutumia ujanja wa kuzuia watu wengine wasiweze nao kujitengenezea dawa hiyo na kugawa kwa watu. anajaribu kutengeneza dominancy au monopoly katika jamii. kutakapokuwa na babu wawili au watatu bila shaka idadi ya wagonjwa wanaokuja kwake itapungua na hatimae maslahi kupungua pia.

3. kuna wakati babu hueleza kuwa dawa husika haiwezi kufanya kazi kwa mtu aliyefanya ujanja kwenye foleni kwa kuwapiku wenzake aliowakuta. hii ni njia nyengine ya ajabu kwa kuwa hakuna uhusiano wowote wa kitiba na suala la mtu kupanga foleni au kutokaa foleni.

4. kuhusu malipo ndo ujanja wa wazi kabisa. babu anadai ameambiwa na mungu kuwa atoze shs 500 tu kwa watz na dola 1 kwa wageni. hata hivyo hakusema iwapo kutakuwa na mabadiliko ya kupanda au kushuka thamani ya pesa itakuwaje? jee shs 500 au dola 1 itabakia hivyo milele? na jee binaadamu wanaotoka nchi ambazo hazitumii dola wala shs? au mungu hatambui fedha za nchi nyengine katika dunia yake zaidi ya dola na shilingi?

5. dawa husika anadai ni lazima itolewe loliondo tu. hii pia ni ujanja wa kuhakikisha kuwa hakuna babu wengine wanaoweza kufanya kazi hiyo katika mikoa mengine. ukitaka usitake ni lazima uende loliondo tu. ni kucheza na akili za watu na kwa bahati mbaya watu wamepumbazika.

6. kuhusu kulipia hapa napo pana jambo. kazi ya mungu huwa ya kujitolea lakini hakuna pahala babu anaweka utaratibu kwa watu wasio na uwezo wa hiyo shs500. jee anataka kutwambia kuwa mungu hajali watu mafukara ambao hata hiyo shs500 kwao ni kiwango kikubwa? vitabu vyote vya dini vinataja haja ya kuwahurumia mafukara na wasio na uwezo. lkn kwa hili babu yupo kimya sana. labda baada ya mfuko kujaa ndipo atakapotoa ofa kwa wasio na uwezo.

7. mwisho dawa ya babu haina dozi. hiki ni kituko chengine. kwa aliye mahututi aliye na nafuu nk wote ni kikombe kimoja tu. hili ni la kuchekesha kama sio kusikitisha. hata hao waganga wengine wa kienyeji hutoa dawa kwa mujibu wa hali ya mgonjwa. lakini pia kabla ya mgonjwa kupewa dawa huchunguzwa kama ana aleji au tatizo lolote kama vidonda vya tumbo nk. lkn hilo halipo kwa babu. kikombe hicho hakijali uzito wa ugonjwa wala afya yake. hakijali presha ya mgonjwa wala lishe yake. iwe ameshakula au ananjaa kikombe ni kimoja tu. hii ni hatari kwa jamii. hata katika mambo ya kawaida ya binaadamu hali haipo hivyo. gari la tani 3 litabeba mzigo wa tani 3 na la tani 10 litabeba mzigo wa tani 10. huwezi kusemwa magari yote yabebe tani 10 wakati yana uwezo tofauti.

sikutaka kutumia hoja za kisayansi kuwa dawa hii haijathibitishwa kwa kuwa watu wengi wanajidanganya kuwa dini ni zaidi ya sayansi. kwa maoni yangu dini na sayansi havipingani hata siku moja. ukiona hivyo kuna tatizo pahala.

mbali na hali niliyotaja hapo juu, kuna madaktari na wataalamu wa afya huko arusha ambao walishuhudia wagonjwa wakitolewa hospitali na kupelekwa kwa babu wamethibitisha kuwa baadhi yao pamoja na kupata kikombe hicho na kujidanganya kwa siku chache kuwa wamepona wamejikuta wapo hoi na kurudi tena hospitali. huu ndio ukweli ambao utajulikana siku si nyingi kwa kuwa maji hayo yaliyochemshwa hayana dawa yoyote na hayasaidii kuondoa ugonjwa.

kwa bahati mbaya pamoja na ukweli huu baadhi ya watu hudai kuwa wagonjwa hao waliojiona kuwa hawajapona eti walikwepa foleni au kutofuata utaratibu wa babu!!! huu sasa ni ujinga mwengine. wengine wanadai kuwa madaktari hao wanamuonea wivu babu eti kwa sababu kawanyanganya wateja wao!!! wakati watu wanawatahadharisha wao kuepuka kanyaboya wao bado wamo katika usingizi mzito wa kulewa kikombe cha babu...

kwa ufupi wafuasi wa babu wanataka kusema kuwa ni lazima watu wote waliopata kikombe hicho kumsifu babu na anayekwenda kinyume kwa kudai kuwa hajapona huonekana ndio mkorofi. kuna haja ya watanzania kutafakari na kuchukua hatua. tukumbuke kauli ya mhe rais KIKWETE kuwa AKILI YA KUAMBIWA CHANGANYA NA YA KWAKO....

Wakatabahuuu,

mdau
ughaibuni...

17 comments:

Anonymous said...

Maggid na wanabidii wote habarini za jumapil!!
Kama nilivyokwisha kusema juu ya hili la babu, Binadamu tumefikia mahali tunafikiri kuwa Mungu anfikiria namana tunavyo fikiria. Mwaswali aliyouliza Maggid siyo retorical/ akunogesha story bali ni ya msingi ya kujiuliza. Mungu hakutupa utashi kwa bahati mbaya, ni kwa malengo mahsusi kama kuchunguza/research ili tupange njia ya kupitia/venture route.
Tumechoka sasa kufikiria kupitia njia halisi ambazo ni ngumu, tunaamua kuwa wavivu na kuchagua njia rahisi ya simply believe.
Naamini kuwa nafikiria na napitia njia sahihi kwani binafsi natamani iwe tiba na kama alivyosema paroko wa Dar basi itakuwa endelevu.
Pia naomba Mungu yasiwe kama yale ya Kibwetere kule Uganda.

Anonymous said...

Sisi tulio Wakristo tunaamini katika kuboresha maisha ya wanadamu na kuifanya dunia kuwa mahali bora na pa amani zaidi. Taasisi za kikristo zimekuwa mstari wa mbele kujenga mahospitali, mashule na kila huduma za jamii ili kusaidia wanadamu. Pia Kanisa linahimiza maombi ya kila namna yote kwa lengo la kuleta uzima kwa mwanadamu. Focus yetu kama wa kristo ni kuleta ahueni kwa wanadamu walio katika mateso ya aina mbalimbali.

Mchungaji kwa nia njema ametumiwa na Mungu kusaidia walio kata tamaa na ushahili upo. Mchungaji hajasema anazuia kifo. Ni dhahiri watu wataendelea kufa kwani kifo kipo tu. Lakini ukifaulu kuleta uponyaji wa asilimia 70 ya watu wenye magonjwa yasiyo na tiba hayo ni mafanikio makubwa.

Hata Yesu mwenyewe hakuponya watu wote duniani alipokuwa hapa duniani miaka 2000 iliyopita.

Watu wanaugua kwa sababu mbalimbali. Sasa Mtu akipona ukimwi akaendelea na ngono unafikiri itakuwaje?

Hospitali zote duniani zimeshindwa kuzuia watu wasife hata zile hospitali bora zaidi ulaya na Marekani.

Watu wengi wanaompinga Mchungaji wanaoenekana kutoka dini za wenzetu wasio wakristo.

Lakini watu waliokwenda kunywa dawa wengi zaidi ni wa dini zingine wala siyo wakristo.

You need to give the Retired pastor some credit.

Hata kama baadhi yao hawatapona. Mchungaji ameshajitahidi kuwasaidia. Na ikumbukwe Aliwafanya waugue siyo mchungaji. mchungaji yuko upande wao kuwasaidia wao wapone.

Give the Pastor some Credit.

Anonymous said...

Read the following collection of scientific journal articles on the said tree with respect to this quotation from Rose Shija (NPO-EDM,WHO) in regard to the first article below: "Please find herewith attached some information on the plant being used in Loliondo. Plants from this genus have been used traditionally in Africa and other parts of the world to treat a variety of disease conditions.

The genus has also already been studied and various chemicals extracted and tested for their medicinal properties. The plant in Tanzania is Carissa edulis. It is
also found in Kenya and KEMRI last year did a study and isolated some compounds which have antiviral properties.

NIMRI and the Traditional Medicine Institute are now working on it too. I hope that more African research institutions will be supported to do further studies especially on the identified compounds to make 'medicines'."

Anonymous said...

Watanzania sisi yaani sijui, sisi tunapenda maneno marefu, theory ndefuu, lakini anything practical hatutaki kusikia: hayo maoni nimeshindwa hata kuyasoma yote jinsi yalivyo mengi...

Kwa nini tusiwapime wanaoenda halafu tuwapime wakishakunywa majibu yajionyeshe practically yenyewe?

Mara dawa haifai kwa sababu bei ya dawa mara dola 1 na mara miatano kwa wenyeji, bei inahusika nini hapo... wewe wapime je virusi vya ukimwi havionekani? there are only two possible results either negative au positive no discussion sijui shilingi ngapi bei hiyo haina tija hata ingekuwa milioni issue ni kuwa je dawa inaponesha?

Wino upo lakini wabongo sharti watumie mate.

Kawapimeni kabla hawajaenda, wakirudi wapimeni tena FULL STOP.

Anonymous said...

wamesitisha huduma kwa babu loliondo angalia tbc news kwenye subi wavuti

Rik Kilasi said...

Kaibuka mwingine mbeya sasa sijui hili ni dili au kweli.Na kwakua kila mtu anazingatia shida alizo nazo mjadala haupo bali ni kwenda kupata hio dawa.NTV ya kenya imehoji baadhi ya madaktari Arusha wamesema hawaamini kama inaponya kwani kuna wagonjwa wamerudi wodini hali zao zikiwa mbaya baada ya kuacha kutumia dawa walizo pewa.

Sasa ukweli sijui uko wapi na kwanini wengine wapone wengine wasipone? ndio kusema hio dawa inachagua watu wa kupona? Watu wana hoji sijui huyu mzee anatumia mgongo wa dini je na huyo kijana wa miaka 17 wa mbeya je? ila ukweli naamini utakuja julikana siku 1.waliopona hongera zao na ambao hawajapona wazidi kuwa na imani hakuna mtu anapenda awe na tatizo ila likikufika kwenda kwahuyo babu mtu hujiulizi mara mbili.

Anonymous said...

Yah! Mdau wa ughaibuni. It's obvious you have gone to school. Lakini kama wewe ni msomaji biblia, unakumbuka kile kisima ambacho watu walikuwa wanawahi kujitumbukiza ili wapone wakati wa enzi ya Mfalme wetu Yesu Kristo? Hapo utazungumzia vipi. Please the ground is open. Jackson, Kigoma Tanzania.

Anonymous said...

Mtoa maada maada yako ni nzuri lakini ningependa kuongelea kuhusu bei Tsh.500 na $1 nafikiri kwa watu wa nchi zisizo tumia Tsh.wao watatumia $ watabadilisha pesa zao kwa $ na kama vile sisi tukienda nchi zingine hatutumii Tsh. ila tunabadilisha $au au pese yoyote ya kimataifa. Nafikiri hapo hakuna utata.

Mfiwa said...

Naomba kutoa ushuhuda kuwa nilimpeleka mgonjwa wangu mke wa rafiki yangu mpenzi kwa Babu wiki mbili zilizopita ili kupata dawa kutokana na maradhi ya Breast cancer ambayo yamekuwa yakimsumbua kwa muda mrefu. Kama sote tunavyojua hakuna dawa ya kutibu kansa, lakini baada ya kusikia habari za Babu tulijenga imani kuwa huenda akapona. Tulimpeleka huko, na baada ya kukaa siku mbili kwenye foleni alibahatika kupata dawa na kuinywa. Lakini toka anywe hiyo dawa hali yake imekuwa sio nzuri na kudhoofu siku hadi siku hadi hii leo saa nne asubuhi amefariki dunia. Ninatoa ushuhuda huu si kwa kuwakatisha tamaa watu la hasha bali ni kutaka kuweka vitu hadharani ili watu wajue kuwa pamoja na kuwa huenda dawa hiyo ikawatibu baadhi ya watu lakini watu tujue pia hakuna dawa ya kuponya kifo. Huenda kweli babu anatibu kwa imani, lakini sidhani kama wale wote wanaoenda huko hawana imani. Namalizia kwa kuzidi kuwaomba waliotibiwa na kupona kweli wajitokeze watuthibitishie kwa ushahidi wa kitabibu.

Anonymous said...

Nimeona hiyo dawa ya babu ikiwa na rangi mbalimbali. Je zote zina nguvu sawa?

Anonymous said...

NINAMUUNGA mkono kabisa yule mwandishi wa Mwananchi aliyethubutu kusema kwamba ajabu ya nchi hii ni kuwa viongozi wetu ni wepesi kutuma majeshi au polisi au FFU kwenda kuzima maandamano ya wapinzani kuliko kutuma majeshi hayo kwenda kufanya jambo jema litakalopunguza matatizo ya wananchi au kuwaondolea shida au dhiki fulani.
Kinachoshangaza ni kuwa kweli viongozi wetu wamekuwa wagumu au wameshindwa kutupatia tiba ya bure-sawa; nyumba au vifaa vya ujenzi vya bei nafuu-sawa; elimu au mikopo ya elimu ya gharama nafuu-sawa; lakini hivi kweli ndio hao hao wanashindwa kutupatia 'easy access' kwa babu baada ya kuwa wao weshaenda na kunywa kikombe chao na kila siku tunaona picha zao kwenye magazeti na TV wakinywa vikombe kabla yetu bila aibu. Huu ni ubinafsi wa kupindukia, na ni aibu viongozi wa nchi kuwa na ubinafsi wa namna hii!!!
Ninaamini kwamba kama tuna serikali ambayo inashindwa kutekeleza mawazo ya mwandishi huyu, yaani, kuifanya Loliondo ikapitika kwa urahisi, vyakula, maji, vyoo na huduma zote muhimu zikapatikana bila shida basi ni vigumu kuona ni jinsi gani serikali inayoshindwa kuendeleza tena kwa faida yake na watu wake eneo dogo kama hili litaweza kuendeleza nchi yetu nzima ?
Loliondo imetufungua wengi macho. Tumeuona ubinafsi wa viongozi wetu uchiuchi. Na hakuna siri tena. Nchi hii ina viongozi wabinafsi. Wanataka kila kitu wapate wao kwanza. Na kwa muktadha huu tusahau kabisa kwamba tuna aina ya viongozi ambao wanaweza wakawatoa watu toka kwenye umaskini wakati viongozi hao wametawaliwa na umimi na ubinafsi. Tuna viongozi wa siasa na wa dini, lakini ona fedheha na vichekesho hii leo ya viongozi hao. Huku baadhi redio zao zikimponda babu wao ndio wamekuwa wakwanza kwenda kupata kikombe.
Niwaambie ahlili-kitabu kwamba mwenyezi Mungu hawezi kuwa mjinga hivyo kumpa fisadi, mwizi, mabarakala wa wanasiasa, mla mrushwa, mbinafsi karama zake. Na ndio maana kampa babu akijua fika kuwa sio mchafu kama hao wenye majoho ya sufi na vilemba vya hariri lakini ni wachafu kupindukia.

Viongozi wa serikali nao walivyokwenda na kupata dawa ndio ikawa wamemaliza kazi yao. Wakati kiungwana na kistaarabu kwa miiko ya uongozi wao wangelistahili kuwa wa mwisho kabisa baada ya wagonjwa wa kikwelikweli kwenda kutibiwa kwa urahisi na bila matatizo yanayojitokeza sasa.
Je, amiri jeshi wetu na majeshi yake wanatafsiri neno VITA kuimanisha nini? Na je, mahala panapohitaji akili, vifaa na mijiguvu ya kijeshi hivi unaweza kuwatuma wakuu wa mikoa ambao hata kama wana historia ya kuwa wanajeshi akili zao sasa hazifanyi kazi tena kijeshi na wamekuwa hana tofauti na raia wa kawaida?
Vita sio tu pande mbili zenye silaha kupambana au kuuana. Vita ni hali yoyote ile ambayo inaweza ikasababisha ugumu, dhiki, maradhi, ulemavu na hata kifo kwa wananchi. Hali kama hii ikijitokeza kama tulivyoona kwa wenzetu Wajapani na majeshi yao huwa ni sawa na hali ya kivita.
Wananchi wanaoingia Loliondo hivi leo ni sawa na wale wanaoingia Uwanja wa Taifa kutazama mpira wa miguu kwa mwaka mzima. Na mapato ambayo yanaweza kutokana na dawa ya babu kwa serikali na wananchi yanaweza kuwa mara 10 ya yale yanayopatikana toka uwanja huo wa taifa. Lakini serikali na viongozi wake kwa akili yao wameona ni bora kusaidia mabilioni mpira uendelee na hauendelei lakini serikali hiyo hiyo na viongozi wake wanaona uchungu kutoa bilioni chache ili barabara Loliondo ipitike na huduma bora na nzuri zipatikane wakati wote na kuliondolea taifa hili aibu ya kukutwa watu wake hukoNgorongoro wanakwenda kujisaidia vichakani na takataka zinatupwa ovyo kama viongozi hao hawakwenda kwenye mkutano wa mazingira huko Rio, Brazili na kwingineko duniani.

Anonymous said...

Nimesikia kuna mkakati wa waganga wa kienyeji wote pamoja na wachawi waliokubaliana wote wajitokeze nchi nzima kudai kuwa wameoteshwa kutoa tiba.

Ndio maana wote wanaigiza mtindo wa kutumia kikombe wakati waganga wote walikuwa wanatoa dozi mbali mbali. Na wote wamekubaliana watoze sh. 500 tu kumuigiza mchungaji.

Lengo lao ni kuishinikiza serikali iwafungie wote wanaotoa tiba ikiwemo mchungaji kwa kuwa mchungaji ameharibu soko lao.

Kawaida waganga walikuwa wanaomba kuku, mbuzi na walikuwa wanatoza pesa nyingi lakini ili kupambana na mchungaji wameamua kutoza sh. 500

Anonymous said...

Babu hana kipimo cha ugonjwa wa mtu.Kuna watu wanaenda na magonjwa ambayo dawa yake haitibu, na wakitoka huko hawaponi wanaanza zao.Hata mahospitalini kwani wote wanapona licha ya kuwa wanapelekwa kwa madaktari bingwa?

Hata kama ulimpeleka mgonjwa wako huko na hakupona hiyo si sample ya kama dawa inaponyesha u vipi.Kuna wengine mmetoa mfano wa madaktari wa Arusha ambao wamekana kuponya kwa dawa hiyo, mbona kuna daktari hukohuko Arusha amekiri kuwa dawa ya Babu imemponya ugonjwa ambao aligunduliwa kuwa nao akiwa Ujerumani?

Nadhani tuache mlolongo wa matusi na kebehi tuwaachie wenye shida zao wakatatuliwe na wasiyo na shida wakae wakila na kufurahi kwa sababu hawaugui.

Kam wataalamu na watafiti wamefanya tafiti zao na kukiri kuwa dawa haina madhara kwa binadamu wewe una hofu nini waache watu wanywe maji ya mti huo anajua Mungu alieyeotesha neno lake humo kama babu asemavyo wapone.

Hata Yesu hakuwaponya wote aliokutana nao huku dunianni wengine waliwakataa live sembuse kikombe cha Babu.Watu hawaelewi, babu amesema alipewa huduma hiyo na Mungu, Mungu ameotesha "neno" katika mti huo.sasa wewe unaenda kizegezege tu bila imani unategemea nini> Eti labda na huyo mgonjwa wa kansa atapona!!Tayari una wasiwasi.hata hospitalini waganga wanaanza na kuwatia moyo wagonjwa ili waiamini dawa au vodonge wanavyopewa ndiyo maana kuna counseling kwa mgonjwa mabayo inafanywa na daktari kabala ya kumpa dawa au kumtibu mgonjwa ili aamini huduma anayopewa itamsaidia.

Anonymous said...

Hivi ndugu zangu wale wanaokwenda na Helcopter ama Ndege pale kwa Babu Loliondo wanapitia mlango wa Fast track pale kwa Babu au wakifika wanaingia kwenye foleni kama walahoi wengine??

Anonymous said...

Ndugu zangu kule Loliondo tumesikia baadhi ya watu kulalama
kupoteza ndugu zao na jamaa zao walioenda huko kwa ajili ya matibabu ya dawa hiyo , leo hii huku mtaani kwetu kuna mtu mmoja tunaenda kumzika dakika chache zijazo baada ya kunywa ile dawa na kufariki - hivi ni vifo ambavyo havitangazwi na hata watu hawataki kusikia habari hizi lakini ukweli ni kwamba suala la loliondo limesababisha vifo na kupoteza nguvu kazi nyingi -- ipo siku ndugu jamaa na watu wa karibu wa waliofariki kutokana na suala la babu huyo kupeleka suala hili
katika vyombo vya sheria ichukuwe

Anonymous said...

ANAYESEMA KUWA "BABU" NI TAPELI, KAFILISIKA KIUTU, - KIIMANI,- KIHEKIMA, NA HATA HANA HESHIMA YEYE MWENYEWE - Apuuzwe.
SWALI LA KUJIULIZA NI; JE WOTE WANAOKWENDA KWA "BABU" ANAWASHINDA AKILI NA UELEWA? NASHAURI TUNAPOTOA MANENO TUYAPIME. HUYU ANAMTUKANA MZEE WA WATU, MTUMISHI WA MUNGU KAMKOSEA NINI. KAMA ANGETAKA KUWATAHADHARISHA WATU KUHUSU MATIBABU YA "BABU" BASI ANGETUMIA MANENEO YA HEKIMA. "ASHINDWE NA ALEGEE KABISA" MUNGU ATAFANYA KAZI JUU YA WATU WANAOBEZA UWEZO WAKE.

Anonymous said...

da chem hao wanaosema babu ni tapeli naomba ukipata mda ingia kwenye blog ya frola saloon usome huyo dada kaenda mwenyewe loliondo anaelezea safari yote na jinsi sasa kapona pum iliyokuwa inamsumbua